Mwaka 2018, kuelekea wiki ya sheria, Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliandaa huduma za msaada wa kisheria katika eneo la Mnazi Mmoja, Dar es Salaam. Mahakama imefanya hivyo miaka yote.
Taasisi za kisheria zilialikwa kwenda kutoa msaada kwa wahitaji. Hata hivyo, kuna sanaa ilitokea. Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, naye aliandaa tukio lake la namna hiyo.
Tofauti na Mahakama, Makonda alifanya matangazo kwamba atatoa msaada wa kisheria kwa wote wanaodhulumiwa. Kuna wakati alijielekeza katika migogoro ya ndoa. Baadaye ardhi, madai, na kadhalika.
Makonda alichukua wanafunzi wa Shule ya Sheria kwenda kumsaidia kuendesha zoezi lake alilolifanyia zilipo ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ilala Boma. Mahakama, kwa upande mwingine, ilialika wadau ambao wana utaalamu na uzoefu katika kazi hiyo.
Sanaa
Sanaa ilikuwa ni ipi? Mosi, ni ajabu kwamba taasisi za umma, yaani Mahakama na Serikali, zilishindwa kuratibu zoezi lao liende sambamba. Waonaji tulibaini kwamba Mahakama haikufurahia kwa kuwa zoezi la kuendesha wiki ya sheria liko chini yao, na hivyo walipaswa kuungwa mkono na mtu yeyote aliyetaka kushiriki, au kufanya tukio la namna hiyo wiki hiyo, na siyo kujianzishia zoezi jingine ambalo halikuwa na uendelevu.
SOMA ZAIDI: Haya Hapa Matukio Muhimu Kwenye Safari ya Kisiasa ya Paul Makonda
Pili, Makonda aliamsha matumaini ya wananchi aliowaita wanyonge, lakini hakuwa na msaada kwao. Alijinasibu kuwa na majibu ya changamoto zao za kisheria, lakini alitumia zoezi hilo kujiuza kisiasa na kuvuna utukufu binafsi kwa kupata imani ya wananchi aliowaita wanyonge.
Tatu, Makonda alidhalilisha watu – mfano hayati Edward Ngoyai Lowassa kwamba katelekeza mtoto. Duru zilidai kwamba binti aliyewasilisha malalamiko aliandaliwa kwa malengo tofauti ya kumnyong’onyeza Mzee Lowassa kisiasa na kijamii. Inaweza isiwe kweli, lakini kesi iliishia wapi?
Nne, ukomo wa zoezi lake ulikuwa katika kutoa ushauri tu. Na vilevile, ninafahamu kwamba baada ya kusikiliza changamoto za wananchi, ofisi ya Makonda ilikuwa inaandika barua kwa taasisi zinazotoa msaada wa kisheria nchini, kama vile Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kuomba watu hao wasaidiwe. Hiyo ni baada ya watu hao kufuatilia masuala yao ofisini kwake bila msaada wowote.
Kwa hiyo, kama Makonda alikuwa na nia njema, alitakiwa kuzishirikisha taasisi hizo kwa ajili ya uratibu mzuri, uendelevu na ubora wa mchakato na matokeo. Kuiruka Mahakama, licha ya umuhimu wake, na kujinadi kama mtenda haki pekee, ilikuwa ni fyongo tangu awali.
Tano, Makonda aliwapotezea watu muda kiasi cha ukomo wa kufungua mashauri yao Mahakamani kupita. Kwa hiyo, walipoteza muda ofisini kwa Makonda, walipoelekezwa kwenda Mahakamani wakawa wamechelewa, na ndiyo ikawa imetokea hivyo.
SOMA ZAIDI: Tuitumie Sekretarieti ya Maadili Kuwawajibisha Viongozi
Mashauri, hususan yale ya madai, ardhi, yana ukomo. Muda ambao mtu anautumia kuzurura katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa kufuatilia suala lake, halafu baadaye akaambiwa aende TLS asaidiwe ungetumika vema, mtu huyo angepata haki.
Tabia imejirudia
Kwa nini nimerejea kisa hiki? Nimeona tangu Makonda ‘apewe ulaji’ kama Mkuu wa Mkoa wa Arusha, ameanza tena tabia hii. Anaitisha mikutano kusikiliza kero na kutoa haki papo kwa hapo.
Makonda alibainisha tangu aliporejeshwa kama Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwamba hana imani na Mahakama. Lakini yeye anajigeuza Mahakama na anataka wananchi wamuamini. Hii ni bila kujali kwamba watu wanamfahamu vema na wanaijua haiba yake tangu akiwa Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam. Kivyovyote, historia ya Makonda haimuweki fungu moja na neno haki.
Sasa, katika zoezi lake la kusikiliza kero na kutoa uamuzi, amerudia tena kilekile alichokifanya kwa Mzee Lowasa. Amemdhalilisha mtumishi huko Longido. Kwa kutumia ‘ukuu wake’ alimtamkia mwanamama maneno ya kutweza utu na jinsia yake kwa sababu alikuwa anaongea kwa sauti ambayo makonda aliihusisha na masuala ya kingono.
Kama haitoshi, baada ya taasisi kadhaa kukemea kitendo hicho, Makonda alijitokeza tena katika sura yake ya ubabe akidai anafanya kazi ya Mungu, na kwamba hawezi kuvumilia wala rushwa na wazembe.
SOMA ZAIDI: Teuzi za Watu Wasio Waadilifu Zinawapa Motisha Viongozi Kutumia Vibaya Ofisi za Umma
Ukitafakari mlolongo wa matukio haya utajiuliza kama kweli nia yake ni kutatua kero ama kuendeleza urathi wake wa ukatili na utukufu binafsi. Nimetaja ukatili kwa kuwa anafahamika kwa kauli tata dhidi ya watumishi wa umma.
Aliwahi kuvamia kituo cha televisheni akiwa na askari wenye silaha kushinikiza warushe maudhui anayoyapenda. Kwa ujasiri wa kuyafanya hayo hadharani, haitakuwa ajabu kusikia iwapo alifanya matukio ya namna hiyo gizani.
Tatizo la kimfumo
Ninapata shida kuelewa vikao vya Makonda kwa kuwa havina uendelevu, na badala yake ni jukwaa la yeye kujijenga na kujiimarisha kama ‘mtetezi wa wanyonge.’ Tumekuwa hatuoni mbali kiasi kwamba tunasahau kuwa changamoto zetu za kisheria na kimfumo haziwezi kutatuliwa jukwaani.
Migogoro ya ardhi, jinai, madai, bima, familia, ndoa, na zaidi majibu yake ni ya kisheria na yanatakiwa kupatikana Mahakamani. Na kwa kufahamu mifumo yetu ya kisiasa na kisheria, naongeza kwamba, Serikali yetu, kama taasisi, ni tatizo jingine ambalo tumelifuga kwa miaka sitini sasa.
Lakini watendaji wa CCM, chama tawala, na Serikali, wanataka kutupumbaza tusione kwamba wao, chama chao, na mfumo wanaotumia kuendesha nchi ni tatizo.
SOMA ZAIDI: Akina Makonda Wanatulazimisha Tuendelee Kutafakari Nafasi za Wakuu wa Wilaya, Mikoa: Tunawahitaji Kweli?
Matokeo yake, tutarajie kwamba Makonda anaweza kuwa imara kupita kiasi akawa juu ya dhana zote muhimu kama ‘ukuu wa Katiba,’ utawala bora, na uimara wa taasisi? Ukweli ni kwamba, hata kama haya yatatokea, Makonda hawezi kuwa mbadala wa taasisi muhimu kama Mahakama.
Ingawa Mahakama zetu zinahitaji mageuzi, mbadala wake hauwezi kuwa Makonda au mwanasiasa wa ‘kaliba’ hiyo. Tujenge na tuimarisha mifumo ya utoaji haki na ugatuzi wa mamlaka ya nchi. Usanii unaofanywa kwa jina la kusaidia wanyonge hauna uendelevu. Ni watu wangapi wataenda kwa Makonda, kwa uwezo, utaalamu na rasilimali gani alizonazo?
Kwa hiyo, ninapendekeza kwamba tuimarishe taasisi za utoaji haki na usimamizi wa sheria ili tuepukane na biashara ya wanasiasa kutumia matatizo waliyoyatengeneza kuwapumbaza wananchi kwamba wanawapigania.
Ndiyo, wametengeneza matatizo. Wameua chombo cha uwakilishi wa wananchi, yaani Bunge. Vilevile, wameiweka mfukoni taasisi muhimu ya utoaji haki, yaani Mahakama. Ni wezi wa rasilimali za umma, na kila wanachofanya wanaweka mbele maslahi yao binafsi, kama ambavyo Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anaandika kila mwaka, na wanaongoza serikali inayotumia fedha za walipa kodi kufanya matumizi ya anasa.
Kwa hiyo, tuwaepuke wanasiasa aina ya Makonda ambao kwao uongozi siyo utumishi, bali ni daraja la kuvuna utukufu binafsi, na kuwalaghai wananchi kwamba wamebeba maslahi yao kifuani. Nchi ikiendeshwa namna hii, kuna siku tutajikuta tunaishi kwa neno la wanasiasa, na itakuwa tumechelewa sana kurejea katika misingi.
Tito Magoti ni wakili na mtetezi wa haki za binadamu kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia titomagoti@gmail.com au X kama @TitoMagoti. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.