Search
Close this search box.

Usafi ni Muhimu Sana Katika Makuzi ya Watoto Wetu, Tuuzingatie

subscribe to our newsletter!

Usafi ni nyenzo bora ya malezi na afya ya watoto. Pasipo kuzingatia usafi, magonjwa ya kuambukiza na yale yasiyo ya kuambukiza yamekua yakiathiri afya ya wanadamu na hasa watoto. 

Ndiyo maana usafi ni sehemu kubwa ya maisha yetu na tunapaswa kuuzingatia tukiwa kama wazazi au walezi ili kunusuru afya za watoto wetu. Usafi unatusaidia kuwa salama na kuondokana na vimelea vya magonjwa vinavyoishi katika mazingira yetu. 

Pia, husaidia watoto wadogo ambao kila wapatapo nafasi hushika kila kitu na muda mwingine huweka vitu hivyo mdomoni. Kwa sababu hiyo, tunapaswa kuhakikisha mazingira yetu yako safi na salama kwa ajili ya watoto ili kupunguza uwezekano wa kupatwa na magonjwa yanayotokana na uchafu.

Ni wazi kwamba viwango vya usafi hutofautiana na hutegemea tamaduni, mahali na hali ya maisha ya watu. Ni vigumu kwa maeneo ambayo hayana maji, au mfumo mzuri wa kupitisha maji-taka, kuwa na hali ya usafi. 

Hata hivyo, mzazi anayejali anaweza kufanya mengi katika kudumisha afya na usafi, ingawa anahitaji ushirikiano kutoka kwa familia yote na jamii kwa ujumla.

SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kujenga Mahusiano Mazuri Kati ya Watoto Ndugu?

Tuanze na usafi wa ngozi. Ngozi zetu ndiyo kiungo kikubwa katika miili yetu na ni moja ya kinga yetu kuu dhidi ya vimelea vya magonjwa. 

Kwa hiyo, ni muhimu kuzingatia usafi wa ngozi zetu na za watoto kwa kuwaogesha, kuwasafisha nyuso na kuwanawisha mikono mara kwa mara wakitoka kutumia choo na kabla ya kula kwa maji safi yanayotiririka na sabuni. Pia, tunahitaji kuwafundisha jinsi ya kujifanyia vitu hivi wenyewe kwa ufasaha kadri wanavyokua.

Mfano, mtoto anaporudi kutoka shule anapaswa kufahamu kwamba kabla hajashika chombo chochote kama vile cha maji ya kunywa au kukaa chini kula anahitaji kunawa mikono na sabuni na maji yanayotirirka. Usafi wa nguo pia husaidia kuhifadhi ngozi zetu. 

Tujitahidi kufua nguo zetu na za watoto mara kwa mara kwa kutumia sabuni na maji safi kisha kuzikausha kikamilifu kabla ya kuzikunja na kuzitunza ili kuzuia ukungu na harufu mbaya. 

Watu wazima hasa wale wanaoishi na watoto wadogo wanapswa kuzingatia usafi wa mikono yao kila wanapohitaji kuwashika watoto na pia kuzingatia usafi wa vyombo vya mtoto vya chaklula.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Mzazi Anashauriwa Amnyonyeshe Mtoto kwa Miaka Miwili?

Usafi wa kinywa unahusisha kusafisha meno kwa usahihi kwa ajili ya afya nzuri ya kinywa na kuepuka magonjwa ya meno na fizi. Tunaweza kuwafundisha watoto jinsi ya kuswaki vizuri, na kuhakikisha wanapiga mswaki asubuhi na jioni, ikiwezekana kila baada ya mlo.

Tukiongelea usafi na usalama wa maji, tujitahidi kuhakikisha kwamba maji tunayotumia ni safi na salama, yamechemshwa vizuri na kuhifadhiwa kwenye vyombo safi katika sehemu salama. 

Vivyo hivyo, vyakula vipikwe na maji hayo, mboga na matunda yasafishwe kabla ya kuliwa kuepusha magonjwa kama ya tumbo na kipindupindu. Pasipo kuzingatia hayo, watoto wetu watakuwa katika hatari ya kuugua magonjwa ya kuharisha, kuumwa matumbo na mafua mara kwa mara.

Usafi wa mazingira kwa ujumla, haswa mazingira ambayo watoto huchezea yanapaswa kuwa safi muda wote. Kama ni ndani, sakafu, madirisha na vioo viwe safi kwa kufagia, kupiga deki na kufuta vumbi mara kwa mara kwa maji safi na sabuni. 

Kama ni nje basi tujitahidi kufyeka majani mara kwa mara, kung’oa magugu, kukata matawi ya miti, kuhakisha uchafu unatupwa na kuhifadhiwa sehemu husika na kuwa na mfumo mzuri wa maji taka. Hata kama sakafu ni ya vumbi, ni vizuri kufagia na kuondoa taka zinazoweza kuhatarisha afya ya mtoto.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini ni Muhimu kwa Wazazi Kujifunza Kuhusu Huduma ya Kwanza?

Kama tulivyosema hapo awali, ushirikiano katika familia ni muhimu katika kudumisha usafi. Ni vyema katika familia zetu tuketi na kuzungumza mahitaji yetu na marekebisho tunayohitaji kufanya, ndani na nje ya nyumba, ili kushirikiana katika kudumisha usafi kwa ajili ya afya za watoto wetu. 

Jambo hili huleta umoja katika familia na linamkumbusha kila mmoja jukumu lake katika kuhakikisha nyumba na mazingira yanabaki kuwa safi na salama. 

Familia inapaswa kuwa na siku maalumu ya kusafisha nyumba, inaweza kuwa kila juma na kuwa na ratiba ya kuisafisha kabisa, yaani ‘usafi mkubwa’ mara tatu au nne kwa mwaka wakati huo usafi binafsi wa wanafamilia na ule wa mazingira wa kila mara ukiendelea.

Vipi kuhusu jamii? Ni kweli kwamba mifumo ya kuondoa takataka bado ni tatizo katika nchi yetu kwa kiasi fulani. Kuna baadhi ya manispaa zinachelewa kuokota takataka na hivyo zinarundikana na kuishia kuzagaa mitaani. 

Kama wananchi, hatuna budi kuendelea kujitahidi kusaidia pale tunapoweza kwa kufanya vitu vilivyotajwa hapo juu katika mazingira yetu.

SOMA ZAIDI: Mambo ya Kuzingatia Kabla ya Ujauzito Kama Una Ugonjwa wa Kudumu

Kwa kufuata mbinu hizi rahisi za usafi, tunaweza kuhakikisha kwamba sisi pamoja na watoto wetu tunaishi katika mazingira safi, tunakuwa na afya njema na kufurahia maisha bila vikwazo vya magonjwa yanayozuilika, hasa kwa watoto.


Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *