Kampuni ya kutuma na kupokea fedha ya NALA iliyoanzishwa na Mtanzania Benji Fernandes imepata uwekezaji wa dola za kimarekani milioni 40 sawa na Sh. bilioni 100 hii ni baada ya kampuni hiyo kuendelea kufanya vyema katika kuwezesha mzunguko wa fedha Afrika.
Muendelezo huu wa mafanikio ya kampuni hii unakuja ikiwa ni miaka miwili tu toka kampuni hiyo iweze kupokea uwekezaji wa dola milioni 10 (Bilioni 23) mnamo Januari 2022.
Akielezea juu ya mafanikio hayo, Mkurugenzi wa Nala anasema, ‘kazi yao bado haijafikia mwisho’, huku akiorodhesha changamoto mbalimbali watu wanazokutana nazo wakitaka kutuma fedha Afrika, hasa uwepo wa makampuni mbalimbali na mabenki yasiyokuwa na mawasiliano ya pamoja.
Kampuni hiyo kwa sasa imeenda mbali na kuanzisha huduma ya pili ya kurahisisha utumaji fedha barani Afrika, Rafiki. Huduma hii ambayo inaweka miundombinu muhimu katika kurahisisha utumaji fedha lengo lake ni kuzisaidia biashara kama NALA kuweza kuvuka changamoto zinazosababisha utumaji fedha kuwa mtihani mkubwa unaodhorotesha biashara.
NALA ilianza huduma zake za utumaji fedha kimataifa mwaka mwaka 2021 na kupata kibali chake cha kwanza Afrika Mashariki huko nchini Kenya. NALA ilihamishia ofisi zake Nairobi mnamo mwaka 2022, kwa sasa ina wafanyakazi zaidi ya 100, huku ikiwa inafanya kazi katika nchi zaidi ya 17.
Nchini Tanzania, NALA iliweza kupata leseni ya mtoa huduma za kifedha kutoka Benki Kuu mnamo Machi 2023. Kwa sasa NALA inahudumia wateja zaidi ya laki tano, huku mapato yake yakiwa yameongezeka zaidi ya mara kumi ndani ya mwaka mmoja.
Fedha nyingi zinazotumwa katika App ya NALA zinatoka nchini Marekani na Uingereza. Mwanzilishi wa kampuni hiyo anaeleza kuwa malengo yao makubwa kwa sasa ni kujenga mfumo wa utumaji fedha kwa ajili ya watu bilioni 1 wa Afrika.