The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kwa Nini Baba Anapaswa Kumsindikiza Mama Kliniki Kipindi cha Ujauzito?

Yapo mambo mazuri muhimu ambayo akina baba wakiyajua ni faida sana kwao, lakini hasa kwa watoto wao.

subscribe to our newsletter!

Tunaamini kwamba baba wengi sasa wanajua umuhimu wa kuwasindikiza wazazi wenza, yaani akina mama, kliniki wakati wa ujauzito na hata baada ya kujifungua, lakini bado wapo wengi wenye dhana kuwa kupima afya zao wenyewe ndiyo lengo pekee la kwenda kliniki.

Wengi walio na dhana hii pia huwategemea akina mama kupima afya wenyewe na baada ya matokeo mazuri hujiaminisha kuwa wao ni salama pia. Hii dhana ni potofu kwani yanayofanyika kliniki za uzazi ni zaidi ya upimaji wa afya. 

Yapo mambo mazuri muhimu ambayo akina baba wakiyajua ni faida sana kwao, lakini hasa kwa watoto wao. Hivyo, ni muhimu sana kwa mama kuhudhuria kliniki mara tu anapogundua kuwa ni mjamzito na kuhakikisha anaambatana na mwenza wake. Leo tujifunze baadhi ya manufaa ya baba kumsindikiza mama kliniki.

Moja, kujua afya ya mama na baba ili kumlinda mtoto mtarajiwa. Wakati wa kiliniki, wajawazito na wenza wao hushauriwa kupitia vipimo mbalimbali kujua hali za afya zao ambapo itasaidia pia kumlinda mtoto mtarajiwa ikiwa itagundulika mmoja ya wazazi, au wote, wanaugua magonjwa mbalimbali, ikiwemo kuishi na virusi vya UKIMWI.

Pili, kwenda pamoja kliniki humfanya mama kuwa na furaha na kufurahia ujauzito alionao, kwamba mwenzi wake anamjali na kumthamini na hivyo kuona thamani ya kiumbe alichokibeba. Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa mama hujisikia furaha mno akigundua kuwa mume wake anampenda na kumjali hasa kipindi cha ujauzito.

SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwafanya Watoto Wetu Wapende Kunywa Maji?

Husaidia baba kuongeza uelewa wa majukumu yaliyoko mbele yake, ikiwemo lishe bora kwa mama ili mtoto tumboni akue vizuri. Kliniki za uzazi, pamoja na mambo mengine, hutolewa ushauri wa lishe bora kwa mama, hivyo baba anapokwenda na mama kliniki atapata kujua ni aina gani ya vyakula adhimu kwa mama wakati na baada ya kujifungua. Hii humsaidia kumkumbusha na kumsisitiza iwapo atajisahau.

Humsaidia baba kuelewa mabadiliko ya kimaumbile na mara nyingine tabia kwa mama. Akijua vyema, atapata fursa nzuri kuishi naye kwa upendo na uvumilivu hasa katika kipindi cha ujauzito. 

Wakati wa ujauzito, mama anaweza kubadilika kitabia akawa na hasira, au kumchukia yeyote bila sababu. Baba atapata fursa ya kusikia uzoefu wa akina baba wenzake awapo kliniki na kujipanga kuishi na kutoa huduma kwa mwenza wake. Huna haja ya kukimbia nyumbani wakati wa ujauzito wa mama kwa kuogopa malumbano. Jifunze kutoka kliniki.

Hujenga mahusiano mazuri kati ya baba na mtoto atakayezaliwa. Tafiti zinaonyesha kwamba mtoto hushiriki furaha aliyonayo mama. Mama mwenye furaha, mtoto mwenye furaha. 

Haiwezekani usimpende akiwa tumboni eti unasubiri azaliwe ndiyo uanze mahusiano naye. Siku njema huonekana asubuhi. Mtoto awapo tumboni anapata hisia zake kutoka kwa mama yake. 

SOMA ZAIDI: Jinsi ya Kuwasaidia Watoto Kuepuka Vishawishi vya Makundi-Rika

Uwepo wako karibu na mama mjamzito, ni sawasawa na kuwa karibu na kijacho wenu. Umbali wako na kijacho wenu utahitaji nguvu ya ziada ya kujenga mahusiano pindi akizaliwa. 

Anza mapema!


Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *