Sura yake imeshafutika akilini kwangu, lakini namkumbuka vyema. Alikuwa mama mtu mzima, mnene hivi, sare yake ya gauni jeupe na kofia ya nesi zilimpendeza. Aliketi kwenye kiti akifuta vioo vya taa ya chemli, pembeni ya miguu yake taa nyingine zikisubiri.
Hii ilikuwa ni ada kila jioni kwani taa hizo zilikuwa ndio chanzo cha mwanga pale hospitali usiku. Umeme ulikuwa haujafika bado. Pembeni yake tuliketi sisi, mimi na mama yangu pamoja na wagonjwa wengine wa kila rika na jinsia.
Hii ilikuwa ni foleni ya kusubiria kuchoma sindano. “Hebu nenda kaangalie kama sindano zimechemka niwatoe hawa,”nesi yule alimuelekeza nesi mwenzake ambaye alielekea maabara.
Inaweza kuwa ajabu leo, lakini hii ilikuwa kawaida zaidi ya miaka 14 iliyopita. Ndio, sindano zilichemshwa ili zitumike tena. Akatugeukia, “kila mmoja awe na daftari lake la matibabu aliloandikiwa na daktari.”
Daktari wetu mmoja mpendwa sana, mama wa makamo ambaye naukumbuka vyema muandiko wake. Aliandika kama mtoto anayejifunza kuandika darasa la kwanza. Hii ilinishangaza hadi hapo baadaye nilipofahamu kuwa alipata kiharusi, na baada ya mazoezi tiba alirudi kuendelea na kazi yake. Wakati huo wengi tuliamini kuna watu wamemloga daktari wetu.
SOMA PIA: Kisukari: Ugonjwa Unaohitaji Nidhamu
Sindano zikachemka, tukaanza zoezi. Ilipofika zamu yangu, mama akamkabidhi nesi yule mfuko wa dawa na daftari; nilikuwa nachoma sindano za Quinine baada ya kulazwa kwasababu ya Malaria kali. Ilikuwa ni wiki moja tu baada ya mdogo wangu kuruhusiwa hospitali akiwa na Malaria kali pia.
Niligeuka nikachomwa sindano yangu, nikajikaza nisilie kwani hii haikuwa ya kwanza. Akatuaga turudi tena kesho yake kwa ajili ya kuendelea na dozi. Niliruhusiwa tukarudi wodini, tukakusanya vitu vyetu, tukawaaga kina mama waliolazwa na sisi; nao walikuwa na watoto wao kwa magonjwa mbalimbali, tukaanza kuchanja mbuga kurudi nyumbani.
Ulikuwa mwendo wa dakika 5 kwa miguu. Jua lilikuwa linazama. Nikashusha pumzi nikitoka katika jengo la hospitali. Nje zilipaki baskeli kadhaa zilizokuwa na mizigo, wagonjwa waliotoka vijiji vya mbali hao. Mbele ya hospitali ilisimama misufi mirefu, iliyopukutisha sufi na kufanya udongo mwekundu kupambwa na sufi nyeupe.
Ng’ambo ya pili ya barabara lilikuwa soko, wafanyabiashara walikuwa wanafungasha mizigo yao na wenye maduka wanafunga kutimiza mahesabu ya siku.
Leo, nilikuwa naondoka natembea; siku 5 zilizopita nilifika hapo nikiwa nimebebwa mgongoni na mama, mwili umeishiwa nguvu, ngozi yangu ilikuwa ya moto kama nimechemshwa na mkojo kama CocaCola.
Tukapokelewa na haraka sana nikawekewa dripu, nikatolewa damu kwa ajili ya vipimo na tukapewa kitanda wodini. Neti zikashushwa, nesi akapita na chemli kuhakikisha kila mgonjwa ana kila anachohitaji, usiku ukayoyoma.
SOMA: Huduma za Afya ya Akili Ziingizwe Kwenye Huduma za Mama na Mtoto
Wakati nikiondoka, mama aliwashukuru sana kwa kunitibia vyema. Leo hii, mambo mengi sana yamebadilika. Mengi sana. Ile barabara ya vumbi jekundu imetandikwa mkeka wa lami. Umeme umepita, chemli imebaki historia. Sindano zinatumika mara moja tu, hatuchemshi tena.
Tumetoka mbali hakika. Tangu kampeni ya neti zenye dawa zinaanza kutangazwa, vipimo vya haraka (rapid test) vya Malaria vinaletwa hadi leo mikakati ya kupima bure inawekwa. Na kwa baadhi ya nchi za Afrika, chanjo ya Malaria imeanza kutolewa.
Ni yule ambaye hajaona mabadiliko haya katika sekta ya afya ndio atasema hakijafanyika chochote. Licha ya mabadiliko hayo, Malaria bado ni tatizo hapa nchini. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, watu milioni 19.8 walipima malaria mwaka 2023 na kati yao watu milioni 3.46 walikutwa na Malaria.
Hii ni zaidi ya robo ya waliopimwa Malaria. Vifo vitokanavyo na Malaria vimepungua kutoka vifo 1,882 mwaka 2021 hadi kufikia vifo 1,540 mwaka 2023. Licha ya mabadiliko haya, kwa tulipofikia sasa hatukutakiwa kuwa na vifo vitokanavyo na Malaria kabisa.
Afua nyingi za kujikinga na kupambana na Malaria nchini Tanzania ni juhudi za wafadhili; lakini mikakati ya ndani inachangia kwa kiwango kikubwa katika utekelezaji na mafanikio ya afua hizi. Mojawapo ya juhudi za ndani zinazofanyika ni tafiti mbalimbali zinazohusu Malaria na mbu ambazo hufanyika katika kituo cha tiba Ifakara.
SOMA PIA: Je, Unafahamu Kwamba Hata Mtoto Anaweza Kupata Kifua Kikuu?
Kituo hiki kimechangia kwa kiasi kikubwa hata upatikanaji wa chanjo ya Malaria ingawa bado chanjo hii haijaanza kutumika nchini Tanzania. Kwa mujibu wa ripoti ya Tanzania Demographic Health Survey(TDHS) ya mwaka 2022, umiliki wa neti zenye dawa bado hayaridhishi kwani asilimia 67 tu ya watanzania wanamiliki neti zenye dawa na karibia nusu yao walipewa katika kampeni za ugawaji neti kwa jamii.
Na matumizi ya neti hizi yapo chini zaidi ikiwa ni asilimia 53 tu ya watu hutumia neti hizi. Miaka michache iliyopita, baadhi ya watu waliogawiwa neti hizi walizigeuza uzio wa mabanda ya bata na kuku. Hii inaonyesha kuwa aidha uelewa kuhusu uzito wa ugonjwa wa Malaria bado hautoshelezi, au jamii haijali tena kuhusu Malaria.
Na kusema ukweli kampeni za Malaria zimepoa kwa muda sasa. Labda kwasababu mambo ni mengi na muda ni mchache; magonjwa yasiyoambukizwa yanashika kasi na magonjwa ya mlipuko yanaongezeka duniani kote lakini hii haibadilishi ukweli kuwa kila dakika, mtoto aliye chini ya miaka 5 anafariki kwasababu ya malaria duniani.
Tarehe 25 Aprili, tunaadhimisha Siku ya Malaria Duniani kwa kauli mbiu isemayo Ni wakati wa kuwasilisha Ziro Malaria: Wekeza, Vumbua, Tekeleza. Ni vizuri kuchukua wasaa huu kutazama tulipotoka, tulipo na tunapoelekea katika mapambano dhidi ya Malaria. Juhudi nyingi sasa zielekezwe katika kudhibiti mazalia ya mbu, na hili ni jukumu la serikali na wananchi wote.
Wakati kufyeka majani, kufukia madimbwi na kufunika maji yaliyotuama katika mazingira tunayoishi ni jukumu la wananchi; serikali ina jukumu la kuhakikisha miundombinu ya majitaka na mitaro barabarani inafanya kazi ipasavyo kuepusha mazalia ya mbu.
Ule utamaduni wa usafi wa mazingira uendelezwe wakati tunasubiria chanjo ya Malaria. Waandishi na watengeneza maudhui ya elimu ya afya kwa umma nao wasibaki nyuma; turudishie watoto wetu nao wasome vitabu vya “Juma na Malaria”. Kwa juhudi za pamoja, ifikapo mwaka 2030 tunaweza kufikia lengo la kutokomeza Malaria na kuungana na Algeria na Mauritius kuwa nchi za Afrika ambazo ni huru dhidi ya ugonjwa wa Malaria.
Kuduishe Kisowile ni daktari na mchambuzi wa masuala ya afya ya umma. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia kuduzekudu@gmail.com au kupitia Twitter kama @Kudu_ze_Kudu. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.