The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mahakama Tanzania Isikwepe Wajibu Wake wa Kusimamia Utoaji Haki

Ninashauri Mahakama idhibiti mamlaka ya DPP katika mashauri ya jinai, na ilinde haki za wadaawa pasi na upendeleo.

subscribe to our newsletter!

Kazi ya Mahakama ni kusimamia utoaji wa haki na kuhakikisha usawa mbele ya sheria. Hata hivyo, katika mashauri ya jinai, Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP) ana mamlaka makubwa, ya kipekee, na yasiyodhibitiwa. 

DPP anaiongoza Mahakama tangu kufunguliwa, kusikilizwa, na ama kuondolewa kwa kesi mahakamani. Hali hiyo inapelekea uwezekano wa upendeleo na matumizi mabaya ya mamlaka. Ninashauri Mahakama idhibiti mamlaka ya DPP katika mashauri ya jinai, na ilinde haki za wadaawa, au washitakiwa mahakamani, pasi na upendeleo.

Tangu kujumuishwa kwa masuala ya haki za binadamu katika Katiba yetu miaka ya 1990, Mahakama imetoa maamuzi mengi ya kihistoria. Maamuzi hayo yameleta maendeleo makubwa katika uga wa kisheria, kisiasa, kijamii na kiuchumi nchini.

Mathalani, kupitia maamuzi ya Mahakama, kanuni muhimu kama kuheshimu utawala wa sheria na usawa mbele ya sheria; zuio la ndoa za utotoni; zuio la rushwa katika chaguzi, ambayo iliitwa takrima; wafungwa na mahabusu kupiga kura katika uchaguzi mkuu; na kadhalika, zimefanywa sehemu ya sheria zetu.

Hata hivyo, kumekuwa hakuna mwendelezo mzuri. Mahakama imechukua mtazamo wa kujizuia kushiriki kuijenga mifumo ya kisheria na kisiasa, pengine kwa hofu ya kushutumiwa kufanya uanaharakati. 

Imewahi kusemwa huko nyuma, na baadhi ya waheshimiwa Majaji waliwekewa ‘lebo’ ya wanaharakati. Lakini maamuzi yao yameishi. Na yameimarisha utawala bora.

SOMA ZAIDI: Mahakama Imdhibiti DPP Kuondokana na Kero ya Futa Kesi, Kamata, Shitaki Upya

Maendeleo ya jamii yetu ilitarajiwa yaendane na mageuzi ya kisheria kupitia Mahakama. Hii ni kutokana na aina ya Bunge na Serikali yetu. Si ajabu, hata hivyo, kuona Mahakama ikichukua mwelekeo wa kujizuia zaidi kushiriki kujenga taasisi na mageuzi ya kisheria kama nilivyodai hapo juu.

Hali hiyo imeifanya Mahakama iutose wajibu wake wa kulinda haki za kila mtu. Na katika mashauri ya jinai, Mahakama inatekeleza wajibu mmoja tu: kufuata maelekezo ya DPP, jambo linalohatarisha dhana ya usawa mbele ya sheria. 

DPP anavyopewa kipaumbele

Lakini labda tujiulize swali la msing, kwa nini Mahakama inafuata maelekezo ya DPP? Muundo wa Ofisi ya Taifa ya Mashitaka unamtaja DPP kuwa huru. Uhuru wa kushitaki bila kuingiliwa, na pengine kuondoa mashitaka mahakamani. 

DPP anafanya hivyo baada ya kupokea jalada la uchunguzi kutoka Jeshi la Polisi au mamlaka nyingine kama vile TRA, PCCB, au DCEA. DPP ana mamlaka hayo kikatiba na kisheria.

Hata hivyo, mathalani kati ya mwaka 2016 na 2021, kulikuwa na walakini iwapo ni DPP ndiye anaamua kushitaki au vinginevyo, hususani katika makosa ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha. 

Kesi hizo zilikuwa maarufu sana. Pamoja na watu wengine, kesi za uhujumu uchumi ziliwakumba wakosoaji wa Serikali. Zipo fununu kwamba kesi hizo zilifunguliwa kwa ‘maelekezo kutoka juu.’

SOMA ZAIDI: Rasimu ya Warioba Ina Majibu Yote Samia Anayahitaji Kuhusu Mfumo wa Haki Jinai

Ninakubaliana na fununu hizo kwa kuwa kesi nyingi zimefutwa kwa kukosa ushahidi. Mathalani, mwaka 2022, Mkuu wa Jeshi la Polisi alitangaza kufuta kesi zaidi ya 1,840 kwa kukosa ushahidi. 

Aidha kuna kesi nyingine nyingi, ikiwemo za ugaidi, zimefutwa kwa njia hiyo hiyo. Ni kesi ambazo DPP aliridhia kuzipeleka mahakamani, na akaahidi Mahakama kwamba anaendelea na upelelezi, huku watuhumiwa wakiwa mahabusu gerezani.

Vilevile, kuna watu walifutiwa mashitaka fulani na kubakiza mengine. Mfano, tangu mwaka 2021, baadhi ya watuhumiwa wa makosa ya uhujumu uchumi wamefutiwa kosa la utakatishaji fedha. Kosa hilo lilifutwa baada ya watu hao kukaa mahabusu muda mrefu.

Swali ninalojiuliza, kwa nini DPP anapeleka mahakamani kila kesi anayopelekewa? Rais Samia Suluhu amewahi kukiri hadharani kwamba kuna ubambikiwaji wa kesi. Ripoti ya Tume ya Haki Jinai ya Jaji Mkuu (Mst.) Othman Chande iligusia suala hilo pia.

Ninafahamu, polisi huwa wanaandika maelezo ya onyo – wakati mwingine ya uongo, ya watuhumiwa. Hiyo ni baada ya kipigo na mateso, ambayo hupelekea watuhumiwa kusema maelezo ya uongo na kukiri kosa ili wasiteswe zaidi. 

SOMA ZAIDI: Hivi Ndivyo Serikali Inavyoweza Kuuboresha Mfumo wa Haki Jinai Tanzania

Je, polisi wanampotosha DPP? Labda! Lakini kwa nini DPP hafanyi upembuzi zaidi kabla ya kupeleka kesi mahakamani? Na wakati hayo yanajiri, Mahakama inakuwa wapi?

Ninashauri, DPP afuatilie na ajiridhishe kama maelezo ya onyo yametolewa kwa hiyari, hususani yanayohusu makosa yasiyo na dhamana. Miaka ya nyuma Mahakama kwanza ilijiridhisha kama kuna ushahidi wa awali kabla ya kuruhusu kesi zifunguliwe. 

Mwanasheria Mkuu aliwajibika kuishawishi Mahakama – kwa ushahidi, ili kusajili kesi ya jinai.

Pia, Mahakama zilikuwa na mamlaka ya kuruhusu dhamana kwa makosa yote. Japo kulikuwa na makosa mawili tu yasiyo na dhamana – mauaji na uhaini– watuhumiwa wa makosa hayo vilevile wangeweza kuomba dhamana mahakamani na wakapewa.

Kwa hiyo, tuangalie masuala mawili: kesi zifunguliwe baada ya upelelezi kukamilika na mahakama idhibiti mamlaka ya DPP. 

Usawa mahakamani

DPP ana dhamana ya kufungua na kuendesha kesi za jinai. Na anahodhi mamlaka hayo kiasi cha kuzuia watu binafsi kufungua kesi fulani fulani, kwa kuwasilisha hati yenye maelezo kwamba hana nia ya kuendelea na kesi husika. 

SOMA ZAIDI: Tito Magoti: Barua ya Wazi kwa Rais Samia Kuhusu Hali ya Haki Jinai Tanzania

Mazingira ya sasa yanainyima Mahakama fursa ya kumdhibiti DPP, isipokuwa katika makosa yenye ukomo wa upelelezi, mathalani siku sitini. Hata hivyo, DPP anaweza kutumia polisi kumkamata mtuhumiwa na kufungua kesi hiyohiyo upya.

DPP anaweza kuondoa mahakamani kesi yoyote ya jinai. DPP hahitaji kutoa sababu ikiwa amefuata utaratibu. Tumeshuhudia DPP akifuta na kurejesha kesi mahakamani mara nyingi kwa kadri anavyohitaji. 

Ninafahamu kuna marekebisho ya sheria ya mwaka 2022 kuhusu kanuni hii. Lakini, kama nilivyoandika katika makala yaliyopita, marekebisho yale ni mapambo tu!

DPP anaamua lini upelelezi ukamilike. Katika makosa yasiyo na dhamana – isipokuwa kosa la uvamizi wa kutumia silaha, Mahakama haina kauli yoyote. Kesi hufunguliwa Mahakama za mahakimu ambazo hazina mamlaka ya kuzisikiliza. 

Kwa hiyo, utapiga mbizi mahakamani ukisubiri DPP aseme iwapo upelelezi umekamilika. Mdaawa na Mahakama watasubiri DPP aelekeze hatua inayofuata.

DPP anaamua nani aachiwe na nani ashitakiwe Ni kupitia kanuni ya nolle, au wakati anapeleka taarifa za kuwasomea mashitaka watuhumiwa Mahakama Kuu. DPP anafanya hivyo kwa upekee bila kuhojiwa. 

SOMA ZAIDI: Ucheleweshaji Kesi Mahakamani Unavyokwamisha Upatikanaji wa Haki

Mamlaka hayo, kwa ujumla, yametumika vibaya, hususani katika kesi zinazowahusisha wakosoaji wa Serikali, na makundi mengine katika jamii. Ninapendekeza Mahakama idhibiti matumizi ya mamlaka ya DPP. Licha ya kurekebisha sheria, Mahakama itumie mamlaka yake ya asili kulinda haki ya usawa mbele ya sheria. 

DPP asimamiwe wakati anafungua kesi, angalau kuwe na ushahidi wa awali; atoe sababu – na zibishaniwe, akifuta kesi; mashitaka yafunguliwe ikiwa upelelezi umekamilika, ama sivyo, kuwe na ukomo wa upelelezi kwa makosa yote. 

Pia, Mahakama imuwajibishe DPP akitumia mamlaka yake vibaya. Kuna yanayohitaji marekebisho ya sheria. Lakini mengine yanahitaji umadhubuti wa Mahakama tu.

Tito Magoti ni wakili na mtetezi wa haki za binadamu kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia titomagoti@gmail.com au X kama @TitoMagoti. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *