The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Bila Uhuru, Vyombo vya Habari Vitaendelea Kubaki Kuwa Midomo ya Serikali

Tunahitaji kuwa na vyombo huru vya habari ili wananchi waweze kushiriki kikamilifu kwenye uendeshwaji wa nchi yao na kuuishi u-jamhuri wao.

subscribe to our newsletter!

Mpaka muda huu nadhani utakuwa umeshawahi kumsikia afisa mmoja au mwingine wa Serikali akieleza namna Tanzania ilivyo na vyombo vingi vya habari, akitoa takwimu hizo kwa kuvuma na kujivuna na kueleza kwamba hicho ni kielelezo tosha cha uwepo mkubwa wa uhuru wa vyombo vya habari hapa nchini kwetu. Basi ilikuwa hivyo pia kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari yaliyofanyika Dodoma kuanzia Mei 1 hadi Mei 3, 2024.

Lakini, tuhoji, ni kweli kwamba kuongezeka kwa idadi ya vyombo vya habari sehemu fulani ni ushahidi wa uwepo wa uhuru wa vyombo vya habari mahala hapo? Angalau kwa hapa Tanzania, hiyo siyo kweli hata kidogo, na uhuru mara nyingi huwa haupo hata kwenye vitu vya kuzingatia wakati mtu, au kikundi cha watu, fulani wanapoamua kuanzisha chombo cha habari.

Kuna vyombo vya habari vinaanzishwa kwa malengo tu ya kibiashara, kisiasa, au kidini, na uhuru unaweza usiwe kigezo kikubwa cha uanzishwaji wake ukilinganisha na maelewano mazuri kati ya waanzilishi wake na mamlaka za nchi; kwamba kinachojalisha zaidi siyo hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini bali ukaribu kati ya wamiliki wake na Serikali utakaosaidia kufanikishwa kwa lengo mahususi.

Vipo vyombo vya habari, vichache sana, vinavyoanzishwa kufanya uandishi wa maslahi ya umma, ikiwemo kusimamia uwajibikaji wa viongozi wa umma, huku waanzilishi wake wakijua fika kwamba uhuru wa wao kufanya kazi zao ni mdogo mno, wakiweka kwenye malengo ya chombo husika cha habari kupigania uhuru huo kuongezeka na kupanuka zaidi.

Kwa maneno mengine, kama ilivyo tu kwamba uwepo wa utitiri wa vyama vya siasa nchini Tanzania haumaanishi uwepo wa mifumo inayohakikisha uchaguzi wa huru na haki, vivyo hivyo, uwepo wa utitiri wa vyombo vya habari haumaanishi uwepo wa uhuru wa vyombo vya habari.

SOMA ZAIDI: Labda Suluhu ya Serikali Kudharau Maoni ya Wananchi ni Kuacha Kushirikiana Nayo?

Kama ilivyo kwenye vyama vya siasa, wapo waanzilishi wa vyombo vya habari wasaka fursa na wenye malengo binafsi yasiyohusiana na lengo halisi la chombo cha habari, na wapo wenye malengo ya kweli ya kulihabarisha taifa ili kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu kwenye uendeshwaji wa nchi yao.

Hakuna uhuru

Pia, siyo kweli kwamba kuna uhuru wa vyombo vya habari Tanzania, na ingawaje kuna mjadala mpana kuhusu uhuru wa vyombo vya habari unajumuisha nini haswa, hapa nchini kwetu hali ni mbaya sana kiasi ya kwamba hakuna hata haja ya kufanyika kwa mjadala kuhusu swali kwamba uhuru upo au la!

Kwa mfano, hakuna uhuru wa vyombo vya habari katika mazingira ambapo mwandishi wa habari analazimika kisheria kuomba kibali, au press card, kutoka kwa Serikali ili aweze kufanya uandishi wa habari, kibali ambacho unapaswa kukiomba kila mwaka. Fikiria hapo mamlaka makubwa Serikali iliyojipa katika kudhibiti uandishi wa habari!

Hakuna uhuru wa vyombo vya habari katika mazingira ambapo waziri mwenye dhamana ya habari anaweza kusimamisha uchapishwaji wa gazeti, au kulifutia leseni kabisa, kwa sababu tu anadhani habari iliyoandikwa ni ya “uongo” au ya “kichochezi.” Hapa Tanzania, Serikali inakuwa mlalamikaji, mwendesha mashitaka na hakimu kwa wakati mmoja inapotokea haijafurahishwa na habari fulani.

Hakuna uhuru wa habari katika mazingira ambapo Serikali imejipa jukumu la kumtafsiri “mwandishi wa habari” ni nani, ikijitwisha zigo zito la kumaliza mdahalo wa kitaaluma ambao wanazuoni wameshindwa kuumaliza kwa miaka na miaka. Uhuru wa vyombo vya habari, bila shaka, hauruhusu Serikali ijipe jukumu la kusema nani ni mwandishi wa habari na nani siyo.

SOMA ZAIDI: Tutawezaje Kubuni Katika Mazingira ya Uhuru wa Mashaka?

Hakuna uhuru wa habari katika mazingira ambapo kashfa imefanywa kuwa kosa la jinai wakati ulimwenguni kote kashfa ni kosa la madai. Ukinikashifu leo, natakiwa kwenda Mahakamani kulalamika, na Mahakama ikikubaliana na hoja zangu, itakuamrisha unilipe fidia. Hapa Tanzania, Serikali inaweza kuitaka Mahakama imfunge mwandishi wa habari baada ya kumshutumu kuhusika na kashfa!

Naweza kuendelea kuorodhesha mifano zaidi ya mia mingine inayodhihirisha kwamba hakuna uhuru wa habari Tanzania, lakini nahofia kukuchosha bure. Itoshe tu kusema kwamba nchi yenye uhuru wa habari haimlazimishi mwandishi apate kibali cha mkurugenzi wa halmashauri ili aweze kuongea na mwalimu mkuu wa shule ya Serikali au afisa mtendaji wa kijiji.

Midomo ya Serikali

Kwa hiyo, utitiri wa vyombo vya habari katika mazingira kama hayo niliyoyaonesha ya kukosekana kwa uhuru wa vyombo vya habari, unamaanisha nini katika maisha ya kila siku, na mwananchi wa kawaida anaathirika vipi? Unamaanisha kwamba vyombo vya habari vinaacha kuwa midomo ya wananchi hao na badala yake vinakuwa midomo ya Serikali, au watawala, na wapambe wao.

Angalia kwenye chombo chochote cha habari unachokitegemea kujua yanayoendelea na hutahangaika kuona ukweli kwenye kile ninachokisema. Vyombo vyetu vya habari vimekuwa kasuku wa matamshi ya watawala na wapambe wao, huku takriban asilimia 60 ya habari zinazoandikwa ikidaiwa hutokana na matamko ya Serikali.

‘Habari’ imekuwa ni yale yote yanayomuhusu kiongozi mkuu wa nchi, wasaidizi wake, au wapambe wengine wa watawala. Habari zote, hata zile zinazohusu masuala yanayoathiri ustawi wa wananchi, zinatolewa kwa mtazamo wa viongozi wa Serikali, chama tawala, NGO au watu wengine wenye ushawishi, iwe ni polisi kukanusha taarifa hii, au Serikali kufafanua kuhusu taarifa ile.

SOMA ZAIDI: Watanzania Tupo Kwenye Hali Nyerere Alitutahadharisha Nayo: Utii Ukizidi Unakuwa Woga, na Uoga Huzaa Unafiki na Kujipendeza

Nadra sana kuona vyombo vyetu vikijikita kuelezea masuala yanayoathiri ustawi wa wananchi kutoka kwa mtazamo wa wananchi wenyewe, ikijengeka dhana kwamba wananchi hawajuwi matatizo yanayowakabili, wala suluhisho zao, na ni Serikali tu ndiyo inayoweza kufanya hivyo. 

Siyo ngumu sana kujua kwa nini vyombo vyetu vingi vya habari vinafanya hivi: vinafanya hivi kwa sababu ni njia rahisi ya wao kuendelea kuwepo bila kuiudhi Serikali; ni matokeo ya kupindishwa kwa kanuni ya msingi kwamba wajibu wa mwandishi na chombo chake ni kwa jamii na badala yake sasa waandishi wanawajibika kwa Serikali!

Na wala hatupimi uhuru wa vyombo vya habari kwa kuangalia nini vyombo hivyo vinaripoti kila siku, bali kwa kuangalia vinaripoti vipi yale vilivyoamua kuyaripoti. Muhimu zaidi kwenye kupima uhuru wa vyombo vya habari ni kuangalia ni masuala yepi vyombo vya habari vinaacha kuripoti kabisa kwa sababu ni kutofanya, badala ya kufanya, ndiko kunakoelezea hulka ya mtu fulani.

Haikubaliki

Hata hivyo, hali haipaswi kuendelea kama hivi kama kweli tunakusudia kujenga taifa la watu wanaojitawala badala ya kutawaliwa, kama ambavyo Katiba yetu inalitambulisha taifa la Tanzania kupitia U-jamhuri wake. Huwezi kujenga jamii ya watu wanaojitawala kama una vyombo vya habari vinavyoshindwa kuwa majukwaa ambayo wananchi wanaweza kuyatumia kuchagiza ushiriki wao kwenye uendeshwaji wa nchi yao.

Ni wakati kama wananchi tuiambie Serikali ijitoe kwenye jukumu la kusimamia maadili ya waandishi wa habari, na kazi hiyo ibaki kwenye vyombo huru na vya waandishi wa habari wenyewe. Serikali haihusiki kusimamia maadili ya mawakili, wala wauguzi au wakunga. Kwa nini Serikali ihisi ina jukumu la kusimamia maadili ya waandishi wa habari? Haiwezekani!

SOMA ZAIDI: ‘Mhariri Msalabani’ Inatueleza Nini Kuhusu Historia ya Uhuru wa Habari Tanzania?

Mwalimu Julius Nyerere, muasisi wa taifa la Tanzania, angeweza kumuacha Malkia wa Uingereza aendelee kuwa mtawala wa Tanganyika, lakini alikataa na kuifanya Tanganyika, na baadaye Tanzania,  kuwa Jamhuri ili Watanzania wajitawale wenyewe. Vyombo vya habari, vikiwa kama mhimili wa nne wa dola, vinapaswa kutoa mchango mkubwa katika kufanikisha mchakato huo, lakini hilo haliwezekani katika mazingira ya sasa.

Tupiganie u-jamhuri wetu, tukatae kutawaliwa, tuvisimamie vyombo vya habari vipiganie maslahi yetu, na tuiambie Serikali kwamba msisitizo wake wa kutaka kusimamia maadili ya vyombo vya habari unakinzana na maslahi yetu kama wananchi, na hivyo iwaache waandishi wa habari wajisimamie wenyewe na kufanya kazi zao kwa uhuru. 
Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *