The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Unawezaje Kutambua, Kumlinda Mtoto Wako Dhidi ya Kuonewa na Wenzake?

Uonevu huwaathiri watoto kimwili pale mtoto anapopigwa na mwezake na kubaki na maumivu sehemu za mwili, michubuko au alama za kupigwa.

subscribe to our newsletter!

Uonevu, au bullying kwa kimombo, kwa watoto ni aina ya tabia ya uchokozi ambapo mtoto mmoja huonesha tabia ya usumbufu kwa makusudi mara kwa mara kwa mtoto mwingine na hata kuwadhuru kimwili, kihisia au kiakili kwa njia ya matusi, mashambulizi ya maneno na vipigo.

Tabia hii hufanyika shuleni, mazingira ya nyumbani na hata mitaani. Mtoto wako anaweza akawa anapitia uonevu katika mazingira hayo bila ya wewe kujua. 

Watoto hutaniwa kutokana na hali yao ya kiuchumi, nafasi ya familia zao katika jamii, umri wao, maumbile yao – kimo, rangi, ugonjwa, ulemavu, nakadhalika –, uwezo wao darasani na hata nguvu za mwili. 

Watoto waonevu hudhani kwamba wao ni bora kuliko wenzao. Mara nyingi mtoto anayeonewa huwa na tofauti zinazojikita katika mambo hayo tajwa hapo juu.

Mtoto anaweza kuwa na tabia ya uonevu kwa sababu mbali mbali, ikiwemo kufata mkumbo, yaani kuiga tabia za marafiki zake, ili kujipatia sifa au kuonekana mjanja kwa wengine. 

SOMA ZAIDI: Kama Mzazi, Umejiandaaje Kuimarisha Uhusiano na Mtoto Wako 2024?

Wakati mwingine, watoto huwa na hali ya woga au kutojiamini, hivyo, huficha hali hiyo kwa kuonea wenzao na kuwafanya wajisikie vibaya. Tabia hii huwafanya wajione wako juu na ndio wajanja kuzidi wengine.

Baadhi ya dalili zinazoweza kukusaidia kujua kwamba mwanao anapitia changamoto hiyo ni pamoja na mtoto anapochukia na kukataa kabisa kwenda shule, maeneo au mazingira fulani, mabadiliko katika matokeo yake ya mtihani, kuwa na mtazamo hasi kuhusu shule au yeye binafsi, au kuwa mkimya mara kwa mara, jambo ambalo sio la kawaida kwake.

Mtoto pia anaweza pia akawa amebadilisha marafiki, kwa kuwaacha waliokuwa wakimuonea. Au anaweza kuwa na alama za kupigwa, au michubuko kwenye mwili wake zisizokuwa na sababu za kueleweka, inaweza pia kuwa ni viashiria kwamba anaonewa kwa namna moja au nyingine.

Mtoto anaweza kujenga tabia ya woga na kujitenga akakosa marafiki kabisa. Mtoto anaweza kuonesha tabia za woga na kushindwa kushiriki michezo na wenzake katika mazingira ya shuleni, mtaani au nyumbani. Pia, mtoto anaweza kupoteza vitu vyake mara kwa mara kama vile madaftari, kalamu, nakadhalika.

Uonevu huwaathiri watoto kimwili pale mtoto anapopigwa na mwezake na kubaki na maumivu sehemu za mwili, michubuko au alama za kupigwa. Uonevu pia huleta madhara kisaikolojia kwa namna tofauti, watoto wanaweza kuwa na hali ya kujiona hawana uwezo fulani, kukosa furaha, kutokujiamini, kuwa na hofu, huzuni, na hata msongo wa mawazo. 

SOMA ZAIDI: Tuzungumze Kuhusu Umuhimu wa Lishe Bora kwa Watoto na Misingi Yake

Hali hii huweza kusababisha kushuka kwa maendeleo ya shule, ikiwemo kufeli masomo na hata kupoteza umakini kuzingatia maelekezo anayopewa.

Mzazi, au mlezi, usalama wa mtoto upo mikononi mwako, hivyo jitahidi kujenga uhusiano wa karibu zaidi na mtoto ili aweze kuwa muwazi na huru kwako kukueleza yale yote anayoyapitia au yanayomsumbua. 

Tenga muda wa kuzungumza na mtoto na ujitahidi kuwa msikivu zaidi. Pia, mtamkie maneno mazuri ya upendo kumjengea ujasiri kwa kumuwezesha kujiamini na kujikubali yeye binafsi. 

Mueleze kwamba wanaomuonea wanahitaji kusaidiwa na wazazi wao kwa sababu hawajafundishwa kuthamini wengine, hivyo hawajui walitendalo.

Mueleze mtoto kwamba, endapo akionewa na mtu yeyote anaweza kukuambia wewe au mtu mzima yeyote wa karibu anayemuamini. Endapo uonevu umezidi, aondoke eneo hilo na kutafuta eneo ambalo atakuwa salama. 

SOMA ZAIDI: Kama Mzazi, Unawezaje Kujali, Kulinda Afya Yako ya Akili?

Pia, jenga mawasiliano mazuri na walimu wake, kwa pamoja msimamie usalama wake. Wazazi tunapaswa kulea na kusimamia watoto wetu vizuri kimaadili ili wajifunze kuheshimu na kuthamini hisia za wengine ili kuzuia wasiwe watoto wanevu. 

Tunaweza kufanikisha suala hili kwa kuwa mfano bora kwenye jamii kwa kutokubagua wengine iwe kikabila, kiuchumi, kiumri, kimwili au hali yoyote ile.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *