Huu ni mwendelezo wa mazungumzo kati ya Jenerali Ulimwengu na Khalifa Said ambaye ni Mhariri Mkuu wa The Chanzo. Katika mazungumzo haya Jenerali amempa nafasi Khalifa kumuuliza maswali juu ya uzoefu wake katika harakati na masuala binafsi ambayo, mtu yeyote anayemfahamu Jenerali Ulimwengu angependa ayajue.
Jenerali Ulimwengu: Nadhani kama ilivyo kawaida siku hizi ukimhoji mtu mwisho inabidi umuambie na wewe unalolote unataka kuniuliza?
Khalifa Said: Mimi kwa kweli kwanza niseme tu ni faraja sana kwangu kupata fursa hii ya kuzungumza na wewe. [Wewe] ni mtu ambaye nimekuwa nikikufuatilia kwa siku nyingi, ni mfano kwangu wa mtu ambaye natamani kuja kuwa, au I’m striving to be like you.
Nakumbuka licha ya kwamba nilishakuona kwa siku nyingi lakini nakumbuka kuna kipindi wakati nafanya kazi The Citizen, The Citizen ilikualika kuja kuzungumza na waandishi. Kwa hiyo na mimi nilikuwepo pale na ukatoa ushauri ambao mimi kusema ukweli siku zote umekuwa ukikaa kichwani mwangu. [Kipindi kile] bado nilikuwa ni mwandishi mchanga, najitafuta na ule ushauri kusema ukweli ulinisaidia kwa kiasi kikubwa sana.
Ulisema kwamba kazi ya mwandishi wa habari ni kusoma, ambayo ulisema lazima ifanyike mchana usome mchana uandike usiku. Na kusema ukweli nadhani ni ushauri ambao naweza nikasema ni timeless na nimekuwa nikiwahimiza pia waandishi wenzetu ambao wapo The Chanzo kwamba lazima usome mchana kutwa lakini kwamba kusoma inabidi kuchukue sehemu kubwa ya kazi yako kuliko kuandika. Kwa hiyo mimi nashukuru sana.
Lakini katika kukufuatilia nimegundua kwamba ni nadra sana kwako wewe kuzungumza kuhusu wewe, kuhusu wewe maisha yako binafsi.
Nakumbuka wakati unazindua kitabu chako cha Rai ya Jenerali Juzuu ya Tatu hapa hapa Mbezi Beach, Zitto Kabwe kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo alikuuliza sasa Jenerali unatuandikia tu haya mavitabu kuhusu siasa, kuhusu nini lakini vipi kuhusiana na kitabu chako kuhusu maisha yako wewe? Na wewe ukasema ukatoa jibu kwa ufupi ukasema mimi sijalishi [kwa kimombo] I don’t matter.
Nimekuwa nawaza huu ni uamuzi wa makusudi ambao umeamua kuuchukua au ni kwa vile tu hajapta au fursa haijajitokeza. Kwamba pengine ukialikwa kwenye kongamano unaalikwa kwenda kuzungumzia historia ya Katiba ya Tanzania, historia ya uandishi wa habari kwamba haijawahi kutokea ukapata hiyo fursa. Au ni uamuzi wewe umeuchukua kwamba mimi sitokuwa nazungumzia kuhusu maisha yangu binafsi kama mtu?
Jenerali Ulimwengu: Asante, ni swali zuri sana nilimjibu hivyo Zitto, Mheshimiwa Zitto Kabwe wakati wa uzinduzi wa Juzuu ya Tatu ya Rai ya Jenerali. Na ninaiamini kwa sababu nilivyokuwa bado kijana niliangalia mahojiano nadhani ilikuwa Algiers, alikuwa mtu mmoja anaitwa Kirk Douglas ni muigizaji mmoja mkubwa sana wa zama zile Hollywood. Akazungumza juu ya maisha yake na nini, mwishoni mwandishi akamuambia sasa hayo yote uliyozungumza ulivyonieleza toka umetoka Ulaya ya Mashariki ukaingia Ulaya ya Magharibi ukawa mashuhuri ukajulikana si ungeandika kwenye wasifu wako?
Akasema na silisahau jibu lake kwanza, [alisema] sitaandika wasifu wangu. Kwa sababu watu wengi ninaowajua mimi wameandika wasifu kwa kusema uongo. Halafu wale waliobahatika kuandika riwaya ndiyo wakaeleza maisha yao.
Inawezekana hata Mwalimu, Mwalimu [Julius Kambarage Nyerere, tumemzonga sana Nyerere. Hii miaka ya mwisho hii Mwalimu hujatuandikia wasifu wako na nini na kadhalika. Akasema akatoa majibu mbalimbali mojawapo ni mtaandika nyie, wataandika wengine na kadhalika.
Kishawishi cha kusema uongo kwenye kuandika wasifu ni kikubwa sana. Na ni kwa sababu tu mtu ambaye amefika umri kama wa kwangu mimi kukubali kuandika kwenye wasifu wake kwamba nilivyokuwa mdogo nilikuwa nikichapwa na mama yangu kwa sababu nilikuwa nakojoa kitandani kidogo kidogo ngumu. Tuna sanitize stori zetu.
Ukiangalia vitabu vilivyotoka hapo katika miaka michache iliyopita Tanzania, Kuna marais wastaafu wameandika vitabu wakasema uongo. Kwa bahati mbaya kwao sisi bado tunaishi. Lakini ikipita miaka mingine wao watakuwa wameondoka na watu wanaowajua vyema watakuwa wameondoka. Kwa hiyo, huo ndiyo utakuwa uongo watakaorithishwa watoto Watanzania, ambao ni uongo kabisa.
Kuna mambo yametokea hapa miaka ya 1990 na mtu anaandika kama vile sisi tulikuwa wadogo lakini siyo udogo wa kutojua. Mpaka tumeshiriki katika michakato mingine ya wakati huo lakini wameandika uongo kabisa. Sitaki kuwataja.
Khalifa Said: Ndiyo, kwa hiyo ni uamuzi wa makusudi umeuchukua.
Jenerali Ulimwengu: Ni uamuzi wa makusudi.
Khalifa Said: Lakini siyo kwamba huamini kwamba kama wengine wanafanya uamuzi wa makusudi wa kuandika uongo wewe unaweza ukachukua uamuzi wa makusudi ukaandika ukweli?
Jenerali Ulimwengu: Inawezekana lakini sitakuwa tofauti na binadamu wengine. Kupamba huwa inatokea inakuwa ni mshawasha mkubwa sana. Lakini sijasema kwamba sitaandika inawezekana nikapata nafasi nikaandika.
Khalifa Said: Hiyo ni habari njema.
Jenerali Ulimwengu: Nakuwa muangalifu nisiseme, nisipambe sana. Na mara nyingi nikiandika sasa hivi naandika kwenye The East African, nimeamua kusudi kutoandika nyumbani na niandike kwenye The East African. Sasa nilipewa ofa hiyo nyumbani naandika Twitter. Mara moja moja natoa mawazo yangu na kadhalika.
Katika baadhi ya maandiko yangu natoa wasifu wangu, ndiyo kusema kitu ambacho kinaeleleza maisha yangu. Sijafanya vya kutosha, kwa mfano sijapata mahali pa kuandika kwa nini mwaka 1993 niliomba kuacha kazi nikiwa mkuu wa wilaya. Sijaeleza vizuri na nimeona kuna mahala mjinga mmoja akasema alikuwa mkuu wa wilaya akatimuliwa.
Kama kutimuliwa unaomba kutimuliwa basi nilifanikisha kutimuliwa kwa kuomba. Hainisumbui sana. Lakini mimi nadhani kwamba ninachoandika katika mawazo ninayotoa katika mazungumzo kama haya hayo ni muhimu kuliko kujua.
Khalifa Said: Lakini siyo kwamba kuna hiyo haja ya rekebisha, kwa sababu kwa mfano leo upo hai mtu anaweza akazungumza uongo kuhusu wewe ukapata fursa ya kusema jamani huu ni uongo. Iko hivi na hivi na hivi. Hudhani kwamba ni muhimu kufanya hicho kitu kuweka rekodi sawa kwamba baadaye hata sisi wananchi [tunasema] hapana huo siyo [ukweli] kwenye kitabu chake amesema hivi.
Jenerali Ulimwengu: Mtu aliyezoea kusoma vitabu vya wasifu ambavyo vinasema uongo atasema hata hii uongo. Kwa mfano, nilikuwa nazungumza na watu kwenye kundi dogo tu, nikawa nawaeleza mapenzi yangu nimetoka kuangalia mpira juzi mechi ya mwisho ya Arsenal mimi maana yake ni mpenzi wa Arsenal, sasa nikawa nimewaambia mpira wa miguu nilivyokuwa napenda mpira wa miguu shuleni lakini siwezi kucheza.
Nimejaribu kweli kweli lakini kila wakipanga timu naambiwa wewe bwana kaa huku. Mwisho mwalimu wa michezo akaona kwamba nina ari kubwa sana ya kufuatilia mchezo huu. Akasema sasa nije nikufundishe utakuwa mwamuzi. Na nikawa mwamuzi wa shule. Nikaanza kuchezesha mechi za mabweni, nyumba kwa nyumba lakini baadaye nikawa sasa ni mwamuzi wa shule yangu na shule nyingine na mambo niliyoyapata kama uzoefu ya ujasiri ambao unatakiwa utumie wakati wa kupambana na hali ngumu.
Kwa mfano, timu yako, unachezesha mpira kati ya timu yako mwenyewe na timu ya shule jirani. Halafu mtu kanawa mpira, kashika kabisa mpira wazi wazi mbele ya goli upande wa timu yako unafanyaje? Unapiga filimbi ya penati wenzako wanataka kukunyonga wanataka kukuchinja kabisa lakini nasema hii ni penati na sibadilishi msimamo wangu na kadhalika. Mwisho mkuu wa shule anaingilia kusema kwamba asiyekubali hii penati iliyoamuliwa na mwamuzi basi aondoke na asirudi shuleni kwangu. Na hiyo ndiyo inakuwa salama yako wewe. Lakini mwishoni wanakubali wameshinda mwisho wa mechi unajua kwamba tulijua tumefanya kosa lakini hatukuamini kwamba wewe unaweza kutuadhibu [kama] ulivyotuadhibu. Ni mambo kama hayo.
Nikiyaandika sasa hivi watu watasema muongo. Na ubaya wake nini, nadhani katika watu waliokuwa wanacheza katika mechi ile nawajua na naweza kuwagusa ni mmoja tu naye ni mgonjwa kila siku yuko Muhimbili, [kufanyiwa] dialysis na vitu kama hivyo.
Kwa hiyo inakuwa ni ngumu na riwaya itaaminika vizuri kuliko hata huo wasifu. Watu wanasema huyu bwana ana mawazo makubwa sana kumbe ni habari yako. Kwa hiyo, kwa kweli siahidi kwamba nitaandika wasifu wangu lakini nikipata nafasi nitafanya hivyo. Na inawezekana mtu akajitokeza akasema embu tuzungumze nikurekodi halafu nitakupa uhakiki nilichoandika.
Hiyo siikatai kikanuni, isipokuwa naona thamani ya wasifu huo ni ndogo sana. Lakini masuala mahususi kwa mfano mtu akiniuliza nitamjibu tu.
Khalifa Said: Natafuta neno sahihi au tafsiri sahihi ya kiswahili ya consistency lakini nashindwa. Na nilikuwa nataka kufahamu wewe kwa ninavyokufahamu mimi kwa sababu lazima niseme hivyo, umekuwa very consistent kwenye mapambano haya ya kupigania haki, jamii yenye usawa, uwajibikaji, demokrasia [na] utawala bora. Ni vitu ambavyo umekuwa ukivifanya mara kwa mara kwa miaka yote hii ambacho kusema kweli ni kitu si wengi wanaweza kufanya hivyo.
Wewe umemudu vipi hii consistence, kwamba Jenerali wa miaka ya 1970 kwa vile ninavyofahamu japo sikuwepo [miaka hiyo], kwa mfano hapo umezungumza kujiuzulu kwako kama mkuu wa wilaya na harakati zako zingine bado unaendelea kusimamia misingi ile ile. Kunaweza kuwa kuna mabadiliko ya hapa na pale lakini zile kanuni za msingi ambazo umekuwa ukiziamnini miaka yote umeendelea kuziamini na kuzipigania, umemudu vipi?
Jenerali Ulimwengu: Hilo ni swali rahisi sana, nimemudu vipi ni kwa sababu sina ujanja. Mimi si mtu mjanja na akili yangu ni akili ya kawaida sana. Nikijifanya kubadilisha badilisha misimamo nitasahau juzi nilikuwa nafikiria nini na jana nilikuwa nafikiria nini nikijifanya nabadilisha badilisha. Kwa hiyo, ni rahisi kwangu mimi kubaki hivyo hivyo nilivyo.
Kwanza tuambizane ukweli juu ya jambo muhimu katika maisha. Binadamu katika jamii ya kawaida labda apate misukosuko mikali sana tetemeko la ardhi zito sana. Baada ya umri fulani watalaamu wanasema binadamu huwa akishakamilika anakuwa ni mtu wa aina fulani na ataendelea hivyo mpaka anazeeka anakufa. Kama alikuwa ni mdokozi mdokozi wa nyama jikoni kwa mama yake ndiyo huyo wa BoT au wa kwenye Wizara ya Fedha anaiba mahela mengi ambayo CAG anaandika kila siku.
Ukimuangalia nyuma kule alivyokuwa na [umri wa] miaka minne mitano alikuwa mama akiacha chungu kina nyama anadokoa na hakupata namna ya kurekebishwa wakati ule. Kwa hiyo, akaendelea na tabia hiyo alivyokwenda shuleni alikuwa ni mtu wa kuiba chai ya wenzake na kadhalika sasa yuko Serikalini na amepata nafasi ya kuiba kutoka hazina au benki kuu na kadhalika. Kwa hiyo watu hawabadiliki.
Mimi nawajua watu ambao wana umri karibu na wa kwangu miaka 70 na kitu ambao tangu tumekutana tukiwa na [umri wa] miaka saba hawajabadilika na wanakufa wakiwa vilevile.
Khalifa Said: Lakini wapo watu wanabadilika.
Jenerali Ulimwengu: Nakuambia kama msukosuko mkubwa sana umepata maishani.
Khalifa Said: Lakini tumeona hapa Jenerali Ulimwengu bwana, wewe ulikuwepo unaona watu sitaki kutaja majina kama wewe ambavyo hujataja majina lakini walikuwepo watu ambao hapo zamani walikuwa na misimamo hii, kikatokea hiki wakaja.
Jenerali Ulimwengu: Zamani hawakuwa na misimamo yoyote iliyobadilika. Ni kwamba hata huko walikokuwa walibadilika badilika. Kwa hiyo tabia ya kubadilika badilika haijabadilika. Ile tabia ya kubadilika badilika ili kujiingiza kwenye hali njema zaidi ili apate faida fulani kuwazidi wenzake hiyo haijabadilika.
Ndiyo hao ndiyo anaweza kuwa kwenye, kwa mfano akaapa kwamba mimi nitakufa niko ndani ya Chama Cha Mapinduzi halafu wiki tatu baadaye anakwenda NCCR au CHADEMA na kadhalika. Halafu baada ya miaka miwili anarudi tena [kwenye] hiki chama alichokuwa anasema hakifai na kadhalika. Lakini ule uzabizabina haujabadilika tangu akiwa na miaka saba. Na uangalie vizuri wewe bado ni mdogo kwa umri, angalia watu, ulisoma wapi Zanzibar?
Khalifa Said: Pemba.
Jenerali Ulimwengu: Hebu waangalie watu uliokuwa nao walivyokuwa na miaka saba na uwaangalie watakuwa na miaka na miaka 30 na kitu. Waangalie kama wamebadilika tangu ile Pemba unavyomkumbuka Pemba kule na leo hii utaona ni mtu yule yule kama muongo muongo [ni] muongo, kama mtu wa ukweli wa ukweli.
Kuna wale watu ambao nilikuwa juu ya mpira hapa, chandimu [wakati] mko watoto 10 kwa hiyo mnagawana watano watano. Ni ndiki ndikiki tulikuwa tunasema sisi. Ndiki ndikiki ni Khalifa ndi Jenerali, mnagawana hivyo halafu mnajikuta hamna mwamuzi. Inabidi mmoja wenu katika wale 10 awe mwamuzi na anacheza. Utaona kwamba kuna mtu mmoja kila mnapokutana wenzake watasema wewe kuwa mwamuzi, pamoja na kwamba unacheza upande huo lakini kuwa mwamuzi, kwa sababu wewe ni mkweli unapenda haki.
Wote hao ukiwakuta leo ni majaji au mahakimu watakuwa wanatenda haki. Lakini wa uhakimu wa kwenda kusoma sheria Mlimani na kupata degree ya LLB halafu unakuwa hakimu kama ulikuwa mwizi utaendelea kuwa mwizi na mla rushwa katika mahakama. Kwa sababu ile ndani yako hakuna ule moyo wa kutoa haki.
Kwa hiyo, mimi tuseme ni kwamba ndivyo nilivyo. Unajua kusema uongo na kujibadilisha na kujipindua pindua yahitaji akili kubwa sana, ni kazi. Inahitaji akili na uongo uliosema jana uukumbuke basi leo ni kazi kubwa sana. Ni kazi kubwa sasa uongo kama mwingine huo unauacha katika wanasema uongo mtakatifu inapobidi kabisa kusema uongo sema uongo kujiokoa nafasi yako lakini isiwe ndiyo tabia yako. Kwamba yule bwana muongo yule.
Khalifa Said: Kwa mfano, najua ni kitu ambacho hakiwezekani lakini kwa mfano ingetokea ungepata fursa ya kuanza maisha yako upya ungechagua maisha ambayo umeyaishi au kuna kitu ungebadilisha?
Jenerali Ulimwengu: Ningechagua maisha niliyoyaishi kwa sababu nimekuwa na maisha mazuri sana. Si hakuna mtu anayeweza kusema nakudai uliiba kitu changu. Ni bahati nzuri kwa baba yangu, marehemu baba yangu na mama yangu walikuwa ni watu wa namna hiyo. Baba yangu alikuwa ni Muislamu wa kweli kwa maana ya Uislamu ule wa kupenda kutenda haki.
Na nimepata misukosuko mara nyingi lakini nisingeweza kubadilisha nafasi yangu na mtu mwingine ili kuepuka hiyo misukosuko. Kwa sababu hii misukosuko imenikuza vilevile. Na mara nyingi nasema kwamba bila kuwa na misukosuko utakuwa wewe ni nani? Ni mchawi au ni nini? Nini kinakufanya usiwe na misukosuko? Na kama unasimamia unaloamini kwamba ni kweli.
Katika maisha yangu ya hivi karibuni msukosuko mkubwa nilioupata na familia yangu ikatisika kidogo ilikuwa ni masuala ya uraia na ikanifundisha vitu fulani fulani. Moja nani marafiki zako? Pili nani watu waongo? Tatu unaweza kumuamini nani na nani huwezi kumuamini? Na kadhalika. Lakini vilevile kuonyesha uongo wa watu fulani fulani.
Tatizo limeanza kwa sababu The African na Rai limemwandika waziri wa Mkapa mwizi. Na tukasema huyu mtu ambaye amepewa ofisi ya kusimamia utawala bora huyu ni mwizi ushahidi huu. Bwana Mkapa akapata tabu sana akaniletea ujumbe kwamba huyu ni waziri anafanya kazi nzuri nikaambia sawa labda anafanya kazi nzuri kwa uwaziri uliompa lakini huyu bwana ni mwizi nakupa ushahidi ni huu.
Na tumefanya ushahidi kwa kutafuta taarifa maana yake tumezungumza juu ya uandishi wa habari. Mara nyingi unaanza kwa kusikia uvumi, tetesi unasema hii tetesi kama ni kweli ni muhimu hii na unaifuatilia. Unakwenda unatafuta nyaraka na kweli ukipata watu wanaokujua unawauliza maswali na kadhalika na sisi tumepata hizo taarifa kwamba hospitali zinazosema kwamba mke wa huyu bwana alitibiwa wanamkana kwa kuzungumza nao na kwa gharama zetu. Na wala siyo Mimi ni watu waliokuwa chini ya uongozi wangu. Lakini bwana Mkapa akakataa kabisa huyu mtu tunamsingizia.
Tunafanya kampeni sasa kama huyu hajiuzulu basi tuambie wewe tuzungumze juu ya kuwa na Serikali safi maana yake nini? Huyu tumemkamata tumekukamatia sisi, wewe wala hukumkamata halafu unakataa nini asijizulu? Tukakaa naye mpaka amejiuzulu. Nikapata matatizo ya uraia.
Sasa hivi nizungumze suala la uraia. Tatizo siyo kwamba nilinyang’anywa uraia, nilifutiwa uraia. Ni kwamba tulipoamua sote, tulikuwa watu wanne, ilivyoamuliwa sasa sisi wanne tutaomba sasa Uraia wa asili kilicholeta vurumai yote ni kwamba wale wengine wakati walipewa uraia mimi nikanyimwa na ni kwa sababu hiyo. Kwa sababu yule waziri tulikuwa tumemfanya ajiuzulu ndiyo alikuwa anasimamia, zamani kachero, mkubwa wa Serikali nakadhalika.
Kwa hiyo ikanichukua kama miaka miwili sina pasipoti, nasafiri na karatasi za dharura, nyaraka za kusafiria na nini. Nikaenda duniani nikiwa na karatasi kama maelezo ya dawa na nini, lakini ilifanya nini? Kwanza ilinionyesha marafiki zangu ni wa kina nani, wale waliokuja na kusema kwamba bwana tulikufanya hivi na hivi, usigombane na Serikali, tafuta tu uraia inawezekana kwamba wazazi wako kweli hawakuzaliwa hapa na nini.
Kwa wazazi wangu nisingeweza kuwa na uhakika kwa sababu na wao wameshaondoka wakati huo.
Khalifa Said: Lakini ulizaliwa Tanzania?
Jenerali Ulimwengu: Ndiyo. Sasa nini imetokea, baada ya kuwa nimetoka na baadaye ikabidi tu wanipe uraia wa asili imenifanya mtu huru kabisa. Mtu huru kabisa hakuna mtu anaweza kunambia tulifanya hivi na hivi na tuonee huruma hasa wale watu ambao niliwaona kama ni watu wa hovyo, ilinipa uhuru mkubwa sana wa kufanya kazi yangu bila woga. Kwa hiyo sidhani kama ninaweza nikabadilisha maisha.
Kuna watu ambao nisingewaunga mkono sasa kwa sababu nawajua kwamba ni wazandiki hiyo ingekuwa ni kweli. Kwamba sasa hiyo binadamu hatupewi fursa ya namna hiyo kwamba urejee nyuma halafu uanze tena.
Khalifa Said: Lakini kitu ambacho cha msingi ni kwamba unajivunia maisha ambayo umeyaishi.
Jenerali Ulimwengu: Sana na katika umri huu nashukuru sana kwamba nimepata maisha, nimekuwa na afya njema. Miaka 75 sasa nimekuwa na afya njema nimekuwa na kwa kweli nimepata kutambuliwa na wenzangu kila nilikokwenda kila shule zote kote nimepita nimetambuliwa na wenzangu na mimi nimetoa mchango wangu kiasi nilichoweza. Si haba.
Khalifa Said: Jenerali kwenye maisha haya hususan haya ya kupigania haki, jamii yenye usawa na mabadiliko mengine chanya kwenye jamii yetu ni maisha ambayo ni rahisi sana kukata tamaa. Kwa sababu kama ambavyo unajua mabadiliko hayaji kwa uharaka ule ambao sisi tungependa kuona. Ni sababu gani ni nini ambacho kimekuwa kikikupa matumaini ya kuendelea, ya kutokukata tamaa, ya kwamba hiki kitu kinawezekana kama siyo leo kesho, mwakani. Nini kimekuwa kikikusukuma?
Jenerali Ulimwengu: Ni kuepukana na kujitenga, ukiwa unatafuta mshikamano na watu wanaopigania haki utawapata tu. Kama huwatafuti, wala huwataki, wala huwahitaji, wala huoni umuhimu wao hutowasikia. Lakini kama mwelekeo wako ni huo utawasikia. Kila siku unakwenda kwenye mikutano ya kawaida unasikiliza watu wanavyozungumza, unaweza ukasema yule bwana au yule mama anayezungumza pale nadhani kwamba ana kitu ambacho ningependa kukijua zaidi kwa hiyo unamtafuta.
Katika uzee wangu ni majuzi tu nimemgundua mtu anaitwa Deus Rweyemamu. Mdogo sana kwa umri mtoto wangu kwa umri. Lakini wewe jiulize mimi na Deus Rweyemamu tumekutana wapi? Haiwezekani kuwa shuleni haikuwa kijijini maana yake mwenyewe hajaishi sana Bukoba na mimi Bukoba nilishaondoka zamani na kadhalika. Lakini kwamba unafika mahali katika hafla hizi tunazokuwa tunakwenda nawasikiliza watu wanavyozungumza na mtatambuana. Kuna mtu atakuambia bwana kuna hiki na hiki na hiki. Unadhani unaweza ukasaidia kufanya hiki, hiki na hiki kwa misingi ipi basi tumeanza.
Center for Strategic Litigation Tanzania imeanza kwa misingi hiyo, bila hivyo nisingemfahamu Deus na hata wengine akina Fatma Karume nimekuja kuwafahamu kwa sababu, ndiyo nilikuwa namfahamu juu juu lakini kumjua vizuri ni katika kazi kama hiyo. Wapo kama unatafuta kitu fulani, kama unatafuta genge la wezi kwenye mazungumzo utajua wale wezi wale. Kwa hiyo nijiunge nao au niwakimbie niwaepuke. Usikate tamaa, usikate tamaa. Nafikiri kukata tamaa ndiyo hali ya kuelekea kifo.
Khalifa Said: Sawa sawa. Na ulizungumza pale mwanzo kuhusiana na masuala ya uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza. Wewe eneo lako kubwa yapo mengine, lakini eneo lako kubwa ambalo umekuwa ukilitumia kuchochea haya mabadiliko unayotaka kuyaona.
Jenerali Ulimwengu: Unaniambia ni mchochezi?
Khalifa Said: Hapana, kusukuma, kusukuma, ni kusema kwamba ndiyo kama hivi unaongea na sisi waandishi wa habari. Utaalikwa kwenye makongamano, kwenye warsha unasema au utasema pengine kupitia kalamu kwenye makala unaandika umesema The East Africa. Na nilikuwa nataka kukuuliza unadhani kama taifa, unadhani sisi tumeng’amua umuhimu wa hii dhana nzima uhuru wa kujieleza, uhuru wa kusema na unadhani kwa nini muhimu kwa watu kuwa huru kusema maoni yao, hisia zao na mawazo yao?
Jenerali Ulimwengu: Swali la kwanza kwamba tumeing’amua, tumeikamata vizuri tumeielewa? Bado bado. Lakini si mbaya wako wachache wameing’amua hiyo. Na mambo mengi nadhani Shaaban Robert aliandika katika [kitabu cha ] Kusadika. Mambo mengi ya heri hayahitaji sherehe kufanyika wala hayasubiri watu wakusanyike wengi.
Hutokea watu wawili watatu wakaanzisha kitu na hicho kitu kikawa na mvuto mdogo kwa watu wa wakati ule lakini baadaye kikakua na kuwa kitu adhimu na kikashangiliwa sana kinapofanikiwa. Kinapofanikiwa ndiyo kunakuwa na sherehe kubwa na kila mtu anakuwa ni shujaa maana yake na yeye aliona.
Lakini wakati ule wa kuanza mnaweza mkajihisi kama vile mmetengwa hamna maana watu waona mbona watu wapuuzi wapuuzi. Kwa mfano huwa na sema na nalirudia sana hili katika msukumo wa kuleta mabadiliko ya kifikira za kisiasa, kuna mtu mmoja hapa nchini huwa hatajwi sana, wanatajwa wengine kwa kweli, Maalim Seif anatajwa sana na wengine waliotangulia mbele ya haki.
Lakini kuna mtu anaitwa James Mapalala, James Mapalala ndiyo mtu ninayemjua mimi na anajulikana katika nyaraka za kihistoria aliyewahi kumuambia Julius Nyerere akiwa ni Rais kwamba, bwana sasa mimi nataka kuanzisha chama cha siasa kupingana na chama chako. Na kwa kusema hivyo tu na alimuandikia barua kabisa. Na kwa kusema hivyo akaondolewa akapelekwa sijui Mafia. Visiwani visiwani wala siyo Unguja, Mafia. Angalau Unguja kuna mji kidogo. Sasa mtu kama James Mapalala baadaye wamekuja wengine watu wakajitokeza wakaanzisha vyama vyao. Akina nani, akina Mrema akina Malando akina nani na kadhalika. Lakini mara nyingi tunamsahau sana James Mapalala.
Huyu ndiyo mtu ambaye alichukua ujasiri wa kumuandikia Nyerere na Nyerere alikuwa Nyerere wa kweli kweli siyo mchezo na alikuwa ameshaamua kwamba hakuna vyama vya siasa na hata Magufuli alivyokuja baadaye alikuwa anamtolea mfano sana Nyerere. Kwani Nyerere mbona alikataa hivi vyama vya siasa si alikuja kubadilika mwaka 1992 anasema hivyo Magufuli.
Kwa hiyo kung’amua ile bado. Lakini uchache wa watu ambao wanaamini katika uhuru wa watu wa binadamu, uhuru wa jamii usitufanye tudhani kwamba hizi dhana hazina maana.
Kuna watu wengi wanaamini vitu vya kijinga kijinga tu wengi sana. Halaiki kubwa sana ya Watanzania mimi nawajua ni washirikina wanaamini mtu anaweza akatoka Sumbawanga amepanda kwenye ungo akaenda akadondoka Pemba. Hivyo wanaamini watu wengi sana. Lakini sitajiruhusu mimi kuwa pamoja na hao.
Pamoja ni kwamba ni wengi wabaki na wingi waoa lakini najua kwamba ni wapumbavu ni mazuzu na wabaki hivyo hivyo. Unajizuia tu usije ukaambia hadharani wakaja wakakupiga mawe. Lakini usiogope kwa sababu anzisha kitu chako, anzisha kitu chako.
Tulivyoanzisha magazeti ya Rai wakati ule Mimi ndiyo nilikuwa tajiri wa kundi lote lile. Akina Rweyemamu mimi nilikuwa na shilingi 300,000 mfukoni nimetoka bungeni nilikuwa bungeni wakati ule mimi ndiyo tajiri. Nikaja kujifunza kwamba siyo hiyo tu uandishi, uanahabari mahiri tulikuwa makini sana, tulikataa hata kuandika maneno kama Bongo katika dimba tulianza na gazeti la michezo lakini tukapiga marufuku kuita nchi yetu Bongo.
Na kweli ukienda kuangalia miaka ile ya Dimba hakukuwepo na neno bongo, bongoland na nini. Ilikuwa ni michezo lakini kwa umakini. Kwa hiyo tukaanza baada ya muda tukapata mrejesho mzuri. Mbaya ni kwamba tulikuwa hatuna uwezo wa kibiashara, hata kufanya biashara ilikuwa ni ngumu na tukapata matatizo baadaye lakini katika miaka ile michache tuliofanya kazi tukaweza kufundisha vijana wazuri sana. Mpaka leo nawaona wakifanya kazi nasema hawa ndiyo ushuhuda wa nini tumefanya katika miaka ile ya kukazana na kupata matatizo makubwa ya kuvutana na Serikali kushoto kulia lakini tunasimamia ukweli.
Na matokeo yake ni kwamba hatujawahi hata siku moja kushindwa kesi hata moja ya ingawaje tuliwaandika watu kweli kweli. Tuliwaandika watu kweli kweli lakini misingi ni ile ile unasikia uvumi kwanza, unatafuta habari ya ukweli ukishaipata ile taarifa unamuendea muhusika. Tuna habari hizi kuhusu wewe unasemaje? Na vijana wetu walikuwa wanaambiwa ukienda muoneshe ulichokuwa nacho akikufungulia mbwa ukang’atwa ni sehemu ya habari. Sawa sawa. Tutakupeleka hospitali lakini stori inakuwa ni nzuri zaidi.
Khalifa Said: Ni kitu gani ulikuja kukigundua baadaye sana kwenye maisha yako ambacho ungetamani ungekijua mapema sana.
Jenerali Ulimwengu: Kama tunazeeka sote na mtu anasema tunazeeka haraka sana halafu na tunakuwa wajanja tushachelewa. Mwishoni ndiyo unaanza kuwa mjanja lakini kuzeeka umeanza kuzeeka mapema. Labda ningejifunza biashara nilivyokuwa mdogo, kuna vijana wamekwenda Chuo Kikuu wakifanya biashara. Nilikuwa nazungumza nao hapa. Wengine walikuja baadaye chuoni baada ya mimi kuondoka. Wengine unakuta mtu anakuambia mimi nilikuwa na mashine ya kuchapishia karatasi, nilikuwa na nini na nini nawauzia wanafunzi wenzangu na ndivyo hivyo nimepata hela yangu ya maisha pale chuoni.
Sijawahi kuwa na ile karama ya biashara naweza nikanunua kitu kwa shilingi 10 akinipa mtu shilingi tano nitampa. Kwa hiyo bado sijapata.
Khalifa Said: Lakini si kitu unachojutia?
Jenerali Ulimwengu: Sijutii sana, sijutii sana kwa sababu dunia imekuwa karimu kwangu kwamba nimepewa misaada usaidizi mkubwa sana na watu ambao wana uwezo mkubwa wa kifedha kuliko mimi. Wengineo ni wafanyabiashara ambao pamoja na kwamba sijawafanyia kazi yoyote lakini wamekuwa wana utayari wa kusaidia pale ninapata matatizo na kadhalika.
Lakini kwa kweli sidhani kama kuna kitu muhimu ambacho ningenaweza nikasema ningerudi utotoni ningependa nibadilishe mwelekeo wangu. Nadhani mwelekeo niliochukua nikiwa mtoto mdogo wa kupenda haki, wa kutetea haki, wa kusimama kwa haki, wa kusema ukweli na kuona kwamba kweli na kutowaogopa wenye nguvu. Sijapata kuogopa mtu kwa sababu tu ana mabavu au anaonea watu na pale nilipoweza kusema nimesema.
Khalifa Said: Kifo si kitu kizuri cha kukizungumzia.
Jenerali Ulimwengu: Ila lazima ukizungumzie. Kifo lazima ukizungumzie kwa sababu hicho ndiyo jambo moja katika nchi zilizotengama sawa sawa kifo na kodi lazima, hiyo ni uhakika.
Khalifa Said: Lakini ndiyo hivyo kama uvyosema ni kitu cha uhakika lazima tutakikuta tutake tusitake. Safari yako ikifikia mwisho kwa mfano ungependa labda dunia imkumbuke Jenerali Ulimwengu kama mtu gani?.
Jenerali Ulimwengu: Mtu wa kawaida tu. Mtu wa kawaida aliyefanya alichoweza ambaye hakuwa na ubunifu mkubwa sana ila tu aliishi kama alivyojihisi yeye mwenyewe na aliyekubali kwamba muhimu kuliko yote ni utu wa mtu wala siyo mali. Sidhani kama nina kitu nilichokipata duniani na heshima niliyoipata duniani haikutokana na uwezo wangu wa kifedha au wa mali na kadhalika. Ilikuwa ni watu kunikubali kama nilivyo na wengi wanajua nina madhaifu yangu, lakini wamenichukulia hivyo.
Kwamba hata pale nilipokuwa na madhaifu sikufanya hayo mambo yanaonyesha madhaifu yangu makusudi ni basi tu ndivyo nilivyo. Ni kama wewe umezaliwa ni mbwa utabweka tu, kama ni jogoo utawika.
Khalifa Said: Pale mwanzo wakati tunazungumzia suala la uraia ulizungumzia matokeo, kile kilichofuata nini kilikufundisha. Lakini kwa maisha kiujumla unadhani yamekufundisha nini?
Jenerali Ulimwengu: Yamenifundisha kwamba unaweza ukapata matatizo ambayo siyo wewe iliyoyasababisha lakini yakawa matatizo kweli. Kuna watu nilikuwa kuna mtu anaitwa Kihomano Mkurugenzi wa Uhamiaji aliniita ofisini [kwake] alikuwa anajaribu kuwa mtu mkarimu sana unajua bwana ni hivi nikufundishe kitu.
Nikamuambia, Kihomano sikiliza tuambizane ukweli umepewa maagizo na wakuu Serikalini uchukue pasipoti yangu. Usiniambie wewe Kihomano ninayekuona hapo kwamba wewe una ubavu wa kunitangaza mimi kuwa siyo raia wa nchini hii, huna. Sikudharau lakini nakuambia huna. Umepewa maagizo tumalize basi hii shughuli niambie unanipeleka mpaka wapi? [Akasema] hapana bwana. Halafu watu waongo hawezi haya kusema ni kweli nimepewa maagizo. Yaani kama vile walikuwa wanafanya msako wakanikuta niko Mbezi Beach nimejibanza mahali nimejificha kama mhamiaji haramu, nikamuambia Kihomano huna hiyo, huo ubavu huna nakuambia. Sema tu ni kwamba umepewa [maagizo].
Na kweli baadaye si imekuja tu nikaitwa na Mapuri alikuwa waziri pale, unajua bwana wakati ule kulikuwa na kiwingu fulani cha kisiasa sasa kiwingu hicho kimeondoka. Ni maisha unajifunza.
Khalifa Said: Unaridhika sasa hivi na mwelekeo wa nchi inavyokwenda?
Jenerali Ulimwengu: Katika masuala mengine ndiyo, katika masuala mengine sijaridhishwa bado. Kwanza nadhani tatizo la kujadili mustakabali wa nchi hii hatulichukulii kwa uzito wake. Naona kama kuna watu wanacheza mechi, lakini hatuliangalii suala hili kwamba ni suala muhimu sana.
Na nilikuwa nawaambia watu Tanzania ina utulivu, ina mambo yanayotokea chokochoko ya hapa na pale lakini kimsingi kiujumla kuna utulivu. Na mimi huwa nasema unapokuwa una afya njema, ukaamka asubuhi unajisikia u’mzima wa afya ndiyo wakati wa kumpigia General Practitioner (GP) kumuambia nataka kukuona, akikuuliza unaumwa? Unamuambia hapana afya yangu [iko] safi kabisa nataka uniangalie ili afya yangu iendelee hivi hivi kwa muda mrefu.
Akuambie kama sigara acha, vuta sigara kama pombe acha kama hii acha, mazoezi fanya na kadhalika. Huyo ndiyo mtu mwenye akili, una afya timamu unajisikia vizuri kabisa unampigia GP kumuuliza nini ufanye ili hii hali iendelee kwa muda mrefu. Ukisubiri ukawa umelala kitandani jasho linakutoka homa imepanda na kadhalika msichana wa kazi nyumbani ndiyo atakuwa daktari wako. Maana yake atakuambia kwetu kule Singida bibi yangu huu ugonjwa mimi naujua mimi.
Sasa Tanzania isisubiri mpaka ikawa imelala mahututi kitandani. Hivi sasa hivi bado tuna afya tunatembea na nini ndiyo pahala pa kuweza kuangalia nini kinaweza kutuathiri huko mbele ya safari? Kwa hiyo watu wanasema Katiba Mpya wala hawakosei kama ulivyosema si mwarobaini lakini ni vizuri basi uangalie katika mazingira yako nini unaweza kuboresha?
Hata mimi leo nina miaka 75 ningepata nafasi ya kujiboresha mimi mbona ningejiumba vizuri nikawa mrefu zaidi kuliko nilivyo. Nikawa shababi nimependeza na kila wana wa kike wakiniona wanavutiwa na kadhalika, ningeongeza akili kidogo. Sasa tuvyopata hiyo nafasi basi embu tujaze uzuri kidogo, tuongeze akili kidogo, tuongeze mambo mema na tupunguze mambo ya hovyo. Maana yake yako mambo ya hovyo mengi sana yanafanyika, mengi sana.
One Response
Nashkuru nimesoma makala hii na pia nilibahatika kutizama majadiliano haya kupitia channel ya THE CHANZO.
Nimefurahishwa sana na majibu mazuri ya Jenerali kwa kila swali alilokua anaulizwa. Tutaendelea kujifunza zaidi, kongole kwako Jenerali, uishi miaka mingi