The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Viongozi Hawa Kumi wa Tanzania Watakuhamasisha Kupenda Kusoma Vitabu

Yumo Julius Nyerere, aliyekuwa anasoma vitabu mia ndani ya mwaka mmoja, pamoja na Salim Ahmed Salim aliyeona vitabu kama silaha ya kupambana na watu wanaotamani kukandamiza ukweli.

subscribe to our newsletter!

Kuna usemi umedumu kwa takriban karne moja sasa ambao watu weusi, hasa sisi Watanzania, hawaupendi na wausikiapo wanakuwa wakali kama pilipili za mkoa wa Pwani. Msemo huu unasema, Kama unataka kuficha kitu mtu mweusi asikione, kiweke kwenye kitabu. Watu weusi kamwe hawasomi vitabu.

Sisi Watanzania hatuna utamaduni wa kusoma vitabu. Ukiwauliza baadhi ya Watanzania kwa nini hawasomi vitabu, watakwambia, “Tupo bize, hatuna muda.” 

Lakini muda mfupi tu utawakuta vijiweni wakisogoa; kwenye viti virefu ‘wakila bata’ hadi kuku anaona wivu; vibarazani wakiteta na majirani; nyumba za wageni-wenyeji wakivunja amri ya sita; au wakibishana mbungi kwa masaa kuhusu swali, Je, Fabrice Ngoma kwa kuweka blichi, aruhusiwe kuhamia Yanga?

Viongozi ‘wamba’

Katika historia ya nchi yetu, kuna viongozi ambao naweza kusema ni ‘wamba’ wa kusoma. Baada ya kuwafuatilia sana, nimewavulia kofia viongoz hawa. Hapa naweka orodha ya viongozi kumi ambao, kwa maoni yangu, walikuwa na hamu kubwa ya usomaji vitabu kwa matumaini kwamba wanaweza kukuhamasisha kujijengea utamaduni huo.

Nambari moja katika orodha hii ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye tabia yake ya kupenda kusoma vitabu ilifahamika na wengi, wakiwemo wasaidizi wake wa karibu. Hayati Benjamin Mkapa, aliyekuwa Rais wa tatu wa Tanzania, alikuwa mmoja kati ya watu walioliona hili kwa Mwalimu Nyerere.

SOMA ZAIDI: Tamasha la Vitabu Zanzibar: Kitovu cha Vipaji Vipya?

“Mwalimu alikuwa na kiu isiyokatika ya taalamu,” Mkapa, aliyefariki Julai 24, 2020, aliwahi kusema hapo Oktoba 21, 1999. “[Mwalimu] alikuwa msomaji mkubwa wa vitabu, akisoma vitabu vipya 100 kila mwaka. Kilichomshawishi akubali nyumba kubwa ni kwa sababu kwenye nyumba aliyokuwa akiishi hakukuwa tena na nafasi ya kuweka vitabu.”

Nambari mbili kwenye orodha yangu hii ni Dk Salim Ahmed Salim, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kati ya mwaka 1984 na 1985. Salim, ambaye pia alikuja kuhudumu kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), sasa Umoja wa Afrika (AU), ni msomaji hodari sana wa vitabu. 

Inaaminika kwamba kwenye mijadala, kabla hajaugua, Dk Salim alipenda kunukuu, “Vitabu na aina zote za maandishi ni tishio kwa wale wanaotamani kukandamiza ukweli.”

Nambari tatu kwenye orodha hii ni Mkapa ambaye kwenye kitabu chake cha My Life, My Purpose: A Tanzanian President Remembers, kiongozi huyo anaeleza kwa maneno yake mwenyewe kwamba alipendelea zaidi kusoma tawasifu, au autobiographies kwa kimombo. Tofauti na wengi, Rais Mkapa alipenda kusoma pia vitabu vya wajinga, ili kujua nao wanafikiria nini!

Watanzania wengi walinishangaa nilipokuwa mtu wa pili kununua tawasifu ya William Malecela, maarufu kama Lemutuz, iliyopewa jina la My American Experience: An Autobiography. Mara tu ilipotoka, niliinunua tawasifu hii, huku wakosoaji wakisema, “Mzee wa Atikali umechanganyikiwa, utafaidika nini kwa kusoma kitabu cha huyo kubwa-jinga?”

SOMA ZAIDI: Waandishi Bunifu Tanzania Tukisahaulika Sasa, Tutakumbukwa Lini?

Kwenye kabati langu la vitabu niko na tawasifu za marais karibu wote duniani na watu wengi maarufu, lakini hiyo ya Lemutuz, aliyefariki hapo Mei 14, 2023, ipo kwenye Kumi Bora yangu kwa jinsi ilivyo nzuri!

Turudi kwenye orodha yangu ambapo kwenye nambari nne tunakutana na Edward Moringe Sokoine, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, ambaye kipindi cha uhai na uongozi wake, alipenda sana kunukuu Hosea 4:6, isemayo, “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa.”

Nambari tano tunakutana na John Samwel Malecela, akifuatiwa na Pius Msekwa, Abrahaman Mohamed Babu, Samwel John Sitta, Mwami Zuberi Zitto Kabwe na orodha yangu inaishia kwa Tundu Antipass Mugway Lissu anayeshikilia nafasi ya kumi kwenye orodha hiyo.

Hii ni orodha yangu iliyotokana na utafiti wangu wa kina, siyo orodha ya mtu mwingine, maana watu wengine wanaweza kuhoji. Kama nilivyotangulia kusema, nimeandaa orodha hii kwa kudhani kwamba inaweza ikawa chachu kwa viongozi wetu wengine kujenga utamaduni wa kupenda kusoma vitabu.

Viongozi na kusoma

Kila mtu ni lazima apende kusoma vitabu lakini kwa viongozi ulazima huo unakuwa mkubwa mara dufu, maana, kama alivyowahi kusema Rais wa 33 wa Marekani, Harry Truman, hapo Januari 17, 1954, “Siyo wasomaji wote ni viongozi, lakini viongozi wote wapaswa kuwa wasomaji.”

SOMA ZAIDI: Ni Kwa Kiasi Gani Mitaala Yetu Inawawezesha Wanafunzi Kutafakari?

Nitumie fursa hii pia kuwashukuru Watanzania wawili ambao hivi karibuni wameniletea vitabu vya ziada maana nimedhamiria mwaka huu wa 2024 nifikishe vitabu 100, nikijaribu kufuata nyayo za Mwalimu Nyerere!

Watanzania hao ni Humphrey Polepole, Balozi wa Tanzania nchini Cuba na A. Mtoure Kisanga ambaye amenipa kitabu cha baba yake ambaye ni mmoja wa majaji bora kuwahi kutokea nchini, A Biography of Justice Robert Kisanga.

Kwa sasa mimi nasoma kitabu kimoja matata sana ambacho ningetamani viongozi wetu wote wakisome, hususan mawaziri, mabalozi, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wabunge, nakadhalika: The Greatness Guide kilichoandikwa na mwandishi Robin Sharma na kupata pongezi nyingi kutoka pande tofauti za ulimwengu.

Kwa kiongozi wetu yoyote atakayebahatika kukisoma kitabu hiki, basi namsihi aisome mara mbili-mbili, na kwa umakini wa hali ya juu, sura 25 ya kitabu hicho yenye kichwa cha habari, Leadership is not a Popularity Contest, au Uongozi siyo Mashindano ya Umaarufu.


Mzee wa Atikali ni mwandishi na mchambuzi kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia +255 754 744 557. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

3 responses

  1. It’s a very inspiring article or story keep on bringing such to our society you dont know how much change you may form in this digital society.Thanks God bless you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts