The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kwa Nini ni Muhimu kwa Wazazi Kuwashirikisha Watoto Kwenye Kupika?

Wengi wetu tumekua katika jamii ambazo wanawake ndiyo wanaofundishwa kupika, lakini kupika ni ujuzi muhimu wa maisha ambao kila binadamu anapaswa kufahamu.

subscribe to our newsletter!

Kuwahusisha watoto wakati wa kupika ni njia mojawapo ya kutengeneza kumbukumbu nzuri zitakazodumu milele. Pia, kupika na watoto wetu ni njia nzuri ya kukuza na kujenga uhusiano mzuri baina ya watoto na wazazi. 

Tunapowaalika watoto jikoni, hatuwafundishi tu stadi za upishi, bali tunawafundisha ujuzi muhimu wa maisha utakaowasaidia huko mbeleni, na kuwapa nafasi ya kushiriki sehemu ya tamaduni, mila na desturi za familia, pamoja na kujimudu pale watakapoanza kujitegemea.

Sababu nyingine ambayo inaweza kutuhamasisha kuwahusisha watoto jikoni ni kuongeza uwezekano wao wa kuandaa vyakula wanavyopenda. 

Wataalamu wa lishe wanaamini kwamba watoto huchagua na kubagua kula vyakula fulani aidha kwa sababu ya muonekano wa chakula, kuiga marafiki na ladha ya chakula husika. 

Hivyo, namna ambayo tunaweza kutatua suala hili ni kuwashirikisha watoto kupika ili waelewe jinsi gani mlo fulani unavyoandaliwa hatua kwa hatua, viungo gani vinatumika na vitu gani wangependa viongezwe katika mlo huo.

SOMA ZAIDI: Usafi ni Muhimu Sana Katika Makuzi ya Watoto Wetu, Tuuzingatie

Kwa kuzingatia hilo, kama hujawahi kuwaza kuwahusisha watoto wako katika kupika, basi leo tutajifunza hatua kadhaa zitakazokusaidia kufanya hivyo.

Cha kwanza kabisa chagua mapishi yanayofaa kwa mtoto wako. Chagua mapishi rahisi yenye viungo vichache na mbinu za kupikia rahisi ambazo zinafaa kwa umri na ujuzi wa mtoto wako.

Pili, andaa mazingira salama ya upishi. Hakikisha kwamba jikoni ni eneo salama kwa mtoto wako kwa kuondoa na kuhifadhi vitu hatarishi ambavyo hamtatumia, kama vile vitu vyenye ncha kali. 

Kisha mpatie vifaa na vyombo vya jikoni vinavyomfaa kushughulika navyo kama kitambaa cha jikoni na nguo ya kujistiri wakati wa kupika, yaani apron

Pia, mfundishe kuhusu kanuni za usalama jikoni, kama vile kunawa mikono kabla ya kushika chakula au kupika, kutumia kitambaa cha jikoni, au kitu chochote mbadala wakati wa kushika vyombo vya moto, kutokuchezea moto na jinsi ya kushika vitu vyenye ncha kali, pamoja na kuwasha na kuzima jiko kwa tahadhari.

SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kujenga Mahusiano Mazuri Kati ya Watoto Ndugu?

Baada ya hapo, muelezee mtoto pishi mtakalopika. Kabla ya kuanza kupika, pata muda wa kupitia kitu mtakochopika pamoja na kila hatua mtakayopitia na viungo vinavyohusika. 

Mhamasishe mtoto kuuliza maswali kama hajaelewa, na jaribu kuwa na uvumilivu katika wakati huo, hivyo ndivyo atakavyojifunza na kuonyesha udadisi wake. Kwa sababu kuna majukumu ya jikoni ambayo si kila mtoto anaweza kufanya, tunapaswa kugawa majukumu kwa watoto kulingana na umri na uwezo wao. 

Watoto wadogo wanaweza kusaidia katika kazi rahisi kama kuosha matunda na mboga, kuchanganya viungo, au kupanga meza ya chakula, huku watoto wakubwa wakishiriki katika kazi ngumu zaidi kama kupima viungo, kukata mboga, au kufuata maelekezo ya kupikia utakayompa.

Wahimize watoto kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa mapishi kwa kuwaacha wachanganye, wakande, au kugoroga viungo mpaka pale utakaporidhika na watie moyo kuchunguza ladha, muundo, na viungo tofauti mnapopika. Waache watazame na kunusa viungo, na kuwapa fursa ya kufanya marekebisho madogo kwenye pishi kulingana na mapendeleo yao.

Usisite kumsifu mtoto wako kwa juhudi na mafanikio yake mkiwa jikoni. Furahia na thamini ujuzi wake anaojifunza hata pale atakapokosea. Chakula kikiwa tayari keti pamoja kama familia kufurahia chakula mlichopika. 

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Mzazi Anashauriwa Amnyonyeshe Mtoto kwa Miaka Miwili?

Baada ya kula, chukua muda wa kujadili zoezi mililolifanya, muulize alifurahia nini, alijifunza nini, na kama kuna kitu chochote angependa kujaribu tofauti wakati mwingine mtakapopika pamoja. Mnaweza kuainisha aina ya vyakula ambavyo mngependa kupika wote kadri anavyozidi kukua.

Ni vyema pia katika zoezi la kupika kumsaidia mtoto kufahamu aina za vyakula na virutubisho vilivyonavyo. Hii itamsaidia mtoto kupenda kula chakula akijua anapata, au kukosa, faida gani mwilini, na itakusaidia kama mzazi kupunguza uwezekano wa mtoto wako kukataa vyakula fulani.

Wengi wetu tumekua katika jamii ambazo wanawake ndiyo wanaofundishwa kupika, lakini kama tulivyozungumza hapo awali, kupika ni ujuzi muhimu wa maisha ambao kila binadamu anapaswa kufahamu. 

Hivyo, wazazi tuna jukumu la kuhakisha watoto wetu wa kike na wa kiume wana ujuzi huu ili wanavyokua kuwa vijana, na hatimaye watu wazima, waweze kujihudumia vyema.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *