The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tunahitaji Makavazi Mengi Zaidi ya Kidijitali Kama Lile la Salim Ahmed Salim

Hatua ya familia ya Salim Ahmed Salim kuweka hadharani nyaraka zinazowasaidia Watanzania kuifahamu historia yao ni ya kupongezwa na kutiwa moyo.

subscribe to our newsletter!

Niseme ukweli kwamba, kama isingekuwa kwa lengo mahususi la kuandika insha hii fupi kuhusu kavazi hilo, nisingefahamu utajiri wa taarifa, maarifa na historia uliowekwa wazi kwa umma wa Watanzania, na dunia kwa ujumla, na Kavazi la Kidijitali la Salim Ahmed Salim, kavazi pekee, na la aina yake, katika historia ya Tanzania.

Ndiyo, nafahamu umuhimu wake kama hazina ya historia ya Tanzania na Afrika; hili halijawahi kuwa na mashaka akilini mwangu. Lakini kukaa kwa muda kwenye kavazi hilo, lililozinduliwa hapo Septemba 30, 2023, na Rais Samia Suluhu Hassan, kulinifanya niudurusu upya mtazamo niliokuwa nao kuhusu kisima hicho cha maarifa, na kuhitimisha kwamba naweza kuwa niliudogosha umuhimu wake.

Nikiwa kama mwandishi wa habari, na kwa kipekee sana kama mhariri, taarifa, hususan zile zinazohusiana na Tanzania, ni malighafi muhimu sana kwenye jitihada zangu na za chombo changu cha habari kwenye uzalishaji wa maudhui yatakayowasaidia wasomaji wetu kuboresha maisha yao kwa namna mbalimbali. Kingine muhimu sana kwenye mchakato huo ni upatikanaji wa haraka wa taarifa hizo, bila shaka.

Tofauti na uzalishaji wa bidhaa nyingine ambazo malighafi zake huenda zikawa ni rahisi kupatikana, uzalishaji wa maudhui ya habari ni mgumu sana, hususan kutokana na ukweli kwamba taarifa, na sana sana taarifa sahihi, ni bidhaa adimu sana, hali inayokwamisha dhima adhimu ya wanahabari ya kuwahabarisha wananchi mambo yanayowahusu.

Kupata taarifa

Hali ni mbaya zaidi hapa nchini kwetu ambapo motisha ya kuficha taarifa miongoni mwa wenye mamlaka, kama vile Serikali, ni kubwa sana kuliko ile ya kuzitoa taarifa hizo. Sisi waandishi wa habari, pengine kuliko mtu mwingine yoyote yule, tunalishuhudia hili kila siku wakati wa kutimiza wajibu na majukumu yetu ya kulihabarisha taifa ili liwe katika nafasi nzuri ya kuendelea.

SOMA ZAIDI: Samia Azindua Tovuti ya Salim Ahmed Salim. Aagiza Tovuti ya Kumbukumbu Muhimu za Historia Ianzishwe

Utakumbuka kwamba hapa kwetu hakuna utaratibu, uliozoeleka sehemu mbalimbali za dunia zinazoongozwa na mfumo wa kidemokrasia, wa kufichua, au declassify kwa kimombo, siri rasmi na za kitaifa, haijalishi siri hizo zimedumu kwa miaka mingapi. Kumbuka pia kwamba hiyo ni nchi yenye sheria inayohusu upatikanaji wa taarifa na kupata taarifa imewekwa kwenye Katiba kama haki ya msingi.

Ni katika muktadha huu ndipo familia ya Salim Ahmed Salim, moja kati ya wanadiplomasia wa kipekee kuwahi kulitumikia taifa hili, ilipoamua kuweka hadharani maelfu, kama siyo mamilioni, ya taarifa ambazo mzalendo huyu alizikusanya wakati wa utumishi wake, ikiwafungulia pazia Watanzania, na dunia, kuiona historia kupitia jicho la waziri mkuu huyo mstaafu. Nina mashaka kama tunatambua uzito wa hatua hii.

Kavazi hili limesheheni taarifa zilizopo katika miundo mbalimbali – mahojiano, hotuba, maandiko ya kitaaluma, barua, na kadhalika – zinazompatia msomaji mtazamo wa kihistoria kwenye mambo kadhaa ya nchi na kidunia, ikiwemo, kwa mfano, kinyang’anyiro cha kumpata mrithi wa Boutros Boutros-Ghali kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, au Vita vya Gulf kwenye miaka ya 1990.

Kinachonivutia

Binafsi ninavutiwa na namna taarifa hizi zilivyopangiliwa, utaratibu unaomuwezesha msomaji kujikita na sehemu moja tu ya kavazi bila kuingiliwa na sehemu nyingine. 

Msomaji, kwa mfano, anaweza kwenda kwenye sehemu ya mahojiano, na akapata kuona mahojiano na vyombo vya habari tu ambayo Dk Salim aliwahi kufanya kwenye utumishi wake. Akitaka kusoma hotuba, anaweza kwenda kwenye sehemu hiyo na kukutana na hotuba tu, na kadhalika.

SOMA ZAIDI: Viongozi Hawa Kumi wa Tanzania Watakuhamasisha Kupenda Kusoma Vitabu

Kingine kinachonivutia ni kwamba kavazi linaruhusu mtu kutafuta, yaani limejengewa miundombinu inayomuwezesha mtu kutafuta kitu fulani mahususi kwenye kavazi hilo, hali inayompunguzia usumbufu na kumuwezesha kupata taarifa fulani kwa wakati, jambo ambalo ni la muhimu sana kwangu mimi kama mwandishi wa habari. Kavazi linakupa ruhusa ya kuchuja utafutaji, kitu kinachokuwezesha kupata taarifa unayoitafuta kwa urahisi sana.

Lakini kikubwa zaidi kinachonivutia ni kwamba kavazi linampa msomaji uhuru wa kupakua hizi nyaraka, ambazo ukumbuke ni halisi kabisa, yaani kama ni barua ni kama vile ilivyoandikwa na Dk Salim mwenyewe, na kuziweka hizo nyaraka pembeni. 

Hili ni muhimu, kwa watu kama vile watafiti, ambayo inawaepushia usumbufu wa kuja kwenye kavazi kila mara wakati wa utafiti wao. Pia, kuna wengine kama sisi ambao furaha ya kusoma tunaipata kutoka kwenye kile kitu tulichokisha kwenye mikono yetu tu na siyo vinginevyo, na naomba usinishutumu kung’ang’ania ukale!

Vya kuboresha?

Lakini nadhani kuna mambo ambayo familia inapaswa kuyatafakari kuhusiana na hili kavazi, hususan kama lengo kweli ni Watanzania wengi zaidi kulitembelea na kujifunza kutokana na yaliyomo humo. 

Moja ni suala la lugha, na hapa sitaki nieleweke vibaya kwamba Watanzania hawajuwi kusoma lugha ya Kingereza. Ukweli ni kwamba wapo wanaoifahamu lugha hiyo na tupo, wengi tu, ambao hatuifahamu.

SOMA ZAIDI: Mfuko wa Utafiti wa UVIKO-19 wa Amne Salim: Watafiti Wamebaini Nini?

Familia inaweza kulifikiria hili na kuona inaweza vipi kulitatua. Njia moja ambayo naifikiria mimi ni kuwa na chaguzi za lugha kwenye tovuti, ili mtu achague kama anataka Kiswahili au Kingereza. 

Kuhusu nyaraka zilizochapishwa kwenye kavazi hilo, ambazo zipo kwenye Kingereza, familia inaweza kuzitafsiri na kuziweka kwenye Kiswahili. Ni kweli zinaweza kupoteza utamu na ladha yake halisia, lakini, kama tusemavyo Wapemba, msomaji hatakosa kaa na gando!

Hli ni muhimu kwa sababu ili taarifa, na maarifa yanayotokana nazo, ziwe na manufaa yoyote kwa jamii lengwa, ni lazima wanachama wa jamii hiyo wawe na nyenzo na uwezo wa kuzifikia taarifa hizo na kuzielewa. Sihitaji kutoa nadharia kukuonesha uhusiano uliopo kati ya lugha na uwezo wa mtu kuielewa dunia yake. Ni matumaini yangu kwamba familia italitafakari pendekezo hili.

Jambo jingine ambalo nadhani linahitaji tafakuri ni upatikanaji wa kavazi lenyewe, kwamba kwa sasa kavazi hili linapatikana mtandaoni tu, kama jina lake linavyodokeza, Kavazi la Kidijitali la Salim Ahmed Salim. Lakini kama ilivyo kwa lugha, siyo kila Mtanzania ana nyenzo zinazomuwezesha kupata taarifa na maarifa yaliyopo mtandaoni.

Hapa nikiri kuwa sina pendekezo la namna ya kurekebisha kasoro hiyo, lakini kama familia itafikiria kuwa na kavazi nje ya mtandao, pengine kwa kuwa na jengo angalau hata hapa Dar es Salaam, kwa kuanzia, ambapo Watanzania watakwenda kusoma nyaraka hizo, inaweza kuwa mwanzo mzuri.

Mfano wa kuigwa

Lakini yote kwa yote, hatua hii ya familia ya Dk Salim Ahmed Salim kuamua kuweka hadharani nyaraka zinazowasaidia Watanzania kuifahamu historia yao ni hatua ya kupongezwa sana na ya kutiwa moyo. 

SOMA ZAIDI: Nitakavyomkumbuka Mwinyi, Mzee Rukhsa Asiyekuwa na Tamaa ya Madaraka

Ni imani yangu kwamba familia nyingine za viongozi wetu waliowahi kulitumikia taifa hili zinaweza kuiga mfano huo kama sehemu ya mchakato mpana wa kujenga kizazi kinachoifahamu historia yao.

Kuifahamu historia ya nchi yako ni muhimu sana kwani mbali na kukusaidia kuifahamu leo na kesho yako, inakukinga pia na udanganyifu ambao baadhi yetu huufanya kwenye kuelezea matukio muhimu ya nchi yetu ili kukidhi matakwa binafsi na muda mwingine yenye nia ovu ndani yake. 

Nisikuchoshe, nikukaribishe kulitembelea kavazi hili, kama bado hujafanya hivyo, na kujionea mwenyewe utitiri wa maarifa yaliyopo humo. Na kama baada ya kufanya hivyo utakuwa na kitu cha kusema, basi utakituma hapa The Chanzo, na sisi tutakichapisha. 

Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *