Lini Polisi Iliahidi Hadharani Kutekeleza Ushauri Kutoka Chama cha Upinzani?

Kwa chama tawala ilikuwa ni Julai 29, 2022.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe amesema hakumbuki mara ya mwisho Jeshi la Polisi kuahidi kufanyia kazi ushauri kutoka chama hicho ilikuwa lini huku Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika akigoma kutolea maelezo swali hilo, akitaka aulizwe kuhusu Katiba Mpya.

Hili ni swali ambalo wafuatiliaji wa siasa za Tanzania wamekuwa wakijiuliza kwa wiki takribani moja sasa kufuatia hatua ya Jeshi la Polisi kujitokeza hadharani na kuahidi kufanyia kazi ushauri uliotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) – Tanzania Bara Abdulrahman Kinana.

Akizungumza na wananchi wa Mbozi, mkoani Songwe hapo Julai 28, 2022, Kinana alimuagiza Kamanda wa Jeshi la Polisi (IGP) Camillius Wambura kufanya tathmini ya kina juu ya mwenendo wa jeshi hilo, hususan kitengo chake cha usalama barabarani.

Agizo hilo lilitokana na malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba askari hao wamekuwa wakiwasumbua, malalamiko ambayo Kinana alikiri pia kwamba amekuwa akiyapokea kwenye kila mkoa ambao ziara yake imepita.

SOMA ZAIDI: Askari Jamii Bandia Walivyotoa Uhai wa Kamanda wa Polisi Mwanza Liberatus Barlow

Wanawasumbua wananchi

“Nimuombe IGP mpya, na vyombo vyake, kufanya tathmini ya kina juu ya utendaji wa Jeshi la Polisi, kitengo cha usalama barabarani, hasa maeneo ya miji na mijini,” Kinana aliagiza. “[Polisi] wamejazana sana [kwenye haya maeneo]. Wanawasumbua wananchi. Kila baada ya kilomita moja unakuta wamesimamisha gari.”

Siku moja tu baada ya Kinana kutoa agizo hilo, Jeshi la Polisi lilitoa taarifa kwa umma likisema kwamba limepokea “kwa uzito wake” ushauri huo, huku msemaji wake David Misime akiueleza umma wa Watanzania kwamba “mikakati mizuri” imeanza kuwekwa kwa ajili ya kutekeleza ushauri huo.

Wakati Misime akiieleza The Chanzo kwamba ilichofanya Jeshi la Polisi ni sehemu ya kazi zake za kila siku, kwa wadau mbalimbali nchini, hususan wale wa vyama vya upinzani na watetezi wa haki za binadamu na masuala ya kidemokrasia, hatua hiyo ilikuwa ni uthibitisho mwengine kwamba Jeshi la Polisi na CCM ni chanda na pete.

“Hatua ya Jeshi la Polisi kujitokeza na kujibu mapendekezo ya [Makamu Mwenyekiti] wa CCM inakwambia mengi kuhusiana na Jeshi la Polisi,” aliandika Nicodemus Minde, mtafiti na mchambuzi wa masuala ya uhusiano wa kimataifa kwenye mtandao wake wa Twitter.

SOMA ZAIDI: Sintofahamu Mahakamani Polisi Wakizuia Watu Kuingia na Simu Kwenye Kesi ya Mbowe

Madai ya siku nyingi

Madai ya Jeshi la Polisi kuipendelea CCM ni ya muda mrefu na yanakwenda mbali takriban tangu kuanzishwa tena kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi nchini hapo mwaka 1992.

Kwenye miaka takriban sita iliyopita, Jeshi la Polisi limekuwa likilalamikiwa kunyanyasa vyama vya upinzani na viongozi wake, ikiwa ni pamoja na kuwazuia kufanya mikutano ya nje na hata ile ya ndani, huku CCM ikiwa huru kufanya hivyo.

Jeshi la Polisi limekuwa likikanusha madai haya lakini utetezi wao mara nyingi hushindwa kuwashawishi wakosoaji wake kutokana na maafisa wake waandamizi kuonesha kile wakosoaji wanahisi ni upendeleo wao kwa CCM ulio wa waziwazi.

Kwa mfano, mnamo Oktoba 2020, siku chache kabla ya Uchaguzi Mkuu, aliyekuwa OCD wa Hai Lwalwe Mpina alizua gumzo baada ya kumwambia Freeman Mbowe, aliyekuwa akigombea ubunge jimbo la Hai kwa tiketi ya CHADEMA, kwamba hawezi kumshinda mpinzani wake kutoka CCM “hata ufanyeje.”

Naye aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Arusha Jonathan Shana aliibua mjadala mzito baada ya kushiriki mkutano wa kisiasa wa CCM na hata kuhutubia katika mkutano huo kwa kusema kwamba CCM, Serikali na vyombo vya dola, ikiwemo Jeshi la Polisi, “ni kitu kimoja.”

The Chanzo ilimuuliza Misime ni lini mara ya mwisho Jeshi la Polisi limewahi kujitokeza hadharani na kukiri kupokea na kufanyia kazi ushauri uliotolewa na chama chochote cha upinzani nchini kama ilivyofanya kwa CCM ambapo alisema siyo kila mara wanalazimika kufanya hivyo.

“Majibu mengine ambayo yanatolewa yanaonekana kwenye utendaji wetu [ambao] unaboreshwa kila siku. Siyo lazima utoke na kauli,” alisema Misime. “Majibu yanaonekana kwamba uboreshaji wa utendaji wetu unaimarika siku hadi hadi siku. Huo ndiyo mrejesho wa kwamba tumepokea ushauri.”

Siyo kitu cha kawaida?

Kwa Zitto Kabwe, mwanasiasa wa siku nyingi ambaye amewahi kuhudumu kama mbunge, kitendo cha Jeshi la Polisi kujitokeza hadharani na kuahidi kufanyia kazi agizo la CCM “siyo kitu cha kawaida” kama ambavyo Misime angetaka umma uamini.

“[Hiyo] haijawahi kutokea kwetu,” alisema Kabwe wakati wa mahojiano na The Chanzo. “Siyo kitu cha kawaida. Hivyo, nasi tumeamua kuandika rasmi ushauri wetu kwa ajili ya mageuzi ya Jeshi la Polisi ili polisi watoke hadharani kusema wameupokea.”

Lakini kwa Dk Richard Mbunda, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hakuna kikubwa ambacho Jeshi la Polisi imekifanya kustahili kutupiwa lawama, akisema CCM ni chama tawala na ni jukumu la Jeshi la Polisi kupokea maagizo kutoka kwake, akiasharia kwamba ni kitu cha kawaida.

“Huu utawala ni wa Chama cha Mapinduzi, wao ndiyo waliounda Serikali na watu wote walioshikilia nafasi kwenye Serikali, ikiwemo ndani ya Jeshi la Polisi,” alisema Mbunda ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya kiutawala. “Yaani, kuna mkono wa Chama cha Mapinduzi [ndani ya Jeshi la Polisi].”

Mbunda anakiri kwamba hakumbuki mara ya mwisho kwa Jeshi la Polisi kujitokeza hadharani na kuahidi kufanyia kazi ushauri wa chama fulani cha upinzani. Hata hivyo, mwanazuoni huyo anatahadhirisha kwamba chama tawala siyo chama cha upinzani.

“Kuna tofauti kubwa kati ya chama tawala na chama cha upinzani,” Mbunda anatetea hoja yake. “Kwa sababu, chama tawala ndiyo kina dhamana ya utawala. Sasa utashindwa kumsikiliza mdhamini wako, na mdhamini ana mamlaka?”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts