The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tuwape Geita Gold Mining Jina la Mnyama, Wao Watupe Gawio la Faida

Ikiwa makampuni mengine ya madini yameingia ubia na Serikali kuunda kampuni za pamoja, na hivyo kuiwezesha Serikali kupata gawio, kwa nini isiwe GGML?

subscribe to our newsletter!

Machi 21, 2024, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alikuwa mgeni rasmi pale Dodoma Hotel, mjini Dodoma, wakati Tume ya Madini ikikabidhi leseni ya uchimbaji mkubwa wa madini kwa kampuni ya Nyati Heavy Minerals Sands Ltd, na pia leseni ya usafishaji wa madini kwa kampuni ya Tembo Nickel Refinery Ltd.

Binafsi niliguswa sana na majina ya makampuni, huyu Nyati, yule Tembo, wote wana majina ya mnyama pori. Nikajiuliza, mbona Geita Gold Mining Limited (GGML) hawana jina la mnyama? Nikatamani kutoa maoni yangu kwa umma.

Ili kuyaelewa majina ya wanyama, turudi nyuma kidogo. Kabla ya mwaka 2017 kulikuwako na malalamiko mengi kuwa Watanzania hawanufaiki vya kutosha na madini yao, tume zikaundwa, mapendekezo yakatolewa, mojawapo ikiwa ni Serikali kumiliki hisa za makampuni ya madini.

Katika kutekeleza mapendekezo hayo, zikatungwa sheria, mfano, kifungu Nambari 10 cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010, kikarekebishwa. Kwa muongozo wa kifungu hicho, Serikali na mwekezaji, yaani mchimbaji mkubwa ama wa kati, wanapaswa kuingia kwenye ubia, ambapo hisa za Serikali, za bila malipo na zisizofifishwa, hazipaswi kupungua asilimia 16, zinazosalia ni za mwekezaji. 

Kila kampuni ya madini unayoijua nchini ikiwa na jina la mnyama, ni matokeo ya ubia wa aina hii kati ya mwekezaji na Serikali.

SOMA ZAIDI: Utata Leseni Ya Uchimbaji Madini Serengeti Kwenye Maeneo ya Wananchi. Afisa Adai Sio Lazima Kuwashirikisha

Utaratibu huu unayahusu pia makampuni yaliyokuwepo kabla ya marekebisho ya sheria, ndiyo maana kampuni kama vile Barrick Gold Corporation, iliingia ubia na Serikali kwa kuunda kampuni iitwayo Twiga Minerals Corporation, inayomilikiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 16, na mwekezaji Barrick Gold Corporation kwa asilimia 84. 

Kufuatia marekebisho hayo ya sheria, leseni za uchimbaji hazitolewi kwa kampuni za kigeni zinazokuja kuwekeza nchini, bali kwa kampuni ya ubia kati ya mwekezaji na Serikali, ndiyo maana leseni zilizotolewa Machi 21, 2024, pale Dodoma zimetolewa kwa kampuni ya Nyati na Tembo, siyo kampuni zao zenye majina ya kigeni. 

Kwa nini nimeeleza yote hayo? Ni kwa sababu kila mwenye kupenda habari za madini anajua kuwa mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML) ndiyo mgodi mkubwa zaidi hapa nchini. 

Hatuioni GGML?

Hata hivyo, wengi hatujui kwa nini Serikali na GGML hawajaingia ubia na kuunda kampuni ya pamoja ambapo Serikali itamiliki angalau asilimia 16 ya hisa na kupewa gawio la faida. Wakati Serikali inaingia kwenye ubia uliounda makampuni kama Twiga, Tembo, Nyati, Mamba na Kudu, je, haikuiona GGML? 

Kwa kutoingia ubia na GGML, siyo tu Serikali inajikosesha fursa ya kushiriki kikamilifu kwenye sekta ya madini, bali pia inawanyima Watanzania mapato ambayo ingeyapata kama gawio la faida, mapato ambayo yangetumika kuwaletea wananchi maendeleo. 

SOMA ZAIDI: Mawaziri Madini, Nishati na Viwanda Kikaangoni, Waelezea Miradi ya Kimkakati

Nchi yetu inaamini kwenye utawala wa sheria. Profesa Issa Shivji, mmoja kat ya wanazuoni wanaoheshimika hapa nchini, amewahi kuandika kuwa utawala wa sheria siyo tu kuiacha sheria iongoze bali ni kuwa na sheria inayowaweka wote kwenye mizania ya usawa.

Kwa maneno mengine, utawala wa sheria hauna maana ikiwa kuna watu wako juu huku wengine wakiwa chini ya sheria. Ikiwa makampuni mengine ya madini yameingia ubia na Serikali kuunda kampuni za pamoja, kwa nini isiwe GGML? 

Twende kwenye nambari na mifano. Kwa mwaka wa fedha 2019/2020, kampuni ya Twiga Minerals Corporation ilitoa gawio la Shilingi bilioni 100 kwa Serikali, na kwa mwaka 2022/2023 kampuni hiyo ilitoa gawio la Shilingi bilioni 84 kwa Serikali. Ikiwa makampuni mengine yanatoa gawio kwa Serikali, kwa nini isiwe GGML?  

Ni dhahiri kuwa kama Serikali ingekuwa na ubia na GGML ingemiliki angalau asilimia 16 ya hisa za kampuni ya ubia, na ingepata gawio kila mwaka. Sheria inayoipa Serikali haki ya kupata hisa na gawio kutoka kwa makampuni ya madini ilitungwa mwaka 2017, miaka saba iliyopita. Kwa kila siku moja ambayo Serikali inakawia kuingia kwenye ubia na GGML, inachelewa kupata mabilioni ya gawio la fedha. 

“Wakati mwingine tunakimbizana na masikini kuwadai kodi, tunaacha hii kodi hapa tumepewa na Mungu,” aliwahi kusema hayati Rais John Magufuli. Bahati mbaya sana, hata wakati wa urais wake, Serikali haikuingia ubia na GGML.  

SOMA ZAIDI: Maafisa Waandamizi wa Serikali Wadaiwa Kuhongwa Mabilioni ya Fedha na Iliyokuwa Acacia

Hata hivyo, hoja ya Rais Magufuli ni sasa, kwa nini tuwakimbize masikini kuwadai kodi wakati tuna hela zetu ziko pale GGML? Na tusipoenda kuzifuata, GGML watawagawia wanahisa walioko ughaibuni, kama wanavyofanya siku zote. 

Inafaa nini kuwaambia Watanzania kuwa madini ni mali yao ikiwa tunaacha pesa ya gawio iondoke kwenda kwa matajiri huku watu wetu wakiishi kwenye umasikini?

Ikiwa Serikali haitochukua hatua za haraka za kuingia ubia na GGML, ikiwa itaacha gawio la faida liishie kwa matajiri wa ughaibuni, huku ikiendelea kuwakimbiza wabangaizaji kwa kusema ‘inakusanya kodi’ itakuwa inauishi ule mstari wa Biblia (Mathayo 25:29). 

Mstari huo unaosema: “Mwenye nacho ataongezewa, na asiyenacho, atanyang’anywa hata kile kidogo alichanacho.” Hayo yatakuwa makosa makubwa. Tujisahihishe, tuwape GGML jina la mnyama, wao watupe gawio la fedha. 


Clay Mwaifwani ni mwanasheria na mdau wa usimamizi dumivu wa rasilimali za maliasili. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia +255 758 850 023 au claymwaifwani09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts