The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mzazi, Hakuna Ushahidi Kwamba Viboko Vinasaidia Katika Malezi ya Mtoto Wako

Ushahidi unaonesha kwamba adhabu ya viboko, makofi na nyingine kama hizo hazimsaidii mtoto. Badale yake, hupunguza tu hasira alizonazo mzazi juu ya kosa la mtoto.

subscribe to our newsletter!

Kwa sababu adhabu ya viboko ni moja kati ya adhabu zinazopelekea kuongezeka kwa matokeo ya ukatili duniani, kila ifikapo Aprili 30 ya kila mwaka hufanyika maadhimisho ya siku ya kutokomeza adhabu ya viboko ulimwenguni. 

Mnamo Machi 19, 2024, kuliripotiwa tukio la kusikitisha kuhusu mtoto mwenye umri wa miaka sita, Jonathan Makanyaga, aliyekuwa akisoma darasa la kwanza, aliyedaiwa kufariki kwa sababu ya kupigwa viboko na walimu. 

Takribani asilimia 60 ya watoto wa umri kati ya mwaka mmoja hadi 14 ulimwenguni hupitia adhabu hii kutoka kwa wazazi, au walezi, wao, hali inayodhihirisha ukubwa wa tatizo hili na umuhimu wa kuendelea kulipigia kelele.

Hapa nchini Tanzania, Sheria ya Elimu, Sura ya 353, marejeo ya mwaka 2002, inampa mamlaka waziri wa elimu kutunga kanuni za masuala mbalimbali zitakazokidhi utekelezaji wa masuala ya sheria hiyo. 

Mojawapo ya kanuni zilizotungwa ni Muongozo wa Elimu wa Adhabu ya Viboko Na. 294, au The Education (Corporal Punishment) Regulation G.N. 294 ya mwaka 2002.

SOMA ZAIDI: Hatua Tisa Muhimu Kutusaidia Wazazi Kuwarithisha Watoto Wetu Tabia Njema

Kanuni hizi zinatoa muongozo ni wakati gani adhabu ya viboko inatakiwa kutolewa na kwa kiwango gani na ni nani anapaswa kutekeleza adhabu hiyo.

Kanuni ya 3(1), kwa mfano, inasema kwamba adhabu ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhamu, au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima. Kanuni ndogo ya (2) inasema adhabu ya viboko itolewe kwa kuzingatia umri, jinsi na afya ya mwanafunzi, na isizidi viboko vinne kwa tukio lolote.

Nani achape?

Je, nani ana mamlaka ya kumchapa mwafunzi kisheria? Sheria inampa mamlaka mwalimu mkuu wa shule husika kutoa adhabu ya viboko, au kukasimisha mamlaka yake kwa umakini mkubwa kwa mwalimu yeyote kutoa adhabu hiyo. 

Mwalimu anayechaguliwa kutoa adhabu atakuwa na mamlaka ya kutoa adhabu pale tu atakapopata idhini ya mwalimu mkuu katika tukio husika.

Kanuni ya (5) inataka kila adhabu ya viboko inapotolewa kwa mwanafunzi kumbukumbu ya kutolewa kwa adhabu hiyo sharti iwekwe kwenye kitabu, ikitaja jina la mwanafunzi, kosa alilolifanya, idadi ya viboko na jina la mwalimu aliyetoa adhabu, na kumbukumbu hizo lazima zisainiwe na mkuu wa shule.

SOMA ZAIDI: Namna Bora Zaidi ya Kuwathamini Watoto Wetu ni Kusikiliza Mawazo Yao

Sheria hii inataka uchunguzi na kujiridhisha kuwa mwanafunzi amehusika moja kwa moja na kosa analotuhumiwa nalo ndipo hatua ya kupeleka suala lake mbele ya mwalimu mkuu ili atumie mamlaka aliyopewa kisheria kutoa adhabu stahiki kwa mwanafunzi linafuatwa.

Serikali ya Zanzibar imepiga hatua kidogo zaidi ya ile Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutokomeza adhabu ya viboko shuleni. Wakati Tanzania inaruhusu viboko shuleni, Zanzibar inakataza adhabu ya viboko katika shule za bweni na taasisi zingine zote watoto wanakoishi ama kupatiwa hifadhi.

Kwa ujumla, Tanzania na Zanzibar hazijafanya maboresho yeyote ‘makubwa’ na ya kiukombozi toka uhuru katika mifumo ya utoaji haki ili kuilinda haki ya mtoto dhidi ya vipigo shuleni. Kote, majumbani na shuleni, watoto wanapigwa ‘mithili ya wanyama’ kwa kisingizio cha ‘kuwanyoosha.’

Athari

Matokeo yake sote tunayashuhudia. Mwaka 2023, kwa mfano, mwalimu wa shule ya msingi Samanga, wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, aliripotiwa kumpiga mwanafunzi wa darasa la kwanza, mwenye umri wa miaka saba, kwa kosa la kupiga kelele darasani. 

Mtoto huyu aliripotiwa kufariki muda mfupi baada ya kipigo hicho. Wazazi wa mtoto huyo hawakupaswa kupitia maumivu ya namna hii kama Serikali ingetekeleza jukumu lake la kupafanya shuleni kuwa sehemu salama kwa watoto wetu.

SOMA ZAIDI: Baba Simama, Shiriki Kikamilifu Katika Malezi, Makuzi ya Mtoto Wako

Ni vyema kufahamu kuwa kupitia tafiti mbalimbali za malezi, wataalamu wanaamini kuwa adhabu za viboko na vipigo vingine kama makofi, mateke, na kadhalika, havina tija kwenye malezi na makuzi ya mtoto iwe ni nyumbani au shuleni. Adhabu hizi hazimsaidii mtoto bali hupunguza hasira alizonazo mzazi juu ya kosa la mtoto.

Kama lengo la kumuadabisha mtoto ni kumsaidia kurekebisha tabia na kujifunza pale alipokosea, basi hatutatimiza lengo kupitia adhabu zinazowaumiza watoto kimwili, kihisia au kisaikolojia. Vitendo hivi vinaonesha mwisho na ukomo wa mbinu za wazazi, walezi na walimu katika kuwasaidia watoto kurekebisha tabia.

Pia, kabla hata ya kutoa adhabu ni muhimu mtoto apewe fursa ya kujieleza na kusikilizwa, kama ni shuleni mzazi wa mtoto husika aitwe na afahamishwe juu ya tatizo na adhabu ijadiliwe. 

Wazazi na walimu tumekuwa tukiongozwa na hasira katika kuwaadhibu watoto na matokeo yake tunayaona na kujutia. 

Watoto wamekuwa hawakomi kukosea kwa sababu hawapewi nafasi ya kutafakari na kujifunza kutokana na makosa yao, bali wanajengewa nidhamu ya woga na kuwa waongo kwa kufanya makosa kwa uangalifu na kudanganya ili kukwepa adhabu kali.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini ni Muhimu kwa Wazazi Kuwashirikisha Watoto Kwenye Kupika?

Tunatoa wito kwa wazazi, walezi, walimu na jamii kwa ujumla, kujichunguza na kutathmini njia mbadala za kuadabisha watoto bila kutumia fimbo, vipigo au adhabu kali yoyote. Watoto wana haki ya kuishi na kujifunza kwa upendo na amani. 

Mbinu zinazotumika kuwaadabisha zisiwanyime haki hii. Kufanya mazungumzo na mtoto, na kumpa nafasi ya kutambua athari ya kosa alilolifanya tangu angali mdogo, itasaidia kuondoa athari za viboko katika makuzi na maendeleo ya watoto.

Wazazi na walezi pia wanaweza kufikiria kutoa adhabu mbadala kwa watoto, kama vile kumsimamisha masomo, kuita mzazi shuleni kujadili kwa pamoja namna ya kumsaidia mtoto, kumzuia mtoto kufanya mambo anayoyapenda kama kucheza na wenzake wakati wa mapumziko, kutazama TV, na kadhalika.


Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *