The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ni Wakati Kama Wananchi Tuache Visingizio na Kuanza Kutimiza Wajibu Wetu wa Kiraia

Tukisema tusubiri mpaka mambo yawe kama vile tunavyoyatamani inaweza kutuchukua karne mpaka tuweze kutimiza wajibu wetu wa kiraia, au pengine tusiweze kufanya hivyo milele.

subscribe to our newsletter!

Siku chache hizi zilizopita nimekuwa na bahati ya kushiriki kwenye shughuli angalau tatu ambazo zilikuwa na kitu kinachofanana sana, ambacho naweza kusema ni visingizio baadhi yetu hupenda kujanavyo kuhalalisha uamuzi wetu wa kuacha kutekeleza wajibu wetu kama raia wa nchi ambayo, tunaambiwa, mamlaka yake yote yanatoka kwa wananchi wake.

Mei 25, 2024, kwa mfano, niliongoza mdahalo wa vijana kutoka vyama vya siasa ulioandaliwa na chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotegemewa kufanyika Novemba mwaka huu, ambapo vijana wachache walisema watashiriki kwenye chaguzi hizo kama wapiga kura, huku wachache zaidi wakisema watashiriki kama wapigiwa kura, wakiamini mazingira siyo wezeshi.

Mei 30, 2024, shirika lisilo la kiserikali la Twaweza East Africa lilinialika kama mzungumzaji kwenye mjadala lililouandaa kwenye mtandao wa X, zamani Twitter, kuhusu ushiriki wa wananchi kwenye kuchochea uwajibikaji nchini, ambapo wazungumzaji walikubaliana kwamba ushiriki huo ni mdogo, huku wananchi wenyewe wakieleza sababu mbalimbali zinazopelekea hali hiyo, ikiwemo hofu ya “kupotezwa.”

Mei 31 na Juni 1, 2024, nilishiriki kama mzungumzaji na mwendesha mjadala kwenye kongamano la uhuru wa kujieleza lilioandaliwa na asasi ya kiraia ya MISA-TAN, ambapo lawama zilielekezwa kwa waandishi wa habari waliodaiwa kushindwa kufanya kazi yao ipasavyo, ikiwemo kushindwa kuandika habari zinazohusu maslahi ya umma, huku wanahabari wenyewe wakijitetea, wakiihusisha hali hiyo na mazingira magumu ya kisheria na kiuchumi yanayovikabili vyumba vyao vya habari.

Kwanza, lazima nieleze kwamba sababu zote ambazo vijana, wananchi, na waandishi wa habari walizitoa kwenye lile kongamano la ACT-Wazalendo, mjadala ulioandaliwa na Twaweza, na lile la MISA-TAN, mtawalia, zina mashiko, na ni muhimu, kwa umoja wetu, kuzifanyia kazi ili kuona vijana wengi zaidi wanashiriki kwenye chaguzi, wananchi wanashiriki kwenye kuchochea uwajibikaji, na waandishi wa habari wanafanya habari nyingi zaidi za kiuchunguzi zenye kupigania maslahi mapana ya umma.  

Tabia ya kujikosoa

Lakini nadhani pia ni muhimu kwetu kama raia tukawa na tabia ya kujikosoa na kuangalia ni wapi tunashindwa kutekeleza wajibu wetu wa kiraia, badala ya kila siku kulalamika tu kunyimwa haki hii ama ile, na pengine kuachana na tabia ya kubuni visingizio kuelezea kushindwa kwetu kutekeleza wajibu wetu huo wa kutengeneza Tanzania tunayoitaka. 

SOMA ZAIDI: Watanzania Tupo Kwenye Hali Nyerere Alitutahadharisha Nayo: Utii Ukizidi Unakuwa Woga, na Uoga Huzaa Unafiki na Kujipendeza

Maana, lazima tuseme ukweli, tukiamua kutafuta kisingizio ili tu tusitekeleze wajibu wetu fulani, tutakipata. Hata kama mambo yatakuwa kama vile tunavyoyatamani yawe, bado tukitafuta kisingizio ili tusifanye jambo fulani, uhakika ni kwamba tutakipata tu.

Tuchukulie hili suala la kutaka uwajibikaji kutoka kwa watu waliokabidhiwa mamlaka ya kuendesha ofisi za umma kama mfano, kama vile kuwataka askari wa Jeshi la Polisi kufuata sheria na taratibu wakati wanapotekeleza majukumu yao ili kuepusha kuumiza watu, ambapo baadhi yetu tunaweza kuwa na hofu ya kupaza sauti zetu zinazolenga kufanikisha suala hilo.

Hapa, utakuwa na uhakika kwamba mtu pekee ambaye atakuwa na anasa ya kufikiria matokeo ya kitendo chake, kama vile kukamatwa au “kupotezwa,” ni yule ambaye matukio haya hayajamuathiri yeye binafsi, yaani hajawahi kudhalilishwa na kuteswa na polisi, au hakuna ndugu yake ambaye alichukuliwa akiwa hai na polisi, lakini akarudishwa akiwa amefariki, au asirudi kabisa.

Utakuwa na uhakika kwamba mtu ambaye ameathiriwa na matukio hayo hawezi kuwa na hiyo anasa ya kufikiria nini kinaweza kumtokea yeye binafsi endapo kama ataungana na Watanzania wengine kuwataka askari wa Jeshi la Polisi kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo inayoongoza kazi zao za kila siku za usimamizi wa sheria.

Ubinafsi?

Lakini je, ni kweli tunataka kutengeneza taifa ambalo kama mtu kitu hakijamuathiri yeye binafsi na maslahi yake binafsi moja kwa moja basi hawezi kukipazia sauti ili kikomeshwe na kusitishwa? 

SOMA ZAIDI: Je, Ubadhirifu Serikalini Unaweza Kudhibitiwa? Wataalamu Wanaamini Hivyo

Tukifika huko, je, kutakuwa na haja gani ya kujitambulisha kama wanachama wa jamii fulani, au kujitambulisha kama ‘Watanzania,’ utambulisho unaotokana na mtazamo wetu wa kuwa wamoja kama wananchi? Ndugu zangu, hatuwezi kumudu gharama za kuendelea kuwa na mtazamo kama huo.

Ifike wakati kila mmoja wetu atimize wajibu wake katika kuifinyanga Tanzania ya ndoto yake, haijalishi mazingira ya kufanya hivyo ni wezeshi kiasi gani, na hii inahusu pia ushiriki wetu kwenye chaguzi zinazokuja na michakato mingine yote ile ya kidemokrasia. 

Niliwaambia vijana wenzangu kwenye mjadala ule uliokuwa umeandaliwa na ACT-Wazalendo kwamba ni muhimu kushiriki kwenye chaguzi zinazokuja licha ya mazingira ya kushiriki siyo mazuri kwani tukiacha kushiriki hatutakuwa na uhalali wa kuikosoa michakato hiyo. 

Kwa hiyo, tayari unaweza kuona kwamba suala la kushiriki kwenye michakato hii lina maslahi mapana kwetu kama vijana na wakosoaji wa mifumo iliyopo pia. Hatuwezi kuendelea kuendeshwa na ukosefu wa imani yetu kwenye mifumo iliyopo na hivyo kuacha kutimiza wajibu wetu muhimu wa kiraia. 

Wazazi wetu waliopigania Uhuru wa taifa hili walikuwa kwenye mazingira magumu kuzidi sisi, lakini hiyo haikuwazuia kushiriki kwenye chaguzi zilizokuwa zinaandaliwa na kusimamiwa na mkoloni, mkoloni ambaye, kumbuka, hakuwa na maslahi yoyote kwenye kutenda haki kwa wakazi wa iliyokuwa Tanganyika, maana hawakuwa hata raia.

Matarajio ya wananchi

Vivo hivyo kwa waandishi wa habari, kwamba visingizio vyao kwa nini wanashindwa kufanya habari za maslahi mapana kwa umma, na badala yake kufanya kazi kama vile vyombo vyao vya habari vimekuwa mbao za matangazo ya Serikali na idara zake, haviwezi kuingia akilini miongoni mwa Watanzania waliowengi. 

SOMA ZAIDI: Bila Uhuru, Vyombo vya Habari Vitaendelea Kubaki Kuwa Midomo ya Serikali

Hii ni kwa sababu Watanzania hawa wanawasikia wanahabari na viongozi wao wakiusifu uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa “kuboresha” uhuru wa habari nchini, “ukweli” ambao viongozi waandamizi wa tasnia hiyo wamekuwa wakiuelezea hadharani kila wanapopata fursa ya kufanya hivyo.

Ni matarajio ya Watanzania kwamba, kama kweli mazingira ya kufanya kazi kwa waandishi wa habari yameimarika chini ya uongozi wa Rais Samia, na kwamba sasa vyombo vya habari viko huru kufanya kazi zao, basi uhuru huo uakisiwe kwenye maudhui ya habari wanahabari wanazalisha kila siku kwa kufanya habari ambazo kweli zinatetea maslahi ya umma.

Nihitimishe safu hii kwa kusema kwamba kila mmoja wetu ana wajibu wa kuitengeneza Tanzania ya ndoto yake. Kama ilivyo ni rahisi kulalamika kwamba tunanyimwa haki hii au ile, iwe hivyo hivyo kwenye kusimama, mmoja mmoja na kwa umoja wetu pia, kutimiza wajibu wetu kwenye kuzidai haki hizo tunazonyimwa.

Tusisubiri mpaka madhila yatufike sisi binafsi na familia zetu ndiyo tuanze kuzunguma; tuanze kuzungumza pale tu tunapoona Katiba, sheria, kanuni, taratibu, na miongozo tuliyojiwekea kama nchi ili kufanikisha malengo yetu ya kitaifa zinakiukwa, hata kama ukiukwaji huo, kwa wakati huo, hautuathiri sisi binafsi au maslahi yetu ya moja kwa moja.
Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts