The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Bodi ya Ligi Kuu Iongoze Uboreshaji Kanuni za Ligi

Ni muhimu sana kwa mamlaka kuongoza mabadiliko yoyote ya kanuni yanayolenga kuboresha ligi nzima.

subscribe to our newsletter!

Katika kipindi cha redio moja ya masafa mafupi nilisikia mahojiano na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu ya soka (TPLB), Almasi Kasongo, kuhusu maboresho ya kanuni kuelekea msimu mpya.

Kasongo alizungumza kiungwana sana kuhusu washiriki wa vikao maalumu vitakavyojadili mapendekezo hayo na mwisho kupelekwa mbele ya Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka (TFF) kwa ajili ya kuidhinishwa.

Kwa bahati mbaya sana sikusikia Kasongo akidokeza kuhusu mapendekezo ya mabadiliko hayo na alikuwa akizungumza kana kwamba mapendekezo yatatokana na washiriki wa vikao vya wenyeviti wa klabu za Ligi ya Championship na Ligi Kuu.

Kwa maana nyingine ni kwamba hakukuwepo na mchakato wa kuangalia mapungufu yaliyojitokeza katika msimu wa 2023/24 ambayo yalihitaji kujadiliwa kwa kina na wadau kabla ya kuibuka na uamuzi ambao ungejenga kanuni madhubuti za msimu tunaoelekea kuuanza.

Au, kama ungekuwepo, TPLB ingetangaza mapendekezo ya maboresho ya kanuni na kuyaweka hadharani ili hao viongozi wa klabu za Championship na Ligi Kuu wanaoenda kujadili mabadiliko wa kanuni, wawe na uelewa mpana wa kinachopendekezwa kabla ya kukipitisha katika ngazi yao na kusubiri uamuzi wa mwisho wa Kamati ya Utendaji ya TFF.

Udhaifu mkubwa

Huu ndiyo udhaifu mkubwa tulionao katika kufanya maamuzi ya mambo yanayohusu watu wengi au wadau tofauti wa mpira wa miguu.

SOMA ZAIDI: Yusuf Manji Alimuachia Somo Zuri Mohammed Dewji

Ungetegemea kwamba chombo maalum ndani ya TPLB kifuatilie mwenendo mzima wa Ligi Kuu na Championship kwa ajili ya kurekodi matatizo na mafanikio na mwishoni kije na mapendekezo ya nini kifanyike kuboresha kanuni za ligi, lakini inaonekana wazi kuwa kinachoenda kufanyika ni kusikiliza wadau na kufanya uamuzi bila ya kuwepo na utafiti wa kutosha kuhusu kile kinachoamuliwa.

Hii si sahihi. Pamoja na ukweli kwamba ushirikishwaji wa wadau ni muhimu, bado wasimamizi wa mashindano hayo wanatakiwa kuongoza mchakato wa maboresho ya kanuni. 

Yaani chombo maalumu kinachofuatilia mwenendo wa mashindano hayo mawili, kichunguze na kuona umuhimu wa kufanya mabadiliko, au kuboresha kanuni na kufanyia uchunguzi mapendekezo hayo kabla ya kuyawakilisha kwa wadau kwa ajili ya maamuzi.

Yaani kama tatizo ni wachezaji kutohudhuria tamasha la wanamichezo bora wa msimu wa soka, hiki chombo kiangalie ni sababu zipi zinawafanya wachezaji wasione umuhimu wa tuzo hizo binafsi na kutohudhuria na baadaye kuja na mapendekezo ya nini kifanyike ili wadau hao wakubwa waone umuhimu na kuhudhuria kwa wingi.

Lakini kutokana na kutokuwa na chombo hicho, viongozi wa soka, kwa fikra zao, wanadhani tamasha hilo ni kubwa na asiyehudhuria ni mkosefu ambaye anastahili adhabu. 

SOMA ZAIDI: Lini Tutapunguza Kukimbilia Wachezaji wa Kigeni?

Matokeo yake wanapitisha kanuni ya kumzuia mchezaji ambaye hatahudhuria sherehe hizo, kutocheza mechi kadhaa za msimu unaofuata eti kwa sababu hakuhudhuria “sherehe.”

Hakuna umakini

Haya ni mambo yanayoonyesha wazi kuwa hakuna umakini katika kuboresha kanuni zetu na badala yake mambo yanafanywa kiholela kutokana na jinsi wadau au vyombo vya habari vilivyoripoti mapungufu ya msimu uliopita na kutaka kufanya maamuzi ya kuridhisha waliolalamika.

Ni muhimu sana kwa mamlaka kuongoza mabadiliko yoyote ya kanuni yanayolenga kuboresha ligi nzima. Huwezi kutegemea kikao cha siku moja cha wenyeviti wa klabu za Championship au Ligi Kuu kujadili kwa kina mapendekezo tofauti ya viongozi 16 au 20 ya nini kifanyike kuboresha ligi, bila ya kuwa na mwongozo wa mapendekezo ambayo yameshafanyiwa utafiti kuhusu uzuri na ubaya wake.

Huwezi kuamua kumfungia mchezaji kucheza mechi, labda tatu au nne za msimu unaofuata, eti kwa sababu hakuhudhuria sherehe za wanamichezo bora wa msimu uliopita. 

Pendekezo kama hilo likiwasilishwa mbele ya kikao cha wenyeviti wa klabu za Ligi Kuu ni lazima litapingwa kwa nguvu zote kwa kuwa hakuna uhusiano wowote kati ya kucheza mechi za klabu yake na kutohudhuria sherehe zinazohusu mambo binafsi ya mchezaji.

SOMA ZAIDI: Hivi Wachezaji Wazawa Hawazidai Klabu Zinazowaacha?

Klabu zimelipa fedha nyingi kwa ajili ya mchezaji, ikiwa ni pamoja na bonasi ya kusajili, bonasi ya mechi, mshahara na marupurupu mengine, halafu mchezaji huyohuyo asicheze mechi tatu za msimu unaofuata eti kwa sababu hakuhudhuria sherehe, ni kituko!

Kwa hiyo, ni muhimu TPLB ikajipanga na kuunda chombo kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa ligi zake na kurekodi matukio ambayo yalifurahisha au yalikera ligi na baadaye kuyadili kwa kina baada ya uchunguzi kabla ya kuyawasilisha kwa wadau kwa ajili ya maamuzi.

Ilivyo kwengineko

Hivi ndivyo inavyofanyika kwa taasisi zote duniani zinazohusisha wadau. Hata unapoenda kwenye mkutano mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) unaojadili mabadiliko ya ibara fulani, ni lazima shirikisho hilo liwe limetuma mapendekezo ya mabadiliko ya ibara husika na kueleza sababu za mabadiliko hayo na hivyo wajume wanapoenda kwenye mkutano huo wanakuwa wana ufahamu mpana wa nini kinachotakiwa.

Huku ndiko kuongoza mabadiliko na si kushirikisha wadau kwa lengo la kuidhinisha tu kile kinachokusudiwa. Naelewa kuwa huenda TPLB inajua inataka nini katika kuboresha kanuni za ligi, lakini kutokana na ukweli kwamba wadau na jamii kwa ujumla haijui uboreshaji utahusu maeneo gani, ni dhahiri kuwa bado tunaendesha mambo kizamani.

Hadi kufikia leo tulitakiwa tujue mabadiliko ambayo yanatarajiwa kufanyika, sababu za mabadiliko hayo na maoni ya wadau kuhusu mapendekezo ya mabadiliko hayo. Hayo yangeibua mjadala ambao ungekuwa ni afya kwa soka la Tanzania. 

SOMA ZAIDI: Tujipe Muda Kabla ya Kuanza Kuitumia V.A.R

La sivyo, kufanya mambo kienyeji namna hiyo ndiyo kunazua kanuni mbovu kama za kuwaadhibu wachezaji wasiohudhuria sherehe bila ya kujua kunaathiri timu zao.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *