Changamoto Zinazokabili Utoaji Haki Jinai Kwa Watoto Tanzania Zatajwa

Moja ni kukosekana kwa mbinu za kitaalaam za mahojiano baina ya watoto ambao ni wahanga wa ukatili wa kingono na maafisa wa polisi na Ustawi wa Jamii

Dodoma. Kukosekana kwa mbinu za kitaalaam za mahojiano baina ya watoto ambao ni wahanga wa ukatili wa kingono na maafisa wa polisi na Ustawi wa Jamii kumetajwa kuwa ni moja kati ya changamoto nyingi zinazokwamisha utekelezaji wa utoaji haki jinai kwa watoto nchini Tanzania.

Hayo yalibainishwa hivi karibuni na Afisa wa Ustawi wa Jamii Ikusubisya Kasebele wakati wa mkutano wa siku mbili ulioandaliwa na Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) jijini hapa na ambao uliwakutanisha wadau mbalimbali wanaohusika na utoaji haki jinai kwa watoto wanaoathirika na ukatili wa kingono.

Akiwasilisha mada yake juu ya Haki Jinai kwa Watoto Waliokinzana na Sheria na Wahanga wa Ukatili wa Kingono, Kabesele alibainisha changamoto kadhaa zinazolikabili zoezi zima la utoaji haki jinai kwa watoto nchini Tanzania, ikiwemo la ukosefu wa mbinu za kitaalamu.

Ukosefu wa weledi

“Baadhi ya Maafisa wa Polisi na Maafisa Ustawi wa Jamii [wanakosa] mbinu za kitaalamu  za mahojiano na watoto wahanga wa ukatili au mashuhuda wa matukio ya  jinai,” Kabesele alibainisha.

Hali hii, pamoja na ile ya baadhi ya Maafisa Ustawi wa Jamii kutokuwa na weledi  katika usimamizi wa mashauri ya ulinzi wa mtoto, hupelekea kesi nyingi za ukatili kuwa na mwendelezo usiofaa kwani maafisa hao hushindwa kuomba amri za Mahakama za ulinzi na huduma kwa watoto waliofanyiwa ukatili.

Changamoto nyengine zinazohusiana na zoezi zima la utoaji haki jinai kwa watoto nchini Tanzania kwa mujibu wa Kabesele ni pamoja na: Desturi ya kuficha taarifa za ukatili dhidi ya watoto katika familia na jamii; familia kuwaficha watoto  wahanga wa ukatili hasa pale wanajamii wanapotoa taarifa; na mashahidi kutokuwa tayari kushiriki  katika mashauri ya ukatili dhidi ya watoto.

Changamoto nyengine ni ucheleweshwaji wa upelelezi, hususan kwenye makosa ya jinai ambayo hayana dhamana, kama vile mauaji, utakatishaji fedha, uhaini, uhujumu uchumi  na  uvamizi  wa kutumia silaha, kitu ambacho hupelekea watoto kukaa mahabusu muda mrefu. Pia, kuna changamoto ya watoto kuwekwa Mahabusu za magereza ya watu wazima  maeneo yasiyo na mahabusu za watoto.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Joaquine De Mello, ambaye alikuwa ni mgeni rasmi wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano huo, alibainisha kwamba kwa miaka ya hivi karibuni, unyanyasaji wa kingono kwa watoto nchini Tanzania umeendelea kuchukua sura mpya, hususan ukizingatia ukuaji wa utandawazi na matumizi makubwa ya mitandao.

Jaji De Mello amebainisha kwamba suala la ulinzi thabiti wa mtoto unahitajika na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola wale wote wanahusika na vitendo hivyo.

Anafafanua: “Mtoto yeyote unayemfahamu na usiyemfahamu kila siku yuko hatarini kunyanyasika kingono kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea duniani pamoja na tabia zetu kuathirika katika jamii zetu. Nikiwa sehemu ya wapiganaji katika ya vita hii ya unyanyasaji dhidi ya ukatili wa kingono kwa watoto, sina budi kusema kwamba kwa pamoja tutaweza.”

Ushiriki wa jamii

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) lililoandaa mkutano huo Koshuma Mtengeti alibainisha kwamba hivi sasa kumemekuwa na wimbi kubwa la watoto wanaofanyiwa vitendo vya ukatili na hivyo juhudi za pamoja zinahitajika miongoni mwa wadau kukomesha vitendo hivyo.

Akielezea umuhimu wa ushiriki wa jamii kwa ujumla wake katika kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, Mtengeti aliieleza The Chanzo pembezoni mwa mkutano huo:

“Unakuta hapa kuna masuala mazima ya ushahidi kutokamilika  na tunajua kosa la jinai  lazima Mahakama ijiridhishe  kiasi ya kwamba haina mashaka yoote. Kwa hiyo, kama jamii haitatoa ushirikiano katika masuala mazima ya kutoa ushahidi mahakamani, basi unakuta wale wanaotenda ukatili wanarudi kwenye jamii [na] wanarudia tena [kufanya huo ukatili].  Kwa hiyo, inakuwa akama hakuna kilichofanyika.’’

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Dodoma. Unaweza kumfikia kupitia jaquelinevictor88@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii pia unaweza kuwasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Jackline Kuwanda

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved