Operesheni ya Polisi Dar Dhidi ya Wanaodaiwa Kuwa Panya Road Ichunguzwe

Hatuwezi kutengeneza mazingira ambapo wananchi huku wanaogopa Panya Road na huku wanaogopa Jeshi la Polisi.

subscribe to our newsletter!

Kukithiri kwa vitendo vya Panya Road jijini Dar es Salaam kumezua hofu miongoni mwa watu katika jamii. Wahalifu hao huvamia watu na kuwapora na kuwajeruhi. Angalau kisa kimoja cha kifo kimerikodiwa kutokana na vitendo hivyo vya kihalifu ambavyo vinadaiwa kufanywa na vijana walio na umri kati ya miaka 18 na 30.

Hofu hii ya kimsingi miongoni mwa wakazi wa Dar es Salaam imepelekea vyombo vya ulinzi na usalama jijini humo, vikiongozwa na Jeshi la Polisi, kuendesha operesheni kali inayolenga kusambaratisha mtandao huo wa kihalifu. 

Tayari mamia ya washukiwa wamekamatwa, na viongozi mbalimbali wamejitokeza hadharani kusema kwamba hakuna jiwe litaachwa kwenye operesheni hiyo inayoendelea.

Hata hivyo, ikiwa Tanzania ni taifa linaloongozwa kwa utawala wa sheria, wananchi walitegemea Jeshi la Polisi liendeshe operesheni hiyo siyo tu kwa mujibu wa sheria za nchi na taratibu za kipolisi bali pia kwa weledi na umakini wa hali ya juu ili wasije kumuhusisha aliyemo na asiyekuwemo. 

Lakini inaonekana ni kama vile hivi sivyo operesheni hii inavyofanyika. Inaonekana ile kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla ya Septemba 15, 2022, kwamba wazazi wenye watoto Panya Road wasipowaona nyumbani, wasihangaike, bali wakamfuate polisi au hospitali inatekelezwa kwa nguvu zote.

Tathmini yangu ya siku za hivi karibuni, iliyotokana na mazungumzo niliyofanya na familia ambazo vijana wao wameuawa na polisi baada ya kushukiwa kuwa sehemu ya mtandao wa Panya Road, inaonesha kwamba Jeshi la Polisi limejipa mamlaka ya kutuhumu, kukamata na kuhukumu kwa kutoa adhabu ya kifo.

Mwandishi wa makala haya (mwenye notibuku) akizungumza na baadhi ya ndugu waliofiwa na ndugu zao baada polisi kuwashuku ni Panya Road. PICHA | KWA HISANI YA MWANDISHI

Kwa bahati nzuri ni kwamba hata Jeshi la Polisi lenyewe limekiri kuua vijana sita wanaosadikika kuwa Panya Road, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na  Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Jumanne Muliro hapo Septemba 18, 2022. 

Muliro, hata hivyo, hatangazi kila mauaji ambayo maafisa wake wanafanya katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.

Moja kati ya tukio ambalo mpaka sasa Muliro hajalizungumzia ni lile linalohusisha mauaji ya vijana watatu waliotuhumiwa kuwa ni Panya Road kutoka katika familia tatu tofauti huko Tandika, wilaya ya Temeke. Taarifa zinadai kwamba vijana hawa walikamatwa na polisi wakiwa nyumbani kwao na kupelekwa kituo cha Polisi Maturubai kilichopo Mbagala. 

Vijana hawa hawakurudi nyumbani na taarifa zinadai kwamba waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi. 

Maiti za vijana hawa zilipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuhifadhiwa kwenye chumba cha maiti hospitalini hapo. Kitendo cha mtuhumiwa kuuwawa kwenye mikono ya polisi, pasipo na sababu za kueleweka, siyo tu ni kinyume na Katiba ya nchi lakini pia ni kinyume na sheria zote na kanuni na taratibu zinazotawala masuala ya utoaji haki nchini mwetu.

Mauaji ya kijana Amiry

Moja kati ya familia zilizopoteza vijana wao katika mazingira haya ambazo nilibahatika kuonana nazo ni ile ya Amina Allawi Alli ambaye mtoto wake, Amiry Athuman Hassan, 25, aliyekuwa akiishi na wazazi wake huko Tandika, mtaa wa Nyambwela, anadaiwa kuuwawa na maafisa wa Jeshi la Polisi.

Inadaiwa kwamba mnamo Septemba 17, 2022, majira ya saa 10 alfajiri, polisi walivamia nyumbani kwa akina Amiry, wakigonga mlango kwa nguvu kabla ya kuusukuma na kufanikiwa kuingia ndani. 

Polisi wanadaiwa kuvunja milango ya vyumba vitatu wakimtafuta Amiry ambaye walimtuhumu kuwa Panya Road. Walipomkuta ndani amelala, polisi wakamuamsha Amiry na kumwambia kwamba yeye ni mwizi. Polisi walidai kwamba hata TV waliyoikuta nyumbani kwao Amiry ni ya wizi. Wakamchukua yeye na ile TV wakaichukua.

Amiry, kwa mujibu wa maelezo ya familia yake, alijaribu kujitetea kwamba hana hatia na hata TV hiyo alinunua dukani Tandika, duka linaloitwa Gaza Electronics na kwamba anaweza kuthibitisha hilo kwani risiti ya manunuzi bado alikuwa nayo. Hata hivyo, polisi wanadaiwa hawakuwa tayari kusikiliza maelezo ya mtu waliyekuwa wakimtuhumu na hivyo wakaondoka naye.

Risiti inayoonesha uhalali wa TV ambayo polisi walidai Amiry ameiba. PICHA | KWA HISANI YA MWANDISHI.

Asubuhi yake, wazazi wa Amiry walifuatilia katika vituo vyote vya polisi. Makangarawe. Chang’ombe. Maturubai. Stakishari. Tazara. Kote huko hawakuweza kumpata kijana wao. Walienda mpaka kituo kikuu cha polisi bila mafanikio yoyote. 

Siku ya pili, baada ya kutafuta sana bila mafanikio, wazazi wa Amiry ‘walitonywa’ waende chumba cha kuhifadhia maiti Muhimbili. Ni kweli walienda na wakamkuta kijana wao amefariki, huku akiwa na alama mbili za risasi shingoni.

Wazazi wa kijana huyu waliniambia kwamba uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili uligoma kuwapatia maiti ya kijana wao mpaka wapate kibali cha polisi. 

Ndipo walipokwenda Kituo cha Polisi cha Maturubali, Mbagala, ambako walidai polisi waliwaomba Sh20,000 ili waweze kupata kibali hicho. Walitoa. Wakarudi Muhimbili ambako nako walitoa fedha ili waweze kuchukua maiti ya kijana wao. 

Nilikwenda kwenye duka la Gaza Electronics, lililopo karibu na Stendi ya Gari za Mbezi. Nilipowaonesha wenye duka hilo risiti ya manunuzi ya TV ambayo polisi walidai Amiry ameiba walikiri kwamba ni kweli risiti hiyo walitoa wao na kwamba ni kweli TV hiyo, aina ya Solar Max nchi 32, waliiuza kwa kijana huyo.

Hata juhudi za Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nyambwela Bushiri Ali Napwiri, ambaye aliniambia alikwenda Kituo cha Polisi cha Maturubai, Mbagala, na kuwaambia polisi kwamba Amiry hakuwa na tabia walizokuwa wakimshutumu nazo, na kuwataka wamuachie, hazikusaidia kuokoa maisha ya Amiry.

Napwiri alinieleza kwamba polisi walimjibu kwamba ili wamuachie Amiry akubali wamkamate yeye, hali iliyomfanya aondoke kituoni hapo. Napwiri anasema hata alipopata taarifa za kifo cha Amiry alisita kwenda kuwaeleza wazazi wake kwani, kama anavyosema, “Sikujua wapi pa kuanzia.” 

Familia ya Amiry siyo familia pekee niliyokutana nayo yenye majonzi ya kuondokewa na wapendwa wao baada ya kuhusishwa na mtandao wa Panya Road. Kuna familia nyingine ya Asha Ally na kaka yake Swedy Ally Shoo ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) huko Kiwalani, Temeke. 

Mauaji ya kijana Tosha

Asha Ally alikuwa na watoto wawili tu, mmoja wa kike na mwingine wa kiume. Huyu wa kiume, ambaye jina lake ni Khatibu Said Kabwele, au Tosha, ndiye aliyeuwawa na polisi. 

Taarifa zinadai kwamba mnamo Septemba 17, 2022, majira ya saa 12 asubuhi, polisi walifika nyumbani kwa akina Tosha, wakagonga mlango, na walipokaribishwa walisema wanahitaji kuongea na Tosha. 

Walipoulizwa wao ni nani, watu hao walijitambulisha kama polisi, na kwamba walitaka tu kuongea na Tosha halafu watamuacha hapo hapo nyumbani. Asha akaenda kumuamsha kijana wake, lakini polisi wakaondoka naye, wakimhakikishia mama yake kwamba kijana wake yupo kwenye mikono salama.  

Siku ile Tosha hakurudi. Mnamo Septemba 19, wazazi wake walitembelea vituo vya polisi, ikiwemo Kituo cha Polisi Maturubai, Mbagala, ambako waliambiwa waende chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. 

Walipofika Muhimbili, wazazi hao walimkuta kijana wao akiwa amefariki, huku akiwa na alama za risasi begani na katika koromeo.

Matukio haya mawili, hata hivyo, siyo ya kipekee kwani kuna tukio jingine linalomuhusisha kijana aliyejulikana kama Khalfan Jongo, mkazi wa Sandali-Tandika, ambaye alifuatwa nyumbani kwa kutajwa na wenzake, akachukuliwa mnamo Septemba 16. 

Familia yake inasema walikuja kujua baada ya siku kadhaa kupita, wakaenda Muhimbili wakakuta maiti ya kijana wao ikiwa na alama za risasi shingoni.

Tukio jingine linamhusisha kijana aitwaye Mbwana Kambi, mkazi wa kata ya Tandika, mtaa wa Nyambwela, aliyekamatwa na Sungusungu mnamo Septemba 23, 2022, akapelekwa Kituo cha Polisi Makangarawe, akaambiwa atoe Sh200,000 na kwamba asipotoa atapewa kesi ya Panya Road.

Kambi hakutoa fedha hiyo na hivyo ilipofika Septemba 24, 2022, akakamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Chang’ombe na kupewa kesi ya Panya Road. Kambi alikaa Chang’ombe akipigwa kwa nyaya hadi Septemba 27 baada ya ndugu zake kushinikiza ndugu yao aachiwe.

Uchunguzi ufanyike

Matukio yote haya yanaonesha kasoro ya msingi iliyopo kwenye operesheni ya polisi ya kukabiliana na Panya Road. 

Wito wangu ni kwamba operesheni hii inapaswa kuchunguzwa kwani matukio haya yanaonesha ni kwa namna gani operesheni hii inafanywa bila kufuata sheria na taratibu, hali inayohatarisha kuumiza watu wengi.

Kama polisi wanaona uchunguzi na kushtaki mahakamani siyo njia sahihi ya kupambana na uhalifu, basi washinikize sheria zibadilishwe ili mbali na kusimamia sheria, Jeshi la Polisi pia liwe na wajibu wa kutafsiri sheria na kuhukumu watuhumiwa. 

Mpaka hilo lifanyike, polisi hawana budi kufuata sheria tulizojiwekea kama nchi.

Uchunguzi wa huru ni lazima ufanyike kuhusiana na matukio yote haya na wale wote watakaobainika kufanya mambo kinyume na sheria na taratibu wachukuliwe hatua. 

Hatuwezi kutengeneza mazingira ambapo wananchi huku wanaogopa Panya Road na huku wanaogopa Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi dhima yake ni kulinda watu. Ni muhimu likafanya hivyo badala ya kuchukua uhai wa watu.

Abdul Nondo ni Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo Taifa. Pia, ni Waziri Kivuli wa Vijana, Kazi na Ajira wa chama hicho cha upinzani. Kwa maoni, anapatikana kupitia abdulnondo10@gmail.com au Twitter kama @abdulnondo2. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

4 Responses

  1. Makalu nzuri sana. Ahsante sana kwa kutenga muda wako kufanya utafiti na kuandika. Hawa wahanga ni vijana wadogo na ni dhahiri wanatoka kwenye familia maskini. Umefanya kazi kubwa kuibua kuibua na kupaza sauti mauaji ya vyombo vya usalama. Ni matumaini yangu wahusika watasoma na watafanyia kazi mapendekezo uliyotoa.

  2. Kazi nzurii lakini Siku nyingine utafiti pia mazingira hatarishi wanayokutana nayo polisi wakiwa wanatekeleza kazi na majukum yao.

  3. Umenena kitu kizuri kaka tatizo la jeshi letu la polisi wanachukuaga hatua kali pasipo kufanya uchunguzi au upembuzi yakinifu, rai yangu kwao kupitia IGP wachukulie makala yako kama darasa kwao kuepukana na jambo kama hili lisijirudie

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts