Katika malezi, kuna changamoto nyingi na kuna vitu ambavyo kila mzazi angependa mtoto wake awe navyo. Tabia njema ni moja kati ya vitu hivyo. Tukiulizwa leo, kama tungependa watoto wetu warithi tabia zetu, majibu yetu yatakuaje? Swali hili litakuwa rahisi sana kulijibu endapo tutafanya mambo yafuatayo.
Moja ni kuwajulia hali watoto wetu na kuwakumbatia kwa upendo; namna hii itawasaidia watoto kukuza dhana ya upendo na kujiamini baina yao na ndugu wengine wa familia pamoja na kukuza tabia ya kujali na kuwajulia hali watu wengine.
Mbili, kuwa watu wema kwa majirani zetu. Tusiwazungumzie vibaya majirani zetu na watu wengine huku watoto wanasikia, kumbuka watoto wanaiga na kuiishi tabia wanazoona wazazi na walezi wakifanya wakijua ni hali ya maisha ya kawaida.
Tatu, tuwapigie simu au kutembelea wazazi na ndugu zetu mara kwa mara na tuwahimize watoto kuzungumza na kuwatembelea pia. Kwa kufanya hivi watajifunza kutoka kwetu umuhimu wa kuwajali na kuwatunza wazazi na vivyohivyo watafanya wakiwa wakubwa.
Nne, tujenge tabia ya kuwahadithia hadithi za kuwajenga kiakili kwa kujadiliana nao masuala mbalimbali ya msingi kila tukipata wakati, kama vile wakati tunawapeleka shule, siku za mapumziko, tukiwa nao jikoni au shambani.
SOMA ZAIDI: Namna Bora Zaidi ya Kuwathamini Watoto Wetu ni Kusikiliza Mawazo Yao
Pia, tunaweza kuwahimiza watoto wetu kusoma vitabu ambavyo vinafundisha maadili na tabia njema, ikiwemo kuwasomea hadithi zinzotoka kwenye vitabu vya dini. Tusali nao na kuwafundisha jinsi ya kusali ili waige kutoka kwetu, hii itawasaidia kuwa na imani ya dini lakini pia kuwajengea kumbukumbu nzuri ya mahusiano mazuri na mzazi wakiwa wakubwa na wao kuwa wazazi wa mfano kwa watoto wao. Ni vizuri sana kumkuza mtoto anayemjua na kumpenda Mungu.
Tano, tuwafundishe watoto usafi na utanashati kwa namna tunavyojiweka sisi wenyewe. Kuwa mtanashati muda wote, kuoga, kusafisha kinywa, vaa nguo safi na nadhifu, hata tunapokua nyumbani. Hii itawajengea watoto tabia ya usafi na kujipenda muda wote si pale tu wanapotaka kwenda matembezi.
Sita, tujaribu kutokuwagombeza watoto kwa kila kosa watakalofanya, kumbuka bado wanakua na kujifunza, hivyo watakosea. Wakati mwingine kujipa muda wa kuwaacha huru na kutizama matendo na maneno yao kwa kina inasaidia kuzisoma tabia zao na kuwapa muda wa kujifunza na kujiamini. Tusiwe watu wenye gadhabu na kuwakatisha tamaa wanapotoa mawazo au hisia zao.
Saba, tujitahidi kuthamini faragha ya watoto wetu. Tukiingia vyumbani mwao tubishe hodi, siyo tu kuingia bila kutoa tarifa. Hii itawapa fursa ya kujifunza kufanya hivyo pale wanapotaka kuingia chumbani kwa wazazi na kuwafundisha tabia ya kuheshimu faragha.
SOMA ZAIDI: Baba Simama, Shiriki Kikamilifu Katika Malezi, Makuzi ya Mtoto Wako
Nane, tunapotofautiana kama wazazi, tujitahidi kutokutupiana maneno, au kufokeana, mbele za watoto. Ni vyema kuwa na subra na uvumilivu na kujipa muda wa kutatua matatizo yetu nje ya macho ya watoto. Namna hii itawajengea tabia ya kuheshimiana wao kwa wao kama watoto, lakini pia wakiwa watu wazima hapo baadaye.
Tisa, tukiwakosea watoto, tuwaombe msamaha ili kuwafundisha jinsi ya kuthamini hisia za wengine na waweze kutambua wanapokosea na kuomba msamaha, jambo ambalo ni jema na hujenga tabia nzuri ya kuthamini hisia za watu Katika jamii .
Hata hivyo, yote haya hayawezi kufanikiwa kwa siku moja. Tabia hujengwa kwa muda siyo jambo la siku moja, cha msingi ni kuzingatia kwamba tunawafundisha watoto tabia hizo.
Wahenga walituasa, Mvumilivu hula mbivu; hivyo tukiwalea na kuwafundisha watoto wetu kwa uvumilivu na upendo tutazaa matunda mema ya kukuza watu wazima wa baadae wenye tabia njema.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.
One Response
Hakuna acount ya instagram ili niweze kufuatilia taarifa kupitia huko??