The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Labda Suluhu ya Serikali Kudharau Maoni ya Wananchi ni Kuacha Kushirikiana Nayo?

Mara nyingine Serikali inatualika kutoa maoni yetu, tuiambie iendelee tu, maana yenyewe ndiyo Serikali na yenyewe tu ndiyo inayojua nchi hii na watu wake wanahitaji nini ili kufikia maendeleo inayoyatafuta.

subscribe to our newsletter!

Aprili 18, 2024, nilikuwa na bahati, au niseme upendeleo, wa kuwa miongoni mwa waandishi wa habari kutoka Tanzania walioombwa na UNESCO kukutana na kufanya mazungumzo na wajumbe wa Kamisheni ya Vyombo vya Habari ya Zimbabwe, waliokuja nchini kujifunza mambo kama vile sheria zinazoongoza vyombo vya habari, ulinzi wa taarifa binafsi, na uchumi wa vyombo vya habari.

Nikiri kwamba sikuwa nafahamu mambo mengi kuhusu tasnia ya habari katika taifa hilo la kusini mwa Afrika, na kama kuna chochote nilichokuwa nawaza basi hakikuwa chanya, na hivyo wazo la Wazimbabwe kuja kujifunza Tanzania halikunishangaza sana. Mtazamo huu, hata hivyo, ulibadilika baada ya Mwenyekiti wa kamisheni hiyo, Profesa Ruby Magosvongwe, kuelezea namna kamisheni hiyo ilivyopatikana.

Magosvongwe alisema kwamba kamisheni hiyo inayosimamia tasnia nzima ya habari nchini Zimbabwe imeanzishwa kwa Katiba ya nchi na kwamba wajumbe wake wanapatikana kupitia mchakato wa wazi na baada ya kuthibitishwa na Bunge la nchi hiyo. 

Pamoja na mambo mengine, makamishna wako huru kufanya kazi zao na mchakato wa kuwaondoa ni mrefu na ambao pia hupitia bungeni. (Unaweza kusoma kwa kirefu kuhusu kamisheni hiyo hapa).

Mpaka kufikia hapa, mimi, nikiungana na Mhariri Mkuu wa Fama Magazine, na moja kati ya waandishi wa siku nyingi nchini, Neville Meena, na muasisi wa mtandao wa JamiiForums, Maxence Mello, tukawa tayari tumeshashawishika kwamba ndugu zetu hawa kutoka Zimbabwe hawana cha kujifunza kutoka kwetu, na badala yake, sisi Watanzania ndiyo tulio na mengi ya kujifunza kutoka kwao.

SOMA ZAIDI: Sheria ya Huduma za Habari Yadaiwa Kufanyiwa Marekebisho kwa Asilimia 31 Tu

Punde tu baada ya Profesa Magosvongwe kumaliza utangulizi wake mfupi, na hata sidhani kama alimaliza, tulianza kutilia mashaka nia yao ya kuja Tanzania, tukiwaambia ndugu zetu hawa, kwa heshima kubwa, kwamba kwa kweli hapa hakuna kitu wanaweza kujifunza, hali iliyomhuzunisha kidogo mwenyeji wetu, Nancy Angulo, anayesimamia kitengo cha habari na mawasiliano UNESCO, aliyekuwa akitusihi tusahau kwa muda mambo yetu hasi na tukumbuke yale yaliyo chanya.

Udhibiti

Lakini unakumbuka vipi yaliyochanya katika mazingira ambapo unaelezewa hali ambayo wakati kwako iko ndotoni tu, wenzako tayari wanaiishi? Hapa Tanzania, tumekuwa siku zote tukihimiza kwamba udhibiti wa waandishi wa habari uondoke kuwa chini ya waziri mwenye dhamana ya habari na badala yake waandishi wajisimamie wenyewe, au angalau wasimamiwe na chombo kilicho huru. Kwetu hii bado ni ndoto ambayo wenzetu Wazimbabwe wanaiishi tayari.

Basi, kuanzia hapo tukaanza kuelezea matatizo yanayoikumba sekta ya habari Tanzania, tukigusia, pamoja na mambo mengine, namna Serikali ilivyotuchezesha shere kwa kuanzisha mchakato wa kupata maoni ya wadau ili kurekebisha Sheria ya Huduma za Habari, 2016, ambayo imelalamikiwa sana na wadau kama kandamizi, inayompa waziri mwenye dhamana mamlaka makubwa na ya kipolisi ya kuingilia uhuru wa vyombo vya habari. Marekebisho yamefanyika, na malalamiko yako palepale!

Mjadala ukahama kutoka tasnia ya habari na kuangazia miktadha mingine ambapo Serikali iliomba wadau wajitokeze kutoa maoni yao kuhusiana na sheria na mambo mengine mbalimbali yahusuyo nchi na matokeo yake yakawa ni kuja na vitu, ikiwemo sheria, zisizoakisi kabisa maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wadau wa sekta husika.

Mbali na Sheria ya Huduma za Habari, Serikali iliacha kabisa mapendekezo yaliyotolewa na wadau kwenye mchakato wa kutengeneza Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, 2022. Serikali, katika hali iliyowashangaza wengi, ilifanya hivyo pia kwenye sheria tatu za uchaguzi zilizosainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, katikati ya kelele nyingi za “maridhiano” na “mageuzi” ya kisiasa.

SOMA ZAIDI: Miswada ya Uchaguzi Iliyopitishwa na Bunge Inakinzana na Nia ya Rais Samia ya Kuleta Mageuzi ya Kisiasa Tanzania

Katikati ya malalamiko yetu, Profesa Magosvongwe, kwa huruma iliyoje, akasema labda hali hii inatokana na namna tunavyoamua kuishirikisha Serikali kwenye uchechemuzi wetu, akitutaka tutafute namna bora na nzuri zaidi ya kufanya hivyo ili iwe rahisi kwake kuyachukua. 

“Kama mwanamme anayejaribu kumtongoza mwanamke,” namkumbuka Magosvongwe, ambaye ni mwalimu wa fasihi kitaaluma, akituelekeza namna ya kuishirikisha Serikali. “Mwanamme anayemtongoza mwanamke hafanyi hivyo kwa kutumia kisu, akijaribu kumtishia nacho.”

Unyenyekevu

Lakini nikawaza, hivi si ndivyo ambavyo tumekuwa tukifanya hadi sasa? Kwa mtazamo wangu mimi, kama wananchi, tumekuwa watulivu na wanyenyekevu sana kwenye juhudi zetu za kuwasilisha maoni yetu kwenye michakato yote inayozinduliwa na Serikali, tukiwa makini sana kwenye kuchagua mbinu na lugha zetu ili tusijetukawaudhi wakubwa wakayapiga chini mawazo yetu.

Kimsingi, tumekuwa watulivu na wanyenyekevu sana kwa Serikali yetu tukufu na viongozi wake wakifu kiasi ya kwamba hata wakiweka hadharani muswada wa sheria asubuhi na kututaka tufike Dodoma kutoa maoni yetu jioni, basi tutafanya hivyo bila ukinzani wowote, au malalamiko yoyote ya wazi na ya hadharani.

Na nini imekuwa malipo yetu mara zote kwa utiifu na unyenyekevu wetu huo? Dharau. Kebehi. Kupuuzwa. Licha ya malipo hayo, Watanzania tumeendelea kuwa watulivu, haijalishi ukweli kwamba tabia hiyo haijawahi kutusaidia kutuletea mabadiliko yoyote chanya katika historia ya nchi yetu. 

SOMA ZAIDI: Watanzania Tupo Kwenye Hali Nyerere Alitutahadharisha Nayo: Utii Ukizidi Unakuwa Woga, na Uoga Huzaa Unafiki na Kujipendeza

Najua, wapo baadhi watakaojenga hoja kwamba ninachosema hakina ukweli, kwamba kwenye miongo yake sita ya uhuru yapo mageuzi mengi Tanzania imeyapiga. Mimi nitakubaliana na tathmini hiyo, lakini nitaongeza kwamba, kwa kiasi kikubwa, mageuzi hayo hayajatokana na msukumo na shinikizo la wananchi. Kama si matokeo ya wahisani na wadau wengine wa maendeleo, basi mageuzi hayo ni matokeo ya busara za watawala!

Ni katika muktadha huu ndipo nilipoinua mkono kwenye kikao chetu kile cha Aprili 18 na kusema kwamba tatizo siyo kwamba Watanzania hatufahamu namna nzuri ya kuishirikisha Serikali maoni na mawazo yetu. Tatizo, nionavyo mimi, ni kwamba tumeamua kuishirikisha Serikali mawazo yetu ambayo haiyahitaji na haina utashi na maslahi ya kuyazingatia kwenye michakato ya uendeshaji wa nchi.

Pengine ni wakati kama wananchi tujaribu mbinu nyingine ya tofauti kidogo, tuache kushirikiana na Serikali ili tusiipotezee muda kwenye jitihada zake za dhati za ‘kutuletea maendeleo?’ 

Kwamba, mara nyingine Serikali inatualika kutoa maoni yetu kuhusiana na mchakato, au mpango, fulani wa uendeshaji nchi, kama vile utungaji sheria, tuiambie iendelee tu, maana yenyewe ndiyo Serikali na yenyewe tu ndiyo inayojua nchi hii na watu wake wanahitaji nini ili kufikia ‘maendeleo’ inayoyatafuta.

Kwa maneno mengine, tuishauri Serikali isipoteze muda kwenye juhudi zake za ‘kutuletea maendeleo’ kwa kujisumbua kutuuliza mawazo na maoni yetu kuhusiana na mipango yake ya maendeleo. Unalionaje wazo hilo, unadhani litasaidia kuifanya Serikali kuacha kudharau mawazo ya wananchi kwa sababu sasa hakutakuwa tena na mawazo ya wananchi ya kuyadharau? 

Wenzangu kwenye kile kikao chetu walikuwa na mashaka kidogo kuhusu pendekezo langu hili. Niambie, wewe una maoni gani? Nitasubiri kusoma mrejesho wako!

Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *