The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Umalizaji Kesi Kienyeji Unavyochochea Kushamiri kwa Matukio ya Ulawiti, Ubakaji

Wadau wana hofu kwamba kama hali itaendelea kubaki hivyo hivyo, vitendo vya ulawiti na ubakaji dhidi ya watoto vitazidi kushamiri Tanzania.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Maumivu yalikuwa makubwa sana kwa Hussein Hamad Hussein na wazazi wenzake ambao watoto wao waliharibiwa kwa kulawitiwa kiasi ya kwamba waliamua kuiondosha kesi yao mahakamani, wakishindwa kujua ni adhabu gani dhidi ya kijana aliyefanya vitendo hivyo inaweza kweli kuzipa amani nafsi zao.

Baba huyo wa watoto wawili ni kati ya wazazi ambao ilikuja kubainika kwamba watoto wao wenye umri kati ya miaka mitano na sita walikuwa wakilawitiwa na kijana aliyekuwa na umri wa miaka 14 aliyekuwa akiwafanyia vitendo hivyo nyumbani kwao pale mama yake anapokuwa hayupo.

Watoto hao wawili wa Hussein ni kati ya watoto nane ambao kijana huyo anadaiwa kuwafanyia vitendo hivyo vya ukatili wa kingono mnamo mwaka 2022, ambapo inadaiwa kwamba alikuwa akiwaonesha watoto hao picha za ngono kabla ya kuwalawiti, hali iliyoendelea kwa miezi kabla ya kugundulika.

Licha ya kesi hiyo kufika mpaka mahakamani, chombo hicho cha juu kabisa cha utoaji haki nchini kilishindwa kuitolea maamuzi kesi hiyo iliyowahuzunisha watu wengi baada ya wazazi kuamua kuacha kuendelea nayo, na hivyo kesi hiyo kuishia kumalizwa nje ya Mahakama.

“Namna ya kumchukulia hatua [mshukiwa ndiyo] ilikuwa changamoto,” Hussein, 35, aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano naye. “Tukawa tunaulizana na mwenzangu, tunafanyaje? Tunamlipisha yule mtoto? Anapewa adhabu gani? Maana na yeye alikuwa mdogo na anasoma shule.”

SOMA ZAIDI: Utajuaje Kama Mwanao Anafanyiwa Ukatili wa Kingono?

Mnamo Julai 25, 2023, The Chanzo ilimtembelea Hussein, ambaye shughuli yake inayomuingizia kipato ni ujasiriamali, kwenye kituo chake cha kazi hapo Mailimbili, jijini Dodoma, ikimkuta baba huyo ambaye siyo mfupi wala mrefu akitengeneza mizani ya kupimia bidhaa.

Kwa dalili zote, Hussein anaonekana kuwa ni mtu mwenye huzuni, akiiambia The Chanzo kwamba kwa sasa kinachomkosesha usingizi ni kufikiria hatma ya watoto wake wawili waliofanyiwa vitendo hivyo vya kikatili na kijana huyo ambaye hajachukuliwa hatua zozote za kisheria.

“Inaumiza sana,” alisema Hussein huku akiwa ameinamia chini. “Hatma ya watoto wangu siijui; jambo hili limeniathiri sana. Mtoto wa kiume ndiyo tegemezi lako, anapoharibika akiwa mdogo inakuwa inaumiza sana.”

Janga la kitaifa

Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, hususan ubakaji na ulawiti, vimetajwa kama janga la taifa nchini Tanzania, hali ambayo imeendelea kuumiza vichwa vya watendaji wa Serikali, mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs), taasisi za dini na wadau wengine juu ya namna vitendo hivyo vinaweza kukomeshwa.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, kati ya mwaka 2017 mpaka Mei 2022, Tanzania ilirikodi jumla ya matukio 75,787 ya ukatili wa dhidi ya watoto yaliyojumuisha vitendo vya ulawiti na ubakaji.

Matukio ya Ukatili kwa Watoto

Ingawaje takwimu hizi zinaonesha kupungua kwa matukio ya vitendo vya ukatili vilivyoripotiwa kwenye Dawati la Jinsia na Watoto katika Vituo vya Polisi, uchambuzi wa kosa moja moja unaonesha hali siyo nzuri sana, hali inayowataka wadau kuchukua jitihada za makusudi kurekebisha hali hiyo.

SOMA ZAIDI: Hakuna Hiki Wala Kile, Kupiga Watoto Siyo Sawa

Kwa mfano, takwimu hizo kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii zinaonesha kwamba kati ya Januari na Mei 2022, jumla ya matukio ya kubaka 2,445, kumpa mwanafunzi mimba 717 na kulawiti 553 yalirikodiwa nchi nzima.

Takwimu zaidi toka jeshi la Polisi zinaonesha katika kipindi kati ya mwaka 2016 mpaka mwaka 2021, watoto 5,716 waliripotiwa kufanyiwa vitendo vya ulawiti, huku asilimia 90 wakiwa ni watoto wa kiume.

Hii ina maana kwamba ukatili wa kubaka, kumpa mimba mwanafunzi na kulawiti bado ni changamoto kubwa nchini Tanzania, hali inayoita jitihada za pamoja kupambana na vitendo hivyo. Kuchukuliwa kwa hatua za kisheria dhidi ya watu wanaobainika kufanya vitendo hivyo kumetajwa kama moja ya njia imara ya kuvitokomeza.

Matukio ya ulawiti kwa watoto 2016 mpaka mwaka 2021

Hata hivyo, uchunguzi wa The Chanzo umebaini kwamba hatua hiyo inakuwa ngumu kuchukuliwa kwani baadhi ya wazazi na walezi wa watoto wanaofanyiwa vitendo hivi huamua kumaliza kesi zao kienyeji, hali ambayo siyo tu inawanyima waathirika haki bali pia huchochea vitendo hivi kushamiri.

Kusameheana

Ingawaje hakuna takwimu rasmi zinazoonesha ni kwa kiwango gani kesi za ulawiti na ubakaji humalizwa kienyeji nchini, ripoti kadhaa zimekuwa zikigusia hali ya kesi hizo kumalizwa nje ya utaratibu wa kimahakama kama moja ya vichocheo vikubwa vya vitendo hivyo vya aibu nchini humu.

Utafiti wa mwaka 2017 uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (UNICEF) unabainisha kwamba kesi nyingi za ukatili wa kingono dhidi ya watoto humalizwa katika mazingira ya nyumbani, ambapo mara nyingi wazazi hushiriki kwenye michakato hiyo bila ya hata kuwashirikisha watoto wenyewe.

Nayo Ripoti ya Haki za Binadamu kwa Mwaka 2022 iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) mapema mwaka 2023 ilitaja “utamaduni wa kusameheana” na “kuficha aibu ya familia” kama moja ya sababu zinazochochea vitendo vya ukatili dhidi ya watoto Tanzania.

SOMA ZAIDI: Ulawiti Unavyowajaza Hofu Wazazi Kuhusu Hatma ya Watoto wa Kiume Tanzania

Getrude Dyabene ni Afisa Programu anayehusika na masuala ya Jinsia, Watoto, Wanawake na Watu Wenye Ulemavu kutoka LHRC ambaye anafichua kwamba kulingana na tathmini yao, kati ya kesi 100 za ulawiti na ubakaji zinazoripotiwa polisi, ni 15 tu ndiyo hufikishwa mahakamani.

“Na nyingi ya hizo zinazoenda mahakamani, siwezi kusema kwa asilimia ni ngapi, lakini kwa kiwango kikubwa zinakuwa zinamaliziwa na wazazi,” alisema afisa huyo kwenye mahojiano na The Chanzo. “Ukweli ni kwamba kesi nyingi kuhusu haya mambo humalizwa kienyeji.”

Inspekta Jelda Luyangi ni Inchaji wa Dawati la Jinsia Polisi, wilaya ya Dodoma Mjini, ameithibitishia The Chanzo pia kwamba utashi wa kumaliza kesi kienyeji miongoni mwa wazazi au walezi wa watoto waliofanyiwa ukatili ni mkubwa, akiitaja hiyo kama moja kati ya changamoto kubwa wanazokabiliana nazo katika kukomesha vitendo hivyo.

“Unakuta mzazi au mlezi ameshakaa meza moja na aliyetenda kile kitendo kwa mtoto wake na wakayazungumza na wakakubaliana yaishe,” Inspekta Jelda alisema kwenye mahojiano hayo. “Moja kwa moja yule mzazi hataweza kufika mahakamani.”

Hongo, hofu zatajwa

Afisa huyo alisema kwamba mbali na nia ya kuficha aibu, baadhi ya familia hujikuta zikifanya hivyo baada ya kuahidiwa malipo ya fedha na mshukiwa au kutokana na hofu waliyonayo juu ya vyombo vya upatikanaji haki nchini, kama vile Jeshi la Polisi au Mahakama.

Baadhi ya wadau wameelekeza lawama kwa Jeshi la Polisi, wakisema kwamba taasisi hiyo imekuwa ikiwaruhusu wazazi kumaliza kesi hizo la ulawiti na ubakaji kienyeji. Wadau hao hawaelewi kwa nini kesi inafika mpaka polisi halafu wazazi wanaruhusiwa kumalizana kienyeji.

SOMA ZAIDI: Changamoto Zinazokabili Utoaji Haki Jinai Kwa Watoto Tanzania Zatajwa

Hata hivyo, Inspekta Jelda aliiambia The Chanzo kwamba hakuna kitu kama hicho, akisema kesi pekee inayoshindwa kwenda mbele zaidi baada ya kutoka Kituo cha Polisi ni ile ambayo ushahidi wake uko dhaifu.

“Kama ushahidi umekamilika, hizi kesi hazifii polisi,” alibainisha afisa huyo. “Jamii ishirikiane na polisi pindi inapofungua kesi hizi. Hizi kesi watuhumiwa wanafungwa kama ushahidi umekamilika. Kama tutakuwa tunashirikiana pamoja, nadhani watuhumiwa watafungwa; wakifungwa inakuwa ni fundisho kwa watu wengine.”

C-Sema ni shirika lisilo la kiserikali lililojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania ambalo takwimu zake za Huduma ya Simu kwa Mtoto zinaonesha kwamba kati ya mwaka 2020 na 2023 walipokea kesi 3,151 za ukatili kwa watoto.

Asilimia 20.5 ya kesi hizo zote zinahusu ukatili wa kingono kwa watoto, huku asilimia 76 ya kesi zote za ukatili wa kingono zikihusu ubakaji na ulawiti wa watoto. Kwa mujibu wa takwimu hizo, watoto 123 hubakwa na kulawitiwa kila mwaka nchini Tanzania.

Hatua zichukuliwe

Faith Mkony ni Afisa Mawasiliano na Utetezi kutoka C-Sema ambaye ameiambia The Chanzo kwamba sehemu kubwa inayohitaji uangalizi kuhakikisha kwamba waathirika wa vitendo vya ulawiti na ubakaji nchini wanapata haki ni kwenye mchakato wa utoaji wa haki kwa vyombo vinavyohusika na haki jinai.

Mchakato wa upelelezi na uendeshaji wa kesi kuwahishwa ili haki isicheleweshwe itawatia moyo wanajamii kuviamnini vyombo hivi vya haki, alisema Faith.

“Kama unam’baka au kumlawiti mtoto wa mtu na hakuna ‘gharama’ yoyote yenye maumivu kwako unayoipata, utaendelea kubaka au kulawiti,” aliongeza afisa huyo. “Ni muhimu mambo mawili yafanyike.”

“Ulinzi wa mtoto ni zao la malezi makini kwa watoto,” aliendelea kueleza Faith. “Wazazi na walezi walibebe jukumu la kuhakikisha watoto wao wako salama. Pili, kama tulivyoeleza hapo awali, haki jinai isicheleweshwe hasa katika kesi zinazohusu ulawiti na ubakaji kwa watoto.”

The Chanzo ilitaka kujua kutoka kwa Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Nandera Mhando, ni ipi mikakati ya Serikali katika kuhakikisha kwamba waathirika wengi zaidi wa vitendo vya ulawiti na ubakaji nchini wanapata haki na kesi zinakoma kumalizwa kienyeji.

SOMA ZAIDI: Wanawake Wawili Wauwawa Kikatili Zanzibar. Familia, Wanaharakati Wataka Uwajibikaji

Kwenye majibu yake ya maandishi kwa The Chanzo, Dk Mhando alisema kwamba Serikali inatekeleza mikakati kadhaa inayolenga kutatua tatizo hilo mahususi na kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto nchini kwa ujumla.

Moja kati ya mikakati hii ni kuendesha kampeni mbalimbali kuhamasisha jamii kushiriki katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, ikiwemo ile ya ‘Twende Pamoja, Ukatili Sasa Basi’ iliyozinduliwa mwaka 2019.

“Kampeni hii ililenga kujumuisha makundi yote ya jamii katika kupambana na vitendo vya ukatili,” alisema Dk Mhando kwenye majibu yake.

“Kampeni nyingine ni ile ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA) ambayo ni kampeni ya Wananchi Wazalendo waliojitolea kuelimisha jamii na kuibua changamoto za ukatili ili hatua stahiki zichukuliwe na mamlaka husika,” aliongeza.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *