The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

‘Maendeleo ya Watu’ Lazima Yahusishe Ulipaji Fidia wa Haraka Kwa Watanzania

Maendeleo yataacha kuwa ya watu kama upatikanaji wake utawaacha wengine bila makazi au ardhi za kilimo, huku fidia zao zikicheleweshwa.

subscribe to our newsletter!

Kikawaida, inaweza kuwa ngumu kuona tatizo kwenye utekelezwaji wa miradi mbalimbali inayoitwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa miundombinu kama vile ya barabara, reli, maji, na kadhalika. Unawezaje kupinga mradi ambao hakuna shaka yoyote kwamba faida zake kwa wananchi ziko wazi kabisa? Inakuwa siyo rahisi hata kidogo.

Lakini ukweli mchungu ni kwamba yapo mazingira ambapo miradi hii huweza kutekelezwa bila ya wabunifu na watekelezaji wao kusukumwa na dhima ya kuwakomboa wananchi, na hivyo faida yoyote inayotokana na miradi hiyo, kama ipo, inakuwa ni matokeo ya ziada ya lengo halisi lililokusudiwa.

Miundombinu tuliyorithi kutoka kwa wakoloni, ambayo ni mengi kama vile reli ya kati iliyojengwa na Mjerumani, ni kielelezo kimoja wapo cha ukweli huu ninaouzungumzia. Bila ya shaka, reli hii ilikuwa, na inaendelea kuwa, na faida lukuki kwa wananchi walio wengi, lakini hilo halikuwa lengo halisi la mkoloni kuijenga. Mkoloni aliijenga kukidhi maslahi yake ya kiutawala na kibiashara.

Kuna ripoti pia viongozi wa nchi masikini hushawishiwa kuchukua mikopo mikubwa kutoka taasisi za kifedha za kimataifa kama vile Benki ya Dunia na kutekeleza miradi ambayo wakati kwa juujuu inaonekana lengo lake ni kuwaletea maendeleo wananchi, ukweli ni kwamba lengo halisi ni kutunisha mifuko ya wakopeshaji, washauri wao, na viongozi mafisadi na washirika wao.

Tusisahau pia miradi hii inayoitwa ya maendeleo ni sehemu nzuri na salama zaidi kwa viongozi mafisadi na washirika wao kujihusisha na vitendo vya rushwa. Mwananchi anaweza kufurahia ujenzi wa barabara fulani, kama tu anavyopaswa, lakini waliobuni na kutekeleza mradi huo wanajua kwa nini ulibuniwa na kutekelezwa. 

SOMA ZAIDI: Ucheleweshaji Ulipaji Fidia Mbeya Wahofiwa Kuchochea Migogoro Kati ya Wananchi

Hili, kusema ukweli, halihitaji hata mjadala mpana ukizingatia taarifa ambazo zipo zinazoonesha kwamba miradi mingi inayoitwa ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya nchi haiakisi mahitaji halisi ya wananchi wa jamii hiyo, na mwisho wa siku uendelezaji wake unakuwa wa mashaka. 

Kama mradi lengo lake ni kuwarahisishia maisha wananchi wa sehemu fulani, kwa nini wananchi hawashirikishwi kwenye kubuni na kutekeleza mradi huo, na hata pale wanaposhirikishwa maoni yao yanawekwa kando na mamlaka za Serikali kutekeleza kitu tofauti kabisa na kile wananchi wamesema ndiyo kipaumbele chao? Lengo, bila ya shaka, ni tofauti na hilo. 

Hii yote inatuambia kwamba tunapoamua kutekeleza mradi fulani unaoitwa wa maendeleo, na kujiridhisha kwamba hatua hiyo itamuathiri mwananchi mmoja au zaidi kwa namna yoyote ile, iwe ni kuvunjwa kwa nyumba yake au kufutwa kwa ardhi yake, ni lazima watu hao walipwe fidia zao na walipwe mapema kabla mradi husika haujaanza kutekelezwa.

Haisaidii kumwambia mwananchi huyu kwamba aendelee kubaki bila nyumba au shamba la kulima kwa sababu eti mradi unaotekelezwa unalenga kumletea yeye na wananchi wenzake ‘maendeleo.’ Kwa mwananchi huyu, ‘maendeleo’ ni nyumba yake aliyoijenga kwa jasho na damu au shamba linalomuendeshea maisha yake.

Hata haikubaliki kwa Serikali kuanza utekelezaji wa mradi fulani unaoitwa wa maendeleo bila kulipa waathirika fidia zao kwani hatua hiyo inapaswa kuwa ya kwanza kwenye mchakato mzima wa utekelezaji wa mradi husika. Ni jukumu la wabunifu wa mradi kujua gharama zinazopaswa kuingiwa ili kufanikisha mradi fulani, na kama kuna ulipaji fidia, ni lazima gharama hizo zijumuishwe kwenye gharama nzima za mradi.

SOMA ZAIDI: Wananchi, Wawekezaji Wavutana Ulipaji Fidia Mradi wa Uchimbaji Mchanga Kigamboni

Serikali inawezaje kutafuta fedha za kununua nondo na saruji za kujengea mradi fulani na kuacha kutafuta fedha za kulipa watu fidia, hatua ambayo ndiyo ya msingi kabla ya hatua nyingine yoyote ile? Unahitaji kuwa na akili ya wastani tu kufahamu kwamba bila ya kufanya hivyo, utekelezaji wa mradi huo utapata ukinzani kutoka kwa waathirika wake.

Haisaidii sana pia kuwatupia lawama wananchi hawa kwamba wanapinga ‘maendeleo’ kwani kilicho maendeleo kwako, kinaweza kuwa cha laana kwangu. Biashara ya utumwa na ukoloni ilikuwa ni miradi ya maendeleo ya watu wa Ulaya, lakini ilikuwa laana kwetu Waafrika. Kulazimika kubaki bila nyumba ya makazi au ardhi ya kilimo kupisha mradi wa ‘maendeleo’ kunaweza kuwa na maana sawa.

Naisihi Serikali ihakikishe ulipaji wa haraka wa fidia kwa wananchi wote walioathirika na utekelezwaji wa miradi mbalimbali inayoitwa ya maendeleo. Hii ni muhimu kujenga imani kwamba miradi hii inatekelezwa kweli kwa maslahi mapana ya taifa na watu wake, badala ya maslahi finyu ya mafisadi Serikalini na washirika wao.

Kama tunasema maendeleo tunayofanya ni ya watu, basi hatuna budi kuhakikisha kwamba hakuna mtu anaachwa na vilio wakati wa kutekeleza miradi hiyo. Kama mtu anastahili kwa mujibu wa sheria kulipwa fidia kupisha mradi fulani, mtu huyo apewe haki yake kupisha utekelezaji maridhawa wa mradi husika.


Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *