Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekanusha habari zilizokuwa zinasambazwa na wazandiki na wapotoshaji waliokuwa wakishauri na kuhamasisha mashabiki wa mchezo huo kupiga kura kwa wingi kwa ajili ya kuwawezesha wachezaji wateule kushinda tuzo za msimu uliopita.
Tuzo hizo zinaonekana kuwa na ushindani mkubwa, hasa kwa wachezaji wa klabu za Simba, Yanga na Azam, ambazo zinatawala soka la Tanzania kwa sasa, huku vigogo wa Kariakoo wakiwa na mtaji mkubwa wa mashabiki.
Katika taarifa yake ya kukanusha, TFF imewataka mashabiki kupuuzia habari hizo za wazandiki na kusubiri siku ya tamasha la kutuza wanasoka bora wa msimu uliopita ili kujua washindi.
TFF imeeleza kuwa hakutakuwa na kupigia kura wachezaji au washindani wowote wateule waliotajwa kuwania tuzo hizo, ikisema kuwa kitakachofanyika ni shirikisho hilo kutumia vigezo vyake kupata washindi.
Ni kweli kila tuzo zina mfumo wake wa kupata washindi, lakini huu wa kutumia vigezo kutafuta mshindi mmoja kati ya watatu au watano waliotajwa ni kusumbua watu bila ya sababu. Na pengine ndiyo maana wachezaji huwa hawaoni umuhimu wa kushiriki na hivyo tuzo zao kuchukuliwa na watu wengine kwa niaba yao.
Washindi wameshapatikana?
Kwa nini ni kusumbua watu? Kutumia vigezo kupata mshindi mmoja ni sawa na kusema kuwa tayari washindi wameshapatikana na mshindi hawezi kuwa na mpinzani kwa kuwa amewazidi wenzake walioteuliwa kuwania tuzo kwa kuwa na sifa nyingi zinazokidhi vigezo.
SOMA ZAIDI: Bodi ya Ligi Kuu Iongoze Uboreshaji Kanuni za Ligi
Sasa kama ni hivyo, kwa nini uweke wachezaji watatu kuwania tuzo, au timu tatu kuwania tuzo wakati takwimu zako zimeshakuonyesha nani ni mshindi? Na katika dunia ya leo ya maendeleo ya teknolojia, ni wazi kwamba hata hao mashabiki wameshawajua washindi katika kila kigezo na wanachosubiri ni kuona wakizawadiwa.
Utawezaje kuzuia mfungaji bora kujulikana? Au kipa bora kujulikana? Au kiungo bora kujulikana? Labda watamung’unya maneno katika tuzo ya mchezaji bora, lakini zikitumika zile takwimu za muda aliocheza, nidhamu na mchango wake kwa timu, ni dhahiri kuwa washindi watajulikana mapema na hawatakuwa kitu cha kushangaza, kama ambavyo tuzo nyingine duniani huibua sintofahamu hadi siku ya kuzigawa.
Ni kweli kwamba mfumo huo ulikuwepo, lakini haustahili kuendelea kuwepo kwa kuwa dunia imebadilika na uwazi na utandawazi ni mkubwa kiasi kwamba hakuna jambo linaloweza kushangaza watu siku ya kugawa tuzo kama takwimu zitatumika kwa sababu ziko bayana.
Orodha ndefu
Kwa kawaida muandaaji wa tuzo huanza na orodha ndefu ya wachezaji wanaoweza kutwaa tuzo. Kadiri siku ya kugawa tuzo inavyokaribia, ndivyo orodha huzidi kupungua hadi siku chache kabla ya tuzo wanapobakia wateule watatu katika kila sehemu.
Ni zile tuzo maalumu tu ndiyo huwa hakuna wateule wanaoshindana, bali waandaaji humtafuta mtu au taasisi isiyo na shaka katika ushiriki wake au mchango wake kwenye mchezo husika na hi huwa ni heshima ya aina yake.
SOMA ZAIDI: Yusuf Manji Alimuachia Somo Zuri Mohammed Dewji
Lakini orodha hupungua ili kubakiza wale watatu ambao yeyote anaweza kuitwaa hata kama mmoja wao ana takwimu nzuri. Na ndiyo maana kwenye tuzo zote, kuingia tatu bora ni ushindi kwa kuwa unakuwa unastahili tuzo na kinachosubiriwa ni bahati pekee.
Hapa ndipo, waandaaji hutafuta namna ya kupata mshindi kwa kushirikisha makundi maalum. Kwa wenzetu wa Grammy, tuzo kubwa za muziki duniani, au Oscar, tuzo kubwa za sinema, huwa na taasisi maalum ya wataalamu, maarufu kama academy, ambayo inakuwa na watu kuanzia 60 kwenda juu.
Hapa ni pamoja na watayarishaji wa filamu au muziki, waandaaji, waongozaji, waongoza kamera, watunzi na wajuzi wengine wengi. Hawa ndio hupiga kura kuamua mshindi.
Kwa zile za Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), wapigaji kura na pamoja na makocha wa timu za taifa za nchi na manahodha wao, waandishi wateule na wengine.
Shirikishi
Hii ni kuhakikisha kuwa tuzo zinakuwa shirikishi na zinazotengeneza hamu ya kujua washindi, huku mijadala inayoibuka baada ya wateule kutangazwa, ikiendelea kuzitangaza na kuvutia kampuni kujihusisha na tuzo hizo badala ya kuibua mijadala ya kuziponda.
SOMA ZAIDI: Lini Tutapunguza Kukimbilia Wachezaji wa Kigeni?
Nilikuwa namsikiliza mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA) akitumia nguvu nyingi kufafanua sababu za jopo la majaji wa tuzo zilizopita kuwapa tuzo baadhi ya wateule ambao walipondwa na mashabiki, waandishi na wachambuzi.
Alihangaika kueleza mwanamichezo fulani alikuwa na mafanikio zaidi kwenye mashindano ya kimataifa kuliko aliyezungumziwa zaidi. Sikuwahi kuona waandaaji tuzo wakitoa taarifa za kutetea washindi, hadi siku hiyo. Kwa nini? Kwa sababu TASWA ilidhani takwimu ndiyo zinatoa mshindi.
Takwimu pekee hazitoshi kumpa tuzo mshindi bali mambo mengine mengi, ikiwa ni pamoja na jinsi alivyoweza kuwa na athari, au impact kwa kimombo, kwenye mchezo husika, kiasi cha kuwa kama taswira ya mchezo husika.
Pia, kutumia watu wasiozidi 20 kupata mshindi kunaweza kuibua huruma au ile tabia yetu ya kuweka uwiano kwa pande zote, wakati huenda mchezaji mmoja alistahili zaidi ya tuzo tatu.
Teknolojia huingia hapo ili kuwapa wapigaji kura njia rahisi ya kumchagua mshindi, lakini kura hizo huhifadhiwa huwa ni siri hadi siku ya mwisho. Na baada ya washindi kutangazwa, taarifa za jinsi makocha na manahodha walivyopiga kura huwekwa bayana kuondoa zile hisia kuwa kulikuwa na upendeleo.
SOMA ZAIDI: Hivi Wachezaji Wazawa Hawazidai Klabu Zinazowaacha?
Ndiyo maana katika hatua hii taasisi za ukaguzi kama KPMG zilizojijengea heshima duniani, hupewa jukumu hilo la kusimamia hatua ya mwisho, kiasi kwamba hata rais au katibu wa TFF hawezi kujua washindi hadi siku ya mwisho kwa kuwa bahasha huletwa ukumbini na si kutoka ofisi za TFF.
Hapo hata rais wa TFF akisema kwa utani anaomba kujua mshindi hata mmoja, weledi wake utawekwa kwenye mizani na baadaye kuwa kashfa.
Ni muhimu TFF ibadili mfumo wake wa kupata washindi wa tuzo na iendane na dunia ya sasa. Inawezekana kabisa kura zikapigwa ndani ya wiki na dirisha kufungwa ili kwenda na wakati, teknolojia inaruhusu.
Tuzo za kufikia muafaka na kuweka uwiano hazina nafasi katika dunia hii. Tuzo ambazo si shirikishi, hazina nafasi leo. Tuzo ambazo haziibui tashwishi au hamu ya kujua mshindi na hatimaye mshangao, hazina nafasi tena.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.