The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tamasha la Vitabu Zanzibar: Kitovu cha Vipaji Vipya?

Tamasha hilo la kwanza na la aina yake lilivutia zaidi ya watu 1,500 kutoka ndani na nje ya nchi.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Ilikuwa kawaida, siku za nyuma kidogo, kwa mwandishi chipukizi, Sabra Ali Amran kutoka visiwani hapa, kuchapa vitabu mwenyewe kisha kugawa bure. Lakini haikuwa hivyo kwenye Tamasha la Vitabu Zanzibar, lililofanyika kuanzia Oktoba 20 mpaka Oktoba 22, 2023.

“Nashukuru, watu wamenunua vitabu vyangu kwenye tamasha hili,” Sabra alinieleza, sura yake ikidhihirisha bashasha. “Nimepata kiasi cha Shilingi 250,000 ndani ya siku tatu.” 

Sabra ni mwandishi ya vitabu sita vya riwaya na mashairi; amevichapisha kwa uchapishaji binafsi. Vitabu vyake vinauzwa kati ya Shilingi 5,000 na Shilingi 20,000 kwa nakala.

Wazo la kuanzisha Tamasha la Vitabu Zanzibar lilimjia Ally Abdallah Baharoon mara tu baada ya filamu ya Vuta N’kuvute iliyotayarishwa na Amil Shivji kupata nafasi ya kuoneshwa kwenye Tamasha la Kimataifa la Filamu Toronto, nchini Canada, mwaka 2021. 

Filamu hiyo ilitokana na kitabu cha mwandishi Adam Shafi kilichobeba jina hilohilo. Mwaka huohuo, Abdulrazak Gurnah, mwandishi wa fasihi Mwingereza mwenye asili ya Tanzania, alishinda Tuzo ya Nobel katika Fasihi. 

SOMA ZAIDI: Ida Hadjivayanis: Hakuna Kiswahili Kimoja

Japokuwa kazi hizi za kifasihi zilipata heshima katika majukwaa ya kimataifa, wote hawa – Gurnah na Shafi – walikuwa na mizizi Zanzibar.

Heshima

“Nilipoona kazi hizi zimekuwa na mwitikio chanya duniani, niliwaza, kuna vitabu vingapi kutoka Zanzibar ambavyo vinaweza kutuheshimisha jinsi hii?” Baharoon, ambaye yeye mwenyewe ni mwandishi wa kazi za fasihi, ananieleza. 

Mshindi wa Tuzo ya Nobel katika Fasihi 2021, Profesa Abdulrazak Gurnah, akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa fasihi, wakiwemo wachapishaji wa kitabu cha Peponi pamoja na wanakamati wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu wakati wa Tamasha la Vitabu Zanzibar lililofanyika Oktoba 20-22, 2023, visiwani humo. PICHA | ESTHER KARIN MNGODO

“Halafu nikawaza, kuna matamasha kama Tamasha la Filamu (ZIFF) na Sauti za Busara ambalo ni tamasha la muziki,” aliendelea kijana huyo. “Kwa nini kusiwe na tamasha la vitabu la kuitangaza Zanzibar?”

Hata mbuyu huanza kama mchicha, Waswahili husema. Baharoon hakutulia na wazo lake. Akaomba meza kwenye Tamasha la ZIFF pamoja na Tamasha la Utamaduni mwaka jana, 2022, ambapo wasomaji walipata nafasi ya kukutana na waandishi wa vitabu, kusoma na kununua kazi zao. 

“Niliwaza kuwa na meza kwenye harusi mbalimbali ili kuonesha kuwa kusoma kitabu ni jambo la kawaida, lakini sikufanyia kazi wazo hilo,” anasema Baharoon, huku akicheka.

SOMA ZAIDI: Waandishi Bunifu Tanzania Tukisahaulika Sasa, Tutakumbukwa Lini?

Hatimaye, kupitia Jumuiya ya Fasihi Zanzibar, au Zanzibar Renaissance Literary Society kama jumuiya hiyo inavyojulikana kwa kimombo, na ambayo yeye ni mwanzilishi, Tamasha la Vitabu likazaliwa.

Tamasha hilo la kwanza na la aina yake lilivutia zaidi ya watu 1,500 kutoka ndani na nje ya Tanzania. Baadhi yao waliketi katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil kwa ajili ya ufunguzi. 

Bango kubwa liliwekwa mbele, likiwa na picha ya Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi, ambaye alialikwa kama mgeni rasmi, na mada iliyoandikwa kwa Kiingereza kama Zanzibari Literature: A World Within Words, au Fasihi ya Zanzibar: Ulimwengu ndani ya Maneno. 

Kila paneli, kila mzungumzaji, kila kitabu, kilikuwa cha Mzanzibari. Haikuwa bahati mbaya, alisema Baharoon, ambaye anafafanua: “Hili ni tamasha la kwanza linalofanyika Zanzibar. Tulitaka iwe ni zawadi kwa Wazanzibari.”

Bega kwa bega

Akizungumza katika ufunguzi, akimwakilisha Rais Mwinyi, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Simai Mohammed Said, alisema kuwa Serikali ya Zanzibar itakuwa bega kwa bega na Jumuiya ya Fasihi Zanzibar ili kuliendeleza tamasha hilo. 

SOMA ZAIDI: Ida Hadjivayanis Aichambua ‘Peponi’ Ya Abdulrazak Gurnah

“Ally [Baharoon], tunakushukuru kwa kubuni wazo zuri,” alisema Said. “Kwa kulipigania. Ila safari yako imefika hapa. Pamoja na Waziri mwenzangu, Mheshimiwa Lela [Muhamed Mussa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar], tutakusaidia na kulibeba. Sasa nathubutu kusema kwamba, hili tamasha siyo la Ally tena. Ni la Zanzibar.”

“Kuna waandishi wengi waliotokea Zanzibar,” aliendelea kueleza Waziri Said. “[Baadhi yao ni kama] Mohamed Said Abdallah au Bwana Msa, Profesa Said Mohamed, Adam Shafi, Mohamed Suleiman na wengine. 

“Hawa ni chemchem ya fasihi na isimu maridhawa ya Zanzibar iliyopasua anga na kupenya hadi bara la Ulaya. Hii ni kuthibitisha kuwa Tanzania ni kitovu cha fasihi bora yenye mvuto. Utaipenda, utake usitake. 

“Leo hii tuko hapa kuunga mkono tamasha hili, ambalo kuna waandishi chipukizi na wabobevu kwa ajili ya kubadilishana mawazo kuhusu mwelekeo wa usomaji Zanzibar, na duniani kwa ujumla. Bila shaka, kwa jitihada hizi, tutarajie kwamba utamaduni wa uandishi na usomaji Zanzibar utarudi kama zamani.”

Katika ufunguzi huo, Waziri Simai alizindua kitabu cha Peponi kilichoandikwa na Dk Ida Hadjivayanis kama tafsiri ya kitabu cha Paradise cha Profesa Abdulrazak Gurnah. 

SOMA ZAIDI: Washindi Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu Watangazwa Dar

Gurnah aliwahimiza waandishi kuendelea kuandika kwa sababu wana msukumo wa kuandika, na siyo kwa sababu ya kupewa tuzo. Alisema kuwa, yeye aliandika kitabu chake cha kwanza akiwa na miaka 38 lakini alitunukiwa heshima ya Nobel akiwa na miaka 72.

Mshindi wa Tuzo ya Nobel katika Fasihi 2021, Profesa Abdulrazak Gurnah, akizungumza katika ufunguzi wa Tamasha la Vitabu Zanzibar lililofanyika Oktoba 20-22, 2023, visiwani humo. PICHA | ESTHER KARIN MNGODO

Kunaanza utotoni

Naye Dk Ida alisema kuna umuhimu wa kuanza na watoto. Alisimulia jinsi ambavyo bibi yake, Salama Binti Rubeya, alipokuwa mdogo huko Kilwa hakuruhusiwa kwenda shule kwa kuwa alikuwa msichana, japokuwa alipenda kusoma. 

Akamwomba kijana mdogo amsomee, ambaye alikubali kufanya hivyo baada ya kuahidiwa pesa kidogo. 

“Mimi nilipokuwa nakuwa, bibi yangu alikuwa ameanza kuzeeka na hakuweza kuona vizuri,” alisimulia Ida. “Nakumbuka alikuwa anavaa miwani yake iliyofanya macho yaonekane makubwa kwa mbele. Alipenda sana kusoma. 

“Nina uhakika watoto wake wote wamekuja kupata nyadhifa mbalimbali kwa sababu ya msingi mzuri wa mama yao,” aliendelea kusimulia. “Bibi yangu angeniambia, ‘Naomba unisomee.’ Nilikuwa sitaki. Pia angeniambia, ‘Nitakupa pesa.’”

SOMA ZAIDI: Bila Uhuru wa Mwanafasihi, Fasihi Haiwezi Kuwa Chombo cha Ukombozi wa Umma

“Bibi angenipa Shilingi moja au Shilingi tano,” aliendelea Dk Ida, huku wasikilizaji wake wakiangua kicheko. “Nakwenda, namsomea. Baada ya muda mimi mwenyewe nikawa nakwenda nakumuuliza, ‘Bibi, hutaki nikusomee leo?’ 

“Anasema, ‘Ah, leo sitaki kusomewa. Lakini, hebu shusha hayo masanduku yangu ya kanga, nisomee.’ Kwa hiyo, nashusha masanduku, natoa, tunaangalia rinda. Nasoma maneno; na hapo tunajenga simulizi na vicheko, tunajenga mapenzi ya kusoma na tunaona ladha ya maneno kwenye maandishi.

“Nataka kusema kupenda kusoma kunaanza utotoni. Kuthamini vitabu kunaanza utotoni. Kuikubali ladha ya vitabu inaanza utotoni.”

Katika kukuza uandishi wa vitabu vya watoto, siku ya kwanza ilikuwa na warsha ya fasihi ya watoto. Baadaye, kikazinduliwa kitabu cha Zubayda Kachoka cha mwandishi mashuhuri Zanzibar, Ally Saleh, kinachoangazia masuala mbalimbali yaliyowachosha wanajamii. 

Usiku wa mashairi

Na hatimaye kukawa na Usiku wa Mashairi ambapo watu walionja ladha ya ushairi kama burudani. Washairi kutoka Unguja na Pemba walijumuika kughani mashairi kwa ustadi, huku wakicheza na maneno kwa madaha. 

SOMA ZAIDI: Furaha, Matumaini Vyatawala Tukio la Watunzi, Wapenzi wa Kazi za Fasihi Dar

Katika kuufunga usiku huo, washairi walijibizana na kumalizia ubeti kwa kusema, “Nakutania Mtani,” mtindo ambao mshereheshaji wa shughuli hiyo, Balozi Kawthar Iss-hack, anasema ni njia ya kupeleka ujumbe kwa kutumia ushairi na utani.

Shairi la Sangara Kanikanyaga la Dk Salma Omar Hamad liliwakonga mioyo wasikilizaji wengi:

  1. Kanikanyaga sangara na yumo aendelea idhilali anitwisha

Yuanitia madhara na kila hivumilia anambia ‘umekwisha’

      Siyo sirini; jahara kila hijipapatua afoka ‘hebu nipisha!’

      Sijaiona ishara ya siku ijayokuwa ataamua jiondosha

      Kanikanyaga sangara!

  2. Ndimi nalokuwa juu ati kwa udogo wake hamuachia

      Akatumia laghau ‘kanirushia viteke hamzomea

      Nikajitia dharau hahisi mguso wake hapuuzia

      Sasa ‘mekuwa makuu nikitaka nichopoke nadidimia!

      Aniumiza sangara!

  3. Sangara anihiliki anipondaponda moyo anisumbua

      Nalia sinyamaziki kila pembe nipitayo anizuwia

      Nishamwambia sitaki fujo anifanyiayo ataniua

      Ameapa habanduki kwa faida apatayo hatanachia

      Ataniua sangara!

  4. Kashanikanyaga! Toba naumia!

      Ajibwagabwaga anisondogea!

      Nabaki napwaga kashaniumbua!

Siku ya pili ilianza na mafunzo ya uandishi, yaliyoongozwa na Mhadhiri wa Kiswahili kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Salma Hamad Omar, na uzinduzi wa kitabu cha Maisha ya Haji Gora kilichoandikwa na Ally Saleh. 

Fasihi ya Kiswahili

Yakafuata majadiliano katika paneli juu ya ‘Umuhimu wa Matumizi ya Kiswahili katika Uandishi,’ ambapo Profesa Farouk Topan, moja kati ya waandishi nguli wa Kiswahili, akaufahamisha umma kuwa paka aliyeonja pepo yuko njiani kuja Zanzibar maana ameshapachoka Bagamoyo!

SOMA ZAIDI: Namna Fasihi ya Kiswahili Ilivyo Changa Kidhima Licha ya Kuwa Kongwe Kihistoria

Lakini pia, hapa liliibuka swali: Je, fasihi ya Kiswahili inaweza kuwa kwa lugha nyingine? 

Wanapaneli waliozungumzia ‘Umuhimu wa Matumizi ya Kiswahili katika Uandishi’ wakiwa katika mjadala. Kutoka kushoto ni mwandishi na Mhadhiri Profesa Farouk Topan, Mwendeshaji Dk Ida Hadjivayanis, Mratibu Mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) Amour Salim Said na Katibu Mtendaji BAKIZA, Dk Mwanahija Ali Juma. PICHA | ESTHER KARIN MNGODO

Kitabu cha Profesa Gurnah kilikuwa mfano mzuri katika kulijibu swali hili. Japokuwa ameandika kwa Kiingereza, maudhui yake yanaongelea maisha ya Afrika Mashariki. 

“Inawezekana kuwa na fasihi ya Kiswahili, pamoja na fasihi, kwa Kiswahili,” alisema Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA), Dk Mwanahija Ali Juma. 

Baadaye kukawa na uzinduzi wa kitabu cha Malenga wa Pemba; warsha ya uandishi iliyoongozwa na mwandishi wa riwaya Zainab Baharoon; pamoja na warsha ya usomaji iliyoongozwa na Hamza Rijal.

Mafunzo kuhusu tafsiri yaliifungua siku ya tatu, yakiongozwa na Dk Ida pamoja na Dk Meg Arenberg anayefundisha Fasihi na Masomo ya Tafsiri kwenye Taasisi ya Afrika huko Sharjah, Falme za Kiarabu. 

SOMA ZAIDI: Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu: Tumaini Jipya Kwa Waandishi Tanzania?

Katika mafunzo hayo, Dk Meg alisema kuwa watu hudhani kuwa kutafsiri ni kunakili kazi ya awali, akitahadharisha kwamba hivyo sivyo. 

“Kutafsiri ni aina ya ubunifu,” alifafanua Dk Meg. “Mfasiri hubuni ndani ya mipaka aliyowekewa na mwandishi wa kazi ya awali.”

Mafunzo

Naye Ummul-Ayman Issa, mwanafunzi wa Kidato cha Nne kutoka Feza School Zanzibar, alisema kuwa amejifunza mambo mengi kwa kushiriki tamasha hilo, ikiwemo umuhimu wa vitabu. 

“Nimekutana na watu ambao sikutarajia kuwaona, waandishi wa vitabu wakubwa,” alieleza mwanafunzi huyo. “Pia, nimenunua vitabu hapa na nimehamasika kuendelea kusoma vitabu.”

Akifunga tamasha hilo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhamed Mussa, alisema kwamba tamasha hilo limekuwa na faida kwa wasomaji vitabu na waandishi wa vitabu kwani limetoa vitabu vyao stoo na kuviweka ukumbini, ambapo vingine ni kwa mara ya kwanza kuonekana hadharani. 

SOMA ZAIDI: Ushindi wa Gurnah Uikumbushe Serikali Umuhimu wa Uraia Pacha

“Nitoe ahadi kwenu, tutaendelea kuliunga mkono tamasha la vitabu Zanzibar ili kuhakikisha linaendelea kufanyika kila mwaka na kuongeza wigo wa washiriki,” alisema Lela.

“Kwa mara ya kwanza, tamasha limewashirikisha waandishi nguli kwa upande wa kisiwa cha Zanzibar tu,” aliongeza. “Ni matarajio yetu kuwa mwakani mtawashirikisha waandishi nguli kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki, ikiwemo Tanzania Bara, Kenya na Uganda.”

Esther Karin Mngodo ni mwandishi na mhariri anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia mtandao wa X kama @Es_Taa.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *