The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tutawezaje Kubuni Katika Mazingira ya Uhuru wa Mashaka?

Ubunifu hauwezi kushamiri kwenye jamii inayoendekeza uimla na heshima isiyohojiwa kwa mamlaka.

subscribe to our newsletter!

Ili mwanadamu aweze kubuni, ni lazima kwanza awe na uwezo wa kufikiri, na ili kuwa na uwezo huo mtu huyo atahitaji uhuru utakaomuwezesha kuweka hadharani mawazo na tafakuri zake. Wito wa watu kuwa wabunifu umekuwa ukiendelea kwa siku nyingi hapa nchini kwetu; haiko hivyo, angalau siyo kwa sasa, kwenye suala la watu kuwa huru kufikiri.

Namna tulivyoijenga jamii yetu, tukitilia mkazo mkubwa sana suala la utii na mtindo wa kufikiri kimakundi, tunabomoa ari na uthubutu wa watu wetu kufikiria, hali inayojenga mazingira ya kuvutia ya watu kutaka kufanana na wenzao, ikijengekeka dhana kwamba kuwa tofauti ni hatari hakuna mtu yuko tayari kuikabili. Badala ya kuwa wabunifu, tunakuwa chawa!

Nimesema jamii kwa sababu ndiko mambo yote yanapoanzia, iwe ni kufanikiwa au kuharibikiwa kwa taifa, au watu wake. Yetu sisi ni jamii inayotukuza umwinyi na kuabudu uimla; ni jamii inayowekeza umuhimu wa kupitiliza kwenye mamlaka, ikiaminisha wanachama wake kwamba mkubwa hakosei na mdogo hawezi kuwa msemakweli.

Uimla

Katika ngazi ya familia, wengi wetu tumelelewa na wazazi, hususan baba, ‘vichwa vya familia,’ ambao hawajawahi kuona umuhimu wa kutushirikisha kwenye mipango ya familia, hata ile inayohusu maisha yetu binafsi, ikiwemo chuo kikuu cha kwenda na masomo ya kuchukua. Na pale tulipojitutumua na kueleza mawazo yetu hawakuwahi kuona mantiki ndani yao.

Tukiwa shuleni, na hata vyuo vikuu, walimu na wahadhiri ni wajuaji wa kila kitu, wenye motisha hafifu kabisa, muda mwingine ikikosekana kabisa, ya kuwashirikisha wanafunzi, ambao ndiyo sababu ya wao kuwepo hapo, kwenye mipango ya shule, au chuo husika, ambayo, cha kustaajabisha kabisa, inabuniwa “kumsaidia” mwanafunzi!

SOMA ZAIDI: ‘Mhariri Msalabani’ Inatueleza Nini Kuhusu Historia ya Uhuru wa Habari Tanzania?

Niambie, mtu aliyekulia katika mazingira hayo anautolea wapi uwezo wa kubuni jambo lolote linaloweza kuisaidia jamii yake? Mtu ambaye ameaminishwa maisha yake yote kwamba hahitajiki kufikiria na badala yake anapaswa atekeleze tu maagizo anayopewa na wakubwa zake ‘kutoka juu’ anaweza kubuni nini huyu? (Wale wachache walioweza kubuni miongoni mwetu hawajafanya hivyo kwa sababu ya mazingira wezeshi bali ni licha ya kukosekana kwa mazingira hayo, kongole kwao wote).

Mazoea

Na kwa sababu uongozi, uwe wa kijiji au hata Serikali kuu, ni kielelezo cha jamii husika na watu wake, haishangazi kuona jitihada za kukandamiza fikra huru zikitekelezwa na viongozi waandamizi wa Serikali, muda mwingine wakilazimika kutumia vyombo vya dola kuhakikisha wananchi wanakuwa watiifu na wanaoheshimu mamlaka na kutekeleza maagizo yake.

Mara ngapi umesikia Serikali ikipiga marufuku nyimbo kwa maudhui yake eti kuonekana kuikosoa Serikali iliyopo madarakani na kiongozi wake, muda mwingine hata kwa msanii kukamatwa na polisi? Ni mwendelezo wa mkubwa hakosei na mdogo hawezi kuwa msemaukweli. Mtu anakamatwa na kuwekwa ndani eti kwa sababu polisi inaamini amedanganya kwenye nyimbo, nyimbo hivyo? Unabuni nini katika mazingira kama hayo?

Msukumo wa kuwafanya watu waache kufikiri na badala yake wasubiri maelekezo ya wakubwa wao Serikalini ni mkubwa na umefanywa kuwa kitu cha kawaida kiasi ya kwamba sasa wakubwa wanautekeleza muda mwingine bila hata kujua wanafanya hivyo kwa sababu imeshakuwa sehemu ya hulka na utamaduni wao.

Mnamo Machi 21, 2023, kwa mfano, wanachama wa Taasisi ya Mtandao wa Sekta Bunifu Tanzania (CINT) walipigwa na bumbuwazi baada ya Serikali kupiga marufuku mkutano wao kuhusu Sera ya Filamu uliokuwa ufanyike siku hiyo pale Makumbusho ya Taifa, Dar es Salaam, kwa kisingizio eti Serikali tayari ina mipango yake kuhusiana na suala hilo! (Robert Mwampembwa, mkurugenzi wa CINT, analielezea kwa kina sakata hili kwenye mazungumzo yake haya na Jenerali Ulimwengu, mwandishi mkongwe wa habari). 

SOMA ZAIDI: Bila Uhuru wa Mwanafasihi, Fasihi Haiwezi Kuwa Chombo cha Ukombozi wa Umma

Kwamba kwa sababu Serikali inatafakari suala fulani basi watu wengine, hata kama wanaguswa kwa kiasi gani na suala lenyewe, hawana haki ya kulitafakari jambo hilo. Najua unaona jambo hili ni la ajabu sana, na nikuhakikishie tu kwamba na mimi nina mtazamo kama huo wa kwako. 

Siku ya uhuru, ubunifu

Bado tuna safari ndefu kama taifa kwenye kutambua mchango wa watu kuwa huru kufikiri na uwezo wao wa kubuni suluhu za matatizo lukuki yanayotusumbua kama watu. Na ni katika muktadha huu ndipo sisi hapa The Chanzo tumeamua kufanya kongamano kuhusiana na suala hilo Jumamosi hii ya Aprili 20, 2024, pale Makumbusho ya Taifa, Dar es Salaam.

Siku ya Uhuru na Ubunifu wa Kidijitali ya The Chanzo, kama kongamano hilo linavyojulikana, inakusudiwa kuhudhuriwa na washiriki takriban 300 kujadili namna, kama wananchi, tunavyoweza kushajihisha fikra huru na tunduizi na kubainisha umuhimu wake kwenye kutengeneza kizazi cha watu bunifu watakaolipeleka taifa hili kwenye mafanikio.

Kidijitali kwa sababu kwa sasa tupo kwenye zama ambazo maisha yanatokea kwenye uwanda huo, kuanzia nyenzo za kuboresha huduma za afya na kupanua fursa ya elimu kwa wananchi, mpaka biashara na burudani, uwanda wa kidijitali umekuwa mpana sana na athari zake kuwa kubwa kiasi cha kugusa sehemu zote za maisha yetu. Ni huko ambako sasa watu tunaenda na kutoa maoni yetu kuhusu masuala kadhaa ya kitaifa na kimataifa yanayohusu ustawi wetu.

Sikiliza, katika mazingira tuliyonayo hivi sasa, chaguzi ni mbili tu: uendelee kujikunyata kama kifaranga aliyenyeshewa na mvua, ukiamini hakuna kitu unaweza kukibadilisha kuwa bora, au usimame, ukatae hali iliyopo mbele yako na kujiambia kwamba unaouwezo wa kubadilisha mambo. Sisi hapa The Chanzo tumeamua kuchagua hili chaguo la pili.

SOMA ZAIDI: Tutapiga Marufuku Vitu Vingapi Kwa Kuwaletea ‘Ukakasi’ Watu Wengine?

Na kwa hiyo, kwa niaba ya timu nzima ya The Chanzo, ningependa kukukaribisha wewe na rafiki au jirani au mwenza au mwanafunzi mwenzako kwenye kongamano letu hili litakalofanyika kuanzia saa tatu asubuhi mpaka saa tisa mchana, kukiwa na wazungumzaji mbalimbali watakaojadili mada motomoto zinazohusiana na uhuru na ubunifu, na kuchochea mjadala wa wazi utakaofanyika siku hiyo. (Unaweza kujisajili kushiriki kwa kujaza dodoso hili hapa).

Kama asili ina somo lolote la kumpatia mwanadamu basi ni ukweli usiopingika kwamba hakuna hali inayoweza kudumu milele, na kama kuna mabadiliko yoyote chanya yatakayotokea nchini kwetu basi yatapaswa kuletwa na sisi, mmoja mmoja na katika umoja wetu.

Kuzungumza yanayokusibu ni sehemu ya kwanza, na ya muhimu, ya kutatua ugonjwa unaokunyima raha, na hivyo nakukaribisha uje ujumuike na sisi kwenye kuzungumza yanayoisibu tasnia ya ubunifu Tanzania kwa lengo la kuiboresha zaidi.

Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *