Search
Close this search box.

Kama Wazazi, Tunawezaje Kuwalea Watoto Wetu Katika Hulka, Upekee Wao?

Wataalamu wa malezi wanaamini kwamba asilimia kubwa ya malezi ni kutambua, kukubali na kuenzi upekee wa mtoto.

subscribe to our newsletter!

Kama ambavyo inajulikana na kuaminika, kila mwanadamu ni wa kipekee, na hivyo hata watoto wetu ndivyo walivyo. Watoto wanaweza kufanana na ndugu, au wazazi, kwa baadhi ya vitu, kama maumbile au aina ya tabia. Lakini juu ya yote, watoto huzaliwa na hulka, muonekano na tabia zao za kipekee, hata kama ni mapacha wa kufanana.

Ni vyema kutambua kwamba, mtoto azaliwapo, mzazi huwezi kutambua ni mtoto mwenye hulka, au mwenye hali ya upekee wa aina gani. Kadiri akuavyo ndivyo unavyozidi kumfahamu mtoto. 

Je, ni mtundu sana, ni muongeaji sana, anapendelea nini, hapendelei nini, na ni vitu gani ni vya thamani kwake? Kumkuza mtoto katika hulka na upekee wake kunaanza kwanza kwa kutambua, kukubali na kuenzi upekee wa mtoto, hali ambayo humjengea mtoto ujasiri na hali ya kujiamini ndani yake.

Hebu tuangalie baadhi ya dondoo zinazoweza kukusaidia wewe mzazi ama mlezi katika kutambua, kukubali na kuendeleza upekee wa mtoto wako ili umkuze katika hulka na upekee wake.

Kwanza kabisa, anza kwa kutambua na kisha kukubali vitu anavyopenda au kuvutiwa navyo mtoto hata kama siyo chaguo lako wewe. Tambua kwamba yeye anaweza kuwa na mitazamo tofauti na ya kwako. 

SOMA ZAIDI: Umuhimu na Namna ya Watoto Kutambua na Kuthamini Mipaka yao na ya Wenzao

Si vyema kumlazimisha mtoto kufuata vipaumbele vyako mzazi bila kuzingatia yeye angependa nini. Kwa mfano, epuka kumlazimisha kusoma taaluma asiyoipenda. Badala yake, mwongoze afanye kile nafsi yake inachoridhia kulingana na uwezo wake na umtie moyo afikie malengo yake.

Hii ni kwa sababu mtu akifanya anachokipenda, hukifurahia na hukifanya kwa ufanisi zaidi. Cha msingi, hakikisha mambo anayoyachagua si kinyume na maadili au sheria ya nchi kwa namna yeyote ile.

Mzazi ama mlezi jitahidi kutengeneza uhusiano wa karibu na mwanao ili ajisikie huru kuongea na wewe na kukutambua si tu kama mzazi bali hata rafiki pia. 

Jifunze kumsikiliza mtoto anapojaribu kuelezea jambo fulani ili kutengeneza mawasiliano mazuri na kufahamu ni nini anapenda na kufurahia zaidi, au nini hapendelei zaidi. Hii itakusaidia kujua mtoto wako ni mtoto wa aina gani na mwenye hulka gani. 

Usisahau kutoa mwongozo, rasilimali na muelekeo katika vitu ambavyo mtoto wako anapenda kufanya ili kuimarisha ujuzi wake kwenye mambo hayo.

SOMA ZAIDI: Unawezaje Kutambua, Kumlinda Mtoto Wako Dhidi ya Kuonewa na Wenzake?

Pia, jifunze kuwa makini na watoto mnapozungumza. Sikiliza hoja zao na mitazamo yao, kupitia vitu hivyo, tambua upekee wao. Tumia muda huo kusikiliza kwa makini kuthibitisha mitazamo yao na kwa kupitia mazungumzo yenu endelea kumsoma na kumjenga mtoto katika upekee wake.

Jitahidi kutengeneza mazingira ya kuhamasisha uhuru na uwezo wa mtoto kufanya uchambuzi juu ya masuala ambayo anashughulika nayo. Hali hii itamtengenezea ujasiri na kuamini kwamba ana sauti na uwezo wa kufanya na kuamua kitu bila kusimamiwa. Hivyo ataweza kutambua makosa yake kwa kujifunza. 

Pia, tengeneza mazingira ya mtoto wako kuwa na uwezo wa kujieleza kwa ujasiri na kwa kujiamini kwa njia tofauti ikiwemo kuongea, kuandika, michezo, nyimbo na ubunifu wa aina nyingine. Hii itawaruhusu kujenga utambulisho wao.

Wataalamu wa malezi wanaamini kwamba asilimia kubwa ya malezi ni kutambua, kukubali na kuenzi upekee wa mtoto wako. 

Hivyo basi, wazazi na walezi tukumbuke kuwa, tuna mchango mkubwa katika maendeleo ya watoto wetu, na tuna wajibu wa kuhakikisha hulka na upekee wa watoto wetu unakuzwa na kuthaminiwa ili wakue wakijiamini na kuthamini wao pamoja na wenzao.


Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *