The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Dhuluma Baada ya Kuachika Inavyowasukuma Wanawake Zanzibar Kutaka Kumiliki Ardhi Kisheria

Wanawake wanaamini kwamba umiliki wa ardhi kisheria utawasaidia katika jitihada zao za kukabiliana na ukatili wa kijinsia unaotajwa kutamalaki visiwani humo.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Halima Ali Issa hataki kukumbuka machungu aliyoyahisi baada ya kufukuzwa kwenye nyumba aliyoshiriki kuijenga kwa hali na mali pale aliyekuwa mume wake alipoamua kutalikiana naye mnamo mwaka 2018.

Mama huyu wa watoto wawili anasema kwamba kitendo cha mzazi mwenzake huyo kumpora haki na stahiki zake zote juu ya mali alizochangia upatikanaji wake kilimfanya ahisi kama vile dunia imemuangukia, huku akishindwa kuona pahala pa kuitua.

“Sikujuwa kama kuna siku [mzazi mwenzangu] anaweza kunifukuza, au kunitoa kwenye nyumba ambayo sote tuliwekeza nguvu za kujenga na kuisimamisha,” Halima, 35, alisema akikumbuka ukurasa huo mchungu kwenye kitabu cha maisha yake. “Niliwaangalia watoto wangu, kisha nikasema, haya.”

Simulizi ya mkazi huyu wa Dunga, mkoa wa Kusini, kisiwani Unguja inaakisi uhalisia wa wanawake wengi wa Kizanzibari wanaojikuta wakipoteza haki juu ya mali, ikijumuisha nyumba na ardhi, walizozitolea jasho kuzipata punde tu baada ya kutalikiana na waliokuwa waume zao.

SOMA ZAIDI: Ukatili Kwenye Ndoa Watajwa Kuchochea Talaka Zanzibar

Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), ambayo imekuwa mstari wa mbele kuwasaidia wanawake wanaopitia kadhia kama hizo, iliiambia The Chanzo kwamba kwa mwezi mmoja, taasisi hiyo hupokea wastani wa kesi 20 zinazohusiana na malalamiko kwenye ndoa, 10 kati ya hizo zikihusu madai ya wanawake kudhulumiwa mali na waume zao.

Halima Ali Issa akiwa ameshika karatasi zake za maombi za kurasimisha ardhi yake kwenye ofisi ya Kamisheni ya Ardhi Zanzibar. PICHA | NAJJAT OMAR

Umiliki wa kisheria

Ni katika muktadha huu ndipo wanawake wengi visiwani humu wameonesha mwamko wa kumiliki mali zao, hususan ardhi, kisheria ili iwe ngumu kwa wao kudhulumiwa na wenza wao pale wanapoamua kuhitimisha safari yao ya kuishi pamoja kama mume na mke.

Taarifa kutoka Kamisheni ya Ardhi Zanzibar, idara ya Serikali inayosimamia masuala yote yanayohusiana na ardhi visiwani humo, zinaonesha kwamba idadi ya wanawake wanaoomba kupata hati za ardhi imeongezeka kutoka 221 kwa mwaka 2021/2022 mpaka kufikia 234 mwaka 2022/2023.

Dk Abdul-Nasser Hikmany ni Mrajisi wa Ardhi kutoka Kamisheni ya Ardhi Zanzibar ambaye aliiambia The Chanzo kwamba wanawake wengi wamekuwa na hamasa ya kutafuta hati za ardhi wanazomiliki, akisema sababu kubwa inayowasukuma wanawake kufanya hivyo ni “usalama.”

SOMA ZAIDI: Takribani Mwaka Tangu Wapendwa Wao Wauwawe Kikatili, Familia Hizi Zataka Haki Kutendeka

“Inatokana na hamu ya kuwa na usalama zaidi [wa maisha yao],” Dk Hikmany anasema. “Umiliki halali huwasaidia [wanawake] kupata mikopo na hivyo kuwa na uwezo wa kusomesha watoto wao. [Umiliki wa kisheria pia] hutoa ulinzi kwa wanawake wenyewe [dhidi ya kudhulumiwa].”

Moja kati ya wanawake walioonesha mwamko huu ni Halima ambaye tangu arudi kutoka Oman, ambako alikuwa akifanya kazi za ndani, amekuwa akipigana vikumbo na watendaji wa Serikali katika jitihada zake za kutafuta hatimiliki ya ardhi anayomiliki huko Kisakasaka, wilaya ya Magharibi B, mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Mnamo Agosti 2, 2023, The Chanzo iliongozana na Halima, akiambatana na dada yake, Fatma Ali Issa, kwenda ofisi za Kamisheni ya Ardhi kufuatilia upatikanaji wa hati halali ya umiliki wa ardhi yake.

Akiwa ameshika bahasha yenye makaratasi, Halima alianza kwenda chumba cha masijala ya ofisi hiyo, akienda ofisi moja baada ya nyingine, kabla ya kurudi baada ya kama dakika 45 pale The Chanzo ilipokuwa imekaa na dada yake, tabasamu kubwa likiwa limetanda usoni mwake.

“Nimeambiwa nije Agosti 20, [2023] kwa ajili ya kulipia Sh70,000 na kupata hati ya uhalali wa umiliki,” Halima alisema kwa sauti iliyoashiria ushindi. “Lakini [wamesema] naweza pia kuanza kujenga.” (The Chanzo ilimsindikiza tena Halima kwenda ofisi za Kamisheni ya Ardhi hiyo Agosti 20 ambapo aliambiwa hati yake haijakamilika).

Dk Abdul Nasser Hikmany, Mrajis wa Ardhi kutoka Kamisheni ya Ardhi Zanzibar, akizungumza na The Chanzo Ofisini kwake, Zanzibar. PICHA | NAJJAT OMAR

Napata amani

Halima amedhamiria kupata umiliki halali wa ardhi yake, akisema kwamba asingependa kuona aibu aliyoipata baada ya kutengana na aliyekuwa mume wake ikimrudia tena kwenye maisha yake.

“Ukiwa na karatasi zako unapata amani ya kwamba hiki kitu ni changu na hakuna mtu wa kinipokonya, au kukichukua; ni usalama wa watoto wangu pia,” anasema Halima. “Mtu kurudi nyumbani na watoto [baada ya ndoa kuvunjika] ni aibu na kutaabika. Mimi naona kumiliki ardhi ni kuheshimika, maana ardhi inakuwa ya kwako.”

SOMA ZAIDI: Wanawake Wawili Wauwawa Kikatili Zanzibar. Familia, Wanaharakati Wataka Uwajibikaji

Halima siyo mwanamke pekee visiwani humu aliyedhamiria kujikomboa kwa kupigania umiliki wa kisheria wa ardhi yake. Mamia ya wanawake kwenye maeneo mbalimbali ya Zanzibar wako mbioni kurasimisha ardhi zao serikalini, huku wengine wakifanya hivyo kupitia vikundi vyao vya akina mama.

Jina Haji ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Akiba cha Tunaweza kilichopo Fuoni, mkoa wa Mjini Magharibi, kisiwani Unguja chenye wanachama 25 wote wakiwa ni wanawake wajasiriamali ambacho malengo yake makuu ni kuwawezesha wanachama wake kumiliki ardhi kisheria.

Akizungumza na The Chanzo iliyowatembelea kikundini hapo, Jina alisema kwamba tangu kianze kufanya kazi hapo mwaka 2020, kikundi hicho kimewawezesha wanachama wake wanne kununua na kumiliki ardhi kisheria.

“Mwanzo hatukuamini kama tunaweza,” Jina, ambaye wanachama wengi kwenye kikundi chake ni wajane wenye watoto, alisema. “Tulikuwa 35 ila baada wengine kutoka sasa tupo wenyewe na tumeweza, na tunaamini na hao watu wanaotuuzia wanatuamini. Tunafuraha na tunaona mafanikio kuwa na ardhi.”

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake – Zanzibar (TAMWA-Z) ni moja kati ya wadau ambao wamekuwa mstari wa mbele kwenye kuwahamasisha wanawake wa Zanzibar kumiliki ardhi kisheria, ikiamini kwamba hatua hiyo inaweza kuchangia kupunguza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake visiwani humo.

Ukatili wa kijinsia unatajwa kuwa mkubwa visiwani humu. Kwa mfano, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar iliripoti mnamo Januari 17, 2023, kwamba kwa mwaka 2022 ilirekodi matukio 1360 ya ukatili na udhalilishaji, yakiathiri watu wapatao 1361, wengi wao wakiwa ni watoto (asilimia 86.2) na wanawake (asilimia 13.6).

Kukosa haki

Fatma Khamis Ali ni mwanasheria anayefanya kazi na TAMWA-Z ambaye ameieleza The Chanzo kwamba taasisi hiyo imekuwa ikiwasaidia wanawake kumiliki ardhi kisheria baada ya kugundua kwamba wanawake wengi wamekuwa wakikosa haki zao baada ya ndoa kuvunjika.

SOMA ZAIDI: Watoto 1,173, Wanawake 185, Wanaume 3 Wafanyiwa Ukatili Zanzibar 2022

“Kwa mwaka 2022, tulipokea jumla ya kesi za migogoro 19 na 2023, kuanzia Januari hadi Agosti 5, tumepokea kesi 22 huku wanawake wakiwa na kesi 15 na wanaume ni saba,” Fatma alisema. “Hadi sasa, wanawake 11 wamepata umiliki wa hati za ardhi toka tuanze uhamaishaji mwaka 2021 na wengine wapo kwenye mchakato [wa kutafuta].”

Jamila Mahmoud, Mkurugenzi Mtendaji wa ZAFELA, amesema ni muhimu kwa wanawake kuwa na uthibitisho wa mchango waliotoa kwenye kutafuta mali pindi wanapokuwepo kwenye ndoa, akisema kwamba wengi wao hukosa haki zao mahakamani kwa kukosa ushahidi.

“Tunawashauri wanawake kuweka kumbukumbu zinazotambulika kisheria au hata kuwasainisha waume zao kwenye masuala ya mali ili iwapo ikija kutokea ndoa imevunjika, basi naye mwanamke apate haki zake,” Jamila alisema.

“Wanawake wanataka usawa wa mali [baada ya ndoa kuvunjika] lakini ukimdai kithibitisho, hakuna,” aliongeza Jamila. “Hiyo inamfanya ashindwe kupata haki yake.”

Najjat Omar ni mwandishi wa Habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *