The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tukio la Tatu Afrika La Nyaya Za Baharini Kukatika 2024. Namna Kuharibika Kwa Mkongo Wa Mawasiliano Baharini Kunavyosababisha Ukosefu wa Intaneti

katika tukio la Jumapili ya Mei 12,2024, jumla ya nchi 11 zimeathirika ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Mozambique, Mayotte, Malawi, Burundi, Madagascar. Mpaka sasa bado haijaelezwa chanzo cha hitilafu hiyo

subscribe to our newsletter!

Mpaka usiku huu wa Mei 13,2024, bado Intaneti imekua changamoto kubwa kwa watu wengi Tanzania, sababu kubwa inayotajwa ni kukatika kwa mkongo wa mawasiliano baharini (sub marine cable) wa SEACOM na EASSy katika eneo kati ya Msumbiji na Afrika Kusini.

Kwa mwaka huu hili ni tukio la tatu kutokea Afrika, kwa wastani matukio ya namna hii duniani hutokea walau 100 kwa mwaka.  Kabla hatujaendelea mbali tuangalie namna mkongo wa bahari unavyohusika na kukuletea Intaneti.

Intaneti kwa urahisi wake ni mfumo ambao kompyuta mbalimbali zinasomana, yaani kifaa chako kinachukua taarifa toka kifaa kingine, katika mnyororo wa namna hiyo.

Moja ya namna kubwa ya kuhakikisha  kompyuta au vifaa vyote vya duniani vinasomana na kutengeneza Intaneti ni kupitia  ‘mikongo’ au nyaya za chini ya Bahari. Nyaya hizi zina ukubwa sawa na mabomba tunayotumia kunyeshea majumbani.

Kwa ujumla inakadiriwa kuwa nyaya hizi zinachukua takribani kilomita milioni moja na laki nne kuzunguka sehemu mbalimbali za dunia na ipo mikongo takribani 524 dunia nzima.

Mikongo hii ndio inayohusika na asilimia 98 ya kutoa huduma ya intaneti duniani, huku njia nyingine kama satellite zikitumika kwa kiwango kidogo.

Fikiria kwa mfano, unapowasha kifaa chako kufungua barua pepe au kuangalia Netflix, data hutumwa kwa kasi toka sehemu mbalimbali za dunia na kukufikia ulipo kupitia mikongo hii.  Yaani mtandao wako unanunua nafasi ya kutumia mikongo hii, halafu inakuja kukuzia wewe mtumiaji wa mwisho  kupitia vifurushi na namna nyingine.

Kukatika Kwa Mawasiliano

Tanzania tunapata huduma kupitia mikongo mitatu mikubwa yaani: 2Africa (inategemewa kuanza mwaka huu) Eastern African Submarine Cable System (EASSy) na SEACOM. Taarifa tulizopewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ni kuwa shida imetokea kwa mkongo wa EASSy na SEACOM.

Majirani zetu Kenya, ambao nao wamepata changamoto kwa kiasi fulani wao wanahudumiwa na mikongo saba, na miwili inayotegemewa kuanza kazi mwak huu, yaani: Djibouti Africa Regional Express 1 (DARE1), Eastern Africa Submarine System (EASSy), Lower Indian Ocean Network 2 (LION2), PEACE Cable, SEACOM, The East African Marine System (TEAMS) pamoja na 2Africa na  Africa-1

Sababu kubwa inayofanya kuwepo na mikongo michache duniani ni gharama, lakini pia utaalamu wa kuitandaza ni wa kiupekee.

Nyaya hizi ambazo zilianza kutumika mwaka 1858, huku teknologia ikiboreshwa mpaka ujio wa Intaneti, huwa hazichimbiwi baharini bali hutandazwa tu juu ya Bahari kwa kutumia meli maalum, lakini pia utengenezaji wake pakitokea hitilafu huhitaji meli maalum.

Kutokana na namna ambazo nyaya hizi husimikwa, hii hupelekea pia zikumbwe na changamoto za hapa na pale ingawa sio mara kwa mara. Sababu ya changamoto hizi ni za kimazingira na pili shughuli au sababu za kibinadamu.

Sehemu ya sababu za kibinadamu ni pamoja na shughuli za uvuvi, meli kuzikata kwa bahati mbaya lakini pia kuna masuala ya ugaidi na uharamia, kuna wizi wa vifaa hivi ambapo iliwahi kutokea miaka 2007, pamoja na vita.

Lakini pia kuna njia nyingine ya mataifa kuchakachua hizi nyaya kwa ajili ya kuiba taarifa yaani kufanya ushushushu, ingawa mara nyingi sababu hii haiziharibu nyaya hizi moja kwa moja.

Mwaka wa Matukio

Mwaka huu umeanza kwa mfululizo wa matukio wa hitilafu katika nyaya hizi; tukio la kwanza lilitokea katika Bahari ya Shamu (Red Sea) mnamo Februari 24,2024, likikata nyaya za  Seacom/TGN-EA, EIG, and AAE-1. Tukio hili lilisababisha kupungua kwa kasi ya mitandao bila kupotea kabisa kwa mitandao kwa sehemu za Afrika.

Tukio hili la Bahari ya Shamu limehusishwa na mzozo unaendelea Mashariki ya Kati, huku baadhi wakiwanyooshea kidole Houthi wa Yemeni, ingawa wao pia wamewanyooshea kidole mahasimu wao hasa meli za Uingereza na Marekani kuwa ndizo zilizohusika

Tukio lingine ni lile limetokea mnamo Machi 14,2024, ambapo mikongo iliyokatika ilikuwa ya ACE – Africa Coast to Europe; SAT-3 – Submarine Atlantic 3; WACS – West Africa Cable System na MainOne. Tukio hili lilisababisha nchi kumi na tatu kuathirika yaani Benin, Burkina Faso, Kameruni , Cote d’Ivoire, Gambia, Ghana, Guinea, Liberia, Namibia, Niger, Nigeria, Afrika Kusini na  Togo.

Katika tukio hili linatwajwa kuwa lilitokana na miamba ya chini ya maji kupiga na kukata sehemu ya nyaya hizo zilizokutania katika pwani ya Cote d’Ivoire.

Na tukio la Jumapili ya Mei 12,2024, ambapo nchi 11 zimeathirika ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Mozambique, Mayotte, Malawi, Burundi, Madagascar. Mpaka sasa bado haijaelezwa chanzo cha hitilafu hiyo.

Kama ilivyokuwa kwa matukio mengine ya nyuma hatua ya kwanza ya matengenezo ni kubadili uelekeo wa njia ya data (re-routing) makampuni ya Tanzania yameendelea kufanya hivi, kwa makampuni kama ya Kenya ilikua rahisi zaidi kutokana na wingi wa mikongo inayoiunganisha nchi yao na dunia.

Kwenye upande wa matengenezo, moja ya wakurugenzi wa kampuni yenye hisa katika mikongo hii amenukuliwa akisema kuwa meli ya matengenezo itaondoka Jumanne ya Mei 14, inategemewa kutumia siku tatu baharini, na ikifika watatoa tathmini ya muda wa matengenezo.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

9 Responses

    1. Kweli watu wengine tulikua hatuelewi namna tunavyopata mtandao.kwa elimu hii tumejifunza na kuelewa vzr.

  1. Kuna watu niliwaeleza kuhusu hili la Nyaya kuwa Chini ya Bahari Dooh..!
    Kidogo wanitoe roho kwa Ubishi..Asante kwa Maelezo Mazuri na Elimu ya Kutosha

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *