The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mambo ya Kuzingatia Kabla ya Ujauzito Kama Una Ugonjwa wa Kudumu

Ni vyema kufikiria kufanya mabadiliko ya mtindo wa maisha yako na pia jitahidi kupunguza msongo wa mawazo ili kuilinda afya yako.

subscribe to our newsletter!

Magonjwa ya kudumu kama vile pumu, kisukari, kifafa, matatizo ya moyo, nakadhalika ni magonjwa ambayo huendelea kwa muda mrefu au hata maisha yote bila kupona na huhitaji matibabu endelevu. 

Ili kudhibiti magonjwa haya, mgonjwa mara nyingi hulazimika kupunguza shughuli za kila siku, au kufanya mabadiliko maalum katika maisha ili kuhakikisha afya yake inalindwa.

Tafiti zinaonesha kuwa wanawake wanne kati ya kumi wanaaminika kuwa na ugonjwa wa kudumu. Kwa wanawake walio na magonjwa haya, suala la kupata ujauzito linaweza kuja na changamoto zake. 

Wanaweza kujiuliza: Je, nikibeba ujauzito, usalama wangu na mtoto utakuwaje? Au, je, hali ya afya yangu itakuwaje? Na maswali mengine mengi yanayofanana na hayo.

Lakini kutokana na kuboreshwa kwa huduma za kiafya katika nyakati zetu za sasa, pamoja na kupewa huduma maalum chini ya uangalizi wa daktari, kumewawezesha wanawake wengi wenye magonjwa ya kudumu kufanikiwa kubeba ujauzito na kujifungua kwa usalama zaidi kuliko hapo awali. 

SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwajengea Watoto Wetu Misingi ya Maadili na Tabia Njema?

Hivyo, kabla ya kuchukua hatua ya kupata ujauzito, kuna baadhi ya vitu mwanamke mwenye hali hizi anaweza kufanya, ikiwemo kumshirikisha mtoa huduma wake wa afya anayefahamu maendeleo ya ugonjwa wake. 

Mtoa huduma huyu anapaswa kuwa na uelewa wa kina juu ya hali ya ugonjwa wako, hii itampa mwongozo wa hali ya afya yako na uwezo wako wa kupata ujauzito. 

Kutokana na uelewa wa kina alionao juu ya hali yako, ndipo atakapoweza kutoa maoni yake juu ya uwezo wa mwili wako kushika ujauzito na kujua aina ya dawa sahihi au zisizo sahihi kwako kutumia endapo utapata ujauzito. 

Kumbuka kuwa, mtoa huduma wako wa afya yupo hapo kukusaidia na kukupa muongozo wowote unaohitaji wakati wa safari yako ya kupata na kulea ujauzito.

Kuwa makini na maelekezo ya dawa uliyopewa na daktari; hakikisha unatumia dawa kwa wakati bila kuchelewa au kuwahi sana, hii itasaidia dawa ifanye kazi katika mwili kwa namna inavyopaswa.

SOMA ZAIDI: Kama Wazazi, Tunawezaje Kuwalea Watoto Wetu Katika Hulka, Upekee Wao?

Hakikisha unaimarisha ulaji wako wa chakula kwa mujibu wa ushauri wa mtoa huduma wako wa afya, chakula unachokula kinahitaji kua chenye ubora na virutubisho vya aina yote, mwili wenye virutubisho huimarisha kinga mwilini na pia huongeza uwezekano wa kushika mimba na kujifungua kwa usalama zaidi.

Jitahidi kupata muda wa kupumzika wa kutosha ili kuhakikisha mwili wako upo imara na wenye nguvu. Hii husaidia kuimarisha kinga ya mwili wako na pia hukuepusha na upungufu wa kinga mwilini. 

Pia, jenga desturi ya kufanya mazoezi kwa kufuata maelekezo ya mtaalamu wa afya, ili kuimarisha afya yako na kujiandaa vizuri kwa ujauzito.

Jiepushe na matumizi ya pombe, sigara, kahawa na kilevi cha aina yoyote na mengineyo utakayoshauriwa na mtaalamu wa afya, hii itaimarisha afya yako. Matumizi ya vitu hivi yana athari kubwa sana katika mwili wa mwanadamu na hasa kwa mama mjamzito na ujauzito wenyewe. Athari zake zinaweza zisijioneshe mapema lakini ni zenye madhara makubwa sana.

Pamoja na yote, ni muhimu kumshirikisha mhudumu wa afya juu ya mpango wako wa kupata ujauzito, hii ni kwa sababu wengi wetu tunaishi na magonjwa haya pasipokujua kwa sababu hatuna utamaduni wa kupima afya zetu mara kwa mara hadi pale tunapohisi kuumwa. 

SOMA ZAIDI: Umuhimu na Namna ya Watoto Kutambua na Kuthamini Mipaka yao na ya Wenzao

Ni vyema kufikiria kufanya mabadiliko ya mtindo wa maisha yako na pia jitahidi kupunguza msongo wa mawazo ili kuilinda afya yako. Uelewa wa kina kuhusu hali yako ya kiafya utakusaidia kupanga na kujiandaa vizuri kabla ya kufanya uamuzi wa kubeba ujauzito.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *