The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Polisi Lindi Wadaiwa Kumlinda Askari Anayeshukiwa Kumbaka Binti wa Miaka 13

Askari huyo, Madushi Mhogota Ng’wala, anadaiwa kumbaka binti huyo wa Darasa la Sita na kumsababishia maumivu makali.

subscribe to our newsletter!

Lindi. Polisi mkoani hapa wametakiwa kumsaka na kumkamata askari anayedaiwa kumbaka msichana wa miaka 13 ili kuondoa hisia kwamba wanajaribu kuificha kashfa hiyo na kumkingia kifua afisa wao huyo.

Askari huyo aliyefahamika kwa jina la Madushi Mhogota Ng’wala, aliyekuwa akifanya kazi katika dawati la jinsia la kituo cha polisi cha wilaya ya Liwale, anadaiwa kumbaka msichana huyo wa darasa la sita katika moja ya shule za msingi shule hapa Liwale, na kusababisha taharuki na hasira kwa wazazi na wanajamii ambao kwa sasa wanataka haki itendeke.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, Ng’wala anadaiwa kumbaka msichana huyo majira ya saa mbili za usiku wa Februari 18, 2024, wakati binti huyo akitoka nyumbani kwao kuelekea nyumba ya jirani alikokuwa akienda kulala. Inasemekana Ng’wala alimkamata msichana huyo, na kumpeleka kichakani kisha kumfanyia kitendo hicho cha kikatili.

Familia ya binti huyo ilifahamu kuhusu tukio hili siku ya pili asubuhi mara baada ya mama wa mtoto huyo kuona damu ikichuruzika kutoka katikati ya miguu ya bintiye, jambo lililopelekea msichana huyo kusimulia masaibu yake kutoka kwa afisa wa huyo wa polisi. 

Mama huyo alisema kuwa, ni binti yake ndiye aliyefichua jina la askari polisi huyo anayedaiwa kumbaka.

SOMA ZAIDI: Umalizaji Kesi Kienyeji Unavyochochea Kushamiri kwa Matukio ya Ulawiti, Ubakaji

Hidaya Chikawe ni mratibu wa wasaidizi wa kisheria kutoka shirika la Liwale Women Paralegal Aid and Unity (LIWOPAU) ambaye aliiambia The Chanzo kuwa ni lazima polisi wamkamate Ng’wala na kumfikisha mahakamani ili kuthibitisha dhamira yao ya kukomesha unyanyasaji dhidi ya watoto wilayani humo.

“[Ng’wala] ni askari wa Jeshi la Polisi ambaye amevunja sheria maakusudi,” Chikawe alisema. “Alikuwa akifanya kazi katika dawati la jinsia ambapo makumi ya kesi kama hii zililetwa mbele yake. Badala ya kusaidia kuwalinda wasichana hao wanaoishi katika mazingira magumu, Ng’wala aameamua kuchangia unyanyasaji dhidi yao.”

Chikawe alilaani vikali kitendo cha askari huyo huku akilitaka Jeshi la Polisi kumfikisha Ng’wala kwenye vyombo vya sheria ili aweze kujibu tuhuma zinazomkabili.

Kamanda wa polisi mkoa wa Lindi, John Makuri, hakupatikana kuzungumzia suala hilo baada ya majaribio kadhaa ya kumtafuta kupitia simu yake ya mkononi kushindwa kuzaa matunda. Pia, tulimtumia ujumbe mfupi wa maandishi, lakini hadi tunaandika habari hii, hakuwa ametujibu.

SOMA ZAIDI: Matukio ya Ulawiti, Ubakaji Yalivyoendelea Kutikisa Tanzania 2022

Mkuu wa wilaya ya Liwale, Goodluck Mlinga, aliiambia The Chanzo kuwa ofisi yake inafuatilia suala hilo ili kuhakikisha haki inatendeka kwa msichana huyo aliyenajisiwa, huku akiwataka polisi kuharakisha juhudi zinazolenga kumpata na kumkamata mtuhumiwa.

“Mshukiwa anasemekana kuwahonga baadhi ya polisi wenzake ambao walijaribu kuficha suala hilo,” Mlinga alisema kwenye mahojiano yake na The Chanzo. “Wazazi pia walikuwa wamemsafirisha msichana huko vijijini ili kujaribu kuficha tukio hilo.”

Mlinga alisema kuwa baada ya kudokezwa na baadhi ya wasamaria wema, timu yake ilikwenda kijijini hapo na kumtafuta binti huyo, huku akigonga nyumba kwa nyumba hadi walipomkuta na kukimbizwa hospitali kwa matibabu.

“Sasa, suala hili tumeliacha mikononi mwa polisi, na ninatumai litafanyiwa kazi na mshukiwa atafikishwa mahakamani,” Mlinga aliiambia The Chanzo. “Kwa sababu kuna masuala ya rushwa, [Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa] TAKUKURU pia inashiriki katika uchunguzi huo.”

Liwale inaripotiwa kuwa na matukio mengi ya unyanyasaji wa kijinsia na watoto kati ya wilaya sita za mkoa wa Lindi. Zuwena Omary, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Liwale, alitoa tathmini hiyo wakati wa hafla ya kuadhimisha siku kumi na sita za kupinga ukatili hapo Desemba 1, 2023.

SOMA ZAIDI: Matukio ya Ulawiti, Ubakaji Yanavyoitesa Makao Makuu ya Nchi

Zuwena alisema kuwa, kati ya matukio 360 yaliyoripotiwa ya ukatili wa kijinsia, yakiwemo ya unyanyasaji wa watoto yaliyosajiliwa Lindi kati ya Januari na Novemba 2023, 102 yaliripotiwa Liwale.

Katika ripoti yake ya mwaka 2022, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), shirika lisilo la kiserikali la haki za binadamu na utawala bora nchini Tanzania, lilibaini kuwa watoto ndiyo wahanga wengi wa ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Tanzania kwa asilimia 47, wakifuatiwa na wanawake asilimia 33 na wazee asilimia 10.

LHRC iliripoti kuwa ukatili wa kingono ndiyo ulikuwa ukatili mkubwa dhidi ya watoto nchini Tanzania kwa mwaka 2022, ukiongoza kwa asilimia 81, huku shirika hilo likihimiza kuchukuliwa kwa hatua za makusudi ili kuwalinda watoto hapa nchini.

Omari Mikoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *