The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Barua kwa Askari wa Jeshi la Polisi Tanzania: ‘Mmepoteza Imani Yetu Kwenu’

Kama jamii, tunataka kuona maafisa wa polisi ambao ni mfano wa haki, uadilifu na huruma. Kwa sasa, hata hivyo, maafisa hao hawana sifa hizo.

subscribe to our newsletter!

Kwa Askari wa Jeshi la Polisi Tanzania,

Nianze kwa kuwapa pole kwa kazi ngumu mnayoifanya, naelewa jukumu lenu siyo jepesi. Niwape pia hongera kwa kuaminiwa na nchi kwa kupewa dhamana ya kulinda raia na mali zao, ni jukumu kubwa sana.

Ningetamani sana kuandika barua hii nikiwa na tabasamu na katika hali ya ucheshi kama ambavyo siku zote nipo.

Bahati mbaya sana, naandika barua hii moyo wangu ukiwa mzito na wenye maumivu makubwa kutokana na ripoti za mateso, na muda mwingine vifo, vya ndugu zetu Watanzania vinavyotokea wakiwa mikononi mwenu. Lakini badala ya kurusha shutuma na kuwakaripia, natamani tutete kidogo ili mnisaidie kuelewa ni wapi mlipoanguka.

Ripoti za haki za binadamu zinazotolewa kila mwaka na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), zimekua zikionesha matumizi ya mabavu ya polisi yanayopelekea majeraha, na muda mwingine vifo, vya Watanzania wakiwa mikononi mwenu, na bahati mbaya sana sioni ripoti itakayozinduliwa mwaka huu wa 2024 ikiwa inasema tofauti. 

SOMA ZAIDI: Tusiruhusu Uholela wa Matumizi ya Mamlaka ya Kipolisi

Kuna hofu na huzuni inayojengwa ndani ya mioyo yetu tunaposhuhudia namna ambavyo jamii yetu inawaona maafisa wa Jeshi la Polisi. 

Ule wito wenu wa kusaidia sasa umegeuka kuwa tishio la maisha yetu. Kadri siku zinavyozidi kwenda, matukio ya kusikitisha ya watu kuteswa na kupoteza maisha yao katika vituo vyenu yanazidi kuongezeka. 

Vituo ambavyo tumejengwa tukiamini ni vituo vya kutafuta hifadhi vimegeuka kuwa vyanzo vya maumivu makali kwa familia za watu wanaokuja kwenu. 

Vilio ambavyo havina kikomo, kwani haki haijapatikana na wauaji wao hupata kinga kwa kuteteana na kutoa ripoti zisizoeleweka. Hatuko tena salama mikononi mwenu. Tuliowapa dhamana ya kutulinda mmegeuka kuwa chanzo kikuu cha hofu yetu. 

Najiuliza, mmeanguka wapi? Je, ni mafunzo mnapewa au mazingira mabovu ya kazi yenu yamesababisha haya? Au kuna lugha ya amri sisi raia hatuielewi?

SOMA ZAIDI: ‘Kila Kukicha Nalia, Sina cha Kufanya’: Waathirika Vitendo vya Ukatili wa Polisi Wataka Uwajibikaji

Kaka na dada zangu, kama likija kapu la maoni na Watanzania tukaambiwa tuandike kuhusu kundi linaloogopeka, sina mashaka nafasi yenu itakua miongoni mwa nafasi tano za juu kama siyo nafasi tatu za juu. 

Mwaka 2022, wakati wa kukusanya maoni juu ya vyombo vinavyoaminiwa na Watanzania kutenda haki, bahati mbaya sana ni asilimia 19 tu walisema wana imani na jeshi letu la polisi. 

Zile nyimbo tumekuzwa tukiimbishwa shuleni kulipenda Jeshi la Polisi kwa sasa hazipo tena vichwani kwetu. Siyo kwa sababu hatuzipendi, la hasha! Zimefutika kwa sababu mmefanya kazi kubwa ya kuzifuta kwa matendo yenu ya ukatili na matumizi ya mabavu. 

Natamani sana niwatetee nikikutana na watu tukiwajadili. Natamani nirushe lawama kubwa kwa viongozi wa Serikali. Lakini jamii imeona jitihada mbalimbali zikichukuliwa kwa ajili ya kufanya maboresho kwenye jeshi lenu. 

Tulianza kuyapa majina ya Kiswahili enzi za Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, hayakuzaa matunda, tukabadili na kuyapa jina la Kiingereza kidogo livutie na kuwapa tamanio la kukubali mabadiliko, awamu hii tukayaita reforms, lakini bado hatujashuhudia mabadiliko yoyote ya maana. 

SOMA ZAIDI: Haya Ndiyo Mageuzi Yanayohitajika Kwenye Jeshi la Polisi

Naanzaje kuwatetea kwenye mazingira kama hayo? Je, kuna kitu kingine tunachoweza kufanya kama jamii na watetezi wa haki za binadamu  kusaidia kubadilisha hali hii? 

Leo ninawakumbusha kama dada, kwa upole, nikiwa bado kwenye taifa lenye watu wenye vipawa vya uhimilivu. Hofu yangu ni kwamba, kama hakuna badiliko lolote mtafanya, mara nyingine nawaandikieni tunaweza kuwa kwenye taifa ambalo hawa wahimilivu wamechoka, wamesimama, na wameazimia kulipa kisasi, na sitawashangaa!

Ninawasihi, kwa moyo wa dhati na unyenyekevu, kufanya kazi kwa bidii zaidi, kwa sasa siyo tu kulinda tena zile mali na raia bali kuongeza jukumu la kurejesha imani ya jamii kwenu. 

Kama jamii, tunataka kuona maafisa wa polisi ambao ni mfano wa haki, uadilifu na huruma. Tunataka kuona maafisa wa polisi ambao wanashirikiana na jamii kwa lengo la kujenga amani na ustawi wa pamoja. 

Ningetamani sana kupata wasaa nikapata majibu ya maswali yangu tukionana, lakini hofu yangu ni je, nikienda kukutana nanyi familia yangu itakua na amani kwamba nitarudi salama? 

SOMA ZAIDI: Polisi Lindi Wadaiwa Kumlinda Askari Anayeshukiwa Kumbaka Binti wa Miaka 13

Ninachoweza kuwaahidi, mimi na Watanzania wengine wengi wenye mapenzi mema na taifa hili, tuko tayari kuwasikiliza; tuko tayari kujua shida ni nini na ni kwa namna gani tunaweza kuwasaidia. 

Tuko teyari kuwapa ushirikiano na kutangaza mema ya jeshi letu pale ambapo mtabadilika na kutuonesha kwa vitendo kuwa tuna kila sababu ya kuamini sisi na vizazi vyetu tutakuwa salama mikononi mwenu. 

Ninawatakia kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu yenu. 

Kwa heshima na unyenyekevu!
Ayker Peter ni mwanasheria na mtetezi wa haki za binadamu kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia aikapeter2420@gmail.com au @AykerP katika mtandao wa X. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts