Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa takribani watoto milioni tano nchini Tanzania yaani wastani wa mtoto mmoja kati ya watoto wanne wanapitia katika changamoto ya utumikishwaji kwenye ajira zilizopo kwenye sekta mbalimbali hivi sasa, hali ambayo si nzuri kwani inatishia ustawi wa kundi hilo muhimu.
Hivyo, Serikali na wadau wengine wametakiwa kuchukua hatua mahususi ili kukomesha suala hilo na kwa kuanzia imeshauriwa kuwa kinachohitajika ni kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na utekelezaji wa sheria zinazowalinda watoto.
Haya yote yameelezwa leo Alhamisi ya Mei 30, 2024, wakati Mtandao wa Kupinga Utumikishwaji Watoto Tanzania na washirika wake walipokuwa wanatoa tamko lao mbele ya waandishi wa habari katika kuelekea maadhimisho ya siku ya kupinga utumikishwaji wa watoto duniani.
Maadhimisho hayo hufanyika Juni 12, kila mwaka tangu ilipozinduliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) mwaka 2002, kama njia ya kuonesha madhila wanayokutana nayo watoto wanaohusishwa katika utumikishwaji katika sekta mbalimbali duniani.
Shirika hilo kupitia mkataba wa kimataifa namba 138, liliweka umri wa ajira kuwa ni miaka 15 na kuendelea na katika mkataba namba 182 lilorodhesha ajira zisizokubalika kwa watoto na ambazo zinatakiwa kuzuiwa.
“Pamoja na jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Serikali lakini bado zipo changamoto kadhaa ikiwemo watoto kuendelea kufanyishwa kazi ngumu katika maeneo ya kazi za ndani, mashambani, mitaani na migodini,” anasema Ibrahim Samatta ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maadhimisho ya siku hiyo.
“Na katika sekta hizo ambazo tumezitaja changamoto bado ni nyingi. Na kwa mujibu wa takwimu inaonesha kwamba takribani watoto milioni tano nchini Tanzania yaani wastani wa mtoto mmoja kati ya watoto wanne wapo katika utumikishwaji wa watoto.”
“Ajira hizi zimekuwa kichocheo cha utumikishwaji na ukatili dhidi ya watoto ambapo baadhi yao hukosa masomo kwa maana ya fursa za kuwa shuleni, kunyanyaswa kwa maana ya masuala mazima ya ukatili wa kiuchumi kwa kuwa hulipwa ujira mdogo, na kupata matatizo ya kiafya jambo ambalo limekuwa likiathiri ukuaji wao.”
Watoto wa kiume hatarini zaidi
Dk Katanta Simwanza ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Kupinga Utumikishwaji wa Watoto Tanzania. Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika ofisi za Mtandao wa Kijinsia Tanzani (TGNP) zilizopo Mabibo, jijini Dar es Salaam, amesema kuwa nchini Tanzania watoto wa kiume ndiyo ambao wamekuwa waathirika wakubwa wa vitendo vya utumikishwaji.
“Tunapongelea masuala ya kukomesha utumikishwaji wa watoto mara nyingi watu wanafikiria hasa mtoto wa kike,” anaeleza Simwanza. “Watoto wa kiume ndiyo wahanga wakubwa katika kutumikishwa katika nchi yetu, naomba tutambue hilo.”
Anaendelea kusema “kazi nyingi ambazo tunaziona ni zile za kuhatarisha mara nyingi zinafanywa na wanaume. Mfano kama kazi za uchimbaji, kazi kama za uchungaji, masuala ya uvuvi na kazi za gereji.”
“Na kwa sababu watu wanatamani kupata faida kubwa [basi] wanatafuta vibarua. Kwa hiyo imekuwa ni sababu moja wapo ambayo inachangia kwa kiwango kikubwa sana watoto wengi wa kiume kujikuta wakitumikishwa katika maeneo hayo.”
Dk Simwanza ameitaja pia mikoa ya Geita, Mwanza na Shinyanga kuwa ndiyo mikoa vinara hapa nchini kwa utumikishwaji wa watoto. Mikoa hiyo imeelezwa kuwa kinara kwa sababu ndani yake kuna shughuli nyingi za kiuchumi kama vile, uvuvi, kilimo, na uchimbaji wa madini, shughuli ambazo kwa kiasi kikubwa zinahitaji wafanyakazi.
Kwa upande wake Scholastica Pembe, ambaye ni Mratibu wa kitaifa wa Mtandao wa Kupinga Utumikishwaji Watoto Tanzania, ili kutokomeza utumikishwaji wa watoto, ameitaka jamii na Serikali kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mikakati ya kutokomeza utumikishaji wa watoto iliyowekwa kwenye mipango na mikakati ya kitaifa inapewa kipaumbele kwenye ngazi na sekta zote.
“Tunajua tunayo mikakati mbalimbali, tunazo sheria, tunazo sera,” anasema Pembe. “Kwa hiyo tunahitaji pia Serikali iweze kuweka kipaumbele na kuweka nguvu na juhudi katika kuhakikisha kwamba sera tulizonazo, sheria tulizonazo tunazitendea kazi.”
“Pia tunao wito kwa upande wa wazazi na walezi, kwanza kabisa ni kuwatunza, kuwalinda na kuwapa watoto mahitaji yao ya msingi ikiwa ni pamoja na elimu. Tunalisema hilo kwa msisitizo kwamba wazazi na walezi wakisimama kwenye nafasi zao kuwahudumia watoto, watoto hawataenda katika utumikishwaji,” Pembe anamalizia kueleza.
Kwa mwaka huu Mtandao wa Kupinga Utumikishwaji Watoto Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu wanatarajia kufanya maadhimisho ya kitaifa ya siku hiyo mnamo Juni 12, 2024, huko mkoani Simiyu.
Lakini kabla ya kufanyika kwa maadhimsiho hayo, Juni 5, 2024, mtandao huo utafanya mjadala wa kitaifa wa kuangalia utekelezaji wa jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali na wadau wengine katika kutokomeza utumikishwaji wa watoto nchini.
Mjadala huo ambao utakuwa na kaulimbiu isemayo ‘Kuboresha Sera za Ulinzi wa Watoto: Kuelekea Kumaliza Utumikishwaji wa Watoto Nchini Tanzania,’ utafanyika katika ukumbi wa Karimjee Hall, jijini Dar es Salaam na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Pindi Chana, ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria.
Lukelo Francis ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com