Shirika la Reli Tanzania limeomba radhi kwa treni yake iliyokuwa ikisafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma kusimama kwa muda wa saa mbili kati ya stesheni ya Kilosa na Kidete mkoani Morogoro, hapo jana Julai 30,2024. Taarifa za treni kukwama zilianza kusaambaa katika mitandao ya kijamii jana usiku.
“Taarifa za awali zinaonesha kuwa hitilafu za aina hiyo husababishwa na wanyama (ngedere) au ndege (bundi) wanapogusa nyaya za umeme zilizotandazwa juu ya reli (overhead catenary system). Hitilafu ilisababisha kukatika kituo cha kupoozea umeme namba 7 (Godegode) ambayo kitaalamu hujulikana kama (instateneous Overcurrent Protection Trip) majira ya saa 4:20 usiku,” inaeleza taarifa hiyo Iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Jamila Mbarouk leo Julai 31,2024.
TRC inaeleza kuwa mafundi wake walifanikiwa kurejesha umeme majira ya 6:30 usiku na safari hiyo kuelekea Dodoma iliendelea na kuwasili majira ya 7:57 usiku.
Treni katika reli ya SGR ilianza safari za Dar es Salaam-Morogoro mnamo June 14,2024 ambapo zaidi ya abiria 600 walisafirishwa, na safari nyingine ya Dar es Salaam mpaka Dodoma ilizinduliwa mnamo Julai 25,2024 ambapo zaidi ya abiria 1000 walipanda treni hiyo.
Rais Samia anatarajiwa kusafiri kwa treni katika reli ya SGR kesho Agosti 01,2024 kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma.