The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tunatathimini Vipi Hali ya Uandishi wa Habari? 

Utendaji mzuri ni wa kujisimamia wenyewe, waandishi waachiwe wajisimamie wenyewe.

subscribe to our newsletter!

Katika kipindi cha Jenerali Ulimwengu Exclusive on The Chanzo kilichoanza kuruka rasmi kwenye chaneli ya YouTube ya The Chanzo Julai 9, 2023, Jenerali Ulimwengu ambaye ni mwandishi mkongwe nchini amefanya mazunguzo na Mhariri Mkuu wa The Chanzo, Khalifa Saida juu ya tasnia ya habari nchini.

Katika mazungumzo haya, Mzee Ulimwengu alianza kwa kumdadisi Khalifa kuhusu The Chanzo, na kisha kuendelea kujadilini kwa kina kuhusu dhana nzima ya uandishi wa habari na mazingira yake hapa nchini. Karibu kusikiliza kipindi hiki.

Jenerali Ulimwengu: Habari za leo mpenzi mtazamaji nakukaribisha tena katika kipindi hiki kinacholetwa kwako na Jenerali Ulimwengu. Na leo ninataka kwanza niombe radhi kwamba nilikuwa nimesema kwamba tutakuwa tunaonekana mara kwa mara lakini hapa katikati nikapotea  nikawa sipo katika anga hizi nimesafiri kidogo na nimerejea hivi karibuni. 

Kwa bahati nzuri nimepata wasaa wa kuwa na mtu maarufu kijana mmoja maarufu sana. Mwanahabari ambaye pamoja na udogo wake katika umri lakini amefanya kazi kubwa sana na sasa hivi yuko anahangaika sana mitandao ya kijamii katika kitu nilichokuambia wakati ule The Chanzo. Naye si mwingine ni Khalifa Said, karibu sana. 

Khalifa Said: Shukrani sana. 

Jenerali Ulimwengu: Nakushukuru sana kwa kuja katika kipindi hiki cha Jenerali Ulimwengu Exclusive on The Chanzo, na ninataka tuwe, wewe ni mwanahabari, mimi ni mwanahabari mstaafu, mkongwe, lakini mwanahabari bado, kimsingi bado mimi ni mwanahabari. Kwa hiyo nina ruhusiwa kukuliza maswali. The Chanzo ilianza anza vipi?

Khalifa Said: Asante sana Jenerali, nashukuru. Kusema kweli kwa kupewa fursa naweza nikasema au upendeleo wa kuwa kwenye kipindi hiki. Ambacho kusema ukweli kama ulivyozungumza ni cha kwanza na sisi pia The Chanzo tuwaahidi wasomaji wetu na watazamaji wetu kwamba tutakuwa na kipindi kama hiki kwenye jukwaa letu hili la The Chanzo. 

Sasa, The Chanzo kwa ufupi tu ni chombo cha habari, lakini tunasema ni chombo cha habari cha mtandaoni ambacho mimi na wenzangu wawili, Tony Alfred ambaye ni Mhariri Mtendaji wetu na Joel Ntile ambaye ni Meneja Utawala wetu tulikianzisha mwaka 2020 [mwezi] Julai. Na operesheni rasmi  zikaanza mwezi wa tisa [mwaka huo huo].  

Na tulikianzisha kwa sababu sisi sote watatu ni watu ambao tunapenda kusoma mambo ya habari. Lakini kipindi kile kulingana na uongozi uliokuwepo tulikuwa kama hatufurahishwi na namna mazingira yalivyokuwa. Uwanda wa vyombo vya habari, habari nyingi zilizokuwa zinazalishwa zilikuwa hazituridhishi. Kwanza ndiyo hivyo kuna matukio mengi yalikuwa yanatokea lakini hayaripotiwi. Lakini hata uwasilishwaji ukifanyika unafanyika katika namna ambayo inaacha maswali mengi.

Kwa hiyo, sisi tukajiunga na tukasema  badala ya kulalamika tufanye kitu. Kwa hiyo, tukaanzisha The Chanzo kwa hiyo tumekuwepo hapa tangu Septemba 2020. Na mpaka leo tunaendelea kama ambavyo wafuatiliaji wetu wanavyoona.

Jenerali Ulimwengu: Sasa na  The Chanzo maana yake ni  The Source. Kwa hiyo, mmechukua jina la shughuli kuu ya mwanahabari ambayo ni kupata chanzo. Chanzo, huwezi ukakaa nyumbani au ofisini kwako ukabuni mambo lazima uwe na chanzo. 

Khalifa Said: Swadakta. 

Jenerali Ulimwengu: Na mnajikita katika habari za aina gani hasa? 

Khalifa Said: Sisi kwa kiwango kikubwa tunajikita kwenye habari za kiuchambuzi. Sisi kama nilivyotangulia kusema kwamba tulikuwa haturidhishwi na namna uandishi wa habari unavyofanyika. Kwamba wewe ni mwanahabari unafahamu, kwamba tumezoea kwenye kuandika habari  unatakiwa ujibu nini, lini, nani. Lakini sisi tukaona kuna kipengele cha kwa nini pia kinatakiwa kiwemo kwenye kuandika habari fulani na kwa kiwango kikubwa tukawa hatukioni.

Kwa hiyo, sisi tunafanya habari kama kawaida, lakini tunahakikisha sana kwamba habari zetu zinakuwa ni za kiuchambuzi kwa lengo la kumsaidia msomaji, tunasema kupata maana nyuma ya hiyo habari husika. Ndiyo Rais amezungumza kitu fulani sawa lakini nyuma ya hiki kitu kuna nini, kwa nini hiki kitu ni muhimu?  

Jenerali Ulimwengu: Muktadha mzima, na Rais mwenyewe kazungumza jana, lakini je, wiki iliyopita ilikuwaje? Alifanya nini? Alizungumza nini? Waziri Mkuu alizungumzia suala kama hili kasema nini? Wakati mwingine unaweza ukakuta Rais kazungumza lakini Waziri Mkuu wiki iliyopita tu alizungumza kitu tofauti kabisa, kabisa na ni katika Serikali hiyo hiyo.

Sasa kwa  nini mkafikiria kwamba masuala kama hayo yanaweza kushughulikiwa na kutafutiwa usuluhishi kwa kutumia mitandao ya kijamii?  Mitandao ya kijamii nayo ina matatizo yake, hivi ni vyombo vya kimtandao ambavyo vimefanya kwamba kila mtu anaweza kuwa mwanahabari sasa.   Bora una simu yako unaweza ukanzisha habari na ukaipeleka  dunia nzima. Kuna kosekana ule utaratibu wa kuchuja habari ili kuona kama zimeandikwa kama ulivyosema [kufuata] zile 5W+H. Nani, nini, lini, wapi, kwa nini halafu na kivipi.  

Sasa kwa nini msiende kwenye vyombo vya habari vya kawaida gazeti au redio au televisheni. Mkaenda kwenye mitandao ya kijamii ambayo ina matatizo hayo, kwa sababu haina utaratibu wa kuchuja habari vya kutosha?

Khalifa Said: Kwanza kusema kweli lazima niseme fursa ikijitokeza na uwezo ukiwepo wa kuanzisha kwa mfano TV au gazeti hicho si kitu ambacho sisi tunakinzana nacho. Yaani ni kitu ambacho bila shaka kadiri The Chanzo inavyokua  tutakwenda kwenye hizo njia na tutaangalia. Kimsingi saSA hiVi  tunaangalia uwezekano wa kuanzisha jarida au tunasema ‘magazine’ ambayo tutakuwa tunaitoa kila mwezi. 

Kwa hiyo, si kwamba kitu ambacho tumesema hatutaki, hapana. Kilichotokea ni kwamba tulikuwa tunaangalia sisi kama wananchi tunafanya nini kwa njia zetu wenyewe yaani kwenye hiki tulichonacho, ndani ya uwezo wetu, tunaweza tukafanya nini. Na ndiyo maana tukasema basi twende kwanza tufanye uandishi wa habari wa kidigitali ambao ni rahisi kifedha ukilinganisha na kuanzisha TV, kwa mfano au redio au gazeti.

Jenerali Ulimwengu: Wafanyakazi  250, mafundi mambo yanakuwa mengi na kadhalika. 

Khalifa Said: Kwa hiyo tukasema tunafanya kitu kulingana na uwezo tulionao. Tukiwa tunakua huko mbeleni hivyo vitu vingine vitakuja. Nakubaliana na wewe kwa asilimia kubwa kwamba vyombo vyetu hivi vya mtandaoni ambavyo vinatumia sana mitandao ya kijamii, kumekuwa na hilo tatizo. Kwamba unakuta kwenye hicho chombo cha habari mwandishi ni huyo huyo, mhariri ni huyo huyo, mpiga picha ni huyo huyo hakuna mtu wa kumuambia  kwamba hiki kitu hapana. Hakuna hiyo uchujaji wa habari ambayo umeizungumzia. 

Lakini kwetu sisi hiyo ni tofauti kidogo. Sisi ndiyo ni chombo cha habari cha mtandaoni lakini huo mpangilio wa udhibiti huo upo. Kwamba tuna waandishi, waandishi wanaripoti kwa mhariri, mhariri anashauriana nao, mhariri yeye pia anaripoti kwenye kikao cha wahariri wenzake, kwa hiyo kuna huo mtaririko. Kwa hiyo kabla habari hata kufanywa kuanzia kwenye wazo lenyewe la habari mwandishi anapeleka kwa mhariri anajadiliana na mhariri na mhariri akishawishika yeye analichukua wanakwenda kwenye kikao cha bodi ya wahariri ya The Chanzo, tunaijadili, tunaidadavua kama tunaona ni wazo zuri la kuendelea nalo tunaendelea nalo. 

Na habari hivyo hivyo. Mwandishi atatuma, mhariri ataipitia mhariri akiipitia akimaliza kufanya naye anatuma kwa wahariri wenzake inapitiwa. Kama kuna kasoro, kuna changamoto kwa hiyo mpangilio wa udhibiti upo. Ingawaje  na hili pia linakuja suala tena la uwezo wa rasilimali. Kwa hiyo mpangilio wa udhibiti wa kwetu sisi bila shaka utakua siyo mrefu sana kama pengine ya  gazeti la  The Guardian kwa mfano. Kwamba inatoka kwa mwandishi itakwenda kwa mwandishi mkuu, mwandishi mkuu ikitoka kwake itaenda kwa mhariri wa habari. Mhariri wa habari ikitoka kwake itakwenda kwa mhariri Mkuu. Sisi hatuna huo [mpangilio] mkubwa lakini tunajaribu kuhakikisha kwa ndani ya uwezo  wetu  kuona ni kwa kiasi gani tunaweka huo mpangilio. Kwa sababu ni muhimu kuhakikisha kwamba habari ambazo tunazitoa zinakuwa ni sahihi, za ukweli na zenye kumsaidia mtu. 

Jenerali Ulimwengu: Na ule utaratibu wa kizamani ule wa habari kutoka kwa ripota na kupita kwa watu wengine hadi kwenye kikao cha wahariri ni muhimu kama una kampuni kubwa sana. Kama una kampuni ndogo inabidi uwekeze zaidi katika ubora wa watu wanaofanya hizo kazi. Hata kama ni mmoja anaweza kufanya kazi kama mbili hivi lakini ni mtu mwenye uhakika. Ikipita mikononi mwake huna wasiwasi kwamba jambo la hovyo litaingia kwenye kupokelewa na watu, na ukajikuta kwamba una jambo jingine. 

Lakini bado kuna watu wanafanya kusudi, makusudi kabisa, kuondokana na uchujaji wa taarifa ili habari iwe tamu hili ni tatizo vilevile. Kwamba kuna media nyingine ambazo ama kwa kutaka kuvutia wasomaji wengi ama  wafuatiliwe, watazamaji wengi zaidi wanatoa taarifa ambazo hazina ukweli kabisa. Hamna uwezekano kabisa kwamba hii itakua  ni ukweli kuna watu wanafufuka, kuna watu wanakwenda mbinguni, watu wanakwenda kila mahala, na yote ni uzushi.

Khalifa Said: Na hili ni tatizo la kidunia, hicho kitu ambacho umekizungumza. Mifano ipo mingi sana. Kwa mfano, kwa sasa hivi hususan kwa nchi za Ulaya na Marekani kuna huu mtandao ambao unaitwa Substack na waandishi wengi wanaacha kazi  kwenye vyombo rasmi  na kwenda kuanzisha akaunti kwenye huu mtandao wa Substack. Na sababu kubwa ambayo   wao  wanayoitoa ni ya kukimbia huo mpangilio wa udhibiti. Kwa mfano kuna mtu anasema mimi stori yangu iliuliwa bila ya maelezo yoyote  kwa sababu tu wamiliki walikuwa hawataki hiyo habari itoke. Kwa hiyo nimeamua kuacha kazi.  

Jenerali Ulimwengu: Ambayo ni kweli wakati mwingine.  Wamiliki wa vyombo vya habari wana mahusiano mengine ambako nje ya vyombo vya habari vyenyewe. Na watawala, lakini na watu vilevile wafanyabiashara, wanasiasa na maslahi mengine ambayo kwa hiyo inawezekana kama kuna ukweli kwamba mara nyingine huwa inatokea kwamba stori zinauliwa makusudi kabisa. 

Khalifa Said: Kama  kwa mfano kuna waandishi wakubwa tu, watu wa kama unamfahamu huyu Seymour Hersh ambaye aliitoa ile habari My Lai Massacre na Vietnam. Ameacha kabisa kuajiriwa na vyombo vya habari rasmi ameamua kufungua akaunti kwenye huo mtandao wa Substack

Kwa hiyo, kwa namna moja unaweza ukasema kwamba haya mabadiliko ya kiteknolojia yanatoa uhuru zaidi kwa waandishi. Lakini sasa ndiyo changamoto unakuja kwamba je tunahakikisha vipi uthibiti wa taarifa. Kwa sababu ni muhimu, mhariri hayupo kwa ajili ya kuua tu habari. Lakini pia ni kwa ajili  ya kumuhoji mwandishi umepataje hii taarifa, na tunaiboreshaje, tuna hakiki vipi hizi [taarifa] za hiki ambacho unachokizungumza. Kwa hiyo  nadhani ni changamoto sijui wadau wa habari wanaweza kuitatua vipi. 

Jenerali Ulimwengu: Sawa. Tunayo matatizo mengi sana, kuna matatizo haya ya ukwasi, watu kutokuwa na fedha za kuwekeza. Maana yake inahitaji uwekezaji kidogo na kila mtu kufuatana na uwezo wake tunapishana. Lakini kuna mambo mengine, kuna suala la maadili kwa mfano kutotoa taarifa za uongo kama tuna tatizo kubwa sana, tumekuwa na utamaduni wa watu kusema uongo makusudi kabisa. 

Kuna hiyo inakwenda katika kila idara ya maisha yetu siyo tu katika uandishi lakini vilevile katika siasa, katika biashara. Uongo imekuwa ni hulka ambayo   wala mtu haoni tatizo kusema uongo.  Na uongo wa waziwazi kabisa.  Hii inaweza ikapigwa vita ndani ya uandishi na uanahabari wakati jamii nzima ndivyo ilivyo.  

Khalifa Said: Ni ngumu, ni ngumu na pia ni kitu kinawezekana. Ni ngumu kwa sababu kama unavyozungumza waandishi wa habari wa Tanzania hawatoki nje ya nchi wanatoka kwenye jamii yetu. Na kama jamii yetu imekifanya kiwe kitu cha kawaida, imefanya ni mazoea kuzungumza uongo bila shaka kutakuwa na upenyo fulani. Lakini ni kitu kinawezekana kukizuia kwenye uandishi wa habari.

Kwa sababu kama unavyozungumza waandishi wa habari tunafungwa na miiko na maadili yetu ya kitaaluma. Ukiingia kwenye chombo cha habari kama mwandishi wa habari wewe siyo raia tu lakini ni mwandishi wa habari sasa. 

Kwa hiyo kunaweza kukawa kuna mambo ya kijamii ambayo jamii inayachukulia kama ni ya kawaida lakini wewe unapoingia kwenye tasnia unakuwa umepanda ngazi fulani. Kwamba ni mwananchi ndiyo, ni mwana Dar es Salaam, lakini pia ni mwandishi wa habari na hii ni miiko na taratibu zetu za uandishi wa habari, na taratibu zetu zinakataza kusema uongo au kuandika uongo. Miiko yake inazungumza hivyo.

Jenerali Ulimwengu: Ni kama kuwa na mapenzi ya kucheza mpira, unapiga chandimu mtaani ni tofauti na kuingia kwenye ligi. Ukiingia kwenye ligi inatakiwa ufate  taratibu zile ambazo zimewekwa kwa ajili ya mchezo wa mpira wa miguu.

Khalifa Said: Na kuna wanasemaje kuna matokeo za kusema uongo. Ikithibitika kwa mfano kama umesema uongo kuna matokeo yake. Kwa hiyo, kwa mfano Tanzania watu ambao wanasimamia maadili ya uandishi wa habari ni Baraza la Habari Tanzania (MCT). Kwa hiyo kwa mfano kama The Chanzo imeandika uongo kuhusu wewe upo uwezekano, unaweza ukaenda MCT, ukasema kwamba hawa watu wameandika uongo kuhusu mimi na ukasema unachokitaka. Na MCT wakishindwa kutatua hilo jambo mtaenda kwenye chombo kikuu cha utoaji haki Tanzania kwenye mahakama. 

Jenerali Ulimwengu: Na hiyo umeizungumzia MCT hapo umezungumzia suala la muhimu sana juu ya MCT kama chombo cha usimamizi wa maadili na maslahi, na ustawi wa habari na uanahabari nchini. Na ni chombo, hiki ni chombo ambacho ni cha hiari si chombo cha Serikali. Na huko nyuma tuliwahi kupatwa na msukosuko Serikali kutaka kutuundia chombo cha kiserikali, cha kisheria, na tukakataa nakumbuka nilikuwa bungeni wakati ule. 

Bado Serikali inataka kuanzisha chombo cha namna hiyo, ambacho kitakuwa ni cha sheria, kuna makatazo mengi, kuna mtu anaitwa msajili imekuwa msajili, msajili. Kila mahali unapoangalia kuna mtu anaitwa msajili. Msajili amekuwa ukiacha Mungu , chini yake anakuja msajili. [Kuna msajili] wa vyama vya siasa, wa vitu gani, NGO, baada ya Mungu tu anakuja msajili pale. 

Sasa wanahabari wanalishughulikia vipi? Kwa sababu lazima mimi, kwangu mimi katika uzoefu wangu ni kwamba Tanzania tumefanya kitu ambacho kimeigwa na nchi nyingine. Wamekuja hapa watu wengine kujifunza kuona ni nini tumefanya. Na Baraza la Habari la Tanzania linafanyaje kazi na nchi nyingine wameiga. 

Lakini bado kuna utashi ndani ya Serikali wa kufunga na kuzuia kitu chochote ambacho hakina udhibiti kamili wa asilimia 100 wa Serikali wanakiona kama vile ni kitu hatari, kuna utashi fulani wa namna hii. 

Ni nini unadhani kinatakiwa kifanyike ili jamii yote ielewe kwamba nia dhamira ya kufanya vyombo vya habari viwe chini ya kidole gumba cha Serikali si dhamira nzuri na itaua kweli uhuru na ustawi wa vyombo vya habari.

Khalifa Said: Nimefurahi sana mimi kuniuliza hilo. Mimi mtazamo wangu au maoni yangu yako wazi kuhusiana na hili jambo. Na najaribu, nimekuwa nikizungumza kila ninapopata mualiko wa kuhudhuria warsha hizi kujadili uhuru wa habari Tanzania, kwa kupitia MCT na wadau wengine. Na leo tu tulikuwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Deodatus Balile tukizungumzia hili hili. 

Mimi msimamo wangu mzee Jenerali upo wazi kabisa kwamba Tanzania hatuhitaji Sheria mahususi ya vyombo vya habari. Na umezungumza sisi kama waandishi tunalipigania vipi hilo kuhusiana na hii sheria, na nadhani mimi maoni yangu ni kwamba tunaelekeza juhudi zetu pasipo sahihi kama tasnia kama waandishi. Na kwa nini nasema hivyo, kwa sababu ukisikiliza matamko  na harakati zinazoendelea ni kama vile waandishi tunasema tunataka sheria nzuri. Kwamba Sheria hii ni mbaya tunahitaji Sheria nzuri. 

Lakini mimi ninachoamini ni kwamba hata ukiwa na sheria nzuri, hata ukiwa na sheria nzuri lile wazo tu kwamba kuna Serikali ndiyo inakudhibiti kwenye utendaji wako wa kazi moja kwa moja inakupelekea wewe mwenyewe kujithibiti unapofanya kazi zako za kiuhariri na za kiuandishi wa habari. Na mimi nasema kwamba duniani kote, utendaji mzuri ni wa kujisimamia wenyewe.  Waandishi waachiwe wajisimamie wenyewe. 

Kama kweli kwa mfano Waziri wa Habari Nape Nnauye na Serikali kwa ujumla na mama Samia Suluhu Hassan wanadhamiria kama wanavyozungumza kwamba tunajali uhuru wa habari na tunajali haki za binadamu tunataka waandishi na vyombo vya habari viwe huru. Lazima wawaachie waandishi wa habari wajisimamie wao wenyewe, kupitia  vyombo ambavyo wataviunda wao wenyewe.  

Nchi nyingi tu duniani hazina sheria mahususi hasa za vyombo vya habari. Marekani kwa mfano nimekuwa nikizungumza hili mara nyingi,  Marekani Katiba yao iko wazi kabisa kwamba Bunge halitatunga sheria mahususi itakayo dhibiti uhuru wa vyombo vya habari. Ufaransa hakuna sheria mahususi, nchi zote za Scandinavia hakuna sheria mahususi ya chombo cha habari. 

Na kwa nini uwe na sheria mahususi ya chombo cha habari. Kwa mfano leo hii tusiwe na sheria mahususi mimi nikiandika habari nikikudhalilisha hakuna sheria? 

Jenerali Ulimwengu: Ipo. 

Khalifa Said: [Sheria] ambayo mimi itaniwajibisha? 

Jenerali Ulimwengu: Ndiyo. 

Khalifa Said: Chombo cha habari ni kampuni hatuna sheria ambazo zina ongoza haya masuala ya kiuwekezaji. Mimi huwa nasema kwamba Sheria hutungwa kwa ajili ya kutatua tatizo mahususi. Sasa Serikali itueleze ni nini? Ni tatizo gani lililowasukuma mpaka wakaamua kuja na sheria mahususi ya vyombo vya habari? Na hili tatizo wamelitambua vipi kwa sababu labda pengine tuna tume ambayo iliundwa ikaona kwamba kwenye vyombo vya habari kuna tatizo moja, mbili, tatu. Na wao wakapendekeza namna ya kutatua matatizo haya itunge na sheria mahususi kwa  vyombo vya habari. 

Kwa hiyo na  pale mwanzo tulizungumza kuhusu maadili ya uandishi wa habari. Kusema kweli Tanzania mahali popote penye sheria mahususi ya vyombo vya habari maadili hayana kazi, hayana kazi. Kwa sababu mimi leo nikimuandika Rais Samia vibaya Msemaji wa Serikali au Msajili haendi MCT kunishitaki mimi hapana ananifungia tu. Sasa hayo ni maadili gani ya uandishi wa habari. Ni katika nchi gani mimi najiuliza ipo kama hivyo.

Jenerali Ulimwengu: Inakuwa si maadili tena ni vitisho na udhibiti, na udhibiti. 

Khalifa Said: Na hapo ndiyo linakuja swali, kwa nini Serikali inakuja na sheria kama hizi hakuna sababu nyingine ni udhibiti. Serikali inapenda  masuala ya udhibiti. 

Jenerali Ulimwengu: Na kuficha, kila panapotokea udhibiti mkali wa vyombo vya habari ina maana kwamba watawala wanataka mambo yao yasitolewe nje. Wasiambiwe mnakosea, waambiwe kila siku kwamba nyie watu wazuri sana, tunakupendeni sana, bila nyie tungekuwa wapi siye. Maskini siye, wanafurahi wananawili. 

Lakini nia yenyewe ni kudhibiti maovu yasitoke na yako maovu mengi ambayo yanafanyika. Kwa mfano, fedha zinavyotumika vibaya. CAG akitoa taarifa kila mwaka, tunaona mambo ni yale yale Serikali haioni kama ni jambo muhimu. Na vyombo vya habari nchini kwa kweli vimedorora huoni vikichukua mambo ya kuyadadavua na kuchunguza ni nini na kadhalika.

Ukiangalia, mimi huwa naangalia barabarani  naangalia aina ya magari yanayoendeshwa yameandikwa STH na vitu gani sijui nini, STL, STK nimekuwa nasema ni magari yanaendeshwa [na] kina Beyonce.  Marekani watu wa namna hiyo ndiyo wanaendesha magari hayo siyo watu wa Serikali. Kwa sababu Serikali  hairuhusiwi kutumia pesa kiasi kile kwa jambo si la maana sana kama gari la fahari na kadhalika.

Kama unataka kuendesha gari kama Diamond, Beyonce nenda kapige mziki tengeneza hela zako nyingi, mabilioni ya pesa nunua gari lako. Lakini gari ya inanunuliwa na mlipa kodi inayoendeshwa kwa fedha ya mlipa kodi haitakiwi kuwa ya anasa kiasi hicho. Kwa hiyo utashi wa udhibiti ni watu wasiseme kama hawana hela, ukisema hivyo ukifika mahala fulani  utaambiwa kwamba wewe unatukana, unadhalilisha, unadhalillisha viongozi  ambao wengi si viongozi ni watawala tu. Lakini wanapenda kujiita viongozi.  Ukiuliza wametoa wapi uongozi ni kwamba wana ofisi, ukishakuwa na ofisi unakuwa kiongozi.

Sasa, ufundishaji wa taaluma ya uandishi wa habari, elimu. Kwanza nani mwanahabari mara nyingi kuna suala hilo. Kuna mdhibiti anaitwa nani sijui msajili sijui na hilo baraza linatakiwa na Serikali   ndiyo litakuwa linatoa vyeti  kusema kwamba huyu ni mwandishi wa habari. Usipopewa cheti cha namna hiyo wewe siyo mwandishi wa habari. Hii inawezekana kweli? 

Khalifa Said: Haiwekezekani, halafu pia wanasemaje kwamba ni kinyume na mantiki. Mimi na ndiyo maana napata shida nasema nani hawa aliwashauri. Yaani walitafuta watu gani wakaenda wakawashauri mpaka wakaja na masharti kama haya.  Kwa sababu mimi ninavyofahamu labda pendekezo zuri lingekuja kwamba kama unataka kuwa mwandishi wa habari za afya, basi angalau uwe na stashahada ya masuala ya afya. Kama unataka kuwa mwandishi wa habari za mazingira basi angalau uwe na astashahada. Hii moja kwa moja inaenda kusaidia ubora wa maudhui ambayo unaenda kuzalishwa. 

Lakini hii ya kusema kwamba ili ujiite mwandishi wa habari ni lazima uwe na stashahada. Mimi hili pendekezo sijui limetokea wapi. Na mtu, ofisi fulani ikutambue, sasa wewe ni mwandishi wa habari na cheti chako hiki. Na inashangazi kwa sababu watu kama wewe moja kati ya waandishi ambao  wanaheshimiwa Tanzania yaani ulianza bila kupata mafunzo maalumu. 

Mimi huwa nawauliza watu kwani uandishi wa habari ni nini? Mimi ninavyofahamu kwamba uandishi wa habari ni sanaa ya kuhadithia hadithi. Kwamba mimi nipo kijiji kwetu hapa tembo amemuua mtu wakati alipo vamia shamba lake nimeliona, nimechukua hiyo, nimeandika natuma. Kwa sababu hata zamani ilikuwa iko hivyo. Uandishi wa habari  wenyewe uliibuka vipi  kwamba watu wametoka Ulaya au Asia wanakuja Afrika wanaandika kwenye machapisho wanasema huku Afrika tumeona watu hawa tunaweza tukawatumia kwenye mahitaji yetu ya viwanda, tena wana nguvu za kutosha za kufanyia kazi  wanatuma kule jeshi linatumwa ndivyo hivyo. 

Baadaye tukatengeneza viwango kwamba ili tufanye vizuri kuwe kuwe na utaratibu huu.

Lakini kimsingi uandishi wa habari wewe umeona kitu na unataka kuwapasha wenzako habari. Sasa kwa nini uweke masharti kwamba ili mimi niweze kufanya hivyo lazima niwe na astashahda. Na inashangaza pia kwa sababu kama ninavyosema mimi na ninaweka hii katika rekodi zangu kwamba ambao wamenisaidia na mimi nikiwa na mafunzo rasmi ya uandishi wa habari, unafika kwenye chumba cha habari hujui chochote. Kwa sababu tunajua namna vyuo vyetu vinavyoandaa waandishi unafika kwenye chumba cha habari hujui chochote. Watu ambao wanakukamata mkono wanakuambia usijali tutakuelekeza ni watu ambao walikuwa hawana mafunzo rasmi ya uandishi wa habari. Hawakusoma kabisa. 

Jenerali Ulimwengu: Hawakusoma katika chuo,  ila wamepitia katika mikono ya watu waliokuwa katika habari. Na wao hawakufundishwa na shule yoyote. Kwanza vijijini umetoa mfano wa kijiji kuna tembo, kuna balaa la njaa. Wakati mwingine balaa Kiswahili chake huwa ni nini baa, baa la njaa, nzige mtu yupo kijijini anaona wingu linakuja. Na akiangalia anajua hii nzige anapiga baragumu kukiambia kijiji kizima jamani nzige wanakuja. Okoeni chakula mnachoweza kuokoa maana  baada ya hapa hakuna chakula tena. 

Na hiyo imefanyika, yule mpiga baragumu yule alifundishwa na nani kama si mila za kawaida anajua kwamba wale ni nzige. Na hii ni hatari niwaarifu watu wangu. Kwa hiyo ni jambo ambalo halina mantiki hata kidogo. 

Khalifa Said: Na hapo hapo, ndiyo tunarudi tena huo uamuzi umeletwa kutokana na nini nini sasa. Kwa sababu  sisi kama  na sijui kama wengi tunaelewa hilo, kwamba vitu, sheria na sera lazima ziwe uthibitisho wa dhahiri. Unapokuja na sera au sheria lazima useme hii imeletwa na nini?

Kwa mfano mimi nataka kujua, sana sana na nimekuwa nikijaribu kuuliza Serikali ilipoamua kuja na hili sharti la kwamba ili mtu aitwe mwandishi wa habari lazima awe na stashahda ya uandishi. [Serikali] ilitaka kutatua tatizo gani, yaani tatizo ni lipi ambalo wao waliliona kwamba hili ni tatizo na walilionaje hilo tatizo. Na wakaamua kwamba ili kulitatua hili tatizo lazima tuje na hiki kipengele, sipati jibu mimi. 

Jenerali Ulimwengu: Kiswahili fasaha ni chamno nini? Chamno nini? Nini hasa, tatizo lako nini? Hiyo sheria mnataka kuleta chamno nini?

Khalifa Said: Kwa sababu wanasema, wanasema muda, anasema kwamba ukiangalia magazeti mara sijui wanavyoweka picha, wanavyofanya nini. Na mimi huwa nawasikiliza nasema hivi mnajua namna kwa mfano kwenye gazeti unajua namna operesheni zinavyofanyika. Kwa sababu kama mtu anasema unaona kwa mfano kwenye magazeti stori inahusu Magufuli lakini wanaweka picha ya Mange Kimambi. Sasa mimi mtu namuuliza wewe unadhani hilo ni kosa la mwandishi? Kwa sababu mimi ninavyoona hilo siyo kosa la mwandishi hilo ni kosa la mtu aliyepanga picha na wabunifu na hii sheria haiwahusu. 

Siyo uandishi wa habari, siyo uandishi wa habari. Kwamba  hapa tuweke picha gani, hapa kwenye gazeti kikae kidude gani hiyo siyo kazi ya mwandishi. Mwandishi mimi naenda eneo la tukio naandika habari yangu kwa mhariri kazi imeisha. 

Jenerali Ulimwengu: Ndiyo, ni utashi kweli wa kudhibiti na awepo msajili. Kuna kitu kinaitwa msajili katika nchi hii kama kuna mambo ya kupigania sijui Katiba Mpya, lakini lazima pia kupigana vilevile ili wasajili wapungue. Kuna usajili kila mahali, naona hata wenza katika ndoa siku hizi  mtu akifanya matata nyumbani anaelezwa mbona unataka kuwa msajili hapa.  Hii kitu inaitwa msajili ni kitu cha ajabu sana sijui nani kakigundua. Kuna watu wana akili sana nchi hii. 

Khalifa Said: Mimi nadhani ni mawazo ya kikoloni. 
Jenerali Ulimwengu: Kuna mtu kaa akafikiri akasema tutakuja na msajili. Matatizo yetu tutayamaliza kwa msajili.      

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts