Kisukari sio ugonjwa mpya masikioni kwa watu wengi, na kwa muda mrefu ugonjwa huu kama ilivyo kwa magonjwa mengine yasiyoambukiza ulionekana ugonjwa wa wenye pesa na watu wa mjini.
Kadri miaka inavyosonga, magonjwa yasiyoambukiza yameongezeka kwa kasi na dhana hii potofu imebadilika. Hali hii inachangiwa na mabadiliko ya mitindo ya maisha. Takwimu zinaonyesha kuwa mnamo mwaka 2011, asilimia 2.8 ya watanzania walikuwa na kisukari lakini kufikia mwaka 2021 namba hii imeongezeka kufikia asilimia 12.8, ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.
Licha ya kuwepo kwa taarifa nyingi kuhusu ugonjwa wa kisukari na namna ya kujikinga, bado kuna uelewa mdogo kwa jamii kuhusu namna ugonjwa huu huathiri mifumo ya mwili, hivyo kupelekea wagonjwa wengi wenye kisukari kuchelewa kupata matibabu pale wanapopata athari za ugonjwa huu.
Hii hupelekea ongezeko la ulemavu unaoepukika na gharama kubwa za matibabu. Imani za kidini na kitamaduni pia zinachangia kuchelewesha matibabu sahihi kwani wagonjwa wengi kituo chao cha kwanza baada ya kupata athari za kisukari huwa ni kwenda kwa waganga wa jadi kuaguliwa au viongozi wa dini kuombewa.
SOMA: Je, Unafahamu Kwamba Hata Mtoto Anaweza Kupata Kifua Kikuu?
Kisukari huathiri vipi sehemu mbalimbali za mwili?
Ili kuelewa namna gani kisukari huathiri mifumo ya mwili, kwanza hatuna budi kuelewa unapoambiwa una kisukari inamaanisha nini? Ni nini kimekwama katika mfumo wako wa mwili hadi kusababisha sukari inashindwa kuchakatwa vema na kupelekea damu yako kuwa na kiwango kikubwa cha sukari kuliko kawaida?
Ni kati ya hivi viwili, aidha kongosho imeshindwa kutengeneza homoni ya insulini ambayo ina jukumu la kuchakata sukari au mwili umeshindwa kuitikia kazi ya insulini licha ya kwamba kongosho inafanya kazi vizuri.
Sukari inapokuwa nyingi katika damu, huathiri mfumo wa mzunguko wa damu kwa kuanzia kwenye mishipa midogo na mikubwa ya damu. Hiki ndicho kiini cha athari nyingi za kisukari zinazoonekana katika sehemu mbalimbali za mwili.
Uwepo wa sukari nyingi katika damu hupelekea kutengenezwa kwa mafuta katika kuta za ndani za mishipa ya damu; baada ya muda mafuta haya husababisha mishipa ya damu kuwa na kipenyo chembamba hivyo kupunguza mtiririko wa damu katika mishipa hiyo.
Matokeo ya mabadiliko hayo ya mishipa ya damu katika macho hupelekea kuona maruweruwe au kupata upofu; katika figo hupunguza uwezo wa figo kuchuja takamwili; katika ubongo husababisha kiharusi (stroke); na katika moyo husababisha shambulio la moyo.
Sukari nyingi katika damu huathiri pia mfumo wa fahamu wa mwili kwa kuharibu mishipa ya fahamu na kupelekea kushindwa kuhisi stimuli mbalimbali. Hii hutokana na kuharibiwa kwa mishipa midogo ya damu inayopeleka virutubishi kwenye mishipa ya fahamu.
Kitendawili kikubwa cha wagonjwa wa kisukari kuwa na vidonda vinavyochelewa kupona hasa miguuni na mikononi, kinateguliwa na namna ambavyo sukari huathiri mishipa ya damu na mishipa ya fahamu. Mgonjwa wa kisukari anapopata kidonda ilhali mishipa yake ya fahamu ya miguuni imeathiriwa na kisukari, hatapata maumivu na hivyo anaweza kuumia asijue hadi atakapoona kidonda.
Uponyaji wa kidonda chochote huchangiwa na mzunguko wa damu katika eneo hilo, ili kufikisha dawa, seli hai nyeupe zinazopambana na vijidudu na virutubishi ambavyo ni muhimu. Hivyo basi, mishipa ya damu ya miguuni iwapo imeharibiwa na kisukari, mzunguko wa damu katika miguu unapungua na uponyaji pia hupungua.
Lakini muhimu zaidi, sukari nyingi hutengeneza mazingira ya mazalia ya bakteria hivyo kuchelewesha zaidi uponyaji wa kidonda. Ndio maana mgonjwa wa kisukari anapofika na kidonda katika kituo cha kutolea huduma za afya, hatua ya kwanza huwa ni kumpima sukari na kudhibiti kiwango chake cha sukari; kwani bila hivyo hata kidonda kisafishwe na dawa gani, kupona ni ndoto za Alinacha.
Jilinde, Fahamu Namba Zako
Ingawa athari nyingi za kisukari hutibika, nyingine nyingi hupelekea ulemavu wa kudumu na magonjwa ya muda mrefu kama upofu, kukatwa miguu, figo kushindwa kufanya kazi na kupooza kutokana na kiharusi.
Hivyo basi, kama wahenga walivyosema kinga ni bora kuliko tiba. Kwa wagonjwa wote wa kisukari, unywaji sahihi wa dawa au uchomaji sahihi wa sindano ni ufunguo wa kuepuka madhara haya. Hudhuria kliniki kama ulivyoelekezwa na daktari, kula mlo sahihi na hakikisha unajipima sukari kama ulivyoelekezwa.
Fanya mazoezi na epuka matumizi ya pombe. Lakini muhimu zaidi ni kujichunguza kabla ya kulala iwapo umepata jeraha lolote hasa miguuni. Inashauriwa kuvaa viatu vya kufunika ili kupunguza uwezekano wa kupata majeraha.
Nunua viatu wakati wa jioni kwani wazoefu wanasema jioni miguu inakuwa imevimba kidogo hivyo ile ndio saizi sahihi ili usije vaa viatu vinavyobana vitakavyopelekea michubuko na vidonda.
Kisukari ni ugonjwa usioambukizwa na unagharimu kiasi kingi cha fedha kupata matibabu. Tabia bwete huchangia kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kupata kisukari hivyo unashauriwa kufanya mazoezi angalau kuhakikisha umetembea hatua 10,000 kwa siku.
Fahamu uzito wako, kiwango cha sukari na shinikizo la damu. Magonjwa yasiyoambukiza ni janga linaloongezeka kwa kasi hasa katika nchi zinazoendelea, na kiwango cha uchumi kinatishia madhara makubwa kwani matibabu yake ni gharama si tu kwa fedha lakini pia kwa muda na nguvukazi. Inahitaji nidhamu ya hali ya juu kuweza kuushinda ugonjwa huu.
Kuduishe Kisowile ni daktari na mchambuzi wa masuala ya afya ya umma. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia kuduzekudu@gmail.com au kupitia Twitter kama @Kudu_ze_Kudu. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.