Matukio kadhaa ya kitaifa, kikanda, na kimataifa yalikuwa yanaendelea wakati naandaa tafakuri hii na kudhihirisha, kwa mara nyingine tena, ukweli wa kihistoria ambao mara nyingi husahauliwa na wengi na hivyo kushindwa kutumiwa ipasavyo, kwamba kila wakati watu, hususan wale wanaoonewa, walisimama pamoja kutetea maslahi yao, walifanikiwa sana na kuandika historia.
Ukweli huu ni mzito sana kiasi ya kwamba haishangazi kwa nini kwa kiwango kikubwa unasahaulika kwa sababu wale wanaokandamiza, wanaodhulumu na kuonea wengine wanajua endapo tu kama wale wanaowakandamiza, kuwadhulumu na kuwaonea wataupata na kuuelewa dunia inaweza kubadilika kwa namna ambayo haitakidhi matakwa yao ya kitabaka, na hivyo kufanya kila linalowezekana kuuficha.
“Hivi ndivyo mambo yalivyo, na yamekuwa hivyo kabla hata wewe hujazaliwa, unadhani unaweza kubadilisha nini?” Hii ni kauli ambayo wengi wetu tutakuwa tumeshawahi kukutana nayo iwe ni kutoka kwa watu tunaowajua, vyombo vya habari, nyumba za ibada, na kadhalika, haijalisha ni mbali kiasi gani kauli hiyo iko mbali na ukweli. Lakini mambo yanaweza kubadilika, na tunaona watu mbalimbali wakishiriki kwenye michakato hiyo.
Minyukano
Hapa nchini kwetu, kwa mfano, tunaona myukano mkali ukiendelea kati ya wafanyabiashara na Serikali katika maeneo mbalimbali ya nchi, huku wafanyabiashara wakikubali kuingia hasara kubwa kwa kuamua kufunga maduka yao kuzishinikiza mamlaka husika kufanyia kazi madai yao ambayo, kwa kiwango kikubwa, yanahusiana na utendaji haki kwenye mfumo mzima wa ukusanyaji kodi.
Mnyukano huu, ambao hata hivyo siyo mpya, umeendelea kwa siku takriban nne sasa licha ya Serikali kujitokeza hadharani na kudai kwamba imekubali yaishe na wafanyabiashara hao ambao wanadai mageuzi makubwa kwenye mfumo wa kodi yatakayowawezesha kujihusisha na biashara yenye tija bila ya kuwa na hofu ya biashara hizo kufungiwa au kunyang’anywa kwa kisingizio cha kutokulipa kodi. Watafanikiwa.
SOMA ZAIDI: Kelele Zinazoshinikiza Kufungwa kwa Mitandao ya Kijamii Zinadhihirisha Uwezo Mdogo wa Kufikiria wa Watu Wetu
Jirani na nyumbani, hapo nchini Kenya, tumeona Rais William Ruto akikataa kusaini sheria tata ya kodi baada ya walalahoi nchini humo kuingia barabarani na kuikataa, wakisema mpango huo unaenda kuwaumiza na kuwadidimiza zaidi kwenye dimbwi la umasikini. Hatua hiyo imekuja baada ya Wakenya kadhaa kufariki na wengine kujeruhiwa kwenye maandamano ya kuipinga sheria hiyo. Wamefanikiwa kidogo, lakini mapambano lazima yaendelee.
Huko nchini Uingereza nako, baada ya miaka takribani 20 ya vuguvugu na harakati kutoka kwa mamilioni ya watu ulimwenguni kote, Marekani imefikia makubaliano na mwandishi wa habari Julian Assange yaliyopelekea mwanzilishi huyo wa mtandao wa WikiLeaks kuachiwa huru baada ya kuwa gerezani kwa miaka mitano, na kizuizini kwa miaka 15, akishutumiwa kuvujisha siri za Serikali ya Marekani, hususan kwenye uvamizi wake haramu kwenye nchi za Iraq na Afghanistan. Wapigania haki wamefanikiwa.
Kwa ufupi, kunaweza kuwa na mifano mingi zaidi ya hii katika kona mbalimbali za dunia ambayo hatuwezi kuiweka yote hapa inayodhihirisha kwamba watu wakisimama pamoja, na wakiongozwa na nia safi na thabiti kwenye kile wanachokipigania, mwisho wa siku watafanikiwa. Mafanikio kwenye michakato hiyo ni matokeo ya uhakika, kama ambavyo historia inatuonesha. Mafanikio yanaweza kuchukua miaka mingi, hata karne, lakini yatatokea.
Mafunzo
Mafanikio katika muktadha huu si lazima yahusu kupatikana kwa kile kinachopiganiwa kwa wakati husika. Yanaweza yasihusu Tanzania, kwa mfano, kukubali yaishe na wafanyabiashara, au Ruto kukataa kusaini sheria tata, au Assange kuachiwa huru na dola kandamizi la Marekani linalohubiri kitu kimoja na kufanya kitu kingine kabisa. Mafanikio, katika muktadha huu, yanaweza kuhusu pia mafunzo wananchi wanayapata wakati wa harakati na mavuguvugu yao.
SOMA ZAIDI: Jinamizi la Ajali za Barabarani Litatumaliza Watanzania. Ni Kweli Serikali Haiwezi Kufanya Kitu?
Na moja kati ya mafunzo muhimu tunayoweza kuvuna kutoka kwenye historia ndefu za mapambano na ambayo yamechangia kwenye upatikanaji wa ushindi kwenye harakati nyingi ni uwezo wa wanaharakati na wapigania mabadiliko wengine kumtambua adui anayepaswa kushambuliwa kuwezesha mchakato mzima wa ushindi, ambayo, kwa muktadha huu, ni mabadiliko.
Tukiangalia kwenye historia ya mapambano ya kupigania uhuru wetu hapa Tanganyika, kwa mfano, wazazi wetu waliweza kumtambua mkoloni kama adui yao, wakijikusanya wao na rasilimali chache walizokuwa nazo na kuelekeza nguvu zao kwenye jitihada za kumuondoa, mabadiliko waliyodhani yangewawezesha kuishi maisha ya uhuru yenye kuheshimu utu wao kama binadamu.
Uwezo wa kumtambua adui ni muhimu kwenye mapambano kwani inakusaidia kuokoa rasilimali chache zinazokuwepo kwa ajili ya mapambano, ikiwemo rasilimali muhimu ya muda, kwa kuepuka kushughulika na mambo yasiyo ya msingi, kama vile wapambe wa adui yako, na kushughulika na adui mwenyewe moja kwa moja.
Hii ilikuwa rahisi kidogo wakati wa ukoloni kwani pengo kati ya mkandamizaji na mkandamizwaji lilikuwa la wazi sana kutokana na rangi za matabaka haya mawili, yaani Mzungu kwa upande wa mkandamizaji na Mwafrika kwa upande wa mkandamizwaji, hali iliyowezesha uhamasishaji wa wengi waliokandamizwa kujiunga na mapambano, ingawaje ni ukweli kwamba walikuwepo pia Waafrika kwenye tabaka kandamizi.
Ugumu
Urahisi huu, hata hivyo, uliondoka punde tu baada ya Tanganyika, na baadaye Tanzania, kupata “Uhuru” kutoka kwa mkoloni, na nafasi yake, kama mtawala, kuchukuliwa na Waafrika. Utofauti kati ya mkandamizaji na mkandamizwaji uliacha kuwa rahisi kwani matabaka yote mawili yalihusisha watu waliofanana, yaani Waafrika, hali iliyopelekea ugumu kwenye kuunganisha watu kwa ajili ya kupigania mabadiliko.
SOMA ZAIDI: Ni Wakati Kama Wananchi Tuache Visingizio na Kuanza Kutimiza Wajibu Wetu wa Kiraia
Ilikuwa ngumu wakati ule, na imebaki hivyo hata sasa kwa kiwango fulani, kuonesha ukinzani wa wazi dhidi ya watawala kwani waonevu hao wamekuwa wepesi kuitumia historia ya mapambano dhidi ya wakoloni kama silaha ya kumnyamazisha yoyote anayekosoa namna wanavyoendesha nchi, wakiwadanganya wananchi eti wao ni “wenzao” licha ya kujua kwamba huo ni uongo dhahiri.
Wakati kunaweza kuwa na nadharia nyingi zinazoweza kueleza kwa nini Tanzania bado ni nchi masikini licha ya miongo yake sita ya “Uhuru” wa kisiasa ni imani yangu kwamba kushindwa kwetu kumtambua adui yetu halisi anayekwamisha maendeleo yetu kunaweza kuhusika na hali hiyo.
Mapambano yote ya wananchi yaliyofanikiwa ni yale yaliyoelekezwa kwa adui ambaye watu wameweza kumtambua kwa urahisi kama sababu kubwa ya matatizo yao, kama vile mababu na mabibi zetu walivyoweza kumtambua mkoloni. Nadhani hili ni funzo muhimu tunaloweza kuvuna kutoka kwenye historia mbalimbali za mapambano.
Kwa hiyo, kwa kuhitimisha, swali linagoma kuwa kama harakati za mabadiliko zitafanikiwa au hazitafanikiwa. Historia tayari imemaliza mjadala kuhusu swali hili kwa kutoa jibu kwamba kama harakati zinahusu haki, basi zitafanikiwa. Watu wanaweza kuboresha maisha yao kama watasimama kwa pamoja na kuwakabili wale wanaowafanya washindwe kuwa na maisha bora.
Swali linalobaki ni kuhusu uwezo wa watu wanaopigania mabadiliko hayo kama wana uwezo wa kumtambua adui anayesimama mbele yao, wakaelekeza nguvu na rasilimali zao dhidi yake, na wakafanya harakati hizo kwa mwendelezo, yaani kila siku bila kusita kama wazazi wetu walivyopambana na mkoloni, basi ushindi utakuwa wao mwisho wa siku.
SOMA ZAIDI: Akina Makonda Wanatulazimisha Tuendelee Kutafakari Nafasi za Wakuu wa Wilaya, Mikoa: Tunawahitaji Kweli?
Kwa hiyo, ndugu zangu, tuendelee kupigania mabadiliko tunayotaka kuyaona kwenye familia, shule, kanisa, msikiti, chuo kikuu, jamii, nchi na dunia yetu tukijuwa kwamba historia iko upande wetu na kwamba ushindi ni kitu cha uhakika, haijalishi ni miaka mingapi itatuchukua kuufikia!
Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.