The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

‘Kila Kukicha Nalia, Sina cha Kufanya’: Waathirika Vitendo vya Ukatili wa Polisi Wataka Uwajibikaji 

Wasema bila kuwa na mifumo inayochochea uwajibikaji katika Jeshi la Polisi ukatili dhidi ya raia hautakoma.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Amina Ally alikurupushwa kutoka usingizini na kelele za mlango uliokuwa ukigongwa kwa nguvu nyingi kama vile mgongaji alikuwa anahitaji hifadhi dhidi ya jambo baya alilokuwa analikimbia. Isipokuwa, mgongaji hakuwa mtafuta hifadhi bali maafisa wa Jeshi la Polisi.

Ilikuwa ni majira ya saa kumi alfajiri, siku ya Jumamosi, Septemba 17, 2022, pale maafisa hao walipofika nyumbani kwa mama huyo wa watoto wanne maeneo ya Tandika, Dar es Salaam, wakisema nyumbani mwake humo amehifadhi ‘Panya Road.’

“Nikawaambia mimi siwezi kufungua [mlango] kwa sababu dunia imeharibika,” Amina alisema wakati anasimulia kisa chake kwa The Chanzo. “[Nikasema] kama kuna Mjumbe au Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, mimi naweza kufungua. [Polisi wakasema], ‘basi sisi hatuwezi kushindwa kufungua, hakuna nyumba ya kushindwa sisi kuingia ndani. Sisi tutaingia ndani na tutamtoa huyo tunayemtaka.’”

Mtu aliyekuwa anatakiwa na maafisa hawa ni Amir Athuman Hassan, kijana mwenye umri wa miaka 25 ambaye Jeshi la Polisi lilikuwa likimtuhumu kujihusisha na vitendo vya uhalifu wa kupora kwa kutumia silaha, au ‘Panya Road’ kama watu wanaofanya uhalifu huo wanaitwa.

SOMA ZAIDI: ​​​​Operesheni ya Polisi Dar Dhidi ya Wanaodaiwa Kuwa Panya Road Ichunguzwe

Amina, mama wa Hassan, anasema maafisa hao walijilazimisha kuingia ndani mwake, wakaenda mpaka chumbani kwake, wakitoa vitisho na maneno mengine mengi ya kashfa kwa familia hiyo, na kuondoka na kijana wake huyo. Amir, mfanyabiashara mdogo, aliondoka mzima, akarudi akiwa amekufa.

Utambuzi kwamba kijana wake amekufa ulitanguliwa na jitihada za Amina kumtafuta kijana huyo kwenye vituo mbalimbali vya polisi bila mafanikio. Hatimaye aliamua kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambapo alifanikiwa kuukuta mwili wa mtoto wake ukiwa umehifadhiwa mochuari, huku ukiwa na alama mbili za risasi shingoni mwake.

Amina anasema alilazimika kwenda MNH baada afisa mmoja wa polisi kumwambia, kwa nia njema, kwamba akimkosa kijana wake kwenye vituo vya polisi, aende katika hospitali hiyo.

Kimsingi, ushauri huo uliendana na “angalizo” alilokuwa amelitoa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla kwa wazazi wa Dar es Salaam hapo Septemba 15, 2022, siku mbili tu kabla polisi hawajavamia nyumbani kwa Amina na kumchukua kijana wake.

SOMA ZAIDI: Safari Yangu ya Gerezani Bila Kupitia Polisi Wala Mahakamani

“Angalizo, mzazi yoyote, kuanzia leo, akipotelewa na mtoto, akamtafute kituo cha polisi au hospitali,” Makalla alisema kwenye mkutano. “Narudia, mzazi yoyote, akipotelewa na kijana wake leo, au kuanzia jana operesheni ilivyofanyika, awahi kituo cha polisi au hospitali.”

“Nimeteseka,” Amina alisema kwa uchungu, machozi mithili ya maji yakimiminika machoni mwake, huku ndugu yake akimsihi ajikaze.

“Kwa kweli nimeteseka. Maisha yangu [kwa sasa] nawaza nitaishije na wakati mwanangu ndiye aliyekuwa ananisaidia kulea ndugu zake? Ndugu zake wanasoma, alikuwa ananisaidia [kuwasomesha]. Hivi sasa kila kukicha nalia sina cha kufanya. Nafanyaje?”

David Misime, Msemaji wa Jeshi la Polisi, aliiahidi The Chanzo kuwezesha mahojiano na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camillius Wambura ili kujibu tuhuma hizi zinazoelekezwa kwa jeshi hilo. Mpaka wakati wa kuchapisha habari hii, hata hivyo, Misime alikuwa bado hajamrudia mwandishi.

Ncha ya theluji

Amina ni mmoja tu kati ya Watanzania kadhaa wanaohisi kudhulumiwa na Jeshi la Polisi huku wakiwa hawajui nini cha kufanya kurekebisha dhuluma hiyo; ni ncha kwenye theluji ya ukatili wa polisi dhidi ya raia.

Malalamiko ya watu kuteswa, na hata kufariki, wakiwa mikononi mwa chombo hicho chenye dhamana ya kulinda raia na mali zao yamekuwa yakiongezeka kila kukicha, hali inayoibua maswali kama kweli Jeshi la Polisi ni chombo sahihi cha kufanya kazi hiyo.

Uonevu unaofanywa na Jeshi la Polisi umekuwa ni jambo la kawaida sana nchini Tanzania kiasi ya kwamba hata Rais Samia Suluhu Hassan mwenyewe anaamini hakuna chombo cha dola kinacholipiku Jeshi la Polisi kwa kulalamikiwa na wananchi, hali iliyomsukuma kuunda tume maalum ya kutathmini taasisi za utoaji haki jinai nchini.

“Tumesema twende tukaliangalie Jeshi la Polisi ambalo, mara nyingi, kama utazungumza na watu 100, basi [watu] 70 watanyoosha kidole kwa Jeshi la Polisi,” alisema Mkuu huyo wa Nchi hapo Machi 31, 2023, alipokuwa akizindua tume hiyo.

Hatua hiyo ya Rais Samia ilikuja takriban mwaka mmoja tangu Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) hapo Septemba 9, 2022, ilitaje Jeshi la Polisi kama “kinara” kwa kulalamikiwa zaidi na wananchi.

SOMA ZAIDI: Lini Polisi Iliahidi Hadharani Kutekeleza Ushauri Kutoka Chama cha Upinzani?

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji (mstaafu) Mathew Mwaimu alisema malalamiko mengi kwa jeshi hilo yanahusu matukio ya watuhumiwa kudaiwa kufa au kuteswa wakiwa chini ya mikono ya polisi.

Kwenye mahojiano yake na baadhi ya familia zilizopoteza wapendwa wao mikononi mwa polisi, The Chanzo ilishuhudia jinsi familia hizo zilivyoachwa na maumivu makali mioyoni mwao, huku wengi wakioneshwa kusikitishwa na namna Jeshi la Polisi linavyofanya kazi zake kiholela, na hata pale inapotokea maisha ya mtu yanapotea kunakuwa hakuna uwajibikaji katika jeshi hilo.

Serikali imekula mbegu zake

Sued Ally Shoo alimpoteza mpwa wake, Khatibu Said Kabwele, kijana mwenye umri wa miaka 30, ambaye baada ya kuchukuliwa akiwa hai na maafisa wa Jeshi la Polisi baada ya kumshuku kuwa ni ‘Panya Road’ alipatikana akiwa amepoteza maisha katika chumba cha kuhifadhia maiti, MNH.

Shoo, mkazi wa Tandika, aliiambia The Chanzo kwamba kinachomuumiza zaidi ni kwamba polisi walipofika nyumbani kwao hapo Septemba 17, 2022, majira ya saa 12 asubuhi wakimtaka mpwa wake huyo, walitoa ushirikiano wote kwa polisi, wakijua hawezi kudhurika kwenye mikono ya vyombo vya usalama.

“Polisi walikuja, wakasema tunamtafuta huyu mtu, akaamshwa ndani, wakakabidhiwa, utii wa sheria bila shuruti,” Shoo anaeleza. “Maana hatukupenda kwenda kuhoji sana. Tulipomuuliza yule aliyekabidhiwa yule mtoto alisema tunakwenda kuongea naye tu hapo.”

Kabwele hakurudi tena baada ya hapo. Baada ya kutafuta sana bila mafanikio, Shoo alienda MNH hapo Septemba 22, 2022, na kukuta mwili wa mpwa wake ukiwa uko mochuari, huku taarifa zikisema kwamba mwili huo ulikuwepo hapo tangu Septemba 19, siku mbili tu baada ya polisi kukabidhiwa kijana huyo.

“Sisi hatujajipanga kifamilia kuchukua hatua ya aina yoyote, tumemwachia Mungu,” Shoo aliiambia The Chanzo. “Hizo hatua zitatupotezea tu muda kwa maana lile jambo tunasema ni Serikali imeamua, kwa sababu sauti ya Mkuu wa Mkoa ni sauti ya Serikali. Kwa hiyo, tunasema Serikali iliamua kula mbegu zake.”

Kwa mashirika na wadau wanaojihusisha na utetezi wa haki za binadamu, hali hii inaweza kuendelea mpaka pale Tanzania itakapokuwa na mifumo imara ya kuhakikisha uwajibikaji ndani ya Jeshi la Polisi.

Uwajibikaji

Wakiongea na The Chanzo, wadau hawa wamebainisha kwamba wakati Jeshi la Polisi limekuwa likitangaza kuwachukulia hatua baadhi ya maafisa wake waliohusika na kutesa na kuuwa watuhumiwa, uwezekano wa kuwajibishana jeshini humo ni mdogo kwani polisi hawawezi kujiwajibisha.

Tito Magoti ni wakili na mtetezi wa haki za binadamu ambaye anasema kwamba mazingira yaliyopo nchini kwa sasa ni kama yamewawekea kinga polisi kwani ni ngumu kuwatofautisha polisi wanapofanya matukio wao binafsi ama wanapokuwa wanaiwakilisha taasisi.

SOMA ZAIDI: Haya Ndiyo Mageuzi Yanayohitajika Kwenye Jeshi la Polisi

“Sasa ni ngumu sana kupata uwajibikaji kwenye mazingira kama haya,” Magoti anaendelea kusema. “Kwa hiyo, mazingira haya yatatatuliwa kwa kuwa na chombo mahususi ambacho kitakuwa na mamlaka ya kuwashughulukia polisi. Ni kama kuwafanyia upolisi mapolisi angalau tutapunguza haya matukio.”

Takwa la kuundwa kwa chombo maalum cha kulisimamia Jeshi la Polisi ni takwa la muda mrefu na linaloungwa mkono na wadau wengi, wengi wao wakitolea mfano wa chombo kama hicho kilichoko nchini Kenya,  Independent Policing Oversight Authority (IPOA), kama mfano.

Lakini kuna wadau wamebainisha kwamba ili kuhakikisha uwajibikaji ndani ya Jeshi la Polisi, mabadiliko hayapaswi kulenga mifumo ya kitaasisi tu bali hata fikra za maafisa wa jeshi hilo ambao kimsingi ndiyo wanaotekeleza maagizo haya.

Mmoja kati ya wadau hawa ni Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo, chama ambacho mara kwa mara kimekuwa kikikemea ukatili unaofanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya wananchi.

“Kifikra kwa maana ya wajibu wa Jeshi [la Polisi] ni upi, yaani hili jeshi linamtumikia nani? Je, linatumikia Chama cha Mapinduzi na Serikali yake ama linatumikia umma?” anahoji Shaibu kwenye mahojiano yake na The Chanzo. “Hayo ni mabadiliko ya msingi ya kifikra.”

Shaibu pia alisema kunahitajika mabadiliko ya kiutamaduni ndani ya Jeshi la Polisi ambayo yatawafanya maafisa wa jeshi hilo wasione kutumia mabavu katika kazi kuwa ni ndiyo u-polisi na kwamba ni kitu cha kawaida.

“Tunapaswa kubadilisha utamaduni wa Jeshi la Polisi,” Shaibu alisisitiza. “[Inabidi polisi] wajione kama wao wana hudumia raia na siyo kwamba wanapaswa kudhibiti raia. Ni lazima tubadilishe mitaala ya Jeshi la Polisi, namna polisi wanavyopatikana, namna polisi wanavyofunzwa na namna polisi wanavyohudumiwa.”

Kwa upande wake, Shoo, ambaye mpwa wake anahisi aliuwawa na Jeshi la Polisi, amewasihi polisi kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo nchini.

“Jeshi la Polisi tunataka wasimame kwenye sheria, wafanye kazi yao kwenye eneo lao, na Mahakama ikafanye kazi yao kwenye eneo lao,” alisema Shoo. “Mimi hicho ndiyo kilio changu.”

​​Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *