Mahakama ya Rufaa ya Tanzania mkoani Arusha, chini ya Majaji watatu Omar Othman Makungu, Stella Mugasha na Dkt. Mary Levira imemuchia huru mwanaume mmoja aliyetambulika kwa jina la Abubakar Shaban, baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa la ulawiti.
Shabani alihukumiwa kifungo hicho na Mahakama ya hakimu mkazi Arusha baada ya kujiridhisha kuwa, tarehe 24 Januari, 2018 katika eneo la Sanawari, Mkoani Arusha, alimwingilia kinyume na maumbile mvulana wa miaka 2 na nusu (jina limehifadhiwa kulinda utambulisho). Kwa wakati huo wa hukumu Shaban alikua na umri wa miaka kumi na nane
Upande wa mashtaka uliita jumla ya mashahidi watano ili kuthibitisha madai yao ambapo Flora Richard ambaye ni bibi wa mwathirika, alitoa ushahidi kwamba alimfahamu Shabani na mtoto aliyelawitiwa.
Bibi huyu aliieleza Mahakama kuwa mwathirika ni mjukuu wake mwenye umri wa miaka 2 na nusu na Shabani alikuwa mfanyakazi wa nyumbani aliyemsaidia kuchunga ng’ombe na walikaa naye pamoja Sanawari.
Tarehe 24 Januari, 2018 alipokuwa akirudi kutoka shambani, aliambiwa na mjukuu wake kuwa Shabani alimlaza chini na kumvua nguo kisha akamwingilia. Bibi huyu alipata wasiwasi na hivyo alimkagua mjukuu wake na kukuta akiwa na michubuko, damu pamoja na manii kwenye makalio yake.
Bibi anaeleza kuwa alipomuuliza Shabani kuhusu tukio, alikiri kutenda tukio hilo na ndipo alimwita mwenyekiti wa kitongoji anayetambulika kwa jina Alfred Loderiek ambaye pia aliieleza Mahakama kuwa baada ya kumhoji Shabani, alikiri kufanya kitendo hicho kufuatia maagizo aliyopatiwa na mganga wa kienyeji. Pamoja na mashahidi watano, upande wa mashtaka uliwasilisha nyaraka mbili ambazo ni Ripoti ya Uchunguzi wa Kitibabu na maelezo ya mtuhumiwa.
Shaban, alifikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Arusha (Mahakama ya mwanzo) akikabiliwa na shtaka moja la kulawiti. Kesi hii iliahirishwa mara kadhaa baada ya mtuhumiwa kutoongea chochote kila walipojaribu kumuuliza, hata hivyo ilibidi kesi kuendelea hivyo hivyo.
Baada ya kesi kusikilizwa kikamilifu, Mahakama hiyo Hakimu Mkazi wa Arusha ilimkuta na hatia na kumhukumu kifungo cha maisha. Kwa kutoridhika na uamuzi wa Mahakama hiyo, alikata rufaa bila mafanikio Mahakama Kuu ambapo rufaa yake ilihamishiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Arusha na kusikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi mwenye Mamlaka Maalum na rufaa yake haikukubaliwa.
Kwa kutoridhiswa na mwenendo wa kesi hiyo, Shabani alikata tena rufaa katika Mahakama ya rufaa ya Tanzania na tarehe 3 na 8 Julai 2024 ndipo kesi yake iliposikilizwa. Mahakama ya rufaa ya Tanzania kanda ya Arusha ilipitia ushahidi wote uliowasilishwa Mahakamani hapo na kufuatilia mwenendo wa kesi nzima ilivyokuwa kuwa awali na kubaini kuwa kuwa kuna makosa yaliyofanyika wakati wa uwasilishaji wa ushahidi na hivyo kutoka na makosa hayo inamwachia huru Shabani aliyekuwa anatumikia kifungo cha maisha jela.
Mahakama ya Rufaa iligundua kuwa kulikuwa na utata katika ushahidi wa upande wa mashtaka na utata huo ni kuhusu tarehe ya uchunguzi wa kimatibabu, kwani ulileta shaka kuhusu uthibitisho wa kisayansi wa kuingiliwa kimwili.
Utata huu unachukuliwa kuwa si mdogo kwa sababu unaathiri moja kwa moja vipengele vya msingi vya kesi ambavyo upande wa mashtaka ulipaswa kuthibitisha: kwamba kulikuwa na kuingiliwa kimwili na kwamba mshtakiwa, Abubakari Shabani, ndiye aliyefanya kosa hilo.
Mashahidi watatu wa upande wa mashtaka walitoa ushahidi kwamba mwathirika alipelekwa hospitalini kwa uchunguzi wa kimatibabu tarehe 24 Januari, 2018, huku ripoti ya kimatibabu (PF3) na ushahidi wa daktari aliyefanya uchunguzi, unaonyesha kwamba uchunguzi huo ulifanyika tarehe 2 Februari, 2018.
Mahakama ilieleza kuwa tofauti hii ya tarehe ni tatizo kwa sababu inatia shaka juu ya ushahidi uliowasilishwa. Ikiwa uchunguzi ulifanyika wiki moja baada ya tukio lililodaiwa, inaweza kuathiri usahihi wa matokeo ya kimatibabu na hitimisho lililofuata kuhusu asili ya majeraha ya mwathirika.
Zaidi ya hayo, ni kwamba ripoti ya kitabibu (PF3) ina tarehe mbili tofauti, jambo ambalo linaongeza mkanganyiko. PF3 inaonyesha kwamba ombi la uchunguzi wa kimatibabu lilifanywa tarehe 24 Januari, 2018, lakini uchunguzi wenyewe ulifanyika tarehe 2 Februari, 2018.
Jambo lingine Mahakama ilionesha kutilia mashaka suala la mtuhumiwa kufikishwa Mahakamani miezi sita toka siku iliyotajwa kuwa ni ya tukio yaani Januari 24,2018, ambapo mtuhumiwa alifikishwa Mahakamani Julai 2,2018. Mahakama ilionesha kushangazwa zaidi na hati ya hukumu kuandaliwa kabla ya mtuhumiwa kufikishwa Mahakamani, ambapo iliandaliwa Juni 29,2018.
Kutofautiana huku siyo tu kunatilia shaka uthibitisho wa kisayansi wa kuingiliwa kimwili bali pia kunatia mashaka juu ya utambulisho wa mwathirika na uaminifu wa mchakato wa kukusanya ushahidi. Mahakama ya Rufaa iliona utata huu kuwa wa msingi, ikikubaliana na malalamiko ya mkata rufaa na kuhitimisha kuwa uliathiri kesi ya upande wa mashtaka.
Jambo lingine muhimu lilikuwa ni kushindwa kwa upande wa mashtaka kumuita mwathirika(mtoto aliyelawitiwa) kutoa ushahidi Mahakamani. Ushahidi wa mwathirika unachukuliwa kuwa ushahidi bora katika kesi za makosa ya kingono, na bila huo, Mahakama iliona ni vigumu kuthibitisha bila shaka iwapo mtuhumiwa ndiye aliyefanya uhalifu huo kwani aliyefanyiwa uhalifu alitakiwa kumtambua na kuithibitishia Mahakama hiyo kuwa yule ndiye aliyehusika.
Aidha Mahakama ya Rufaa ilikubaliana kwamba adhabu ya kifungo cha maisha ilikuwa kinyume na sheria chini ya Kifungu cha 160B cha Kanuni ya Adhabu. Kifungu hiki kinawalinda watoto walio chini ya umri wa miaka 18 dhidi ya adhabu kali, na kwa kuwa mkata rufaa alikuwa na umri wa miaka 18 wakati wa kosa, adhabu hiyo ilionekana kuwa kinyume cha sheria.
Kufutia hoja hizo, Mahakama ya Rufaa ilikubali rufaa, ikafuta hukumu, na kuamuru kuachiwa huru kwa mkata rufaa mara moja isipokuwa kama anashikiliwa kihalali kwa sababu nyingine. Hukumu ilitolewa tarehe 8 Julai, 2024.
2 responses
Story hii ina mkanganyiko sana. Kwanza ilitakiwa ieleze mwanzoni kabisa kwa nini mahakama ilimwachia huru mtuhumiwa, na siyo kumlazimisha msomaji apitie story yote ndio aelewe sababu.
Pili inatuambia licha ya mtuhumiwa kukiri kosa mwenyewe na kukataa kusema chochote akiwa kizimbani, aliendelea kukata rufaa BAADA ya kuhukumiwa. Huo ni utata mkubwa ambao ni jukumu la mwandishi kuutolea ufafanuzi kwa faida ya wasomaji.
maelezo haya yananikumbusha tamthilia ya “When They See Us” ya 2019 ambayo ilizungumzia kisa cha vijana wanne (4) walio chini ya miaka 18 kubambikwa kesi ya ubakaji kupitia ushahidi wa kulazimishwa (forced admittance and plea of being guilty).
Ushahidi kama ungekuwa wa kweli nadhani vyombo vya upelelezi vingeashughulikia kesi mapema.