The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Lini Tutapunguza Kukimbilia Wachezaji wa Kigeni?

Kwa kuwa tumeruhusu wachezaji 12 wa kigeni kusajiliwa, ni muhimu klabu zetu zikapewa jukumu pia la kuhakikisha zinahusika kukuza vipaji vya ndani.

subscribe to our newsletter!

Ni msimu wa usajili wa wachezaji wa mpira wa miguu Tanzania na duniani kwa ujumla, huku baadhi wakinufaika na donge nono linalowekwa katika ada ya kutia saini na mishahara na posho nyingine.

Ni kipindi ambacho kinataliwa na taarifa za wachezaji wa kigeni wanaotakiwa na timu za Tanzania, kama ilivyo sehemu nyingine duniani, huku wale wazawa wakipewa nafasi ndogo sana katika habari hizo.

Ni dhahiri kwamba mchezaji anapokuwa ugenini anajituma zaidi, hasa kutokana na ukweli kwamba asipofanya jitihada hana kingine cha kumuwezesha kutengeneza maisha na atalazimika kurudi nyumbani pale itakapoonekana hana msaada kwa timu kutokana na kutokuwa na jitihada zinazoridhisha.

Ndiyo maana viongozi wa klabu huelekeza sana macho yao kwa wachezaji wa nje kuliko wa ndani, wakiamini kuwa wakiwapata watakuja kujituma kuliko wale wa ndani. Na hilo hujionyesha hata katika maslahi yao. 

Wachezaji wageni hulipwa mshahara wa kuanzia Shilingi milioni 10 hadi Shilingi milioni 40 ambako ndiko tunakoelekea kwa sasa, huku ada ya kutia saini, au sign-on fee kwa kimombo ikiwa ni kuanzia Shilingi milioni 40 hadi hata Shilingi milioni 100 kwa wageni. Na ukichanganya na ada ya uhamisho, unakuta mchezaji anagharimu hadi Shilingi milioni 400 au 500.

SOMA ZAIDI: Hivi Wachezaji Wazawa Hawazidai Klabu Zinazowaacha?

Bila shaka kunahitajika wachumi na wataalamu wa majadiliano katika kuziepusha klabu kuingia kwenye matumizi makubwa ya kiasi hicho, huku matokeo katika mashindano ya kimataifa yakiwa hayalingani na kiasi kinachosemekana kutumika katika kukusanya kikosi.

Klabu kama Bayern Munich huwa haihusishwi sana katika taarifa za kugombea wachezaji wa bei ghali, bali huonekana zaidi katika kuwawekea mikakati wachezaji wanaochipukia na wale ambao wanakaribia kumaliza mikataba yao na hivyo kutotumia fedha nyingi katika kukusanya kikosi chao kila wakati wa usajili.

Sifa 

Pamoja na kwamba haya yote ni ya kawaida katika usajili duniani kote, inaonekana katika nchi yetu kusajili wachezaji wa gharama kubwa, au wachezaji wa kigeni, kuwa ni sifa na ndiyo njia sahihi ya kupata wachezaji wenye ubora, kitu ambacho naamini si sahihi.

Nchi kama Brazili, pamoja na kufanya mageuzi katika umiliki na uendeshaji wa klabu za soka uliozifanya zivutie wawekezaji kutoka nje ya nchi, bado tegemeo lao kubwa ni wachezaji vijana wazawa na si kununua kutoka nje.

Uwekezaji katika klabu za soka nchini Brazil unalenga kuziwezesha kuwa na uwezo wa kujiendesha na kustahimili gharama za kukuza wachezaji hadi kufikia kiwango cha kuwauza kwa bei kubwa. 

SOMA ZAIDI: Tujipe Muda Kabla ya Kuanza Kuitumia V.A.R

Leo hii si rahisi kuvuna kipaji nchini Brazil kwa bei nafuu kama ilivyokuwa awali kabla ya mageuzi yaliyoongozwa na Serikali baada ya miswada ya nyota wa zamani wa nchi hiyo, Zico na Pele.

Na barani Afrika, Misri na nchi nyingine za Kiarabu zimefanikiwa kuwapa thamani wachezaji wazawa, huku kanuni ya kuweka idadi ya wachezaji wa kigeni ikisaidia kulinda vipaji vya ndani. Misri inaruhusu wachezaji watano tu wa kigeni kusajiliwa na klabu moja.

Kanuni hizi hulazimisha klabu kufanya kila jitihada kuhakikisha zinapata wachezaji wazuri wazawa na hivyo kuwa na timu bora ya taifa, huku vipaji vingi katika maeneo ya nchi hiyo vikiwa na uhakika wa kupata ajira nzuri na bora katika Ligi Kuu.


Kwa hiyo, Misri na Brazil haziwezi kutawaliwa na habari za klabu kugombea wachezaji wa kigeni, bali nyota gani wazawa wanatazamiwa kung’ara kwenye klabu zao mpya msimu unaofuata.

Wachezaji watoto

Lakini unaweza kulifanya hilo kama tu utakuwa umeweka mazingira na miundombinu inayoendana na ndoto yako. Kama zilivyo nchi nyingi za kiarabu, programu za kuendeleza wachezaji watoto na vijana zinazingatiwa sana na klabu huwa na uhakika na uwekezaji wao kwenye program hizo katika kipindi cha miaka michache.

SOMA ZAIDI: Simba Inahitaji Kutathmini Safari Yake ya Mabadiliko

Na programu hizo si za maonyesho kama zilivyo hapa kwetu. Yaani kama ni kanuni inalazimisha klabu kuwa na timu ya vijana, basi hilo haliwezi kuwa tatizo wakati itatakapotakiwa kuthibitisha hilo. 

Yaani mashindano kama ya vijana walio na umri chini ya miaka 20 yakifika, klabu itaingiza uwanjani timu yake ya U17. TFF inachotaka ni timu na si imetokea wapi au hao wachezaji walikuwa wapi. Kwa hiyo, ni kitu rahisi kwa klabu.

Na kwa sababu hizo timu ni za maonyesho ni nadra sana viongozi kuelekeza nguvu zao katika wachezaji wahitimu wa program za vijana kwa kuwa wanaotumiwa ni wale wa maonyesho na si wanaokuzwa na taasisi hizo.

Wale wachache waliotokea programu za vijana ni wale waliofikia kiwango cha kuchezea timu za taifa na hivyo kuwa kivutio kwa klabu za Ligi Kuu na Championship. Wale waliokosa nafasi ya kuingia timu za taifa za vijana kutoka timu za maonyesho, ndiyo wanakuwa wanapotea taratibu.

Ni katika misingi hiyo, usajili wa hapa kwetu utaendelea kutawaliwa na taarifa za wachezaji wa kigeni, huku mishahara, posho na ada za kusaini zikiwa hadi mara mbili ya ile ya wageni. Hakuna wazawa wanaozalishwa wenye kiwango cha Luis Miquisson, Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua, Emmanuel Okwi, Kipre Junior au Cloutus Chama.

SOMA ZAIDI: Olimpiki ya Paris Imeshatupita, Tujiandae ya 2028

Na kama wapo wanaokaribia kiwango hicho, wachezaji kama Feisal Salum, Raphael Daudi, Zawadi Mauya, Athuman Idd, Said Demla na wengine, tunakuwa na hofu na uwezo wao na wakati mwingine viongozi kutoa maelekezo ya matumizi ya nyota wazawa.

Wenzetu wa barani Ulaya wameliona hilo na kwa sababu sheria zinatoa uhuru wa ajabu wa sheria za kazi, wao wameamua kuwa na sheria ya matumizi ya kiungwana ya fedha kudhibiti bajeti za klabu katika kununua wachezaji na kuwahudumia.

Lakini sisi bado kufika huko. Kwa kuwa tumeruhusu wachezaji 12 wa kigeni kusajiliwa, ni muhimu klabu zetu zikapewa jukumu pia la kuhakikisha zinahusika kukuza vipaji vya ndani. Na itawezekana kwa kuzilazimisha kuwa na timu za kweli za watoto na vijana na si zile za maonyesho.

Kanuni zetu pia zinatakiwa zizilazimishe klabu kuonyesha asilimia ya bajeti inayotengwa kwa ajili ya soka la watoto na vijana na pia kuwa na makocha sahihi, wenye elimu na stadi sahihi za kufundisha vijana, huku waendeshaji wa mashindano ya vijana wakiwajibika kuweka wasimamizi sahihi wa mashindano hayo na si hali kama ilivyo sasa kwa mashindano ya vijana wa U17.

Hii itabadili mwenendo tulio nao sasa wa kukimbilia wachezaji wa kigeni kila wakati msimu wa usajili unapowadia. Fedha zinazopatikana kutokana na uwekezaji, udhamini, haki za televisheni na mapato ya milangoni, zisitapanywe kwa kununua wachezaji wa kigeni ambao viwango vyao havitofautiani sana na wazawa.

Ni lazima tuhakikishe mchezo wa mpira wa miguu, ambao unaingiza fedha nyingi kuliko michezo mingine Tanzania, unachangia katika kupunguza tatizo la ajira kwa vijana huku uzuri wake ukiendelea.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *