The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ucheleweshaji Ulipaji Fidia Mbeya Wahofiwa Kuchochea Migogoro Kati ya Wananchi

Watu wapatao 78 kutoka kijiji cha Ifiga, Mbeya Vijijini, wanasubiri kulipwa fidia na Jiji ambalo limeuza ardhi zao kwa wananchi wengine.

subscribe to our newsletter!

Mbeya. Serikali mkoani hapa imeshauriwa kumalizia malipo ya fidia kwa wananchi wa Ifiga, kata ya Ijombe, wilaya ya Mbeya Vijijini, mkoani hapa waliouza ardhi zao kwa Halmashauri ya Jiji kabla ya mamlaka hiyo kuuza ardhi hizo kwa wananchi wengine ili kuepusha migogoro kati ya wananchi inayoweza kusababishwa na kadhia hiyo.

Wananchi hao wanaokadiriwa kufika 78 wanaidai Halmashauri ya Jiji la Mbeya Shilingi milioni 300 wakiwa ni sehemu ya wananchi wa eneo la Mwahala, lililopo karibu na mpaka wa wilaya ya Mbeya Vijijini, ambalo Jiji ililinunua mwaka 2021 kwa kile ilichosema ni “kuweka jiji katika mpango maalum.”

Jiji liliwaahidi wananchi hao, waliokuwa wakijishughulisha na kilimo cha nafaka na mbogamboga, kwamba ingewalipa fidia zao mapema tu baada ya kuondoka kwenye eneo hilo. Hata hivyo, ni miaka miwili sasa imepita na baadhi ya wananchi hawajapokea fidia hiyo, hali wanayosema inawasababishia usumbufu mkubwa.

Kuna hofu ya kuibuka kwa migogoro kati ya wale wananchi waliouza ardhi zao kwa Jiji na wale ambao wamenunua ardhi hizo kutoka mamlaka hiyo kwani pande mbili hizo zimekuwa zikivutana juu ya nani ana uhalali wa matumizi ya maeneo hayo.

Richard Samson ni mkazi wa eneo hilo anayepaswa kulipwa fidia na Halmashauri ya Jiji ambaye aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano naye kwamba usumbufu ni mkubwa kwani kwa sasa hawezi kutumia shamba lake na wala hajapewa fedha ambayo ingemuwezesa kutafuta eneo jingine.

SOMA ZAIDI: Askari wa Uhifadhi Kilwa Wadaiwa Kukiuka Haki za Binadamu Wakihamisha Wananchi Kwenye Ardhi Yenye Mgogoro

“Wanasema shamba limenunuliwa, ina maana huyo mtu aliyenunua hilo shamba, ina maana Serikali inachukua mashamba bure bila malipo yoyote?” Samson, 32, alihoji. “Serikali ina tabia ya kupokonya watu shamba bila kumlipa fidia yeyote? Tunahitaji kulipwa.”

Oliva Msunganila ni moja kati ya wananchi walionunua ardhi hiyo kutoka kwa Halmashauri ya Jiji ambaye ameshindwa kulitumia kwani mamlaka hiyo bado haijamlipa aliyekuwa mmiliki wake, hali anayodai inasababisha usumbufu mkubwa kwa wote wawili.

“Nimenunua kiwanja Serikalini na nilishalipa hela zangu zote, nishamaliza, mpaka sasa hivi [watu wa Jiji] hawajamkabidhi mwenye eneo nililonunua mimi hela zake na mimi nina shida na eneo langu nataka nilitumie,” alilalamika Msunganila. 

“Jiji wanapaswa wawape hawa watu hela zao ili sisi tuwe huru na viwanja vyetu,” Msunganila, 30, aliongeza. “Hivi sasa inaonekana mimi ndiye ninayemnyanyasa mwenye eneo lake kwa sababu mimi si nimeuziwa na Serikali, wenyewe hawaitambui Serikali, wananitambua mimi ninayemiliki hilo eneo.”

SOMA ZAIDI: Dhuluma Baada ya Kuachika Inavyowasukuma Wanawake Zanzibar Kutaka Kumiliki Ardhi Kisheria

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Ifiga, Yohana Julius, ameieleza The Chanzo kwamba kushindwa kwa Halmashauri ya Jiji kuwalipa wananchi hao fidia zao inasababisha mgogoro miungoni mwao, akitoa wito kwa mamlaka husika kuingilia kati haraka iwezekanavyo.

Julius alisema kwamba uongozi wake umefuatilia sana sakata hilo ili kuhakikisha kwamba Jiji linawalipa wananchi stahiki zao, akisikitika kwamba kwa kiwango kikubwa juhudi zao zimeshindwa kuzaa matunda.

“Sasa hivi imekuwa ni shida,” alidokeza Julius. “Mwenye eneo anaenda kupanda maparachichi kwenye eneo lake ambalo halijalipiwa. Sasa ugomvi utakaotokea hapo kesho na kesho kutwa ni mkubwa. Jiji lifanye liwalipe hawa watu.”

The Chanzo ilimtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, John Nchimbi, kufahamu ofisi yake ina mpango gani kumaliza kadhia hiyo ya wananchi ili kuepusha migogoro hiyo inayotarajiwa miongoni mwao.

Nchimbi alimuelekeza mwandishi wa habari hii kwa Mkuu wa Idara ya Mipango Miji Mkoa, Dicklay Anasi Nyato, ambaye alisema mchakato wa kuwalipa wananchi hao ulishaanza, akibainisha kwamba ni watu wachache tu ndiyo ambao bado hawajalipwa.

SOMA ZAIDI: CCM Yadaiwa Kupora Ardhi ya Wanakijiji Kilimanjaro

Kwa mujibu wa maelezo ya afisa huyo, Jiji lilipaswa kulipa Shilingi bilioni 1.5 kama fidia, na mpaka sasa jumla ya Shilingi bilioni 1.2 imeshalipwa, huku mchakato wa kumalizia Shilingi milioni 300 iliyobaki ukiwa uko mbioni.

“Tunatarajia kwamba kati ya Novemba 2023 na Januari 2024 tutakuwa tumekamilisha malipo hayo,” alisema Nyato kwenye mahojiano na The Chanzo, akihusisha ucheleweshaji huo na “matatizo yaliyojitokeza” ya kifedha ambayo hakuyataja.

“Wananchi ambao hawajalipwa katika hiyo Shilingi milioni 300 wabaki kwenye mashamba yao mpaka pale watakapokuwa wamelipwa,” aliagiza Nyato. “Wale ambao tumemaliza kulipa, basi watapaswa kuondoka kwenye mashamba yao, wapishe wale walionunua.”

Modesta Mwambene ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Mbeya. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia mwambemo@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *