Dunia itaelekeza macho jijini Paris kuanzia Julai 26 hadi Agosti 11 wakati miamba ya michezo mbalimbali itakapokuwa ikipambana kuwania medali tatu katika kila mchezo kwenye tamasha kubwa kuliko lote michezoni, maarufu kama Michezo ya Olimpiki ya majira ya joto.
Ni michezo ambayo washiriki wake hufuzu kwa kushindana katika mabara yao, kufikia viwango vilivyowekwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, au kuwa katika nafasi nzuri ya orodha ya ubora duniani.
Ni tukio linalojumuisha michezo 32 kwa mujibu wa orodha iliyopangwa kwa Michezo ya Olimpiki ya Paris, huku safari hii ukiingizwa mchezo mpya wa breaking maarufu Tanzania kama break dancing, yaani kudansi kwa staili ya kujinyonganyonga kwa kufuata midundo ya muziki.
Breaking ni dansi iliyoibuka miaka ya sabini ikiwa sehemu ya utamaduni wa hip-hop nchini Marekani na vijana wakawa wanashindana mitaani. Dansi hiyo ilisambaa duniani kwa kasi na imeendelea kuwepo hadi sasa na IOC imeamua kuiingiza katika orodha yake kama mchezo wenye vigezo vya Olimpiki.
Tangu ishiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1964 ikiwa Tanganyika, timu ya Tanzania ya mwaka huu itakwenda Paris kushiriki Olimpiki kwa mara ya 14 mfululizo. Haikushiriki Olimpiki ya mwaka 1976 kutokana na mgomo ulioongozwa na Congo.
Mafanikio hafifu
Lakini ushiriki huo mfululizo haulingani na mafanikio ambayo nchi imepata. Hadi sasa Tanzania imefanikiwa kushinda medali mbili tu za shaba kwenye Michezo ya Olimpiki inayofanyika kila baada ya miaka minne. Medali hizo zilipatikana kwenye michezo ya Moscow mwaka 1980, michezo ambayo ilisusiwa na Marekani na washirika wake.
SOMA ZAIDI: Kwa Hili, Serikali Imeheshimu AFCON 2027
Mwanariadha gwiji wa Tanzania, Filbert Bayi, ambaye alivunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 1,500 kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola, alishinda medali ya shaba katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi, pamoja na Suleiman Nyambui aliyetwaa medali kama hiyo katika mbio za mita 5,000.
Baada ya hapo timu yetu imekuwa ikiendelea kurudi mikono mitupu na wakati fulani vyombo vya habari viliwapachika wanamichezo wetu wanaoenda Olimpiki jina watalii.
Ni mara tatu tu Tanzania ilipeleka zaidi ya wanamichezo 10 kwenye michezo hiyo; ilipeleka wanamichezo 15 mwaka 1972, wanamichezo 41 mwaka 1980 na wanamichezo 18 mwaka 1984. Lakini miaka mingine nchi imekuwa ikipeleka wanamichezo kuanzia kumi kushuka chini.
Na idadi inazidi kupungua kadri miaka inavyokwenda licha ya mchezo wa kuogelea kuongeza idadi katika michezo ya mwaka 2008 jijini Beijing na mwaka 2012 jijini London. Idadi ya wanamichezo wanaoenda Olimpiki inazidi kupungua huku ushiriki ukizidi kujikita kwenye mbio za marathoni.
Katika michezo iliyopita ya 2020 jijini Tokyo, Tanzania ilipeleka wanariadha watatu; Gabriel Gerald Geay, ambaye hakumaliza, Alphonce Felix Simbu (2:11:35), akishika nafasi ya saba, na Failuna Matanga (2:33:58), akishika nafasi ya 28 kwa wanawake.
SOMA ZAIDI: Ni Muda Makocha Wazawa Tanzania Waanze Kufanya Kazi Kisasa
Jijini Paris, Tanzania itapeleka wanariadha wanne ambao ni Geay, Simbu, Jackline Sakilu na Magdalena Shauri ambao wote watashiriki mbio za marathoni.
Kwa hiyo, wale Watanzania wazalendo wenye kufuatilia wanamichezo wao tu, watapata nafasi hiyo siku ya mwisho ya michezo hiyo inayodumu kwa takriban siku 30. Lakini kwa wale wengine wapenda michezo, wana kitu cha kufuatilia.
Hakuna uwajibikaji
Mchezo wa soka hujumuisha vijana wenye umri chini ya miaka 20, lakini wachezaji wanaozidi umri huo huwa watatu na hivyo unategemea nyota kama Kylean Mbappe (Ufaransa), Endrick (Brazil) na Jude Bellingham (Uingereza) kujumuishwa kwenye vikosi vya nchi zao na hivyo kusababisha watu wengi kufuatilia mpira wa miguu.
Wengine watakuwa wakifuatilia ustadi katika mbio fupi ambazo zimetengenezwa kwa jinsi ambayo wanariadha wanaweza kuonekana mara kwa mara hadi fainali.
Lakini kwa nini Watanzania wasubiri siku moja tu kufurahia au kushangilia wanamichezo wao kati ya siku 30 za michezo hiyo? Hapa vyama kama vya mpira wa wavu, wa kikapu, wa mikono, wa miguu, riadha, judo, karate au ngumi wanaliambia nini taifa kuhusu wanamichezo wao kukosa nafasi Paris?
SOMA ZAIDI: Tathmini Inahitajika Kuondoa Mazoea Kwenye Soka la Tanzania
Ni kama vile hakuna uwajibikaji kwa wananchi au kutofuzu ni kawaida ambayo imeshazoeleka kwa Watanzania na hivyo hakuna hata haja ya kuwaambia kilichosababisha tusifuzu.
Hata Chama cha Riadha (AT) hakiwezi kujivunia kutokana na ndicho pekee kinachopeleka wanariadha mara zote. Kadri miaka inavyokwenda ndivyo inavyoonekana kuwa wanamichezo wanaofuzu ni wale wanaofanya jitihada binafsi na si programu za vyama.
Kinachoweza kuwa kinafanywa na AT ni mawasiliano tu na Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF), Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kwa ajili ya taratibu za ushiriki.
Lakini hazionekani programu za kuinua wanariadha wa michezo mingine ya riadha hasa mbio fupi na za masafa ya kati kama zilizotuletea medali za akina Bayi na Nyambui.
Mabondia wetu wanazidi kupotea katika ramani ya ngumi za ridhaa, timu za mpira wa mikono ni kama vile hazipo, wakati ile ya mpira iliyoonekana kuwa inaweza kufanya kitu, inaangushwa na ukata.
Kutafuta majawabu
Wakati huu ambao michezo mingi inazidi kuporomoka, ndio wakati ambao Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ambalo ni mkono wa Serikali katika michezo, halina budi kutafuta majawabu ya nini kifanyike kurudisha ushiriki wa vijana katika michezo tofauti.
SOMA ZAIDI: CAF Ilitafutie Suluhu ya Kudumu Suala la Morocco
Serikali imesema itajenga uwanja wa ndani kwa ajili ya michezo kama mpira wa wavu, mikono, kikapu na mingine, lakini ikishakamiliki itatumika vipi kama michezo hiyo haionekani kuwa na uhai? Labda mpira wa kikapu ambao umekuwa ukijikongoja kujiendesha kwa kutafuta wadhamini na kuonyesha kuna uhai.
Zisipofanyika jitihada, uwanja kama huo na hivi vingine vikubwa vinavyojengwa jijini Arusha na Dodoma vitakuwa sehemu ya kuangalia wanamichezo wakubwa wa nje na si vijana wetu.
Najua muda wa wanamichezo kuondoka kwenda Paris utakapofika kutaibuka mijadala mingi kuhusu ushiriki wa Tanzania Olimpiki, lakini mijadala hiyo ilitakiwa ifanyike miaka minne iliyopita na wakati huu tuwe tunapima tulifanikiwa wapi na tumefeli wapi. Ni kwa jinsi hiyo, michezo ijayo ya Olimpiki inatakiwa ianze kuwekewa mkakati sasa.
Ukiwa na timu nzuri ya soka kwa ajili ya kushiriki Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2028, maana yake umejenga msingi mzuri kwa ajili ya michezo ya kufuzu ya Kombe la Dunia ya mwaka 2030 kwa mwanasoka huanza kufikia ubora wa juu akiwa na miaka kuanzia 20 na hivyo ukichanganya na wazoefu wachache una timu bora.
Hiyo ndiyo mikakati inayotakiwa ianze sasa. BMT inaweza kukaa pamoja na viongozi wa vyama kuweka mikakati ya nini kifanyike wakati huu ili mwaka 2028 usitustukize. Tukubali kwamba Olimpiki ya mwaka huu imeshatupita na juhudi za makusudi na za wazi zianze sasa.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.