The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kwa Nini Mzazi Anashauriwa Amnyonyeshe Mtoto kwa Miaka Miwili?

Maziwa ya mama ni mazuri kwa mtoto kwani huwa yana antibodi zinazosaidia kumlinda mtoto mchanga dhidi ya maradhi mbalimbali.

subscribe to our newsletter!

Unyonyeshaji ni jambo la muhimu sana katika kuwapatia lishe bora watoto wachanga na pia huleta faida kubwa kwa afya ya mama anayenyonyesha. 

Akina mama wengi huwa na wasiwasi kama wana maziwa ya kutosha kwa ajili ya watoto wao na hivyo hujikuta wanakata tamaa ya kunyonyesha. Hata hivyo, ni muhimu sana tukafahamu kwamba katika siku za kwanza baada ya kujifungua, mama huwa anatoa maziwa ya njano ambayo huitwa dang’a au kolostramu. 

Maziwa haya ni mazuri kwa mtoto kwani huwa yana antibodi zinazosaidia kumlinda mtoto mchanga dhidi ya maradhi. Lakini pia husaidia kuandaa tumbo la mtoto mchanga kwa ajili ya umeng’enyaji wa maziwa.

Faida za unyonyeshaji kwa mama na mtoto ni nyingi haswa katika miezi sita ya mwanzo na zinathibitishwa na utafiti wa kisayansi. 

Tafiti zinaonesha kuwa, kunyonyesha pia hupunguza hatari ya mtoto kupata magonjwa kama vile pumu, mzio, kisukari, na uzito kupindukia kwani maziwa ya mama yana kingamwili ambayo husaidia mwili wa mtoto kupambana na virusi na bakteria hatari wanaosababisha magonjwa mbalimbali. 

SOMA ZAIDI: Kwa Nini ni Muhimu kwa Wazazi Kujifunza Kuhusu Huduma ya Kwanza?

Watoto wanaotunzwa kwa maziwa ya mama pekee hadi miezi sita wanaepuka hatari ya maambukizi ya magonjwa ya njia ya upumuaji. Zaidi ya hayo, maziwa ya mama yanaaminika kuchangia katika kuongeza werevu kwa watoto, na pia kusaidia katika ujenzi wa uhusiano wa karibu kati ya mama na mtoto.

Faida za kunyonyesha

Maziwa ya mama humpatia mtoto virutubisho vyote muhimu katika miezi sita ya mwanzo baada ya kuzaliwa. Maziwa haya yana uwiano mzuri wa wanga, protini, mafuta, vitamini, na madini, yanayohitajika kwa ukuaji na maendeleo mazuri ya mtoto. 

Tofauti na maziwa ya kopo, maziwa ya mama yanameng’enyeka kirahisi na vyema zaidi na ni bora kwa mfumo wa mmeng’enyo wa mtoto.

Ni muhimu kufahamu kwamba mtoto akinyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita ya kwanza, maziwa yanaweza kumsaidia mtoto kupunguza hatari ya kupata kifo cha ghafla . Hii ni faida muhimu sana ambayo inaonyesha umuhimu wa kunyonyesha kwa maisha ya mtoto yenye afya.

Hata pale ambapo maziwa yako ni machache, au unadhani hayatoshi, ni vyema ukaendelea kumnyonyesha mtoto wako. Unaweza ukaamua kumnyonyesha mwanao kwa wakati fulani tu, huku wakati mwingine ukimnyonyesha maziwa ya kopo au ya ng’ombe kuliko kuacha kabisa. 

SOMA ZAIDI: Mambo ya Kuzingatia Kabla ya Ujauzito Kama Una Ugonjwa wa Kudumu

Hata hivyo, wasiliana na daktari atakuelezea njia za kuongeza maziwa kwani wakati mwingine si suala la maziwa machache bali ni jinsi unavyomuweka mtoto wako kwenye titi au vyakula unavyokula. Na pia daktarai atakushauri juu ya umri sahihi wa kumpa maziwa ya ng’ombe na namna ya kuyaandaa.

Kuhusu faida za unyonyeshaji kwa mama anayenyonyesha, kunyonyesha husaidia mwili wa mama kurudi katika hali yake ya kawaida baada ya kujifungua. Kichocheo cha oxytocin kinachotolewa wakati wa kunyonyesha husaidia mji wa uzazi kurudi katika umbo lake la kawaida na kupunguza kutokwa na damu baada ya kujifungua.

Zaidi ya hayo, kunyonyesha husaidia mama kupunguza uzito alioupata wakati wa ujauzito, kuzuia hatari ya kupata saratani ya matiti na mfuko wa mayai pamoja na magonjwa mengine ya hatari.Kunyonyesha pia husaidia kupunguza gharama za matumizi, kwani hakuna haja ya kununua maziwa ya kopo na vifaa vingine vinavyohusiana na lishe ya mtoto.

Baadhi ya mama wanaonyonyesha hukosa maziwa ya kutosha kutokana na namna yao ya unyonyeshaji hasa jinsi ya kumpakata mtoto na namna ya kushika na kuweka chuchu kwenye mdomo wa mtoto. 

Jinsi ya kunyonyesha

Kuna njia mbalimbali za kumpakata na kumuweka mtoto vizuri kwenye titi ili apate maziwa ya kutosha. Njia iliyozoeleka ni kumpakata mtoto kwa kumuegemeza kichwa chake kwenye uvungu wa kiwiko chako huku mwili wake ukielekea kwako. Kisha, tumia mkono wako mwingine kumkumbatia na kuegemeza kichwa chake na shingo kuelekea kwenye miguu yake ili miguu yake iegemee vizuri.

SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwajengea Watoto Wetu Misingi ya Maadili na Tabia Njema?

Kuna njia nyingine kama mtindo wa mpira wa miguu ambapo mama anaweza egemeza mgongo wa mtoto kwa mkono na kiganja chake kama ameshika mpira wa miguu. Akiwa ameeegemeza kichwa, shingo, na mgongo, mtindo huu ni mzuri kwa mtoto mchanga au mdogo au kama mama umetoka kwenye upasuaji waa uzazi ili kulinda kidonda chake kisidhurike.

Kulala ubavu ni njia nyingine inayofaa na kushauriwa, hususani kwa kunyonyesha wakati wa usiku au kama mama alifanyiwa upasuaji wa kupanua njia ya uzazi wakati wa kujifungua. 

Unapokuwa unataka kunyonyesha kwa njia hii, weka mto chini ya kichwa chako ili upate unafuu wa kulala vizuri na ziwa limfikie mtoto vizuri kwenye mdomo ili kumuepusha na kupaliwa. 

Kisha, sogea karibu na mtoto, halafu tumia mkono wako mmoja kushika ziwa lako huku ukivizia mwanao kupanua mdomo wote, kisha baada ya kupanua mdomo, weka chuchu ndani ya mdomo wa mwanao na hakikisha eneo lenye weusi unaozunguka chuchu unaingia kwenye mdomo wa mtoto. 

Baada ya mwanao kupokea nyonyo, egemeza kichwa, shingo, na mgongo wa mwanao kwa mkono wako mwingine ulio huru. Mtoto anaponyonya vizuri, utahisi mguno wa sauti ya kumeza wakati wa kunyonya.

SOMA ZAIDI: Kama Wazazi, Tunawezaje Kuwalea Watoto Wetu Katika Hulka, Upekee Wao?

Mama anashauriwa asishtuke pale mtoto akipungua uzito kidogo baada ya kuzaliwa, kwa sababu watoto wengi hufanya hivyo katika siku tatu hadi tano za mwanzo, kupungua huko kwa uzito hakutokani na unyonyeshaji wako, hivyo huna haja ya kuhamaki. 

Maziwa huongezeka kadri hitaji la chakula (maziwa) linapoongezeka. Watalaamu wa afya hupendekeza maziwa ya mama pekee mpaka umri wa miezi sita. Inashauriwa kuendelea kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama kwa vipindi katika siku, huku ukimchanganyia vyakula vya kawaida baada ya miezi sita ya mwanzo.

Kwa kuzingatia faida hizi kwa mama na mtoto, inashauriwa kuendelea kunyonyesha kwa muda unaofaa, ambao ni miaka miwili, na kuhakikisha kuwa mazingira ya kunyonyesha ni salama kwa afya na ustawi bora wa mama na mtoto.


Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *