Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana amejiuzulu nafasi yake leo Julai 29,2024.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makalla, Mwenyekiti wa Chama hicho Samia Suluhu ameridhia ombi la Kinana kujiuzulu nafasi yake.
Kinana alichaguliwa katika nafasi hiyo mnamo April 01,2022, baada ya wajumbe wa mkutano mkuu maalum wa CCM kumchagua kwa kura za ndiyo 1875.
Akiijibu barua hiyo ya kuomba kujiuzulu, Rais Samia Suluhu ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM amesema amekubali ombi hilo kwa moyo mzito.
“Ni kweli nilipokuomba utusaidie kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti nilikuahidi utakaa muda mfupi kama ulivyoomba, na kwa kweli nilipenda uendelee kutusaidia lakini kwa kuwa umeomba sana na ahadi ni deni nalazimika kwa moyo mzito kuridhia kujiuzulu kwako, inaeleza sehemu ya taarifa hiyo ikiwa ni nukuu ya jibu la Rais Samia.
Moja ya mambo ambayo Kinana aliyaongoza katika nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti ni maridhiano kati ya CCM na CHADEMA, maridhiano yalifanikiwa kuwa na mafanikio ya wastani, huku yakiishia kwa kutupiana maneno kati ya CCM na CHADEMA huku kila mmoja akionesha kuwa upande wa pili ndio kikwazo.