The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Shauku ya Kujitegemea Yawasukuma Wanawake wa Kizanzibari Masokoni

Wengi wao wamejikuta wakichukua uamuzi huo baada ya kuachwa au kutelekezwa na waume zao.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Bikombo Hamad Issa huamka kila siku asubuhi na mapema na kuwahi katika Soko la Kwerekwe, lililopo mjini Unguja, kuwahi wateja wanaofurika katika soko hilo kubwa kisiwani hapa kujipatia mahitaji mbalimbali ili awakidhie baadhi ya mahitaji hayo.

Bikombo, 56, hana biashara ya kudumu anayoifanya sokoni hapa. Mama huyo wa watoto nane, mkaazi wa Meli Sita, kisiwani Unguja, huuza bidhaa zinazoendana na msimu. Hivi sasa ni msimu wa maembe, kwa hiyo, Bikombo hiyo ndiyo biashara yake kwa sasa.

The Chanzo ilimkuta Bikombo akiwa amekalia ndoo ya rangi ya njano, akiwa amevaa baibui jeusi na kanga aliyojifunika kichwani, huku mkono wake wa kulia akishika kipochi chenye pesa na mkono wa kushoto uko kwenye ndoo ya lita kumi yenye maembe dodo, biashara yake kwa sasa.

Kwenye mazungumzo na Bikombo, ilibainika kwamba kilichomsukuma mama huyo kujiingiza katika biashara sokoni hapa ni shauku yake ya kutaka kujitegemea kiuchumi ili aweze kuihudumia familia yake ambayo, kwa maelezo yake, imetelekezwa na mwenza wake.

SOMA ZAIDI: Ushauri Watolewa kwa Wanawake Wajasiriamali Mtandaoni

“Mimi niliolewa kwa mara kwanza nikiwa na umri wa miaka 23 na kubahatika kupata watoto sita na mume wangu wa kwanza, baada ya mume wangu kuongeza mke wa pili maisha yakabadilika, mume wangu akawa haleti chakula na akileta analeta Sh3,000.

“Mwisho akatuacha kabisa na hakuwahi kurudi tena. Nikakaa na kuhangaika na maisha mwisho nikaolewa tena. Kumbe mume ana mke mwengine na huko nikapata watoto wawili na baada ya muda yale yale ya mwanzo yakajitokeza. Nikaondoka na watoto wangu,” Bikombo aliiambia The Chanzo.

Fatma Abdi, mfanyabiashara wa miguu ya kuku, utumbo akiwa kwenye sehemu ya biashara kwenye soko la Kwerekwe Zanzibar.

“Sikuweza kurudi nyumbani kwetu na watoto nane niliokuwa nao, hivyo niliuza kitanda changu kimoja na kupata mtaji wa kuanza biashara ya kuuza bidhaa katika soko hili [la Kwerekwe],” aliongeza mjasiriamali huyo.

Ukatili wa kijinsia

Utekelezaji wa familia ni moja tu kati ya aina nyingi za ukatili wa kijinsia unaofanywa dhidi ya wanawake wa Kinzanzibari, ukatili ambao kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) ni “uhalisia wa kila siku” kwa wanawake na watoto visiwani humo.

Asilimia 14 ya wanawake wa Kizanzibari hukabiliwa na ukatili wa kimwili kutoka kwa wenza wao na takriban mwanamke mmoja kati ya kila wanawake 10 hukabiliwa na ukatili wa kingono, kwa mujibu wa UNICEF.

SOMA ZAIDI: Watoto 1,173, Wanawake 185, Wanaume 3 Wafanyiwa Ukatili Zanzibar 2022

Shinikizo la kuhudumia familia ama baada ya kuachwa au kutelekezwa na waume zao huwasukuma wanawake wengi wa Kizanzibari kuangazia fursa zilizopo kwenye ujasiriamali kama sehemu ya juhudi zao za kujikomboa.

Hata hivyo, kutokana na changamoto zinazowakumba, kama vile kutokumiliki ardhi na kutokuwa na akaunti ya benki, miongoni mwa sababu nyingine kadhaa, wanawake hawa, kwa kiwango kikubwa, hujikuta wakijihusisha na biashara zisizo rasmi, kama vile za kuuza bidhaa masokoni.

Akizungumza na The Chanzo, mwanamke mwengine anayefanya shughuli zake katika soko hili la Kwerekwe, Fatma Abdi, alisema kwamba alilazimika kutafuta shughuli yoyote tu itakayomuingizia kipato ili aweze kuhudumia familia yake baada ya kutelekezwa na mwenza wake.

Fatma, 37, anasema alikaa kwenye ndoa kwa muda wa miaka sita ila baada ya kupata watoto maisha yalibadilika na kuanza kuona huduma, hususan za chakula, zikipotea na kuona watoto wake wanahangika.

“Mimi napewa Sh2,000 ya siku nzima, chakula mara tatu na watoto nitakula nini na ndani hakuna kitu?” alilalama mama huyo wa watoto watatu, mkazi wa Kwarara, kisiwani Unguja. “Nilikuwa nalalamika mwisho [mume] akanikimbia kwenye nyumba ya kupanga nikiwa na watoto.”

SOMA ZAIDI: Nini Kitatokea Pale Wanawake Wengi Wakiwemo Kwenye Nafasi za Maamuzi?

Fatma, aliyeingia sokoni kwa kuanza kuosha kuku kwa wenye mabucha, kwa sasa anauza vichwa na miguu ya kuku sokoni hapo, akisema kwamba japo kazi hiyo haikidhi mahitaji yake yote ya msingi angalau inamsaidia kuitunza familia yake.

Sharifa Issa, 35, mama wa  watoto wanne, alikimbiwa na mume wake baada ya kupata kazi na kuongeza mke wa pili na kuamua kuuza vitu vyake vya dhahabu ili apate mtaji wa biashara ya viazi mvirigo kwa bei ya jumla.

“Mume wangu alipopata kazi nzuri ya udereva serikalini akaoa na kuniacha na watoto,” Sharifa aliieleza The Chanzo. “Nikarudi nyumbani na watoto kisha nikauza kidani na pete zangu tatu za dhahabu, nikapata mtaji wa kununua viazi na sasa wanangu wanasoma na nimeanza kujenga.”

Uhuru wa kifedha

Hata hivyo, siyo wanawake wote wanaojishughulisha na biashara mbalimbali sokoni hapa wametelekezwa na waume zao. Wengine wamelazimika kuja hapa kwa shauku ya kutaka kujitegemea kiuchumi, wakisema hiyo inawapa uhuru zaidi wa kifedha kama wanawake.

Moja kati ya wanawake hao ni Riziki Juma Haji anayejishughulisha na biashara ya kuuza mboga za majani. Riziki, 48, amekuwa akifanya biashara hiyo sokoni hapa kwa kipindi cha miaka 10 sasa.

SOMA ZAIDI: Fatma Taufiq: Wanawake Tunahitaji Ukombozi wa Kiuchumi

“Mimi ndiyo ‘mwanaume’ kwenye nyumba,” anasema Riziki, mama wa watoto saba. “Mume yupo kwa ajili ya kula nguvu zangu na siyo kuhudumia. Mimi ndiyo nawasomesha watoto na nahudumia nyumba na nimeshazoea.”

Amina Maulid Mkasaba ni mwanaharakati wa masuala ya dini kwa upande wa wanawake pia ni msaidizi wa kujitolea katika Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, ambayo, pamoja na majukumu mengine, hujihusisha na kutoa fat-wa ya mambo mbalimbali ya dini ya Kiislamu.

Kwenye mahojiano na The Chanzo, Amina amesema: “Ni kweli wanawake wanapitia hali ya kuachwa kwa sababu kadhaa, pia suala la wanawake wengine kujihudumia kwa ajili ya kupata stara lipo.”

Najjat Omar ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *