The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Dondoo Hizi Zitakusaidia Mzazi Kumlinda Mtoto Kipindi Hiki cha Mvua

Mvua inaweza kuwa na athari kubwa na ni jukumu letu kama wazazi na walezi kuhakikisha tunatengeneza mazingira ya usalama kwa ajili ya watoto.

subscribe to our newsletter!

Katika kipindi hiki cha msimu wa mvua ni muhimu kwa wazazi na walezi kuchukua hatua za ziada kuhakikisha watoto wanabaki salama na wenye afya. Mvua inaweza kuwa na athari kubwa na ni jukumu letu kama wazazi na walezi kuhakikisha tunatengeneza mazingira ya usalama kwa ajili ya watoto.

Mvua kubwa inaweza kusababisha mafuriko, ambayo yanaweza kuwa hatari kwa watoto na kusababisha kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza kama vile malaria na kipindupindu. 

Tujitahidi kuhakikisha watoto wanalala katika vyandarua na wanatumia mavazi yanayofaa kuzuia maambukizi kutoka kwa maji machafu. Pia, tuhakikishe watoto na familia nzima wanapata chanjo zote muhimu na kuzingatia usafi wa mazingira.

Pamoja na kwamba mvua na mafuriko huongeza uwezekano wa magonjwa tajwa hapo juu kwa sababu mifumo ya maji machafu kutoka katika maeneo ya viwanda na mifumo ya maji taka kuathiriwa, pia husababisha uharibifu kwenye mazao na kusababisha changamoto katika upatikanaji wa chakula. 

Hivyo, tujitahidi kuhifadhi vyakula vizuri kuepuka kula vyakula vilivyoharibika, au kuchafuka kwa maji machafu.

SOMA ZAIDI: Mzazi, Hakuna Ushahidi Kwamba Viboko Vinasaidia Katika Malezi ya Mtoto Wako

Katika kipindi hiki barabara zinaweza kuwa si salama kwa sababu ya uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja kutokana na mafuriko. Tumesikia habari za magari na watu kusombwa na maji barabrani. 

Hivyo, tuwe makini kwa kufuatilia mamlaka ya hali ya hewa na taarifa ya habari ili kufahamu ni barabara zipi zimefungwa na zipi hazipitiki. Pia, tuzungumze na watoto kuhusu uvukaji wa barabara na kucheza nje. 

Tuhakikishe usalama wa watoto wanapokwenda na kurudi shule, ikiwezekana wabaki nyumbani kama hali ya mvua inatishia usalama wao kama ilivyoagizwa na Serikali mwezi Aprili mwaka huu wa 2024.

Kuhusu mavazi, tujitahidi kuwavalisha watoto nguo ambazo zitawastiri na baridi, yaani nguo nzito au masweta. Wakiwa wanaenda shule, tuwapatie miamvuli na viatu vinavyokinga miguu na maji.

Wazazi pia tujitahidi kuzifahamu na kufuatilia sheria za shule kuhusu usalama wakati wa msimu wa mvua. Hii inaweza kujumuisha mavazi maalum ya shule, njia salama za kufika na kuondoka shuleni, na hatua za kuchukua wakati wa dharura.

SOMA ZAIDI: Hatua Tisa Muhimu Kutusaidia Wazazi Kuwarithisha Watoto Wetu Tabia Njema

Vidokezo hivi ni muongozo tu wa vitu ambavyo vipo ndani ya uwezo wetu kama wazazi na walezi; cha msingi ni kuwa makini katika kusimamia ulinzi na usalama wa watoto wetu katika kipindi hiki.


Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *