The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

China Ilikuwa na Deng, Tanzania Ikapata Mwinyi

Tunaweza kabisa kumpa maua yake Hayati Ali Hassan Mwinyi kama Baba wa Mageuzi nchini. Hajapewa hii heshima yake vya kutosha.

subscribe to our newsletter!

Historia za nchi duniani zinafundwa na mapito ya viongozi wao wakuu ama, wakati mwingine, na watu wenye ushawishi kwenye mataifa hayo. 

Kama ambavyo tuliona na bado tunajadili mapito ya taifa kama Marekani miaka ya Franklin Delano Roosevelt na The New Deal na vilevile Ronald Reagan katika ukuaji wa ubepari, ama Uingereza ya Magreth Thatcher na kilichoitwa Thatcherism kwa kuvunja vunja nguvu ya vyama vya wafanyakazi, ndivyo tunaona na kujadili mageuzi makubwa ya taifa la China na Tanzania pia. 

Baada ya Kiongozi Mkuu wa China Mao Zedong kufariki mwaka 1976, ndani ya mwaka mmoja aliibuka Deng Xiaoping ambaye alichukua hatua za kuifungua China kiuchumi bila ya kuathiri mfumo wa kisiasa. 

Mpaka leo wanazuoni na watafiti bado wanachambua maamuzi yale ya Deng kufanya mageuzi ya kiuchumi ya China ambayo yalipelekea taifa hilo kukuza uchumi wake kwa kasi kubwa kupata kutokea duniani kwa miongo mitatu mfululizo na kuwezesha mamilioni ya watu kuondoka kwenye umasikini uliokithiri.

Hapa Tanzania, tulianza mageuzi makubwa ya kiuchumi wakati wa uongozi wa Rais wa Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi. Rais Mwinyi alichukua madaraka ya urais baada ya Rais wa Kwanza, Julius K Nyerere

Faida kubwa aliyokuwa nayo Rais Mwinyi ilikuwa ni kwamba kabla ya kuwa Rais wa Tanzania alikuwa Rais wa Zanzibar kwa mwaka mmoja na miezi kumi ambapo, kwa kushirikiana na Waziri Kiongozi wake, Maalim Seif Sharif Hamad, walifanya mageuzi ya kiuchumi na kutuliza hali ya kisiasa Zanzibar. 

Walifungua uchumi wa Zanzibar kwa kauli moja muhimu iliyosema, Zanzibar ni njema, atakaye aje ambayo iliwawezesha Wazanzibari waliokuwa wanaishi nje ya Zanzibar kuanza kuleta bidhaa mbalimbali kwa ndugu zao na kurejesha nafasi ya Zanzibar kama kituo cha biashara. 

Vilevile, yeye Rais Mwinyi na Maalim Seif wakafanya mageuzi ya kikatiba kwa kuweka haki za msingi za watu kwenye Katiba ya Zanzibar kwa mara ya kwanza. Katiba ya Tanzania wakati huo haikuwa na sura ya haki za watu, yaani Bill of Rights. Hivyo, Mwinyi alipokea madaraka ya urais wa Tanzania akiwa tayari ana kumbukumbu za mageuzi makubwa aliyoyafanya Zanzibar katika kipindi cha chini ya miaka miwili tu.

SOMA ZAIDI: Nitakavyomkumbuka Mwinyi, Mzee Rukhsa Asiyekuwa na Tamaa ya Madaraka

Wakati Deng anasifiwa kwa mageuzi ya kiuchumi, kiongozi huyo hakuvumilia mageuzi ya kisiasa kabisa. Hii inadhihirishwa na namna alivyoshughulika na maandamano ya wanafunzi ya Tiananmen ambapo aliagiza Jeshi la China kuua maelfu ya wanafunzi na aliyekuwa Mkuu wa Serikali wakati huo kuwekwa kizuizini. 

Mageuzi ya kiuchumi

Rais Mwinyi aliongoza mageuzi ya kiuchumi na ya kisiasa kwa kadiri alivyojaaliwa, akiendeleza kazi aliyoifanya Zanzibar kwa upande wa Jamhuri ya Muungano.

Katika Kitabu chake, Mzee Rukhsa: Safari ya Maisha Yangu, Rais Mwinyi anaeleza namna alivyoipokea nchi na nini kilikuwa kipaumbele chake cha kwanza kama Rais. 

“Kipaumbele changu cha kwanza kikawa hali ngumu sana ya uchumi niliyoikuta, na kwa maana hiyo maisha duni ya wananchi na uhaba mkubwa wa bidhaa na huduma muhimu,” anaandika Mwinyi kwenye kitabu hicho. 

Wakati Rais Mwinyi anachukua madaraka mwaka 1985, nilikuwa mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Kigoma. Ninakumbuka hali hii anayoeleza Mzee Rukhsa. Nilikuwa nakwenda shule ama nikiwa sijatia chochote tumboni au nikiwa nimekunywa uji usio na sukari. 

Miaka miwili ya mwanzo shule ya msingi, 1984 na 1985, nilikwenda shule bila viatu – mpaka siku moja nilipopewa zawadi ya viatu na Mama Coretha Furugunya, viatu vya Asante Bora Shoes, Asante Salim tukiviita. 

Hapakuwa na vitambaa vya kushona mashati ya shule kiasi tulishona mashati kwa kutumia sanda za kuzikia; shuleni hapakuwa na madawati na madarasa yalikuwa machache, hali iliyotulazimu tusome chini ya mwembe. 

Tulikaa kwenye matofali na hivyo kujikuta tunaweka viraka kwenye kaptura zetu kutokana na kuchanika chanika kwao mara kwa amara. Kwa kifupi, hali ya maisha ya wananchi ilikuwa mbaya sana.

Kila mara nipatapo nafasi nasoma ukurasa wa 213-246 wa Kitabu cha Mzee Rukhsa kupata mafunzo ya hatua mbalimbali alizochukua kurekebisha uchumi, na kila nikisoma kurasa hizi namwona mtoto wa miaka tisa akitokea mtaa wa Kisangani, Mwanga Kigoma, akiwa pekupeku na shati lake la sanda na kaptura ya kaki yenye viraka makalioni akienda shuleni kwa mguu kilometa mbili tumboni akiwa hana chochote. 

Halafu napata picha ya kijana wa miaka 14 akiwa Kidato cha Kwanza, Shule ya Sekondari Kigoma, akiwa na viatu jozi saba kiasi cha kugaia wenzake baadhi ya viatu, akiwa na matumaini makubwa ya maisha kiasi cha kutoa hoja kwenye Tume ya Nyalali bila woga kutaka nchi iwe na mfumo wa vyama vingi vya siasa, tume ilipotembelea shuleni hapo mwaka 1991. 

Huu ni ushuhuda wa mageuzi ya miaka michache kwa maisha ya kijana aliyekuwa pembezoni kabisa mwa Tanzania.

Uamuzi wa kufuata masharti ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) uliochukuliwa na Rais Mwinyi na Waziri wake wa Fedha Cleopa David Msuya, chini ya ushauri wa Profesa Ibrahim Lipumba na Benno Ndulu, haukuwa uamuzi wa kawaida. Ni uamuzi uliochukuliwa Mwalimu Nyerere akiwa hai. 

Wakati Deng wa China alifanya mageuzi yake Mao akiwa amekufa, Mwinyi alifanya mageuzi yake Nyerere akiwa hai na mwenye afya tele, tena akiwa mwenyekiti wa CCM kwa miaka mitano yote ya mwanzo ya urais wake. 

Kwa unyenyekevu mkubwa mwenyewe Rais Mwinyi anasema, “Mageuzi tuliyoyafanya [..] hayakutanguliwa na falsafa kubwa au mijadala ya itikadi. Mie si mtu au kiongozi wa aina hiyo. Nilichojua ni kuwa ilikuwa wajibu wangu kupunguza mateso ya wananchi na kuondosha vikwazo vya uchumi na nchi kuendelea.” 

Kwa maneno haya, Mwinyi alikuwa, kwa kimombo, a pragmatist. Deng Xiaoping alikuwa hivyo pia.

Mageuzi ya kisiasa

Mageuzi ya pili ni mageuzi ya kisiasa. Tunaweza kusema kuwa eneo hili Rais Mwinyi hakuwa na wakati mgumu kwani tayari mtangulizi wake alishatamka wazi kuwa anaunga mkono Tanzania kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa. 

Hivyo, kuundwa kwa Tume ya Nyalali na hatimaye vikao vya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Bunge kuidhinisha maamuzi haya haikuwa na mikinzano sana. Japokuwa ukisoma kitabu cha Mzee Rukhsa, na hata kitabu cha Rais Mkapa, Maisha Yangu, Kusudi Langu, utaona kuwa kulikuwa na minyukano mikali ndani ya vikao vya CCM kuhusu mageuzi. 

SOMA ZAIDI: Rais Mwinyi, Aliyefariki Feb. 29, Hakuwahi Kujutia Uamuzi wa Kujiuzulu Uwaziri

Katika ukurasa wa 253 wa kitabu chake, Rais Mwinyi anaeleza kuwa hata baada ya ripoti ya Nyalali kupendekeza kuwa mfumo wa vyama vingi ukubalike, watu wengi ndani ya CCM hawakutaka. Simulizi hii inaonyesha hali halisi ilivyokuwa. Ni simulizi ya chakula cha mchana kati ya Rais Mwinyi na Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru, adhuhuri moja, Ikulu, Dar es Salaam.

“Comrade Kingunge akajaribu sana kunishawishi kuwa turuhusu mfumo wa vyama vingi, ingawa naye alikiri kuwa itakuwa kazi kubwa kuwashawishi wapinzani wa mfumo wa vyama vingi, hasa kwa kuzingatia matokeo ya Tume ya Nyalali. 

“Akasema inawezekana, lakini tunahitaji ujasiri mkubwa. Akasema hata yeye alipingwa sana kwenye Sekretariati ya Chama na akina Gertrude Mongella na Daudi Mwakawago, walipojadili jambo hili awali, lakini hakuyumba na hatimaye Chama kiliridhia wananchi wapate fursa ya kujadili uwezekano wa mabadiliko. 

“Alipoona bado sijashawishika vya kutosha, akajitolea kuandaa mada itakayojenga hoja ya kukubali mfumo wa vyama vingi, nikamkubalia, na nikamjulisha aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, marehemu Horace Kolimba, kuwa nimempa Kingunge kazi hiyo ili hatimaye tuamue pamoja.”

Simulizi hii inaonyesha mambo makubwa mawili, moja ni kwamba haikuwa rahisi kabisa CCM kukubali demokrasia ya vyama vingi vya siasa na, mbili, kwamba Rais Mwinyi alikuwa anapenda maamuzi ya pamoja na wenzake. 

Hatimaye, Julai 1, 1992, Tanzania ikawa taifa linalofuata demokrasia ya vyama vingi vya siasa baada ya mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuandikwa kwa sheria ya Vyama vya Siasa. 

Mageuzi haya yaliungwa mkono na mtangulizi wake, Rais Nyerere, isipokuwa walipishana kwenye suala la mgombea binafsi ambapo Mwalimu alitaka, Mwinyi alikataa. Tanzania haina mgombea binafsi wa nafasi yeyote ya uongozi wa nchi mpaka sasa.

Deng hakufanya mageuzi ya kisiasa. Siyo tu hakufanya bali aliyapinga kwa kumwaga damu, Rais Mwinyi aliongoza mpito kuelekea demokrasia na nchi ikabakia salama. 

Akiwa Rais, Mwinyi alisimamia uchaguzi wa kwanza wa ushindani wa vyama vingi na kukabidhi usukani wa nchi kwa Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa, akiwa amepigiwa kura na chini ya theluthi mbili ya wapiga kura, na Bunge la kwanza lenye vyama tofauti vya siasa – CCM, NCCR-Mageuzi, CUF, UDP na CHADEMA.

Tunaweza kabisa kumpa maua yake Hayati Ali Hassan Mwinyi kama Baba wa Mageuzi nchini. Hajapewa hii heshima yake vya kutosha. Vilevile, demografia yetu imebadilika mno kwani asilimia 71 ya Watanzania wamezaliwa baada ya Mzee Rukhsa kuondoka madarakani mwaka 1995,  hivyo hakuna kumbukumbu za kutosha. 

Bahati nzuri mwenyewe Rais Mwinyi ametuachia kitabu chenye sehemu ya mapito yake. Tukisome, tukumbuke alipotutoa huyu Deng wa Tanzania.

Hamba Kahle Mzee Rukhsa, Kwaheri Tata!

Zitto Kabwe ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo. Unaweza kumpata X kupitia @zittokabwe. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts