The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Utata Leseni Ya Uchimbaji Madini Serengeti Kwenye Maeneo ya Wananchi. Afisa Adai Sio Lazima Kuwashirikisha

Leseni hizo zimejumuisha majina ya wananchi wachache ambao wanametajwa kuingia ubia na mwekezaji na hivyo kutambulika kama miongoni mwa wamiliki wa leseni bila ridhaa yao.

subscribe to our newsletter!

Wananchi wa kitongoji cha Kitarahota, kijiji cha Nyamakobiti wilaya ya Serengeti mkoani Mara, wameingia katika mgogoro na wafanyabiashara waliopewa leseni za uchimbaji mdogo wa madini, PML 1326 MAR na PML 1327, ambazo zinawaruhusu wamiliki wa leseni kufanya uchimbaji katika maeneo yao.

Leseni hizo zimejumuisha majina ya wananchi wachache ambao wanametajwa kuingia  ubia na mwekezaji, Mohammed Athuman Msema na hivyo kutambulika kama miongoni mwa wamiliki wa leseni bila ridhaa yao.

Bigeso Mantage (68), mmoja ya wakazi wa Nyamakobiti ambaye jina lake ni miongoni wa wabia waliotajwa katika leseni PML 1326 ameieleza The Chanzo kuwa hatambui hiyo leseni na kwa mtazamo wake ni batili. 

“Huu ni uhuni”, alisema Mantage, “haiwezekani uniweke kwenye leseni bila kunipa taarifa, mimi nimejikuta tu, sitakubali kamwe.”

Eneo hilo la machimbo ya dhahabu  linatambulika kama Mgodi wa Mahenge 1, shughuli za uchimbaji madini ziliibuka mwaka 2013, kutoka machimbo madogo ya Nyakamoti yaliyokuwepo awali. 

Leseni za Uchimbaji

Tangu mwaka 2013 wananchi na wakazi wa maeneo hayo walianza kuchimba kiholela  kila mtu kwenye eneo lake la makazi na mashamba kwa utaratibu wa ‘rashi’ ambapo Ofisi ya Madini na Ofisi ya Wilaya zilianza kuchukua hatua kuhakikisha uchimbaji hauathiri wakazi wa maeneo hayo.

Wananchi waliendelea kuchimba chini ya utaratibu wa ‘rashi’ na ilipofika mnamo tarehe Aprili 7, 2023, Mkuu wa Mkoa wa Mara alifika katika kijiji cha Nyamkobiti na kushauri wananchi waunde vikundi vya uchimbaji kisha waombe leseni kwa vikundi ili waweze kuchimba wao wenyewe kwenye maeneo yao.

Wananchi wakiwa katika mchakato huo mnamo Julai 18, 2023, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti alienda  katika kijiji hiko na kutambulisha leseni mbili za uchimbaji mdogo PML 1326 MAR na PML1327 na kuwakabidhi wamiliki 20 mbele ya mkutano wa hadhara. 

Baada ya majina ya wamiliki kusomwa iligundulika kuna majina ya baadhi ya wananchi yaliyosomwa kuwa ni miongoni mwa wamililki wa leseni bila ya wao  kushiriki kwa lolote katika upatikanaji wa leseni hizo.

“Mkuu wa Wilaya alipokuja hakuwa anataka kusoma majina”, alieleza Flavian Gitano, mkazi  wa Nyamakobiti.

“Tulitumia nguvu kumtaka asome majina na aliposoma majina ndipo tulipigwa na butwaa, inakuwaje mtu anakuwa mmiliki bila kumshirikisha?” aliongezea Gitano, mzee wa umri wa miaka 65.

Nyaraka za leseni toka tovuti ya leseni za madini inaonesha wamiliki ni wote waliotajwa na mwekezaji wana hisa sawa kama ifuatavyo:- Aloyce Jospehat machota (6%); Filbert Ditrick nyoni (6%); Hassan Virozo Athuman(6%); Hawa Salum Mahinda(6%); Igonga Tengera Nyahego (6%), Joseph Maro Chacha (6%); Joseph Anthony Nyahego(6%);Machota Nyamhanga Machota (6%) na Masese Wambura Kenyunko(6%).

Wengine ni Matyenyi Koromba Magabi (6%); Mohamed Athuman Msema (6%); Ramadhan Athuman Msema (6%); Robert Nyamangu (6%); Silvester benard (6%); Bigeso Muntage isuto(3%); Gidion James (3%); Mosena Matwiga (3%); Sasi Maro Mosi (3%); Mbwana Hamza (2%) na Prosper William (2%).

Wananchi wa Nyamakobiti kwa umoja wao waliamua kufuatilia kwa ukaribu suala la uhahali wa leseni hizo na jinsi ambavyo nyaraka zao zimetumika bila idhini yao kupata leseni hiyo. 

Ushirikishwaji wa Wananchi

Wakiwasilisha barua na nyaraka mbalimbali za malalamiko kwenye Ofisi ya Afisa Madini kutotambua leseni hizo, ambapo ilimlazimu Afisa Madini wa Mkoa (RMO), Julai 24, 2023 na timu yake kwenda katika kijiji cha Nyamakobiti.

RMO alipofika kijijini hapo aliashawishi wakazi hao wakubaliane na leseni na kuendelea na mchakato wa kuwakabidhi wenye leseni eneo hilo licha ya kwamba walishawasilisha barua ya malalamiko.

“Wenye leseni wanasema wao wako kwenye shamba, sasa wewe ukiangalia hapa hakuna shamba hata moja hapa,” alieleza mzee Nyakarahita Mwita (72) mkazi wa Nyamakobiti.

“Wao wanasema kwamba ili kuwe na mlipuko wa kupasua mwamba mita 200, sasa angalia mita 200 ambayo ni urefu wa kiwanja cha mpira mara mbili. Hapa mita 200 iko wapi,” aliongeza mzee huyu.

Ofisi ya Afisa Madini Mkazi mkoa wa Mara kupitia Kaimu Afisa Madini Bwana Hamad Kallaye alikiri kutambua mgogoro huo na kudai kuwa wananchi ndio wanaomvamia mwenye leseni.

“Wananchi hawaelewi sheria”, alisema Kallaye. “Sheria haitaji mahali kokote kuwa mtu anayeomba leseni anatakiwa kuwashirikisha, hapana! Mtanzania yeyote kutoka popote anaruhusiwa kuomba leseni sehemu yeyote, akionekana ana vigezo anapewa leseni bila shida yeyote,” alifafanua.

“Haikuwa haki yao kuwekwa kwenye leseni, bali ni busara za RMO aliyepita,” Kallaye aliongeza. “RMO baada ya kuona namna ya watu hawa alipendekeza wawekwe ili isije ikalatea mgogoro, hivyo hawakuwa na haki hata kidogo, ni busara tu”.

Bwana Kallaye alifafanua kuwa wahusika waliopo kwenye leseni walishikirishwa na wakatoa namba zao na utambulisho wa taifa (NIDA).

Afisa Madini huyo aliongezea kuwa mwombaji yeyote wa leseni ndogo ya uchimbaji madini anatakiwa kuambatanisha jina lake kamili na uraia, anwani ya posta na mahali alipo, pasipoti saizi ya hivi karibuni, nakala ya kitambulisho na iwapo mwombaji ni mgeni ataambatanisha na kibali cha ukaaji na kibali cha kufanya kazi.

Sheria ya Madini ya Mwaka 2019 sura 123 inatoa ufafanuzi  jinsi ambavyo shughuli za madini zinapaswa kuendeshwa pale ambapo madini yamegundulika kwenye eneo lolote nchini. 

Kwa mujibu wa kifungu cha 95 cha sheria hiyo, mmiliki wa haki ya madini yaani mwenye leseni haruhusiwi kutumia leseni aliyopewa kwa kuingia kwenye eneo ambalo limetengwa kwa shughuli maalumu bila kibali.

Maeneo yaliyotengewa kwa shughuli za kijamii, eneo la makaburi, eneo la jeshi au eneo lolote la hifadhi, mwenye leseni haruhusiwi kufanya kazi mpaka apate kibali cha maandishi toka kwa Waziri husika. 

Pia mmiliki hataruhusiwa kutumia leseni hiyo na kuingia kwenye eneo bila mashauriano na Serikali za Mitaa ikijumuisha halmashauri za vijiji na kibali cha mmiliki halali wa eneo hilo.

Aidha sheria hiyo inafafanua kuwa endapo mmiliki wa leseni hatapewa ridhaa na mmiliki wa ardhi bila sababu ya msingi, Waziri kwa kushauriana na Tume ya Madini ana mamlaka ya kumruhusu mmiliki wa leseni kuendesha utafutaji au uchimbaji wa madini.

Wakazi hao wanadai kuwa hawakutoa chochote kati ya viliyoanishwa hapo juu. 

The Chanzo ilipomtafuta Katibu mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba alisema kuwa ili kumaliza mgogoro katika eneo hilo wananchi waandike barua ya kuomba kutolewa kwenye leseni hiyo.

“Ni jambo jepesi tu, wananchi waandike barua ya kuomba kutolewa kwenye leseni” alisema bwana samamba. “Kwa upande wangu sioni kama kuna shida mtu anadai hajashirikishwa, kama hajaridhia basi atoke wabaki wanaoridhia”.

Sheria za madini zinahitaji mwenye leseni za madini kulipa fidia pale anapotaka kuchukua eneo kwa ajili ya shughuli za kuchimba madini. Hii ikimaanisha, haki za wanakijiji hao haziwezi kumalizwa kwa uwepo wa leseni peke bila kupokea fidia stahiki kama sheria inavyotaka.

Matonyinga Makaro ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Mwanza. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia matonyingamakaro@gmail.com  

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *