The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

LHRC Yalaani Tukio La Kutekwa Mtoto Mwenye Ualbino Mkoani Kagera

Tukio hili linakuwa la pili kutokea ambapo tarehe 04 Mei, 2024, tukio kama hili lilitokea mkoani Geita mtoto mwenye ualbino aliyefahamika kwa jina la Kazungu Julius, mwenye umri wa miaka kumi, alivamiwa na watu wasiojulikana na kukatwa mapanga

subscribe to our newsletter!

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu LHRC kimeitoa wito kwa Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama kuhakikisha mtoto mwenye ualbino mwenye umri wa miaka miwili aitwaye Asiimwe Novati aliyetekwa na watu wasiojilikana, anapatikana na wahusika wote wanafikishwa mbele ya sheria.

Tukio la kutekwa kwa mtoto huyo limetokea tarehe 30 Mei, 2024 katika Kijiji cha Bulamula, Kitongoji cha Mbale, Kata ya Kamachumu, Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera.

Katika tukio hilo vijana wawili wanadaiwa walifika nyumbani kwa mtoto huyo huku wakijifanya kuomba msaada wa dawa ya nyoka kwa mama wa mtoto huyo, wakati mama wa mtoto akiwasaidia kijana mmoja wao alimkaba mama huyo kisha kutokomea naye.

Kupitia tamko lake lilitolewa leo tarehe 04 June, 2024, LHRC imelaani vikali muendelezo huo wa matukio ya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino nchini na kutoa wito kwa serikali kufanya upelelezi wa matukio yote na kuhakikisha unakamilika na wahusika wote wanafikishwa mahakamani ili haki itendeke na kukomesha vitendo hivi.

Vile vile LHRC imeisahuri serikali kuweka mifumo ya ulinzi shirikishi katika ngazi zote kuanzia Kitongoji, Kijiji, Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa ili kuhakikisha maisha ya watu wenye ualbino yanalindwa na waendelee kufurahia maisha yao kama wengine katika jamii.

SOMA ZAIDI: Bubujiko la Machozi ya Watu Wenye Ualbino Tanzania

“Ukatili dhidi ya watu wenye ualbino umekuwa ukitokea mara kwa mara kwa namna mbalimbali ikiwemo unyanyapaa, uonevu, na imani za kishirikina,”inaeleza taarifa hiyo.

“Wahalifu wamekuwa wakiwinda watu wenye ualbino kwa imani potofu kwamba viungo vyao vina uwezo wa kimiujiza kama zitatumika katika uchawi na madawa ya kienyeji. Imekubalika kwamba imani hizi potofu zimeenea sana katika maeneo ya chini ya Jangwa la Sahara,” ilieleza zaidi taarifa hiyo ya tamko la LHRC.

Tukio hili linakuwa la pili kutokea ambapo tarehe 04 Mei, 2024, tukio kama hili lilitokea mkoani Geita mtoto mwenye ualbino aliyefahamika kwa jina la Kazungu Julius, mwenye umri wa miaka kumi, alivamiwa na watu wasiojulikana na kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake, hali iliyopelekea kuvuja damu nyingi.

Hata hivyo LHRC imesema kuwa, kipindi cha miaka mitatu iliyopita, matukio haya yalipungua kwa kiasi kikubwa hivyo kutokea kwa tukio hili kumeongeza mashaka ya kurudi kwa kasi kubwa kwa matukio haya.

Katika hatua nyingine, LHRC imetoa wito kwa jamii kutoa taarifa kuhusu watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo ili vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za kipelelezi.

“Tunatoa wito kwa jamii kutoa taarifa kuhusu watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo ili vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za kipelelezi,” ilieleza taarifa hiyo.

Akizungumzia tukio hilo jana Juni 03,2024, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera Yusuph Daniel, aliiambia The Chanzo kuwa jeshi la polisi mkoani humo kwa linashughulikia kwa karibu tukio hilo ambapo mpaka sasa watu watatu akiwemo baba mzazi wa mtoto huyo wanashikiliwa  kwa ajili wa uchunguzi.

Omari Mikoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com. Habari hii imehaririwa na Lukelo Francis.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts