The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Fanya Hivi Kujenga Mahusiano Bora na Mfanyakazi wa Nyumbani

Kujenga mahusiano mazuri na mfanyakazi wa nyumbani kuna faida kubwa kwani kufanya hivyo ni kumuongezea ufanisi katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku.

subscribe to our newsletter!

Tunakubaliana kuwa wafanyakazi wa nyumbani ni mhimili mkubwa majumbani, hasa kwa wengi wetu tulioajiriwa kwenye sekta ama za umma au binafsi – hata wale walojiajiri. 

Ipo wazi kwamba tunatambua umuhimu wa wasaidizi hawa katika kutekeleza majukumu ya nyumbani pindi tunapoondoka kwenda kazini, na hata tuwapo majumbani. Tatizo lipo kwenye mahusiano yetu na hawa wasaidizi wetu majumbani.

Uzoefu unaonyesha kuwa wafanyakazi wa nyumbani hawadumu katika ajira zao. Leo yupo, kesho hataki tena kazi, anataka kurudi kwao. Wengine hawatulii ndani ya nyumba, kutwa kuzuruRa mtaa hadi mtaa, huku kazi na huduma kwa watoto zikilegalega. 

Vitendo vya namna hii huwaweka waajiri wao katika hali ya taharuki, wakiwa hawana uhakika wa huduma zinazotolewa na wafanyakazi wa namna hii.

Kama waajiri, ni muhimu sana kutambua kuwa wafanyakazi wa nyumbani hutofautiana, kila mtu huvaa uhusika tofauti na sifa ambazo huathiri utendaji wao wa kazi. Kujenga mahusiano mazuri na mfanyakazi wa nyumbani kuna faida kubwa kwani kufanya hivyo ni kumuongezea ufanisi katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Baba Anapaswa Kumsindikiza Mama Kliniki Kipindi cha Ujauzito?

Tafiti zinaonyesha kwamba kukosekana kwa mahusiano mazuri kati ya mwajiri na mfanyakazi ni chanzo cha wasiwasi na migogoro inayojitokeza makazini mwetu. Vivyo hivyo, hata majumbani mwetu, sisi kama waajiri tunahitaji kuhuisha mahusiano ili mazingira ya kazi yawe rafiki.

Mlipe mshahara mzuri. Mshahara mzuri ni kichocheo katika kufanya kazi kwa bidii na weledi. Hatuna budi kutambua kwamba wafanyakazi wa nyumbani hutegemea mishahara tunayowalipa kwa ajiri ya kujikimu. 

Aidha, hutumia pesa hizo kwa kusaidia familia zao, kwani wengi wao hutokea kwenye familia duni na zisizojiweza. Tatizo linakuja pale tunapowapangia kazi lukuki, huku tukiwalipa mishahara isiyolingana na majukumu wanayoyatekeleza. Hapa ndipo mgongano unapoibukia.

Lugha ya staha na busara itumike wakati wa kuzungumza na mfanyakazi wako wa nyumbani na hasa wakati wa kutoa maagizo. Ugomvi na kumkaripia siyo njia bora za kutumia wakati wa kuwasiliana nae kwani kutaleta uhasama kadiri siku zinavyozidi kwenda. 

Hakikisha unampa maelekezo sahihi ambayo hayataweza kumchanganya, na endapo kama utakugundua kuwa anafanya kosa kwenye jambo fulani, basi msahihishe katika njia ambazo hazitaonyesha kumdharau.

SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwafanya Watoto Wetu Wapende Kunywa Maji?

Usimbague. Onyesha unauthamini mchango wake kwa kumfanya sehemu ya familia, hasa unapopata wasaa wa kununua vijizawadi nyumbani usimsahau walau mara moja moja. 

Upo ushahidi wa kutosha wazazi tunawanunulia watoto wetu nguo nzuri ilihali mfanyakazi wa nyumbani unamletea nguo kuukuu. Kwa nini umbague? Mfanye ajue kuwa unamthamini kwani itasaidia katika kujenga uhusiano bora baina yake na hata kwa watoto wako pia.

Mheshimu. Hakikisha mfanyakazi wa nyumbani haonewi pasi sababu. Watoto, ndugu na jamaa zako wampe heshima inayostahili. Asitukanwe na mtoto wako na ukakaa kimya. 

Asinyanyaswe na wageni wako na ukaa kimya. Huyu anakaa na watoto wako ukiwa haupo, hivyo ni vyema umpe heshima. Atakulipa heshima. Mlipe dharau na madhara yake yataonekana!

Haya ni baadhi tu ya mambo unayoweza kufanya kujenga mahusiano na mfanyakazi wako wa nyumbani. Hatusemi ukimpa haya basi uhakika wa kuhusiana naye vyema upo asilimia 100. 

Bado unaweza ukampa kila atakacho, pamoja na heshima, na ukorofi atakuonyesha. Hili, hata hivyo, lisikuvunje moyo wa utu wema!

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts